002-Swahiyh Twibbin-Nabawiy: Mfumo Wa Afya Katika Uislamu Athari Yake Kuhifadhi Nafsi Na Jamii
Swahiyh Twibbin-Nabawiy
002-Mfumo Wa Afya Katika Uislamu Na Athari Yake
Katika Kuhifadhi Nafsi Ya Mwana Aadam Na Jamii
Mafunzo ya kiafya yana kazi kubwa katika kulinda siha ya mtu mmoja mmoja na jamii. Ifuatayo ni baadhi ya mifano kwa ufupi:-
1. Binaadamu ni muungano kwa mwili na roho, na kila moja kina nguzo zake; nguzo za mwili ni chakula, vinywaji, makazi, mavazi, na matamanio ya kimaada ya kihisia.
Uislamu umeshughulikia mahitaji na maumbile kwa kuyaweka vema na kunyoosha ili kulinda siha ya mwili na kutimizia haki zake, katika hayo ni kama ifuatavyo:
a. Uislamu umeamrisha usafi wa mwili ikiwemo kutawadha, kunawa, kuosha au kuoga, kwa sababu nyingi, baadhi ni wajibu na sehemu zingine ni mustahab.
b. Uislamu umehimiza kuosha mikono baada ya kuamka, na kabla ya kuiweka kwenye vyombo.
c. Uislamu umehimiza usafi wa kichwa, nywele na viungo vyote.
d. Uislamu umefundisha usaji wa nyumba na viwanja vyake.
e. Uislamu umehadharisha uchafuzi wa maji, kama maji ya kisima na mito.
f. Uislamuu umefundisha unadhifu wa vyakula na vinywaji kwa kufunika vyombo kwa kutunza visichafuliwe kwa vumbi, nzi, au sumu.
g. Kadhalika Uislamu umekataza kutaabisha mwili kupita kiasi hata katika ‘ibaadah. Kwa mfano Uislamu umekataza kufunga mfululizo siku zote au kusimama usiku kucha kuswali.
h. Uislamu umebainisha tabia za maumbile na kuwahimiza Waislamu kusimamia tabia hizo na kuzifanya kuwa ni ‘ibaadah.
Kwa hiyo ni wazi kuwa:
Uislamu unatimiza nguvu za kiwiliwili na kuleta afya njema kwa mtazamo wa kisasa.
Kwa kuongezea kutilia mkazo Uislamu kwenye afya ya miili, kupendeza kwake na uzuri wake. Kwa sababu hiyo Uislamu umekataza kuhatarisha mwili katika hali za kuudhoofisha na kwa ajili hiyo umeweka shariy’ah za ruhusa za ki-shariy’ah ili mtu aweze kutekeleza wajibu wake wa ki-‘ibaadah katika hali za udhaifu unao tokezea katika mwili – kati ya hali hizo ni:-
a. Msafiri ameruhusiwa kadhalika mgonjwa, mama anayenyonyesha, mjamzito na kikongwe, hao wote wameruhusiwa kula mchana katika mwezi wa Ramadhwaan.
b. Uislamu umemharamishia Swawm mwenye hedhi kwani, Swawm katika hali hiyo inaambatana na kudhoofu kwa mwili na damu ya mwenye hedhi hupungua kwa hali aliyonayo.
c. Kumuwekea vizuizi mtu anayekwenda Hijjah au ‘Umrah ambaye anaweza kupatwa na taabu na kwa ajili hiyo hupewa nafasi ya kuleta fidia, kufunga au kutoa swadaqah au kuchinja.
d. Na katika hali ya kuwa maji yanaweza kumletea madhara mtu katika kiwiliwili cheke Uislamu umehalalisha kutayammam.
2. Kinga ya maradhi na kupambana na majanga:
a. Uislamu umefungamanisha baadhi ya ‘ibaadah na udhuu au kuoga kwa mfano Swalaah haiswihi bila udhuu au kukoga; na hapana shaka kudumu na udhuu kunapelekea kuwa na mwili msafi, hilo linaulinda mwili kutokana na maradhi.
b. Uislamu umeamuru kumtenganisha mgonjwa mwenye maradhi ya kuambukiza ili kuweza kuzuia maradhi hayo kuenea.
c. Uislamu umeelekeza kuweka karantini ya kiafya, ikizuka tauni au magonjwa kama hayo kama kipindupindu au ndui hakuna kutoka wala kuingia kwenye eneo lililowekewa karantini.
d. Uislamu umeamrisha mtu kujitibu kutokana na maradhi.
3. Elimu ya Vyakula.
Uislamu umetilia mkazo mambo ya lishe kwa namna mbalimbali:
a. Kubainisha vyakula haraam. Navyo ni mzoga, damu, nyama ya nguruwe na kila kimojawapo kati ya hivyo vilivyo haramishwa, kuna hekima kubwa ya kitaaluma katika kuviharamisha. Mwenye chembe ya akili hawezi kubisha juu ya hili.
b. Uislamu umeharamisha pombe, chache na nyingi, kwani ina madhara ya kiafya, akili, tabia, na jamii. Pombe ndio mama wa mambo maovu. Kinachofuata baada ya pombe ni madawa yote ya kulevya ambayo yanaondosha akili, mfano wa Bangi, Opium (Afyun), au yanayodhuru mwili, kama sigara.
