Kisa Cha Rachel Nuur

 

Kisa Cha Rachel Nuur

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Rachel Nuur ni  ndugu yetu aliyesilimu mwezi  wa Agosti, 1999. Kusilimu kwake kumechangiwa na matatizo aliyokumbwa nayo katika mazingira ya ndoa yake, kama anavyosimulia mwenyewe.

 

"Katika mwaka wangu wa mwanzo nikiwa Muislamu ulikuwa ni wa hamu sana, ingawaje hukosi kuwa na mitihani midogo midogo ya hapa na pale.  Baadhi ya wakati unashukuru na kufurahi sana kuutambua na kuutekeleza Uislamu, na baadhi ya siku unafikiria maisha ni mapesi zaidi kwa mtu asiye Muislam. Na hasa unapokuwa huna marafiki au jamii inayowafikiana nawe, basi mazingira huzidi kuwa magumu. Namshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) siku nyepesi kwangu zilikuwa ndizo nyingi kuliko za wakati mgumu. Na kwa moyo mkunjufu napenda kuwajulisha kuwa sijuti na wala sisikitiki mimi kuwa Muislamu. Yaliyobaki ni ukumbusho tu.  Maisha yangu ya baadae yanaonekana kuwa mazuri kuliko ya zamani.

 

Ilikuwa mnamo Januari 1999 ambapo ndoa yangu ilianza kusambaratika. Nikiwa mke mwenye miaka 23, mwenye mume na watoto wawili wanawake, mdogo niliyemzaa Septemba mwaka huo na mkubwa aliyekuwa na miaka mitano wakati huo. Nikiwa kama mhudumu katika mkahawa wa ki-Mexico ndio kazi iliyokuwa ikinipatia riziki ya kuendesha maisha na familia yangu. Mume wangu mwenye asili ya kihindi alikuwa akifanya kazi na kusoma katika mji wa Virginia.  Mwaka huo yeye alifanikiwa kupata haki ya kuishi Marekani (green card), na ghafla akaanza kubadilika na kupanga mambo ya maisha yake bila ya kunishirikisha mimi na watoto wetu. Akaamua kuondoka kurudi kwao kutazama familia yake.

 

Kwa vile nilikuwa nikifanya kazi na marafiki wa Kiislamu wa ki-Pakistani, walijaribu mwanzoni kunitanabahisha na kunitahadharisha kwa njia moja au nyingine lakini nilifumba macho na kutoyaamini.  Kumbe mume wangu tayari alikuwa keshapangiwa mke wa kikwao na ilihali hao wazee wake walijua kuwa tayari ana familia yake Marekani, lakini hawakujali kabisa hilo. Hivyo baba wa watoto wangu aliondoka bila ya hata kuwafikiria watoto wake.

 

Wafanyakazi wenzangu walikuwa ni wa mchanganyiko, wenye asili ya kihindi na ki-Pakistani waliochanganya na wa-Mexico. Miongoni mwao wengi ni Waislamu poa, yaani  si wenye kufuata sheria na mwendo wa Kiislamu na baadhi yao wameshaghilibiwa na tabia za ki-Marekani, ingawaje sio wote.

 

'Uthmaan alikuwa ni mgeni kutoka  Costa Rica, ni kijana mpole na asiyependa kusema. Akifanya kazi sehemu ya jikoni na akifahamika kama mjomba wake Asjid. Basi siku moja nilichanganyikiwa kazini, najua baadhi ya wenzangu wakifahamu kisa halisi kilichonitokea lakini hawakutaka kujihusisha na matatizo yangu kwa vile ni kinyume na utamaduni wao. 'Uthmaan kidogo kidogo alianza kuzungumza nami wakati tukiwa kwenye mapumziko ya kazi na aliniahidi kunisikiliza matatizo yangu na wala kutoniamulia chochote.

 

Siku moja nikaamua kulitoa joto langu lote kwake, ilikuwa kama wiki moja baada ya kutokea tukio la kuchanganyikiwa kazini. Siisahau siku ile moyo wangu ulipiga sana na kwa haraka. Kila nililolifikiria nililiona haliwi, nilitaka kurudi kusoma shuleni lakini sikuweza kujilipia. Nilijiona sina maana ya kuishi na kudiriki kufikia maamuzi ya kutaka kujiua. Niliona nimeachwa katika njia panda na mume wangu niliyemthamini yeye na familia yake. Lakini wapi? Hawakujali hayo wala watoto wao niliowatunikia. Almuradi nilichanganyikiwa kiasi cha kuona kwamba Allaah Hanipendi licha ya Swalaah na maombi yangu niliyokuwa nayaomba.  Kila usiku nikisoma biblia na kuona hainipatii jawabu hasa ya masuala niliyokuwa nikijuuliza.  Kisha nikawafikiria wanangu watalelewa na nani? Hatimae nikamlani shaytwaani na kuwa mkakamavu. Na ndipo nilipomuomba mama yangu kunipeleka Hospitali kupata matibabu ya kiakili.

