34-Fatwa: Inaruhusiwa Kumpa Zakaatul-Fitwr Mama Wakubwa Na Wadogo?

Inaruhusiwa Kumpa Zakaatul-Fitwr Mama Wakubwa Na Wadogo?

 

www.alhidaaya.com

 

 
SWALI:

 

Je, inafaa kutoa Zakaatul-Fitwr kwa mama mkubwa na mama mdogo   ambaye ameachwa, hana watoto wa kiume bali ana watoto wa kike ambao wameolewa na anamiliki 500 mita mraba ya ardhi.  Hana chanzo cha kipato. Je inaruhusiwa kumpa Zakaah hii au wapewe maskini wengine?

 

 

JIBU:

 

Sifa Zote Ni Za Allaah

 

Kwanza:

 

‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu watu wa kuwapa Zakaatul-Fitwr. Rai ya wengi wao ni kwamba wapewe aina nane ya watu ambao wametajwa kupewa (katika Suwrah At-Tawbah Aayah ya 60). Rai ya wengineo ni kwamba wapewe wote waliomo katika aina nane ya watu na wengineo wameona kwamba itolewe kwa masikini na wenye kuhitaji pekee.

 

Inasema katika al-Mawsu’ah al-Fiqhiyyah (23/344): “Mafuqahaa wamekhitilafiana kuhusu nani apewe Zakaatul-Fitwr na kuna rai tatu:

 

1- Rai ya wengi wao ni kwamba inaruhusiwa kuigawa baina ya aina nane ya watu ambao Zakaah ya mali inapasa kuwapa. – Rai ya Maalik.

2- Rai ya Imaam Ahmad ambayo imependekezwa na Ibn Taymiyyah kwamba wapewe masikini na wanaohitaji pekee.

 

3- Rai ya Shaafi'y igaiwe kwa aina nane ya watu au yeyote aliyekuweko. [mwisho wa kunukuu]

 

Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah amekanusha rai ya kwanza na ya tatu katika Majmuw' al-Fataawa (25/73-78). Ameelezea kwamba Zakaatul-Fitwr inategemea idadi ya watu, sio mali. Baadhi ya aliyoyataja ni yafuatayo:

 

"Hivyo Allaah Ameamrisha itolewe kwa mfumo wa chakula kama Alivyoamrisha kafara iwe pia katika mfumo wa chakula.

 

Kutokana na rai hii, haipasi kuitoa Zakaatul-Fitwr ila wale wanostahiki kupokea chakula kama ni kafara. Nao ni wale wanaopokea kwa sababu wanakihitaji. Hivyo isitolewe kwa wale wa kutiwa nguvu nyoyo zao, au watumwa n.k. Hii ni rai iliyo na nguvu kabisa, kutokana na dalili.

 

Rai dhaifu kabisa ni ile wanaosema kwamba ni fardhi kwa kila Muislamu kutoa Zakaatul-Fitwr kwa (watu) kumi na mbili, au kumi na nane, au ishirini na nne, au ishirini na nane, au thelathini na mbili n.k. kwa sababu hii ni kinyume na desturi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Makhalifa Waliongoka na Maswahaba wote.

 

Hakuna Muislamu aliyefanya hivi zama hizo bali Muislamu alijitolea Zakaatul-Fitwr na Zakaatul-Fitwr ya familia yake kwa Muislam mmoja. Walipomuona mtu anagawana swaa’ baina ya watu wakigawana kitanga cha mkono, walikataza kwa nguvu na ilionekana kama ni bid'ah na kitendo kisichokubaliwa. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kwamba kuamrishwa kwa swaa’ ya tende, au swaa’ ya shayiri, au nusu swaa’ au swaa’ ya ngano imepimwa kuwa inamtosheleza maskini mmoja. Pia ameelezea kwamba iwe katika mfumo wa chakula wapewe siku ya 'Iyd ili wawe wenye kujitegemea. Ikiwa mtu maskini atachukua kitanga cha chakula haitamnufaisha na haitamtosheleza. Hali kadhalika ni hali ya mwenye deni na msafiri. Wakichukua kitanga cha mkono cha ngano haitawatosheleza. Uislamu umezingatia kitendo hiki ambacho hakuna mtu mwenye busara angelikubali na ambacho hakuna Salaf au Maimaam wa Ummah walifanya" 

