Makosa Wanayofanya Hujaji Mara Kwa Mara
Makosa Wanayofanya Hujaji Mara Kwa Mara
Makosa Yanayohusu Ihraam
Hujaji wengine wanavuka kituo kilichoteuliwa kwa ajili ya ihraam katika njia za msafara wao bila ya kuwa katika hali ya ihraam au bila ya kuwa katika ihraam hapo. Wanaendelea hadi wanafika Jiddah au sehemu nyingine katika mipaka ya vituo ambako huko ndio wanaingia katika hali ya ihraam.
Hivi ni kinyume na amri ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo inaamrisha kuwa kila Hujaji anapaswa aingie kwenye ihraam katika kituo kilichoko katika njia ya msafara wake.
Inapomtokea mtu hivyo, ni lazima arudi katika kituo chake cha ihraam ili aingie katika ihraam. Au itambidi afanye kafara kwa kuchinja kondoo atakapokuwa Makkah na kuigawa nyama yote kuwalisha masikini.
Hii inawahusu Hujaji wote, wanaopita kituo wakiwa wamesafiri kwa njia ya angani, baharini au nchi kavu.
Ikiwa mtu hakupitia vituo vitano vilivyoteuliwa kwa ajili ya ihraam katika kila pande ya njia ya msafara, basi ni lazima aingie katika ihraam akiwa katika sehemu iliyo karibu na kituo cha ihraam kilichopo njiani kwake.
Makosa Yanayohusu Twawaaf
1-Kuanza twawaaf katika chanzo kingine kisichokuwa sehemu ya Hajarul-Aswad na hali ni fardhi kuanzia twawaaf hapo.
2-Kufanya twawaaf ndani ya Hijr Ismaa'iyl. Hii itamaanisha kwamba ni kuzungua sehemu tu ya Ka'abah na sio Ka'abah yote kwa vile Hijr Ismaa'iyl ni sehemu mojawapo ya Ka'abah yenyewe. Kufanya hivyo itakuwa imeachwa kufanywa twawaaf, na hivyo itakuwa twawaaf haikukamilika mzunguko wake. Twawaaf kama hii haifai.
3-Kufanya ramal (yaani kupiga hatua ndogo ndogo za haraka) katika twawaaf zote saba na hali ramal inatakikana kufanywa katika mizunguko mitatu tu ya mwanzo ya twawaaful-quduwm.
4-Kusukumana na watu na kusabisha zahma, kuwaumiza watu kutaka kulifikia Hajarul-Aswad ili kulibusu. Vitendo kama hivi vinaleta madhara kwa Waislamu na haturuhusiwi kufanya hivyo.
Itambulike kuwa twawaaf inabakia kuwa sahihi bila ya kulibusu Hajarul-Aswad. Ikiwa mtu hawezi kulifikia au kulibusu Hajarul-Aswad, inamtosheleza Hujaji anapofika sambamba nalo kuashiria tu kwa mkono na kusema 'Allahu Akbar' japokuwa yuko mbali nalo.
5-Hujaji kufuta au kusugua mkono wake katika Hajarul-Aswad akitegemea kupata baraka. Hili ni jambo lisilokuwa na dalili katika Shariy’ah ya Kiislam, hivyo ni bid'ah (uzushi). Sunnah ni kuligusa tu au kulibusu inapokuweko uwezekano wa kufanya hivyo bila ya taabu yoyote.
6-Kugusa pembe nne za Ka'abah au kuta zake, kusugua na kujipangusa nayo kwa kutegemea kupata baraka. Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakugusa sehemu yoyote ya Ka'abah isipokuwa Hajarul-Aswad na Ruknul-Yaman.
7-Kusoma du'aa zilizotajwa kuwa ni maalum kwa kila twawaaf moja, na utakuta kuna vijitabu vidogo vidogo vyauzwa huko Makkah vyenye du'aa maalum kwa kila twawaaf, du'aa hizo za kwenye hivyo vijitabu hazina ushahidi wala asli katika mafunzo ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) isipokuwa chache sana. Ni bora mtu aombe yale yaliyothibiti na pia yale anayoyahitajia yeye zaidi kuliko kukariri du'aa za kwenye hivyo vijitabu ambazo hawaelewi hata maana zake. Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakueleza bayana du'aa yoyote isipokuwa ni kusema 'Allahu Akbar' anapofikia Hajarul-Aswad na kila anapomaliza twawaaf moja baina ya Ruknul-Yaman na Hajarul-Aswad akisoma:
رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ
Rabbanaa Aatinaa fid-duniyaa hasanatan wa fil Aakiharati hasanatan waqinaa 'adhaaban-Naar.
