001-Swahiyh Twibbin-Nabawiy: Ufafanuzi

 

Swahiyh Twibbin-Nabawiy

 

001-Ufafanuzi

 

 

Kitabu cha “Atw-twib An-Nabawiy” ni baadhi ya sura zinazotokana na kitabu: ‘Zaad Al-Ma’ad Fiy Hady Khayril–‘Ibaad.’ cha Al-Imaam Al-Rabbaaniy Shaykh Al-Islaam Ath-Thaaniy Abi Abdillaah  Muhammad bin Abiy Bakr bin Ayyuwb bin Sa’ad Az-Zar’iyy aliyefariki mwaka (751 A.H. = 1350 AD).

 

 

Na mtu wa kwanza aliyechapa kitabu hiki ni Shaykh wa ma-Shaykh zetu[1] Al-‘Allaamah Muhammad Raaghib Atw-Twabaakh (Rahimahu Allaah), mwanazuoni wa Hadiyth na Taariykh wa mji Mtukufu wa Halab (Alepo) amefariki mwaka (1370 AH=1950 AD).

 

 

Katika aliyoyasema katika utangulizi wake: “Katika utafiti wangu kuhusu mabaki ya maandiko yenye thamani kubwa katika maktaba za mji wa Halab nimepata katika maktaba ya shule ya Al-Halawiyah kitabu cha zamani sana kimeandikwa tangu karne ya nane au ya tisa, kimeandikwa jina, ‘Kitaab Atw-Twibb An-Nabawiy’ cha Shaykh Al-Imaam Al-‘Aalim Al-‘Allaamah Abuu Abdillaah Muhammad bin Abiy Bakr bin Ayuwb maarufu kwa jina la: Ibn Qayyim Al-Jawziyyah ambaye amefariki mwaka mia saba na hamsini na moja (751).

 

 

Nilipofungua kitabu; nikakumbuka kuwa sura zake amezitaja mtunzi wa kitabu ndani ya kitabu chake: ‘Zaad Al-Ma’aad fiy Hadyi Khayril-‘Ibaad’ kilichochapwa nchini Misri mwaka 1324 AH katika vitabu viwili vikubwa.  Nilipolinganisha kati ya maandiko mawili sikuona tofauti katika juzuu ya pili nimekuta ndiyo yenyewe kabisa bila ziada au upungufu. Ikadhihirika wazi kuwa, baadhi ya watu walitoa sura hizo kwenye kitabu hiki na kuziweka kwenye kitabu pekee, kwani hakuna maelezo ya kitabu hicho katika wasifu wa mtunzi, kadhalika hakumtaja mtunzi wa kitabu ‘Kashf Adhwunuwn’. Katika maelezo yake juu ya elimu ya Tiba ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

   

Vitabu vya ki-Tiba vya Ibn Al-Qayyim ni:-

 

 

1. “Sharh Al-Arba’iyn Atw-Twibiyyah Al-Mustakhrajah min Sunan Ibn Maajah” cha Abdul-Latwiyf Al-Baghdady.

 

 

2. “Al-Ahkhaam An-Nabawiyyah fiy Asw-Swinaa’at Atw-Twibiyya” cha Al-Kahhaal Ibn Twarkhaan.

 

Imaam Ibn Al-Qayyim Al-Jawziyyah (Rahimahu Allaah) hakuvielezea hivyo ila haijifichi kwa mtu atakayechunguza kwa makini na kufanya malinganisho.

 

 

Kitabu cha Tiba “Atw-Twibb” kina pambanuka kwa yafuatayo:-

 

a. Kina maudhui zinazofanana, na wakati kwengine zinatofautiana.

 

b. Kuachwa yasiyohusiana na Tiba ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

c. Kuachwa kwa makusudi njia za kutibu zisizogongana na ‘Aqiydah ya Tawhiyd kwa mtazamo wa Salaf As-Swaalih.

 

d. Kitabu kinasifika na uslubu wa uandishi wenye kuvutia.

