Kisa Cha Saalim (Mtoto Aliye Kipofu)
Kisa Cha Saalim (Mtoto Aliye Kipofu)
Imefasiriwa Na: Ummu Ahmad
Kisa hiki anakielezea Raashid baba yake Salim.
Sikuwa Muislamu wa kweli. Nilikuwa na marafiki waovu. Nilikuwa napenda kwenda matembezini pamoja nao. Muda mwingi sikuwepo nyumbani, daima nikikusanyika na rafiki zangu kutia domo na kusengenya watu ili tujifurahishe. Rafiki zangu walinijua sana kwa vile walikuwa wakipendezwa sana na masikhara yangu.
Usiku mmoja (nilikuwa tayari nina umri wa miaka 30, tayari nina mke ambaye alikuwa amebeba mimba ya mtoto wetu wa kwanza), kama kawaida nilikuwa nimekusanyika na rafiki zangu, tukizungumza mambo yasiyokuwa na maana. Nilikuwa nawahadithia siku niliyomuona kipofu sokoni nikamuekea mguu mbele ili aanguke, akaanguka kifudifudi, rafiki zangu wakacheka.
Usiku ule niliporudi nyumbani, mke wangu aliniuliza ‘ulikuwepo wapi? nimechoka na ninaumwa, nafikiri ni machungu ya kutaka kujifungua’. Chozi likimdondoka shavuni. Nikajisikia vibaya, kwa vile sikuwa nikimshughulikia ipasavyo.
Haraka nikampeleka hospitali. Alibakia katika hali ya uchungu kwa muda mrefu bila ya kujifungua, nami nilivuta subira ya kusubiri, lakini hatimae nikaondoka na nikaagiza hospitali wanijulishe akishajifungua. Baada ya muda wa saa moja, wakanipigia simu kunijulisha kuwa mke wangu keshajifungua mtoto wa kiume aitwae Salim.
Haraka nikaenda hospitali. Nikaulizia chumba alichowekwa mke wangu. Wakaniambia kwanza itabidi nionane na daktari. Nikawakasirikia na kusema "Daktari gani? Nataka kumuona mtoto wangu". Wakasisitiza kuwa nimuone daktari kwanza.
Hivyo nikaenda kumuona daktari, ambaye akanizungumzia namna mtu apasavyo kupokea misiba inayotaka kwa Allaah (Subhanahu wa Ta’aalaa). Ndipo akaniambia, ‘mtoto wako kipofu!’. Nikainamisha kichwa changu nikikumbuka yule kipofu niliyemuangusha na kuona ni kichekesho.
Sikujua la kusema, nikamshukuru daktari kwa wema wake na nikaenda kumuona mke wangu. Mke wangu hakuwa na majonzi, kwani alikuwa keshakubali uwezo wa Allaah. Daima ilikuwa akiniusia kutocheka watu, kusema na kusengenya.
Tukaondoka hospitali. Sikuwa namshughulikia Salim. Sikumpenda na nilikuwa nafanya kama hakuwa akiishi ndani ya nyumba. Lakini mke wangu alikuwa akimtunza na kumpenda sana Salim.
Salim akawa anakua na kuanza kutambaa, ingawa hakuwa akitambaa kikawaida. Na alipoanza kutembea tukagundua kuwa alikuwa mlemavu. Hili lilizidi kuniathiri. Baada ya muda mke wangu akajifungua watoto wengine wawili wa kiume. 'Umar na Khalid.
Miaka ikapita, Salim na ndugu zake wakakua. Nami nilikuwa naendelea kukaa na rafiki zangu waovu, na sikupenda kuwepo nyumbani. Hata hivyo, mke wangu alikuwa na subira na daima alikuwa akiniombea dua Allaah aniongoze.
