35-Fatwa: Hakuna Masikini Wanakoishi. Je Watume Zakaatul-Fitwr Nchi Nyingine?
Hakuna Masikini Wanakoishi. Je Watume Zakaatul-Fitwr Nchi Nyingine?
SWALI:
Sisi tunaishi Uingereza na hatujui watu masikini wowote hapa. Tumepata mtu wa kuaminika In Shaa Allaah, ambaye amesema: "Nipeni pesa nitanunua mchele nusu yake na kugawa kwa masikini, na nusu yake nitawapa pesa". Sababu yake ni kwamba tuko zaidi ya watu 500 hivyo itakuwa shida kwake kununua kiasi kikubwa cha chakula na kukibeba. Pia kwa vile masikini pengine wasitake chochote ila pesa kwa sababu wataweza kuzitumia vizuri zaidi kuliko kupata mchele. Je tumpe pesa au tuwakilishe ndugu zetu huko Tanzania ili watutolee?
JIBU:
Rai ya ‘Ulamaa wengi (wakijumuuisha Maalik, ash-Shaafi'y na Ahmad) ni kwamba hairuhusiwi kutoa pesa kwa ajili ya Zakaatul-Fitwr, bali lazima itolewe kama chakula kama ilivyoamrishwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) [Al-Bukhaariy (1504) na Muslim (984) iliyosimuliwa na Ibn 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kwamba: "Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amefaridhisha Zakaatul-Fitwr swaa’ moja ya tende au swaa’ moja ya shayiri (ngano) kwa kila mtu, aliye huru au mtumwa, mwanamume au mwanamke, miongoni mwa Waislamu"
Kutokana na hivyo, ikiwa mtu huyo ni wa kuaminika basi unaweza kumsisitiza kuwa atoe kwa mfumo wa chakula. Ikiwa hatokubali hivyo basi ni bora utoe chochote uwezavyo kwa maskini wa nchi hiyo unayoishi. Kisha hakuna ubaya kutuma zilizizobakia nchi nyingine. Sio lazima utume nchi yako ya asili, bali nchi yoyote ambayo kunahitaji na umasikini ni mkubwa zaidi au kwa jamaa ambao ni masikini pia itakuwa bora.
Katika Swali la:
Inaruhusiwa kuhamisha Zakaatul-Fitwr Kutoka Nchi Kwenda Nchi Nyingine?
Tumesema kwamba hakuna ubaya kutuma Zakaah nchi nyingine ambayo inahitaji kama kutuma nchi ambayo ina jamaa wenye uhusiano wa damu au nchi ambayo inahitaji zaidi.
Shaykh Ibn 'Uthaymiyn aliulizwa: 'Anayeishi nchi za ki-Magharibi anaweza kutoa Zakaatul-Fitwr kwa ajili yake na familia yake ikiwa anajua kuwa wameshajitolea wenyewe?"
Akajibu:
"Zakaatul-Fitwr ambayo ni swaa’ ya chakula kama mchele, ngano, tende au aina yoyote ya chakula, ni kitu ambacho mtu inampasa atoe kwa ajili yake kama kwani ndivyo inavyowajibika kwa sababu Ibn 'Umar (Radhwiya allaahu 'anhumaa) amesema: "Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amefaridhisha Swadaqatul-Fitwr kwa Waislamu, aliye huru na mtumwa, mwanaume na mwanamke, mdogo na mkubwa, na ameamrisha itolewe kabla ya watu kwenda kuswali".
Ikiwa watu wa nyumba wameshajilipia, basi hakuna haja tena mtu ambaye yuko mbali na familia yake kuwatolea. Bali ajitolee mwenyewe pekee huko anakoishi na ikiwa wako Waislamu ambao wanastahiki kupewa Zakaah hii. Ikiwa hakuna wanaostahiki basi awakilishe familia yake imtolee katika nchi yake ya asili" [Mwisho wa kunukuu - Majmuw' Fataawa Ibn 'Uthaymiyn 18/ Swali Namba 771]
Aliulizwa pia kuhusu: Kutuma Zakaatul-Fitwr nchi za mbali kwa sababu ya kuweko huko maskini wengi?
Alijibu:
"Hakuna ubaya kutuma Zakaatul-Fitwr nchi nyingine kwa sababu ikiwa hakuna maskini nchi ya anayetoa. Lakini ikiwa itafanywa hivyo na hali nchi yake wako masikini basi hairuhusiwi" [mwisho wa kunukuu Fataawa Ibn 'Uthaymiyn 18/ Swali Namba 102]
Inafuatia pia Fatwa ya Al-Lajnah Ad-Daaimah –
Kiwango cha Zakaatul-Fitwr ni swaa’ moja ya tende, shayiri, zabibu, mtindi mkavu au chakula chochote na itolewe usiku kabla ya 'Iyd hadi kabla ya Swalaah ya 'Iyd. Inaruhusiwa pia kuitoa siku mbili au tatu mapema. Itolewe kwa maskini wa nchi ambayo inakotolewa. Lakini inaruhusiwa kuipeleka kwa maskini wa nchi ambayo mahitaji yake ni makubwa. Inaruhusiwa Imaam wa msikiti na watu wanaoaminika kukusanya na kuigawa kwa maskini madamu tu watahakikisha itawafikia kabla ya Swalaah ya 'Iyd. Haiungani na mfumuko (thamani) bali kiasi kimewekwa katika sheria kama ni swaa’ moja. Asiyekuwa na chochote isipokuwa chakula tu cha kula siku ya 'Iyd pamoja na walio chini ya jukumu lake, hawajibiki kutoa Zakaatul-Fitwr. Hairuhusiwi kuitumia kwa kujengea misikiti au miradi yoyote mingine. [Fataawa Al-Lajnah ad-Daaimah 9/369, 370]
Imeshanukuliwa kwamba Zakaatul-Fitwr ni fardhi na kiwango cha kutoa na kwamba hairuhusiwi kutoa kwa pesa, na kwamba inaruhusiwa kuituma katika nchi ambazo mahitaji yake ni makubwa zaidi.
Na Allaah Anajua zaidi