“Rabb wetu Tupe katika dunia mazuri na katika Aakhirah mazuri na Tukinge na adhabu ya moto.”
Sehemu nyingine katika mzunguko wa twawaaf, anaweza kusoma Aayah za Qur-aan, du'aa zilizothibitika katika Sunnah, Kumtukuza, Kumsifu, Kumpwekesha, Kumshukuru Allah, Kuomba maghfirah, kumswalia Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) n.k .
8-Kupandisha sauti kupita sauti za wengine aidha anapoongoza watu katika hizo du'aa ambazo watu wamejipangia au anapomfuata anayemuongoza. Kufanya hivyo kunasababisha kubabaisha Hujaji wengine ambao wanasoma du'aa zao pole pole, wasiweze kupata khushuu katika ‘ibaadah yao wanapofanya twawaaf.
9-Kujilazimisha kuswali Maqaam Ibraahiym wakati kuna zahma za watu. Hii ni kinyume na Sunnah, pia husababisha maudhi na misongomano ambayo huishia kuumizana na Hujaji wengine. Inatosheleza kuswali rakaa mbili baada ya kumaliza twawaaf mahali popote katika Masjidil-Haraam.
Makosa Yanayohusu Sa’y
1-Kwenye kupanda kilima cha Swafaa na Marwah, baadhi ya Hujaji wanaelekea Ka'bah na kuiashiria kwa mikono wakisema 'Allahu Akbar' kama vile wanavyosema takbira ya Swalaah. Kuashiria hivyo ni makosa kwa sababu Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alinyanyua mikono yake tu kuomba du'aa. Hapo unaweza kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), kuomba du'aa yoyote ile upendayo huku umeelekea Ka'bah. Inapendekezeka kusoma dhikr ambayo Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliisoma katika Swafaa na Marwa nayo ni:
لا إِلهَ إلاَّ اللهُ وَحْدَهُ لا شَرِيكَ لَهُ، لَهُ المُلْكُ وَلَهُ الحَمْدُ وهُوَ عَلى كُلِّ شَيءٍ قَديرٌ، لا إِلَهَ إلا اللهُ وَحْدَهُ أَنْجَزَ وَعْدَهُ، وَنَصَرَ عَبْدَهُ وَهَزَمَ الأَحْزَابَ وَحْدَهُ
Laa ilaaha illa-Allaah Wahdahu laa shariyka Laah, Lahul-Mulku Walahul-Hamd wa Huwa 'alaa kulli shay-in Qadiyr. Laa ilaaha illa-Allaah Wahdahu, Anjaza wa'dahu Wanaswara 'Abdahu wahazamal-ahzaaba Wahdahu))
Hapana muabudiwa wa haki ila Allaah, hali ya kuwa Peke Yake, wala Hana mshirika, ni Wake Ufalme na ni Zake Himdi, Naye juu ya kila kitu ni Muweza. Hapana muabudiwa wa haki ila Allaah hali ya kuwa Peke Yake, Ametekeleza ahadi Yake, na Amemnusuru mja Wake, na Amevishinda vikosi Peke Yake.
2-Kuchapuza mwendo katika masafa yote baina ya vilima viwili. Sunnah ni kuchapuza mwendo baina ya milingoti miwili ya kijani na kutembea mwendo wa wakawaida kwengine kote.
Makosa Yanayotendeka Minaa
1-Hujaji kupoteza muda wao katika mahema kwa kupiga soga badala kumdhukuru Allaah au badala ya kuelimishana hapo mambo ya Dini na hasa yanayohusu utekelezaji sahihi wa ‘ibaadah hii ya fardhi. Hujaji wengi kabisa wanafika huko kutekeleza fardhi hii wakiwa hawana elimu ya kutosha ya jinsi ya kuitekeleza ‘ibaadah hii. Kwa hiyo kuelimishana ni jambo litakaloleta faida kubwa badala ya kupoteza muda kwa mambo yasiyofaa.