Ijumaa moja, niliamka saa 5 (wakati ambao kwangu bado ni mapema) na nilikuwa najitayarisha kwenda karamu (sikuenda kuswali Ijumaa). Nikavaa nguo pamoja na sweta na nilikuwa naelekea mlangoni ili nitoke ndipo nilipomuona Salim (tayari akiwa na umri wa miaka 10) akilia kwa sauti ukumbini. Hivyo, kwa mara ya kwanza katika miaka 10 nilijali. Na nikaenda kumuuliza kwa nini alikuwa analia. Salim alipohisi nakaribia, akanyamaza kulia na akanisukuma kama kutaka kusema, "Sasa ndio unajali, ulikuwa wapi kwa muda wa miaka 10!"
Salim alikuwa anamwita mama yake na ndugu zake lakini hakuna aliyemjibu, hivyo akaenda chumbani kwake. Nikamfuata. Mwanzoni hakutaka kuniambia kwa nini alikuwa analia.
Unajua kwa sababu gani alikuwa analia? Mdogo wake, 'Umar, ambaye kwa kawaida ndiye amchukuae kumpeleka msikitini alikuwa amechelewa. Akahofia kuwa ilivyokuwa ni Ijumaa, hatoweza kupata nafasi kwenye safu ya kwanza huko msikitini. Nikamuulliza, "hii ndio sababu ya kukuliza, Salim?" Akaitika. Mimi, kutoamini niliyoyasikia, nikawasahau rafiki zangu na karamu. Nikamwambia Salim kuwa nitampeleka msikitini. Salim hakuamini aliyoyasikia. Akafikiri baba yake anamfanyia utani. Akaanza kulia. Nikamfuta machozi na kumshika mkono kumuongoza kwenye gari. Salim akakataa. Akasema msikiti upo karibu, na anataka kwenda kwa miguu.
Sikuweza kukumbuka mara ya mwisho nilipokwenda msikitini. Msikiti ulikuwa umejaa lakini nilifanikiwa kumpatia Salim nafasi kwenye safu ya kwanza. Swalaah ilipomalizika, Salim aliniomba nimpatie msahafu. Nikafikiri, vipi atahitajji msahafu akiwa ni kipofu!!! Hata hivyo nikampatia ili nisimuumize hisia zake. Salim akaniomba nimfungulie Suwrah Al-Kahf ili nimsikilize anavyoisoma. Hivyo baada ya kumfungulia akaanza kuisoma akiwa amehifadhi suwrah yote.
Nikafadhaika na kuona aibu. Nikachukua msahafu na kuanza kusoma. Nikamuomba Allaah (Subhanahu wa Ta’aalaa) Anisamehe na Kuniongoza. Na ndipo nilipoanza kulia kama mtoto. Kulikuwa na watu bado msikitini, hivyo nikajaribu kuficha machozi yangu. Sikuweza nikaanza kulia kwa sauti.
Nikahisi mkono mdogo ukinipangusa machozi. Alikuwa Salim. Akanikumbatia na nikafikiri ‘sio wewe uliyekuwa kipofu, bali kipofu ni mimi kwa sababu nilikuwa nawakimbilia watu waovu ambao watanitumbukiza katika moto wa Jahannam’. Tokea siku ile kamwe sikukosa swalaah msikitini. Mke wangu alifurahi sana.
Nikaachana na rafiki zangu wabaya wote na kuonja ladha ya Imaan. Nikahudhuria halaqa. Nikawa karibu na Allaah na familia yangu. Nikamshukuru Allaah (Subhanahu wa Ta’aalaa) kwa fadhila Zake nyingi. Siku moja, rafiki zangu watukufu wakaamua kwenda sehemu ya mbali ili kufanya da'awah. Nikasita kuhusu kwenda, nikasali Istikharah na pia nikamuuliza mke wangu, nikashangaa alipozidi kunipa moyo ili niende. Alifurahi sana, kwani hapo kabla nilikuwa nasafiri bila ya kumuuliza. Nikamwambia Salim kuwa nitakwenda safari, akanikumbatia kwa mikono yake midogo na kuniaga.
Nilibakia safarini kwa muda wa miezi 3 na nilikuwa napiga simu nyumbani, nilikuwa ninawahamu sana, hasa Salim. Mara zote nikipiga simu na nikimuulizia huambiwa amekwenda skuli au msikitini. Kila mara nilimwambia mke wangu namna nilivyokuwa nina hamu na Salim, alikuwa anacheka kwa furaha. Isipokuwa nilipopiga simu mara ya mwisho, hakucheka na sauti yake ilikuwa imebadilika. Nikampa salam za Salim akanijibu "In shaa Allaah" na akanyamaza.