 

Usiku ule nililazwa katika wodi ya watu wenye matatizo ya akili, kwa muda wa siku nilikuwa silali, sinywi wala sili. Nilikuwa nalia na kulia tena. Mwishowe wahudumu wa hospitali wakaamua kunipatia dawa za usingizi na nikalala kwa muda wa masaa kumi na mbili. Baada ya kuamka nilijisikia vizuri ijapokuwa mnyonge lakini nikawa tayari kushauriwa. Nikaeleza mkasa wangu wote karibu ya masaa matatu, na wakaniwaidhi kwamba siku zote amani huanza moyoni na kuwa jitihada ni utaratibu wa kawaida. Basi baada ya kuondoka nilichofanya ni kuandika maazimio na malengo yangu yote ninayotaka kuyafanya, na kuamua kuishi kwa ajili ya watoto wangu.

 

Mara nikajulishwa kuwa nimepata mgeni, hakuwa mtu mwengine yoyote isipokuwa 'Uthmaan, kumuona tu nikaanza kulia. Akaniambia niwe mstahamilivu ili tuongee. Basi yeye hakuwa na maongezi mengi ila aliniambia kauli ambayo sitoweza kuisahau maishani mwangu nayo ni:

 

"Umasikini na matatizo ndiyo yaliyojaa nchini kwetu, lakini hakuna hata mtu mmoja anayechanganyikiwa na kutaka kujiua"  Je,  Unajua kwa nini?" Nikamwambia "Sijui kwa nini?" Akaniambia,  nchini kwao watu wanaamini Uislamu.  Wana Kitabu Kitukufu kiitwacho (Qur-aan) maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Kitabu hichi kinajibu masuala yako yote ujiulizayo na mambo mengineyo. Kitakupa amani na utulivu wa moyo pindi utakapoamini .

Haya ndio yalikuwa majibu ya 'Uthmaan, na tangu dakika hiyo nikaapa kuwa nitafanya uchunguzi kamili juu ya Uislamu pindi   tu nitakapotoka hospitali. Na kusema kweli usiku ule nilifikiria jinsi maisha yangu yanavyoelekea kutaka kubadilika. Nilifikiria sana juu ya Kitabu hicho Kitukufu (Qur-aan) na uchache wa elimu niliyokuwa nayo ya kutotambua juu ya Uislamu. Nililala huku nikifikiria juu ya maajabu ya kitabu hicho na kwanini watu wengi hawana habari nacho?

 

Kulipokuchwa nilikutana na daktari wangu, sikuamini macho yangu, kwani kwa mshangao nilijikuta nakutana na daktari wa kike wa ki-Pakistani aliyekuwa Muislamu. Basi aliniuliza masuala mengi kuhusu matatizo yangu ya unyonge, nami nilimjibu kwa kadiri ya uwezo wangu huku nikiyazuia machozi. Aliniambia kuwa nahitaji ushauri wa mara kwa mara na kuniandikia vidonge vya kuondoa matatizo hayo.

 

Alipokuwa akiniandikia karatasi ya kutoka hospitali niliamua kuitumia nafasi hiyo kumuuliza masuala juu ya Uislamu. Alitulia na kuvuta pumzi huku akifunga kitabu chake.  Kwa uso wa bashasha, aliniambia atanisaidia kunipatia taarifa zote ninazozihitaji kuzijua za Uislamu. Alinieleza kuhusu Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwanini yeye ni Nabiy wa mwisho wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).  Na kuwa Uislamu haukuwa na tofauti baina ya ukiristo na Ujuda, isipokuwa Uislamu una uhusiano wa moja kwa moja baina ya Mja na Rabb wake, na hakuna yeyote anayeweza kuyakatisha mahusiano hayo. Aliendelea kunifahamisha kuwa kila mtu atabeba mzigo wake kwa mujibu wa matendo yake aliyoyafanya wakati yuko hai hapa duniani, na wale wasioamini basi wataadhibiwa siku ya qiyama na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Na Yeye Ndiye majibu na dawa ya masuala na mashaakil (matatizo) yangu yote.

Akaniambia kuwa kama nitafanya huo uchunguzi juu ya kuujua Uislamu basi sitohitaji tena dawa alizoniandikia kuondosha matatizo yangu. Na kunishauri kurudi pindi nikifikwa na matatizo au masuala yoyote.

 

Nilitoka hospitali siku ile ile na kuanza taratibu za kudai talaka yangu.  Pia nilianza uchunguzi wangu juu ya Uislamu kwa bidii na moyo wangu wote. Namshukuru 'Uthmaan na Waislamu wengineo waliojiunga nami katika uchunguzi huo. Alininunulia vitabu vingi vya Uislamu, nikawa nasoma kwa juhudi zangu zote.