Wengine wanafanya mambo ya bid-ah kama kusoma uradi kwa pamoja, na kusoma adhkaar zisizokuwa zenye dalili kutoka katika mafunzo ya Sunnah.
Makosa Katika Kisimamo Cha ‘Arafah
1-Baadhi ya Hujaji wanapiga kambi nje ya maeneno ya 'Arafah na kubakia hapo hadi jua kuzama, kisha wanaelekea Muzdalifah bila ya kusimama 'Arafah kama inavyopasa. Hili ni kosa kubwa ambalo linabatilisha Hijja yao kwani kusimama 'Arafah ni kilele cha Hajj na pia ni fardhi kubakia ndani ya eneo la 'Arafah na si nje ya eneo lake.
2-Kuondoka 'Arafah kabla ya jua kuzama hairuhusiwi kwa sababu Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alibakia 'Arafah hadi jua kuzama kabisa.
3-Kujilazimisha katika zahma ya watu kupanda mlima wa 'Arafah hairuhusiwi, kwa sababu inasababisha madhara na madhara kwa Hujaji wengine. Eneo lote la 'Arafah linahesabiwa kuwa ni kisimamo cha 'Arafah, na si kupanda mlima wa 'Arafah wala kuswali katika huo mlima au karibu yake kuwa ndio idhaniwe kuwa mtu amepata kisimamo cha 'Arafah.
4-Kuomba du'aa akiwa anaelelekea mlima wa 'Arafah ni makosa kwa sababu Sunnah ni kuelekea Qiblah wakati wa kuomba du'aa.
5-Kulundika chungu ya mchanga au vijiwe siku ya 'Arafah katika sehemu fulani, jambo ambao haliko katika Shariy’ah ya Allah.
Makosa Katika Eneo La Muzdalifah
1-Baadhi ya Hujaji wanapofika tu Muzdalifah na kabla ya kuswali Swalaah za Magharibi na 'Ishaa huanza kukusanya vijiwe vya kurusha katika nguzo za huko Minaa.
Mawe hukusanywa popote katika maeneo ya al-Haram Inajulikana kwamba Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuamrisha mawe ya Jamaratul-'Aqabah yaokotwe Muzdalifah. Maswahaba walimuokotea yeye mawe asubuhi baada ya kuondoka Muzdalifah na kuingia Minaa. Aliokotewa mawe yaliyobakia yote kutoka Minaa pia.
2-Baadhi ya Hujaji huyaosha mawe. Sio pendekezo kufanya hivyo wala sio Sunnah.
Makosa Katika Jamarah (kurusha vijiwe)
1-Baadhi ya Hujaji wanadhania kwamba kurusha vijiwee katika nguzo za Jamarah ni kumpiga shaytwaan, hivyo wanarusha vijiwe kwa nguvu na ghadhabu. Kurusha vijiwe imekusudiwa kuwa ni njia ya kumkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), nayo ni ‘ibaadah.
2-Wengine wanarusha mawe makubwa, viatu au mbao. Kufanya hivyo kote ni kuzidisha mambo ya dini ambayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameharamisha. Vile vile ni kusababisha madhara ya Hujaji wengine kwani mtu anaweza kurusha jiwe kubwa kwa mbali likampiga Hujaji aliye mbele yake badala ya kupiga nguzo. Vijiwe vidogo vyenye ukubwa wa harage au kunde au choroko au punje za mahindi ndio bora zaidi kuvitumia.
3- Kusababisha zahma, kusukumana na kugombana na wengine katika maeneo hayo ya nguzo hairuhusiwi. Inavyopasa ni kuwa na upole na kurusha vijiwe bila ya kumjeruhi mtu mwingine.
4-Kurusha vijiwe vyote kwa mara moja ni makosa. ‘Ulamaa wamesema kwamba hii itahesabika kuwa ni kama kurusha kijiwe kimoja. Sharia imetaja kurusha kijiwe kimoja baada ya kimoja na huku Hujaji anasema 'Allahu Akbar' kila kijiwe kimoja kinaporushwa.
