Kusoma Suwrah Katika Rakaa'ah Ya Tatu Na Ya Nne Inajuzu?
Kusoma Suwrah Katika Rakaa Ya Tatu Na Ya Nne Inajuzu?
SWALI:
Asalaam Aleykum
suala langu ni kuuliza wakati mwengine unaposali tuseme unasali salaa ya maghrib rakaa ya kwanza na ya pili unasoma Alhamdu na sura,na rakaa ya tatu unasoma Alhamdu peke yake sasa mara nyengine unasahau unataka kusoma tena sura na ushaanza kusema bismi lahi jee sasa inafaa kusoma sura au undelee kurukuu tu na kuna chochote unasema baada ya salam. Shukran
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kuna ikhtilaaf katika rai za Fuqahaa kuhusu kusoma Suwrah baada ya Raka'ah mbili za mwanzo yaani baada ya kusimama kutoka katika Tashahhud ya mwanzo kama inapendekezeka au la.
Imaam Maalik (Rahimahu-Allaah) ameona kuwa ni makruwh (inachukiza).
Ama Imaam Ash-Shaafi'iy (Rahimahu-Allaah) ameona kuwa ni mustahabb (inapendekezeka) katika rai yake ya mwisho, na sio rai yake ya mwanzo.
Na rai ya Imaam Shaafi'iy ya mwisho inaonekana sahihi zaidi na kutiliwa nguvu na Hadiyth na maelezo yatakayofuatia mbele.
Ilivyo kawaida tunavyojua wengi kusoma Suwrah baada ya Suwratul-Faatihah ni katika Raka'ah mbili za mwanzo. Na Katika Raka'a ya tatu au ya nne ni kusoma Suwratul Faatihah pekee kutokana na Hadiyth ifuatayo:
عن أَبِي قَتَادَةَ رضي الله عنه " أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ كَانَ يَقْرَأُ فِي الرَّكْعَتَيْنِ الأُولَيَيْنِ مِنْ الظُّهْرِ وَالْعَصْرِ بِفَاتِحَةِ الْكِتَابِ وَسُورَةٍ وَيُسْمِعُنَا الآيَةَ أَحْيَانًا وَيَقْرَأُ فِي الرَّكْعَتَيْنِ الأُخْرَيَيْنِ بِفَاتِحَةِ الْكِتَابِ " مسلم
Imetoka kwa Abuu Qataadah (رضي الله عنه) kwamba "Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisoma Suwrah ya kufungulia Kitaab (Suwratul-Faatihah) katika Raka'ah mbili za mwanzo kwenye Swalaah ya Adhuhuri na Alasiri na wakati mwingine akitusikilizisha Aayah mbili za mwisho alikuwa akisoma Suwratul-Faatihah" (pekee) [Muslim]
Hivi ndivyo msimamo wa asili. Lakini inaruhusiwa kusoma Suwrah au Aayah baada ya Suwratul-Faatihah katika Raka'ah mbili za mwisho wakati mwingine, kutokana na Hadiyth ifuatayo:
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ رضي الله عنه "َنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ كَانَ يَقْرَأُ فِي صَلَاةِ الظُّهْرِ فِي الرَّكْعَتَيْنِ الأُولَيَيْنِ فِي كُلِّ رَكْعَةٍ قَدْرَ ثَلاثِينَ آيَةً وَفِي الأُخْرَيَيْنِ قَدْرَ خَمْسَ عَشْرَةَ آيَةً أَوْ قَالَ نِصْفَ ذَلِكَ وَفِي الْعَصْرِ فِي الرَّكْعَتَيْنِ الأُولَيَيْنِ فِي كُلِّ رَكْعَةٍ قَدْرَ قِرَاءَةِ خَمْسَ عَشْرَةَ آيَةً وَفِي الأُخْرَيَيْنِ قَدْرَ نِصْفِ ذَلِكَ" مسلم
Imetoka kwa Abuu Sa'iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisoma katika Raka'ah mbili za mwanzo kwenye Swalaah ya Adhuhuri Aayah thelathini takriban katika kila Raka'ah, na katika Raka'ah mbili za mwisho Aayah kumi na tano takriban, au kasema nusu yake. Katika Raka'ah mbili za mwanzo za Swalaah ya Alasiri alikuwa akisoma katika Raka'ah takriban Aayah kumi na tano, na Raka'ah mbili za mwisho karibu nusu yake" [Muslim]
Shaykh Al-Albaaniy (Rahimahu-Allaah) amesema: "Hadiyth hii inaonyesha kwamba kusoma zaidi ya Suwratul-Faatihah katika Raka'ah mbili za mwisho ni Sunnah na ni rai ya Maswahaba wengi pamoja na Abuu Bakar As-Swiddiyq (رضي الله عنه) . Hii ni rai ya Imaam Ash-Shaafi'iy ikiwa ni katika Swalaah ya Adhuhuri au Swalaah yoyote nyingine. Na miongoni mwa ‘Ulamaa wa karibuni ni rai ya Abul-Hasanaat Al-Laknawi" [Swifatus-Swalaah]
Na hiyo ni aidha akiwa mtu anaswali pekee yake au katika Swalaah ya Jamaa.