 

Siku moja 'Uthmaan akatuchukua mimi na watoto wangu kwenye duka moja la vitabu vya Kiislamu, mwenye duka hilo alifurahi sana na kunizawadia msahafu wangu ya kwanza. Nilirudi nyumbani mwenye furaha kubwa sana na usiku mzima nikawa ninaisoma Qur-aan Tukufu na sikuweza kusita kuisoma. Suwrah Al-Baqarah niliiona nzito. Na nikajiona kama kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anazungumza nami (Allaahu Akbar). Hii ilitosheleza kuwa ni  jibu la masuala yangu, kwani inazungumzia yale mambo yote niliyokuwa nikijiuliza maishani mwangu. Kama vile  nini kinatokea baada ya kifo? Nabiy 'Iysaa alikuwa kweli ni mtoto wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)? Kwanini Nabiy 'Iysaa alikufa kutokana na madhambi yetu? Na iweje afe kwa ajili yetu? Kwanini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alituumba sisi?

 

Qur-aan inatoa ushahidi wa mambo mbali mbali, inazungumzia juu ya mito na bahari na kuwa kwanini bahari ya chumvi haikutani na maji yasiyo na chumvi? Inazungumzia juu ya maisha ya kiumbe ndani ya tumbo la uzazi na vipi Bwana Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) aliyajua haya? Yeye hakujua kusoma na wala kuandika, na kujua mambo ambayo hayakutambulikana wakati wote huo hadi hivi karibuni tu. Qur-aan inazungumzia meli kuelea juu ya bahari wakati Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliishi jangwani? Qur-aan inazungumzia juu ya milima kuwa kama vijiti, vimekwenda chini na kuchomoza juu, haya yote ni uthibitisho kuwa Allaah Yupo na kwamba tuamini na kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) tu.

 

Basi nikataka niwe Muislamu na ndio hasa dhumuni la maisha yangu, kuwa mtumwa wa kumtumikia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Na huu ndio ukweli ulivyo. Nikasilimu kwa kukiri shahada  mwezi wa Agosti 1999 na siku hii ilikuwa ni siku ya furaha kubwa maishani kwangu. Nashukuru nilipata talaka yangu katika mwezi wa Machi 2000. Na wala sikumuona au kumshuhudia au kumsikia tena aliyekuwa mume wangu  tangu kusilimu kwangu. Kwa vile hataki kujua kitu chochote juu ya watoto, na wala sijali. Watoto wangu wanaangaliwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na wanaye mimi mama yao.  

 

Mnamo mwezi wa Aprili 2000, 'Uthmaan akaniuliza kama niko tayari kuolewa tena, nami nikakubali kuolewa naye. Nashukuru tukaowana mwezi wa April 2000. AlhamduliLLaah maisha yetu yamekuwa mazuri na watoto wangu wanaendelea vizuri tu. Sasa najiendeleza kusoma na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akipenda natarajia kumaliza mwezi wa Mei na kupata shahada ya Muuguzi wa hospitali (Nurse) Na Allaah Ndiye Mpangaji na Ndiye Aliyenipangia yote haya AlhamduliLLaah.

 

*********

 

Alhidaaya Inatoa Mafunzo Yanayopatikana Katika Kisa Hiki:

 

 

1)  Ni vizuri kusaidiana katika matatizo bila ya kujali dini kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Huenda Akatia hidaaya ndani yake.

 

2)  Faida ya kutembelea wagonjwa ambao sio Waislamu kwani huenda wakapata Iymani na kuingia katika Uislamu.

 

3)   Tabia njema, ni njia mojawapo ya kuutangaza na kuudhihirisha  Uislamu.

 

4)   Kuipokea mitihani na kuridhika nayo kwani huenda ikawa na kheri ndani yake.

 

5)  Tusikate tamaa na Rahma ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), tunaona baada ya kuamini Nuur aliisalimisha nafsi yake na watoto wake kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na kwa Rahma Zake alimpa mume mwengine ambaye ni bora kuliko aliyemkosa.

 

6)   Iymani ya Uislamu peke yake inatosheleza kuwa ni dawa ya magonjwa na matatizo yote ya binaadamu.

 

7)   Tunapata yakini kuwa kweli Qur-aan ni ufumbuzi wa matatizo yote na kuwa haikuacha kitu, bali kila kitu kiko wazi kama alivyoeleza kuwa alipata majibu ya maswali yake yote kwenye Qur-aan tena kwa kusoma Suwrah moja tu Al-Baqarah.

 

8)    Qur-aan ni Kitabu cha haki chenye miujiza.

 

9)    Allaah  (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anamhidi Amtakaye na Anampotoa Amtakaye.

 

 

Share