5-Kumuwakilisha mtu kurusha vijiwe, kwa sababu tu ya khofu ya zahma au tabu na mashaka, na hali Hujaji mwenyewe anao uwezo wa kufanya mwenyewe ‘ibaadah hii hairuhusiwi. Wagonjwa tu na wale walio dhaifu ndio wanaruhusiwa kumuwakilisha mtu kufanya kitendo hiki.
Makosa Katika Kuzuru Kaburi La Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
1-Kugusa na kusugua mikono katika kuta na nondo za chuma, kufunga nyuzi katika mihimili yake na vitendo vingine vya namna hiyo wakati wa kuzuru kaburi la Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kutegemea kupata baraka. Hivyo ni bid'ah. Baraka zinapatikana kwa kufuata amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na si kufuata mambo ya kuzushwa yasiyo na maana wala manufaa.
2-Kwenda katika mapango ya Mlima wa Uhud au mapango ya mlima wa Hiraa au Thawr karibu na Makkah na kutundika vitambara au kuomba du'aa huko. Haya hayamo katika mafunzo ya kutekeleza fardhi hii. Na yote hayo ni kujitakia mashaka na tabu kwani ni mambo ya bid'ah katika Dini na wala hayana msingi katika Shariy’ah.
3-Vile vile kuzuru sehemu nyingine kwa kudhania kuwa sehemu hizo ni athari za mabakio ya Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Mfano sehemu ambayo ngamia wake alikaa, au kisima cha 'Uthmaan na kukusanya udongo sehemu hizo kwa kutegemea kupata baraka, yote ni mambo ya bid'ah.
4-Kuwaita waliokufa wakati wa kuzuru makaburi ya Al-Baqi'i au makaburi ya mashuhadaa wa Uhud na kurusha sarafu ili kutegemea kupata baraka za sehemu waliozikiwa watu ni makosa makubwa kabisa bali ni shirki kama walivyosema Maulamaa. Ni dhahiri pia katika Qur-aan na Sunnah ya Rasuli Wake (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba aina zote za ‘ibaadah ziwe kwa ajili ya Allaah Pekee. Hairuhusiwi kumuomba mwingine au kuchinja, kuweka nadhiri au aina yoyote ya ‘ibaadah isipokuwa ziwe kwa ajili ya Allah kwani Anasema:
وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ
Na hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Allaah wenye kumtakasia Dini, wenye kujiengua na upotofu kuelemea Dini ya haki [Al-Bayyinah: 5]
Vile vile Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا﴿١٨﴾
Na kwamba Misikiti ni kwa ajili ya Allaah, basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.
[Al-Jinn: 18]
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Awazidishie Waislamu elimu ya Dini, na Atuepushe katika makosa, kuvuka mipaka ya Shariy’ah Yake na kufuata mambo ya bid'ah, hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuitikia du'aa zetu. Aamiyn.
Faharasa |
|
Ihraam |
Hali ya kuingia katika tendo la kufanya ‘ibaadah ya Hajj, au pia nguo za Hajj zinaitwa hivyo. |
Ramal |
Kwenda mwendo wa mbio mbio kwa hatua ndogo ndogo katika mizunguko mitatu ya mwanzo kwenye twawaaf |
Twawaaf |
Mzunguko katika Ka'bah |
Hajarul Aswad |
Jiwe jeusi lilioko pembeni mwa Ka'bah |
Hijr Ismaa'iyl |
Chumba cha Ismaa'iyl |
Twawaaful-Quduwm |
Twawaaf ya kuingia (mwanzo unapowasili) |
Rukn Al-Yaman |
Pembe katika Ka'bah inayoelekea Yemen |
Khushuu |
Unyenyekevu |
Maqaam Ibraahiym |
Jiwe alilokanyaga Nabiy Ibraahiym na kusimama kuomba Du'aa baada ya kujenga Ka'bah |
Masjidul-Haraam |
Msikiti Mtukufu Makkah |
Sa'y |
Kutembea baina ya Swafaa na Marwah |
Al-Haram |
Sehemu Tukufu |
Ram-y |
Kurusha vijiwe |
Jamaratul-'Aqabah |
Mnara ulio karibu na Makkah |
Jamarah |
Kurusha vijiwe katika minara iliyoko Minaa |