Kuanzisha Swalaah Ya Jamaa'ah Nyingine Ikiwa Swalaah Ya Jamaa'ah Imeshamalizika Inafaa?

SWALI: 

Tujaalie nimechelewa Swalah nikaona watu washamaliza kuswali, lakini wakakuwepo watu wengine nyuma bado wanaendelea kuswali kwa vile hawajawahi mwanzo-Je natakiwa nimchukuwe mmoja kati ya wale watu wa nyuma ama kwa kumgusa au kwa njia nyengine, ili apate kuwa kama imamu kwa wakati ule Au natakiwa nianze jamaa nyengine upya mimi na wenzangu tulokosa, ambayo haito mshirikisha hata mtu mmoja kati ya wale waliowahi jamaa kubwa?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ahli zake, Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Ikiwa umechelewa ukafika wakati ambapo jamaa ishamalizika, hapa kuna kauli mbili zenye nguvu zote: 

   1- Inafaa muanze jama'ah yenu pamoja na wale waliochelewa kama wewe. Na ikiwa uko peke yako basi unaweza kumuomba mtu ambaye tayari ameshaswali ili akupatie jama'ah. Hii ni kwa mujibu wa Hadithi kutoka kwa Abi Sa‘iyd Al-Khudriy (Radhiya Allahu ‘anhu) kuwa amesema "Alikuja mtu katika Msikiti wakati ambapo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa tayari ashamaliza kuwaswalisha Maswahaba zake. Akasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):  "Nani atatoa sadaka kwa huyu kwa kuswali pamoja naye?” Akasimama mtu katika kaumu na kuswali pamoja naye." [Ahmad, Abu Dawuwd na at-Tirmidhiy].

2- Kauli ya pili, na ambayo ina nguvu zaidi (wa Allaahu A'alam) ni kuwa HAIPENDEZI kuunga jamaa nyingine kwenye msikiti ambao ushaswaliwa jamaa. Na haswa kama msikiti huo una Imaam wake aliyechaguliwa. Maulamaa wanaounga mkono msimamo huu ni wengi pamoja na Maswahaba, nao ni; Imaam Maalik, Imaam Ash-Shaafi’iy, Imaam Abu Haniyfah pamoja na wafuasi wake kina Abu Yuusuf na Muhammad bin Al  Hasan, na Maulamaa wengine kama kina Al Qaasim, Yahya bin Sa’iyd na Saalim bin ‘AbdiLlaah na Abu Qalaabah na ‘Abdur-Razaaq Asw Swan’aaniy na Ibn ‘Awn na Ayuub As Sakhtiyaaniy na Al Hasan Al Baswry, na ‘Alqamah na Al Aswad na An Nakha’iy na .Sufyaan Ath-Thawry, Allayth, Al-Awza’iy, Az-Zuhry, ‘Uthmaan Al-Baty, Rabiy’ah, na pia Swahaba ‘Abdullaah bin Mas’uud kwa dalili mbalimbali, kama:

     Dalili ya kwanza: Ni ayah ya 107 ya Surat At Tawbah, na katika ayah hiyo ni pale pasemapo (Na kuwafarakanisha Waumini), hapo ni kuwa Jama’ah haipaswi kufarikishwa na kuwa waumini wanapaswa kuungana kalimah yao, na hakuwezi kupatikana hilo ila kwa kuwa na Jama’ah moja ambayo ni ile Jama’ah ya mwanzo, pamoja na Imaam rasmi (aliyepangwa) wa msikiti huo.

    Dalili ya pili: Hadiyth ya Abu Bakrah (Radhiya Allahu ‘anhu) iliyosimuliwa na At Twabaraaniy na pia Ibn ‘Adiy na Shaykh Al Albaaniy kasema ni sahihi: Kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Alirejea kutoka nje ya maeneo ya Madiynah, akakuta watu washaswali, akaelekea nyumbani kwake na kuwakusanya Ahli zake na kuwaswalisha.

    Na dalili hapa ni kuwa, ikiwa jama’ah ya pili inajuzu na si karaha, basi Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) asingeacha kuiswali pale msikitini na kuacha fadhila hizo za kuswali msikitini.

