Kusoma Du'aa Ya Qunuwt Katika Swalah Ya Alfajiri Ni Sunnah?
Kusoma Du'aa Ya Qunuwt Katika Swalaah Ya Alfajiri Ni Sunnah?
SWALI
Assalam alaikum,
Mimi swali langu ni kuhusu du’aa qunut katika sala ya fajr ktk rakaa ya pili. Jee dua hii ni sunnah au fardh? Ahsante.
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Qunuwt kwa maelezo ya Fuqahaa (‘Ulamaa wa Fiqh), ni du'aa inayosomwa katika Swalaah katika sehemu maalum wakati mtu anapokuwa amesimama baada ya kurukuu (au kabla kwenye kauli nyingine). Na inatumika katika Swalaah ya Witr kwenye raka'ah ya mwisho baada ya kurukuu kwa kauli yenye nguvu.
Qunuwt ni du'aa itumikayo wakati wa matatizo, majanga na maafa yanapowafika Waislam. Na wakati huo ndipo du'aa hii huombwa na huwa inaombwa katika kila Swalaah na si Swalaah ya Alfajiri tu kama ilivyozoeleka na baadhi ya watu kwa kutumia baadhi ya Hadiyth ambazo hazijasihi kuhusiana na Qunuwt ya kudumu (katika Swalaah ya Alfajiri).
Du'aa hii si fardhi bali ni Mustahabb (inapendekezwa) na Swalaah ya mtu ni sahihi kabisa hata kama hajasoma Qunuwt, na wala usiposoma Qunuwt huhitaji kufanya Sajdatus-sahw (sijidah za kusahau) kama wanavyodhani wengine. Inapendezwa kufanywa wakati ikifikia dharura kama tulivyotaja juu.
Ni kinyume na Sunnah kuisoma Qunuwt kwenye Swalaah za asubuhi na kudumu nayo kama inavyofanywa na baadhi ya Imaam kwani hilo halijathibiti katika Hadiyth Swahiyh kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisoma du'aa hiyo wakati Maswahaba zake sabini wajuzi wa Qur-aan walipouliwa kwenye sehemu iitwayo Bi-ir Ma'uwnah na Makabila ya Bani Sulaym ya Ra'iyl, Dhakwaan, Ussayah wakati alipowatuma kwenda kuwafundisha Dini yao. Aliisoma du'aa ya Qunuwt kwa muda wa mwezi mzima dhidi ya hao Wauaji. [Hadiyth ya Anas iliyopo kwenye Al-Bukhaariy na Muslim].
Pia kwenye Hadiyth nyingine iliyopokelewa na Abuu Hurayrah, inaonyesha kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahi kuwaombea baadhi ya Maswahaba waliokuwa wamepotea kwa maadui, na aliomba kiasi cha mwezi kisha akaacha, na Abuu Hurayrah alipomuuliza Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwanini ameacha kuwaombea, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu: ((Je,huoni kuwa washarejea?)) [Al-Bukhaariy na Muslim].
Hivyo, inaonyesha kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisoma Qunuwt hiyo ambayo inaitwa Qunuwt An-Nawaazil kwa muda ambao yale aliyokuwa akiyaomba, yamejibiwa ndipo akaacha.
Vilevile imethibiti kuwa alikuwa akiwaombea wale waliokuwa dhaifu, wananyanyaswa na maadui na kuwa chini ya wavamizi.
Imepokewa pia kuwa Abuu Maalik Al-Ash'ariyy alisema: "Nilimuuliza baba yangu, 'Ee baba yangu, uliswali nyuma ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na nyuma ya Abuu Bakr, 'Umar, 'Uthmaan na 'Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhum ajma'iyn). Je, walikuwa wakisoma Qunuwt katika Swalaah ya Alfajiri?' Akajibu, Ee mwanangu, hili ni jambo jipya lililozushwa,'" [Imesimuliwa na wapokezi wote (watano) isipokuwa Abu Daawuwd].
Hakika muongozo mzuri na bora ni ule wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Na Qunuwt inaposomwa, basi ni vizuri kusoma kwa ile shida inayoombewa kwa wakati huo; kama ni njaa au udhaifu au manyanyaso n.k., iombwe kutokana na masuala hayo.
Na endapo utaswali nyuma ya Imaam anayesoma Qunuwt katika Swalaah ya Alfajiri, basi unatakiwa umfuate na Swalaah yako ni sahihi, kwani kumfuata Imaam ni wajibu, na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Imaam amechaguliwa ili afuatwe" na akasema: "Msitofautiane na Maimaam wenu)).
na pia katika Swahiyh Al-Bukhaariy amesema:
"Wanawaongoza katika Swalaah; ikiwa wamepatia, (ujira) ni wenu na wao, na wakikosea, (ujira) ni wenu na (dhambi) ni zao."
‘Ulamaa wengi wakubwa kuanzia Al-Lajnah Ad-Daaimah, Imaam Ibn Baaz, Imaam Ibn 'Uthaymiyn, Imaam Al-Albaaniy (Rahimahumu-Allaah) na wengine wanaonelea kuswali nyuma ya mwenye kusoma Qunuwt na kumuitikia. Baadhi ya Wanachuoni wengine wanaonelea kuwa ikiwa umekosa Msikiti wa Ahlus-Sunnah na ikabidi kuswali nyuma ya Imaam anayesoma Qunuwt, basi unaswali nyuma yake lakini usiitikie Aamiyn ya Qunuwt yake wala kunyanyua mikono kwani kunyanyua mikono haijathibiti hapo.
Na Allaah Anajua zaidi