Nimechelewa Swalaah Vipi Nitajiunga? (Swalatul-Masbuwq)
SWALI:
Tujaalie nimechelewa msikitini na jamaa ishaanza na imamu yupo katika rukuu-je vipi nitaweza kujiunga na jamaa ile? Natakiwa nisubiri mpaka waishe rakaa ile au nami nijiunge katika rukuu kutakua hakuna mashaka ki-sheria?
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ahli zake, Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hili ni suala ambalo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe ametuelimisha ili tusiwe na matatizo wala utata aina yoyote. Nayo inaitwa 'Swalaatul-Masbuuq' (Swalah ya aliyepitwa) ambayo ni
Muislamu anapokuja na akamkuta Imaam yuko katika Rukuu basi huwa amepata Rak‘ah hiyo. Hii ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema, amesema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Mnapokuja katika Swalah na sisi tuko katika sijdah, nanyi pia nendeni katika sijdah lakini msiihesabu Yaani kuwa mmepata hiyo Rak‘ah) na yeyote atakayepata rukuu hakika amepata Swalah (yaani rak‘ah hiyo)” (Abu Daawuud, Ibn Khuzaymah na al-Haakim, naye akasema ni Sahihi).
Kwa hivyo, unapomkuta Imaam popote inafaa umuunge lakini itahesabiwa umeipata Rak‘ah ikiwa utamkuta Imamu yuko katika rukuu au ikiwa yuko katika kusimama kabla ya kurukuu.
Muhimu kuleta Takbira ya kufungulia Swalah kabla ya kumuunga Imaam, kwani Takbira hiyo ni kitendo cha fardhi katika Swalah ambacho kinapokosekana Swalah huwa haikukamilika.
Kulipiza Rakaa ulizozikosa kama ni moja au mbili au tatu, itabidi anapotoa salamu Imaam, unyanyuke na kuziswali Rakaa ulizozikosa ili upate kukamilisha Swalah yako.
Na Allah Anajua Zaidi