Mtu akiona maradhi yanayowasumbua watu wa Magharibi, yanayoharibu viwiliwili vyao, maradhi yanayosababishwa na sigara na madawa ya kulevya, hapo atagundua kwa nini Uislamu uliharamisha uraibu huo mbaya.
c. Kubainisha vyakula halali:-
Uislamu haujaharamisha kitu ila kile kilicho na madhara na kwa ajili hiyo Uislamu umeshajiisha kula vyakula vyenye kuleta faida kwenye mwili, na kupinga dini ya matumizi ya mboga mboga peke yake inayokataza kula nyama kama ni ‘ibaadah kwao. Hilo ni kubainisha kuwa kiwiliwili cha mwana Aadam hakiwezi kuishi kwa mboga mboga peke yake; kwani utumbo wa mwana Aadam ni mfupi kuliko utumbo wa wanyama wanaokula majani na nyasi; kwani mwana Aadam hawezi kuchukua kiasi kinachowatosha cha protini kwa njia ya chakula. Uislamu pia umeshajiisha kutumia vyakula vilivyosheheni dawa na vyenye ponyo kama vile asali na maziwa.
d. Uislamu umepangilia chakula kiasi na wakati.
e. Uislamu umefundisha uharamu wa kufuja chakula na kunywa, na kuweka wazi kuwa hakuna chombo kibaya alichokijaza mwana Aadam kuliko kujaza tumbo lake.
f. Uislamu umeweka uhusiano kati ya chakula, vinywaji na hewa, kama ni lazima basi kila sehemu iwe theluthi moja.
g. Uislamu umefaradhisha mfumo wa ajabu wa Swawm kila mwaka mwezi mmoja. Nao ni mwezi wa Ramadhwaan, na kuhimiza mfumo wa kujitolea kufunga kwa hiari siku tatu kila mwezi nazo ni Ayyaamul-Biydhw (Masiku Meupe). Na siku mbili kwa wiki, nazo ni Jumatatu na Alkhamiys. Na hakuna yeyote anayebisha faida za Swawm kiafya ya mwili, akili na nafsi.
4. Uislamu haukuacha kutatua mambo ya kujamiiana, yawe madogo au makubwa isipokuwa utaona Uislamu umeweka mpango thabiti na ufumbuzi makini:
a. Uislamu umetilia mkazo malezi ya kijinsia kwa namna bora kabisa: Uislamu unachambua mahusiano ya mwana Aadam na tendo la kujamiiana, namna mtoto anavyoumbwa katika tumbo la mamake ambapo Qudra ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) inadhihirika.
b. Uislamu umetilia mkazo ndoa na kujenga familia na kupangilia mahusiano yaliyopo kati ya mume na mke, watoto katika mazingira ya kuwa pamoja na kutengana.
c. Uislamu umesherehesha mahusiano ya kiafya yalio salama kati ya wanandoa, mume na mke. Na umebainisha namna ya mmoja kumshibisha kingono mwenzake kwa namna bora ya kulinda mahusiano ya kindoa kati ya mume na mke.
d. Uislamu umeharamisha starehe za haraam, umeharamisha zinaa, ushoga, na kumuendea mke kinyume na maumbile.
e. Uislamu umeamrisha kutahiri, ambako ni kukata govi ambalo linaficha uchafu. Tiba imebainisha kuwa, asilimia kubwa ya maradhi ya saratani ya kichwa cha uume hutokana na kubakia na govi bila kufanya tohara.
f. Uislamu umetilia mkazo usafi wa kijinsia, umeamrisha kuoga janaba, na kustanji baada ya kwenda chooni, na Uislamu umeharamisha kumwingilia mke akiwa kwenye hedhi.
5. Malezi ya kinafsi:
Miongoni mwa matatizo makubwa yanayowasibu watu katika zama hizi ni msongo wa mawazo, tatizo hili ni kubwa zaidi katika nchi zilizoendelea za viwanda, watu wengi huko wanajinyonga na wengi katika wazazi huko wamepatwa na hali ya kuvurugikiwa kwa ghafla, na hivyo kuwapelekea wao kuwauwa watoto na ndugu na familia zao na wengine hukimbilia katika vitulizo, na madawa ya kulaza usingizi, ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kila siku…. na yote haya yanatokana na kile kinachoitwa kuwa ni ‘msongo wa maendeleo’ na miongoni mwa sababu zake ni:
a. Kukosekana misingi ya kiroho na kiitikadi.
b. Kukosekana kwa dhamira ya ndani ya kimaadili.
c. Kupindukia kwa maisha ya kimaada.
d. Kutoweka kwa kuhurumiana, na kusaidiana katika jamii za kiviwanda na kimaada.