Imaam ibn 'Uthaymiyn aliulizwa akasema: "Ikiwa mwenye kuswali amemaliza kusoma Suwratul-Faatiha na Suwrah nyingine katika Swalaah ambazo Qur-aan inasomwa kimya kimya, na Imaam bado hakurukuu, je, anyamaze kimya?"
Akajibu: "Mwenye kuswali asinyamaze kimya anapomaliza kusoma Al-Faatihah na Suwrah nyingine kabla ya Imaam kurukuu, bali aendelee kusoma hadi atakaporukuu Imaam.
Kwa hiyo ikiwa katika Raka'ah mbili baada ya Tashahhud na amemaliza kusoma Suwratul-Faatihah lakini Imaam hakurukuu, basi asome Suwrah nyingine hadi Imaam arukuu, ili kusikuweko ukimya katika Swalaah isipokuwa ikiwa mwenye kuswali anasikiliza kisomo cha Imaam wake" [Majmuw' Fataawa ibn 'Uthaymiyn 15/108]
Na Kusoma Suwrah baada ya Suwratul-Faatihah ni miongoni mwa vitendo vya Sunnah katika Swalaah, kwa hiyo hata kama mtu amesahau kusoma Suwrah baada ya Al-Faatihah, ikiwa ni katika Raka'ah mbili za mwanzo au Raka'ah za baada ya Tashahhud ya mwanzo, basi hana haja kurudia kusoma Suwrah na Swalaah yake ni sahihi, atafanya tu Sajdatus-Sahw mbili (Sajda ya kusahau) kabla ya kutoa salaam.
Kwani katika Swalaah kuna vitendo vya Sunnah na fardhi. Anaposahau mtu kutenda vitendo vya fardhi ndipo inapombidi arudie kile kitendo kwani Swalaah haisihi ikipunguka kitendo cha fardhi. Ama anaposahau mwenye kuswali vitendo vya Sunnah, haimpasi kuvirudia na Swalaah yake ni sahihi. Bonyeza kiuongo kifuatacho upate faida:
Nguzo Za Swalaah Na Yaliyo Waajib Katika Swalaah
Na katika hali yako muulizaji, hakuna ubaya kama ungeliendelea kusoma Suwrah katika Raka'ah ya tatu, na hata kama umeacha hali kadhalika hakuna ubaya na Swalaah yako sahihi.
Ama kuhusu cha kusoma kabla au baada ya salaam imethibitika katika Sunnah kuwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisoma du'aa mbali mbali na zote utazipata katika viungo vifuatavyo:
024-Hiswnul-Muslim: Du’aa Baada Ya Tashahhud Kabla Ya Salaam
025-Hiswnul-Muslim: Nyiradi Baada Ya Kutoa Salaam Ya Kumaliza Swalaah
Na Allah Anajua zaidi.