Allaah Atakuajiri…Tawakkal Kwake!

 

Allaah Atakuajiri…… Tawakkal Kwake!

 

Imefasiriwa Na: Alhidaaya.com

 

Alhidaaya.com

 

 

Kijana mmoja alimaliza kusoma katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Madiynatun-Nabawiyyah na alikuwa mfano wa pekee kwa uhodari wake na mwenye akili nyingi alimaliza na kutunukiwa Shahada yake nzuri na akiwa na vyeti vinginevyo vya mapendekezo.

 

Lakini akazunguka kutafuta kazi katika kila shirika, na idara za serikali bila ya kufanikiwa kupata kazi popote.

 
Na kwa vile alitamani na kuazimia kuwa hatotoka katika uzuri wa vizuri. Nao ni mji huu mtukufu wa Madiynatun-Nabawiyyah, kwani je, nani anayeonja maisha mazuri kabisa katika uzuri na mazuri ya mji huu wa mpenzi wetu Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kisha akataka kuyawacha?  Naye anaona makumbusho ya Mpenzi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwaya Allaahu ‘anhum) katika kila shibiri ya mji huu? Kwani alitamani kuishi Madiynah akitumaini na kutegemea kupata fadhila za hadithi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyosema:

 

“Atakayeweza kufia Madiynah afanye hivyo kwani mimi nitamuombea shafaa’ah atakayefia hapo”.

 

Akaenda kwa mmoja wa walezi wema na miongoni mwa Mashaykh wema ambaye anayemuona humkumbusha Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa, na anayemsikia sauti yake utajua kwamba ana khofu ya Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa wala haifai kumtukuza mtu isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

Kasema: “Nilikwenda kwake nikamwambia” Ee Shaykh je, humjui mtu wa kuniajiri kazi?  Kwani milango imefungika mbele yangu, wala haujabakia mlango nisiougonga na yote haikufaa kitu. Wala sitaki kutoka katika mji huu wa Madiynah”. Shaykh akasema kwa lafudhi yenye kujiamini “Mwenye kuwa na yakini na ahadi ya Allaah, naam Wa-Allaahi namjua nani wa kukuajiri”.

 

Kwa haraka kabisa nikasema (huku furaha yangu  ikidhihirika). Nani huyo ewe Shaykh? Allaah Akuzidishie mema.  Nani huyo? Akasema Shaykh: “Huyo ni Allaah ‘azza wa Jaal

 

Nikapigwa na bumbuwazi!  

 

Akanitizama Shaykh akasema: “Ajabu!  Ningelikwambia kuwa ni Waziri fulani na mhusika fulani ungelifurahikiwa na kuona ni kheri.  Lakini nilipokutajia Yule Ambaye Anamiliki funguo za kila kitu na Yeye ndiye Muweza  wa kila kitu, Ambaye  Anamiliki vyote vya  mbingu na Ardhi na khazina za mbingu na ardhi, naona uso wako umebadilika kama vile kwamba una shaka na ahadi ya Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Ambaye amesema”:

 

وَفِي السَّمَاء رِزْقُكُمْ وَمَا تُوعَدُونَ   

Na katika mbingu kuna riziki yenu na yale mnayoahidiwa. [Adh-Dhariyaat: 22]

 

“Nenda ee mwanangu kwenye msikiti wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kabla ya Alfajiri kwa saa moja   umkaribie Allaah Ta’aalaa katika thuluthi ya mwisho ya usiku (katika masaa ya kabla ya Alfajiri) na mimi nina hakika na kutumainika kwamba Allaah Atakutimizia amri (haja ) yako.

 

Akasema (kijana): "Nilitahayari na kuona haya kabisa, tahayuri ambayo sijawahi kuihisi kabla.  Nikamuaga Shaykh kisha nikaondoka."

 

Nikaegesha kengele ya saa yangu kuniamsha saa tisa baada ya nusu ya usiku wa manane nikamka nikatawadha, kisha nikaenda Masjidi-An-Nabawi mtukufu huku nimejaa joto la imani ambalo siwezi kulielezea.

 

Nilipoingia, nikaswali ilivyopasa nikataka kunyanyua mikono yangu mbinguni niombe, lakini sikuweza kwa kuzidiwa na kilio ambacho kilinizidi nguvu hata nikadhania kuwa roho yangu itatoka na huku nikiwaudhi walio karibu yangu. Nikamuomba Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa maneno machache na Allaah ndiye Ajuaye yaliyomo vifuani.