Mwenye akili yeyote hawezi kutia shaka kuwa matibabu ya kweli ya maradhi kama hayo ni Uislamu kwa sababu jamii ya Kiislamu ndiyo pekee ambayo hushikamana kwa pamoja katika mambo ya kidunia na akhera. Hivyo ndivyo Dini ifaayo kuweza kumaliza matatizo ya kiustaarabu wa kisasa na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
e. Uislamu unajikita katika msingi ya mapenzi, kusaidiana, usalama na amani, imani na kuhurumiana baina ya viumbe.
f. Uislamu hauna mianya ya ufisadi na msongo wa mawazo, kama ulevi, zinaa, kamari, na mihadarati.
g. Ni jamii inayokataa mtu kukata tama na kuruhusu mtu kujinyonga na kughadhibika.
Kwa mafunzo haya ya Kiislamu yanapotekelezwa vema basi haiwezekani kujitokeza sababu za msongo wa maendeleo ya kisasa ya kimaada.
6. Mtazamo wa Uislamu kuhusu maradhi na wagonjwa.
Kuchukia maradhi ni jambo la kimaumbile, lakini Uislamu umegeuza jambo hilo kuwa ni jambo chanya:
a. Ni mtihani kutoka kwa Allaah lakini moja ya faida yake ni mtu kufutiwa madhambi, kuinua daraja za watu; hivyo basi yatakikana kwa Muumini kupokea maradhi bila kuwa na majonzi wala malalamiko au kuchukia.
b. Uislamu umemtendea mgonjwa na kumpa haki maalumu zaidi ya Waislamu wengine. Hivyo ukafanya kumzuru mgonjwa ni katika haki za Muislamu kumfanyia mgonjwa Muislamu.
c. Kumtakia kupona kwa kumuombea du’aa na kumhimiza kustahamili na kusubiri, ili aweze kuwa imara, na hizi ni hali za kinafsi zinazosaidia kukabiliana na maradhi.
d. Uislamu umemtendea mgonjwa kwa namna ya kipekee, hivyo Uislamu umedondosha na umesamehe baadhi ya faradhi kwa mgonjwa mfano, jihadi, na kumpunguzia zingine; kama, Swalaah, Swawm pale ambapo anapata shida kutekeleza faradhi hizo, na afya yake kuharibika zaidi, na kuchelewa kupona.
e. Uislamu umetoa ruhusa kwa mgonjwa na msamaha katika baadhi ya Shariy’ah kulingana na dharura itakavyo kuwa, ikahalalisha matumizi ya dhahabu katika Tiba mbadala na imeruhusu mwenye ugonjwa wa kuwashwa avae Hariri.
Katika hayo yaliyotangulia inadhihiri kwetu kuwa: Uislamu umetazama siha ya viwiliwili kama hitajio la msingi katika maisha ya watu, hivyo imeiunganisha na mambo ya ‘ibaadah mbali mbali. Hivyo basi Muislamu anatakiwa kutilia mkazo afya yake binafsi, na jamii kwa jumla ili jamii ya Kiislamu ibaki imara, yenye nguvu. Hayo hayawezi kutimia bila ya kupitia mafunzo ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika nyanja za ki-Tiba.
Ikiwa Waislamu hivi sasa, wanapitia hatua ya kuwa nyuma ki-Tiba, basi hivyo inatokana na wao kuwa kwao mbali na mafunzo ya Tiba ya Kiislamu kwani mara ya kwanza walipotekeleza mafunzo ya Tiba ya Kiislamu yaliweza kuleta matunda ya kupatikana kwa jamii yenye afya safi ya kupigiwa mfano. Wakati ambapo miji ya Ulaya Magharibi imetapakaa majalala na kuzalisha vijidudu na kuparaganywa kwa nguruwe.
Dr. Dr. Segrate Hookah amesema kwenye kitabu chake: “Jua la Arabuni lachomoza Ulaya’ kwamba msafiri Al-Tartusy wa Andalusia (Hispania) ameandika katika msafara wake kuelekea Ulaya, akisimulia hali ya wakazi wake huko: “Ndevu zao na nywele zao zimerefuka, hawafui nguo zao, hawakogi isipokuwa mara moja au mara mbili kwa mwaka.”
Zingatia pia kukiri kwa Tabibu wa Kiingereza (Bernard Shaw) katika kitabu chake, ‘Kubabaika kwa tabibu’ anaposema: “Uingereza ilipotawala visiwa vya “Sandisk” vilijitahidi sana katika ukandamizaji na kushawishi watu wa visiwa hivyo na kuwageuza kutoka katika Uislamu na waingie katika Ukristo mpaka Uingereza ikafaulu katika jambo hilo, lakini matokeo yake ilikuwa ni kuenea kwa maradhi hatari, na hilo ni kwa sababu ya wao kuwa mbali na mafunzo ya Dini ya Kiislamu ambayo yanaweka shariy’ah ya kuwa nadhifu katika madogo na makubwa, kiasi cha kufikia kutoa malekezo ya kukata kucha na kusafisha uchafu ndani ya kucha na kufukia uchafu”.