Hatimae nikarudi nyumbani nikiwa na matumaini Salim atanifungulia mlango, lakini ukafunguliwa na Khalid. Ndipo nikaona mke wangu sura imembadilika. Nikamuuliza "kumezidi nini" akajibu "hakuna kitu". Ndipo nikamkumbuka Salim, nikauliza "yuko wapi?" Mke wangu akainamisha kichwa, asijibu. Chozi likadondoka kwenye shavu lake.
Nikamtolea ukali "yuko wapi Salim? yuko wapi?" Mwanangu Khalid (miaka 4) akasema, "Baba, Thalem amekwenda Jannah, yupo pamoja na Allaah (Subhanahu wa Ta’aalaa)".
Mke wangu hakuweza kustahamili akaanza kububujika machozi na akaondoka. Baadae nikajua kuwa Salim aliugua homa na akapelekwa hospitali wiki 2 kabla sijarejea. Homa ilimzidi na mama yake alikaa pamoja nae mpaka roho yake ilipowacha kiwiliwili chake.
Khasara iliyoje kumkosa Salim ambaye sikumfaidi tokea utoto wake kwa muda wa miaka kumi. "Ni uchungu wa milele usiotoweka!"
**********
Nyongeza Kutoka Al-Hidaaya Kuhusu Mafunzo Tunayopata Katika Kisa Hiki:
1) Haifai kucheka kilema bali anatakiwa mtu anapoona kilema amshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kuomba duaa hii:
الْحَمْـدُ للهِ الّذي عافاني مِمّا ابْتَـلاكَ بِهِ، وَفَضَّلَـني عَلى كَثيـرٍ مِمَّنْ خَلَـقَ تَفْضـيلا.
"Sifa njema ni za Allaah ambaye ameniepusha na kile alichokupa mtihani na akanifanya mimi kuwa bora kuliko wengi miongoni mwa aliowaumba".
2) Ubaya wa kuambatana na marafiki wabaya.
3) Kushukuru mitihani ya Allaah unapojaaliwa kupata yasiyokuridhisha kama mtoto kilema n.k. Na kuamini Qadhaa na Qadar.
4)
Haki za mzazi kwa watoto, kuwalea na kuwapa mapenzi, rahma, huruma tokea udogoni hadi ukubwani. Kuwafunza adabu na tabia njema, kuwapa elimu, kuwa nao wakati wote na kuwasaidia katika shida na matatizo yao.
5) Faida ya kuwa na mke mwema mwenye imani na dini yake.
6) Kuwazoesha watoto kwenda msikitni ili wawe na mapenzi na nyumba ya Allaah.
7) Allaah Hapofui macho bali anapofua nyoyo kwani Salim kipofu ameweza kuhifadhi Qur'aan na akawa mwema kuliko baba yake mwenye kuona. Allaah Anasema:
فَإِنَّهَا لَا تَعْمَى الْأَبْصَارُ وَلَـٰكِن تَعْمَى الْقُلُوبُ الَّتِي فِي الصُّدُورِ ﴿٤٦﴾
Kwani hakika hayapofuki macho, lakini zinazopofuka ni nyoyo zilizomo vifuani. [Al Hajj: 46]
8) Huenda ukachukia jambo nalo likawa na kheri nawe. Anasema Allaah:
فَإِن كَرِهْتُمُوهُنَّ فَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَيَجْعَلَ اللَّـهُ فِيهِ خَيْرًا كَثِيرًا ﴿١٩﴾
Basi asaa ikiwa mnachukia jambo na Allaah Akalijaalia kuwa lenye khayr nyingi. [An-Nisaa: 19]
Na Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) vilevile:
وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٢١٦﴾
Na asaa mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui. [Al-Baqarah: 216]
9) Majuto ni machungu, hivyo bora kujiepusha kabla ya kukufikia.