     Dalili ya tatu: Hadiyth ya Abu Hurayrah iliyosimuliwa na Al Bukhaariy, Muslim, Maalik, At Tirmidhy na An Nasaaiy kuhusiana na kuchoma nyumba za wale wasiohudhuria Swalah (ya Jama’ah)!

   Hapa hoja ni kuwa, kama ingekuwa jama’ah nyingine inaruhusiwa msikitini, basi kusingekuwa na sababu ya kuchomwa. Lakini makusudio ni kuswaliwe jama’ah maadam wanasikia wito, na hiyo ni ile jama’ah ya kwanza ambayo ndiyo thaabit.  Na pia kama jama’ah ya pili ingekuwa inafaa, basi Mtume asingesema (Layash-haduuna As-Swalaah) bali angesema Swalaah, bila 'alif' na 'laam' kwa maana ya Swalah yoyote ile; iwe jama’ah ya kwanza au ya pili.

    Dalili ya nne: Ni kauli ya Imaam Ash Shaafi’iy: Kukiwa na msikiti una Imaam wake aliyechaguliwa, na ikampita mtu au watu Swalah, basi waswali mmoja mmoja, sipendelei waswali Jama’ah, na ikiwa wataswali Jama’ah, basi inajuzu ila sipendelei wafanye hivyo kwa sababu hawakufanya hivyo wema waliotangulia kabla yetu, bali hata wengine walichukia kufanywa hivyo

    Kisha akaendelea na kusema kuwa hivyo ndivyo tulivyohifadhi kwamba watu walikosa jama’ah pamoja na Mtume na wakaswali pekee na hali walikuwa wana uwezo wa kuswali jama’ah, na kuacha kwao ni kwa kukhofia kupatikana jama’ah nyingine katika msikiti mmoja. Na hayo Imaam Shaafi’iy pia aliyaeleza akikusudia tukio la Ibn Mas’uud alipokuwa na ‘Alqamah na Al Aswad wanakwenda msikitini wakakutana na watu washaswali. Akarejea nao nyumbani na akawaswalisha mmoja akiwa kulia kwake na mwingine kushoto kwake. Hii imesimuliwa na ‘Abdur-Razaaq na Atw Twabaraaniy.

     Pia kuna masimulizi ya Hasan Al Baswry pia kuhusu kuwa wakati wa Mtume watu walikuwa wakikosa jama’ah msikitini basi huswali pekee.  

 Na hoja nyingine ni kuwa, kukiwa na jama'ah zaidi ya ile ya Imaam aliyechaguliwa wa kudumu pale msikitini, basi kutapatikana makundi mbalimbali katika msikiti mmoja na kila kundi na Imaam wake. Na wale wenye kutosikia raha na Imaam wa msikiti kwa sababu mbalimbali kama, kurefusha Swalah n.k. watakuwa wanajichelewesha makusudi hiyo jama'ah ya kwanza ili waje kuswali jama'ah yao na Imaam wampendaye! Pia itasababisha watu kuzembea jama'ah iliyopangwa na msikiti kwa sababu wanajua watapata au kukuta jama'ah zingine na kujiunga nazo.

Ni bora ndugu yetu ujitahidi kuwahi jama'ah ya kwanza msikitini na kujiepusha na jama'ah zingine katika msikiti huo mmoja.

Ila hili halihusiani na misikiti isiyo na Imaam wa kudumu, au kiwanjani, au sehemu za kazi na majiani kwenye vibanda vilivyotengwa kuswaliwa. 

Na mas-ala ya kumgusa mtu bega kumjulisha kuwa uko nyuma yake unamfuata, ni masuala yasiyofaa na yanaharibu pia khushuu ya yule aliyeguswa na pia kusababisha tashwishi. Ikiwa umekuja na umemuona mtu ambaye ndio anaswali basi utakwenda upande wake wa kuume karibu naye na hiyo inatosha kuwa ni ishara kuwa unamfuata yeye.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share