 

e. Tafiti nyingi zimeongezwa ambazo hazikuwemo kwenye kitabu kilichotangulia.

 

 

Kukosolewa Kwa Kitabu Atw-Twibb An-Nabawiy:

 

a. Kwamba Ibn Al-Qayyim (Rahimahu Allaah) hakuonesha rejea zake za ki-elimu na vyanzo vyake vya ki-Tiba, pengine udhuru wake ni kuwa maarifa haya yamezagaa katika vitabu vya Tiba.

 

 

b. Kuwepo kwa Hadiyth dhaifu bali hata mawdhwuw’ah pasina kuelezea daraja zake. Hivyo ameweza kuzitegemea katika Milango ya kitabu na kujengea hukumu mfano: ‘Mlango kuhusu mwongozo wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  katika kutibu Al-Khudraan’  na  ‘Mlango katika mwongozo wake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika kutibu maradhi ya kuungua moto na kuuzima’.

 

 

Nilichofanya katika kitabu:-

 

a. Nimeondosha zile Hadiyth Mawdhwuw’ah na Dhwa’iy  na Milango yote na zile hukumu zilizojengewa kwa msingi wa Hadiyth hizo

 

 

b. Nikiona Hadiyth Swahiyh inaziba nafasi ya Mlango unastahiki kuondolewa, hapo nabakiza Mlango huo kama ulivyo, na kufuta kilicho dhaifu na badala yake naweka kilicho Swahiyh.

 

 

c. Ikiwa taarifa za ki-Tiba hazina uhusiano wa moja kwa moja na Hadiyth Dhwa’iyf, ninaziandika. Kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokea na kukubali yale waliyomsimulia Waarabu kwa ujumla, kama ilivyopokewa kwenye Athar ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa)  iliyotangulia.

 

 

d. Hadiyth zilizothibiti nimezifanyia uchambuzi mwepesi (Takhriyj) nimerejea vitabu vya Imaam Al-Muhaddith Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah), kwani watu wanaokuja baada yake ni wahitaji kwake katika fani hii.

 

 

e. Nimezielezea istilhai mbali mbali za kielimu na kubainisha maana zake.

 

 

f. Nimehusisha mas-ala yake na maarifa ya Tiba ya kisasa. Na kila maelezo ya kitabibu yanayoishia na (ع) ni ya Dr. ‘Aadil Al-Azhariy na kila maelezo yanaoishia na  (ق)basi hayo ni ya Al-Ustaadh Abdul-Ghaniyy Abdil-Khaaliq.

 

 

g.  Nimefanya faharisi zinazomwongoza msomaji kufanya marejeo kwa wepesi.

 

 

h. Nimebainisha umuhimu wa Tiba katika Uislamu na nimewajibu wale waliokosoa ‘Tiba ya Nabiy’ na kuihusisha kuwa katika daraja la Tiba ya ki mwana Aadam inayoweza kusibu na kukosea.

 

 

Hili ndilo ambalo nimeweza kulifanya, Allaah Ndiye Mwenye kufanikisha Naye Ndiye Mwenye kuongoza.

 

 

 

[1]Mwanazuoni mwanahistoria Raaghib At-Twabaakh (Allaah Amrehemu) kukutana na Shaykh wetu Al-Imaam Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu) pindi aliposikia shughuli zake za Da’wah katika Kitaab na Sunnah na kupenda kwake elimu ya Hadiyth (hilo lilikuwa kwa wasita wa Ustaadh Muhammad Al-Mubaarak, hivyo akamhusisha kwa ijaazah yake na yaliyopokelewa kutoka kwake kama ni tuzo kwake na kutambua elimu yake na akafanya utangulizi wa kitabu chake: ‘Al-Anwaar Al-Jaliyyah fiy Mukhtasar Al-Athbaat Al-Halbiya’ ambayo amehitimisha kwa ijaazah ya ma- Shaykh  wake kwake.

 

Share