Juu ya hivyo, maneno ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Kama ni chakula cha masikini)) inaonyesha kwamba hii ni haki ya maskini kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Aayah za Dhwihaar (kafara ya Dhwihaar):

((basi awalishe masikini sitini)) [Al-Mujaadilah: 58:4]

 

Hivyo ikiwa hairuhusiwi kuitoa kuwapa hao aina nane ya watu basi inahusu hapa pia" [mwisho wa kunukuu]

 

Kutokana na  hii, rai iliyo sahihi kabisa miongoni mwa hizo rai tatu ni ya pili ambayo Zakaatul-Fitwr itolewe kwa masikini na wenye kuhitaji na sio mtu mwingine. Hivyo ndivyo iliyochukuliwa kuwa ni rai iliyo sahihi kabisa na Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) kama inavyosema katika ash-Sharh al-Mumtii' (6/17)

Pili:

 

Ikiwa Zakaatul-Fitwr na Zakaah ya mali watapewa jamaa ambao wanastahiki, ni bora zaidi kuliko kuwapa wengineo wanaostahiki kwa sababu katika hali hii Zakaah zote mbili zinaunganisha ukoo. Lakini inategemea na hali ya huyo jamaa kama anastahiki kupewa (yaani kama ni maskini na mwenye kuhitaji)  

Shaykh Muhammad Swaalih bin 'Uthaymiyn (Rahimahu  Allaah) alipoulizwa kuhusu hukmu ya Zakaatul-Fitwr kupewa jamaa walio masikini.

 

Alijibu:

Inaruhusiwa kutoa Zakaatul-Fitwr na Zakaah ya mali kuwapa jamaa walio masikini. Na hakika kuwapa jamaa ni bora kuliko kuwapa watu wageni kwa sababu kuwapa jamaa huwa ni sadaka na pia kuunga ukoo. Lakini sharti isiwe kwa ajili ya kuhifadhi mali yake ambayo ndivyo itakavyokuwa hali ikiwa jamaa yenyewe aliye maskini ni ambaye mwenye jukumu naye kumhudumia. Kwa hali hiyo hairuhusiwi kumtimizia mtu haja kwa chochote katika Zakaah yake kwa sababu akifanya hivyo atakuwa anahifadhi mali yake kutokana na anachokitoa (kwa maana atakuwa anataoa Zakaah yake kwa kumpa mtu ambaye ni wajibu wake kumhudumia) Nayo haipasi wala kuruhusiwa.

Lakini ikiwa hana majukumu naye basi anaweza kumpa Zakaah bali kutoa Zakaah yake kwa jamaa ni bora kuliko kumpa mtu mgeni kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   amesema: ((Swadaqah zenu kwa jamaa ni swadaqah na pia ni kuunga ukoo)) [mwisho wa kunukuu- Majmuu' Fataawa Shaykh Ibn 'Uthaymiyn (18/Swali Namba 301]

 

Hitimisho:

Ikiwa mama mkubwa na mama mdogo wako ni maskini anastahiki Zakaah, japo kuwa anamiliki mita mraba 500 ya ardhi. Lakini ni bora kwake aiuze ili awe ni mwenye kujitegemea mwenyewe ili asitegemee zawadi kutoka kwa watu.

Waislamu wasiwaache jamaa zao hadi mwezi wa Ramadhwaan unamalizika ndio waanze kuwafikiria na kuwapa swaa’ ya chakula, bali Waislamu wanapaswa daima kuwahudumia maskini na wanaohitaji na kukimbilia kuwapa wanayohitaji ya chakula, pesa na nguo na hivi inapaswa ifanyike zaidi na zaidi ili walio matajiri wawe wanawafikiria na kuwahudumia jamaa zao walio maskini.

 

Na Allaah Anajua zaidi 

 

Share