 

Nikaswali Swalah ya jamaa ya Alfajiri kisha nikahudhuria darasa la mmoja wa wanachuoni wetu wenye kuheshimika kisha nikaelekea nyumbani kwangu. Nikawa nimesahau kila kitu isipokuwa Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa wala sikujiandaa kufikiri au kupanga chochote katika mambo ya dunia siku hiyo.

 

"Wakati niko njiani nikahisi kama mtu akiniambia elekea njia hiyo nyingine. Nikaelekea huko, mara nikakuta ofisi ya Idara ya serikali ambayo sijawahi kabla kuipitia.  Nikasema rohoni 'kwa nini nisiende nikawaulize kama wanayo kazi waniajiri?"

 

Nikaingia, kisha nikamkabili bwana mmoja aliyetabasamu usoni kwangu aliponiona naye wala hanijui.

 

Nikamuuliza: "Ee ndugu yangu mimi simjui mtu hapa, lakini ukipenda kupata thawabu, hivi hapa vyeti vyangu na shahada zangu, hakika mimi siku nyingi natafuta kazi sijafanikiwa. Alipotazama shahada zangu akaegemea pembeni mwa maktaba yake kwa mikono yake, akainuka na kunitizama akasema: ”Subhana Allaah! muda mrefu sisi tunatafuta watu wanaomiliki elimu kama hii uliyonayo, ulikuwa wapi? umekuja kutoka wapi? Sasa hivi utapata kazi In shaa Allaah!"

 

Akasema (Kijana): 'Nikainuka kitini nikamsujudia Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa sajda ya kumshukuru hapo hapo ofisini kwake huku machozi yakinilenga machoni mwangu na huku nikimkumbuka yule Shaykh mwema na yakijirudia maneno yake, "Huyo ni Allaah   ‘azza wa Jaal , Huyo ni Allaah   ‘azza wa Jaal"

 

Kisa hiki ni cha kweli.  Na ingawa ni kifupi, lakini utaona kwamba kina mafundisho mengi yenye manufaa kwetu:

 

1.     Kuwa na Tawakkul na Yakini Na Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa. 

 

2.    Sio hoja kusoma na kupata Shahada bali Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Ndiye Mwenye Kumruzuku mtu.

 

3.     Kuupenda mji wa Madiynatun-Nabawiyyah na kupata fadhila zake.

 

4.     Ni vizuri sana kutafuta Nasiha na ushauri kutoka kwa watu wema.

 

5.     Moja ya nyakati nzuri za Du’aa ni katika nyakati za kabla ya Alfajiri (Swalatu-Tahajjud).

 

6.     Swalah ya Jamaa msikitini haswa alfajiri ni muhimu.

 

7.  Kulia kwa sababu ya Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa humkurubisha mtu zaidi kwa Allaah   na humuongezea imani na mapenzi ya Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa. 

 

8.  Kusujudu sajdah ya kumshukuru Allaah Subhaahu wa Ta’aalaa kila unapopata au unaposikia jambo jema.

 

9.  Kuweka Nia ya jambo jema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Subhaanahu wa Ta’aalaa Atakuonyesha njia. 

 

Zifuatazo ni Aayah zenye kutufundisha faida ya Kutawakkal kwa Allaah, na kuwa Wachaji Allaah.

وَمَن يَتَّقِ اللَّهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا 

Na yeyote anayemcha Allaah; Atamjaalia njia ya kutoka (shidani) [Atw-Twalaaq: 2]

 

وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ ۚ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بَالِغُ أَمْرِهِ ۚ قَدْ جَعَلَ اللَّـهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا﴿٣﴾

Na Atamruzuku kutoka njia ambayo hatizamii. Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza. Hakika Allaah Anatimiza kusudio Lake. Allaah Amejaalia kwa kila kitu makadirio. [Atw-Twalaaq: 3]

 وَمَن يَتَّقِ اللَّهَ يَجْعَل لَّهُ مِنْ أَمْرِهِ يُسْرًا 

Na yeyote anayemcha Allaah Atamjaalia wepesi katika jambo lake. [Atw-Twalaaq: 4]

 

Allaahumma tujaalie tuwe wachaji Allaah, wenye kutawakkal  Kwako daima, Utusahilishie mambo yetu, na Uturuzuku kheri nyingi.  Aamiin. 

 

 

Share