003-Swahiyh Twibbin-Nabawiy: Hoja MbaliMbali Kuhusu Mwongozo Wa Nabiy Katika Mambo Ya Kitiba

Swahiyh Twibbin-Nabawiy

 

003-Hoja MbaliMbali Kuhusu Mwongozo

 

Wa Nabiy Katika Mambo Ya Kitiba

 

 

 

 

‘Ulamaa wametofautiana katika maswala haya kwa kauli mbili:

 

 

Kauli ya kwanza: Wapo wanaosema kuwa maneno ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni hoja ya ki-Shariy’ah kwa waja kama itathibiti.

 

 

 Kauli ya Pili: Wapo wanaoona kuwa maelekezo ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni hoja tu katika upande wa Dini; kama kumwamini Allaah na Majina na Sifa Zake, na kuamini Malaika, Vitabu, Rusuli Wake, na Siku ya Mwisho, na zile Hadiyth zinazofafanua hukumu za halaal na haraam, faradhi na namna ya kuekeleza ‘ibaadah mbali mbali, na miamala mbali mbali na mambo mengine katika jumla ya mambo ya ki-Dini na ki-Shariy’ah.

 

 

Ama mambo ya kidunia; sio lazima kuwa kauli zake zilingane na hakika; kwani hakuna uhusiano wa mambo kama hayo na hadhi ya Unabii. Bali huenda ikatokea pia kukosewa kwa rai kuhusu hayo, kiasi kidogo au kingi, bali anaweza akasibu mtu mwingine asiyekuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) naye akakosea katika mambo kama hayo ya kidunia.

 

 

Na katika madai yao wamesema vile vile: Kuwa kusema hivi hakushushi hadhi au cheo cha Unabii ambacho Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alimkirimu, kwani cheo hicho kipo katika eneo la elimu ya mambo ya ki-Dini.

 

 

Ibn Khalduwn (Rahimahu Allaah) amesema katika kitabu chake kiitwacho ‘Al-Muqaddimah’ (Uk. 493): “Tiba iliyopokelewa katika mambo ya ki-Shariy’ah yapo katika mkabala huu (tiba ya ki-mila au ya kizamani na kutoka kwa mabedui yenye uzoefu mdogo), na hayamo kamwe katika Wahyi bali yalikuwa ni mambo yakifahamika na ada kwa Waarabu. Na imetokea kutajwa hali za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika hali zake ambazo ni tabia na silka na sio kwa sababu kuwa hilo limo kwenye Shariy’ah kulitimiza hivyo. Kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitumwa ila aje kutufundisha mambo ya ki-Shariy’ah na hakuja kwa ajili ya kufundisha tiba au mengine katika mambo ya kawaida. Na yaliyotokea katika habari ya kilimo cha mtende na akasema, “Ninyi ndiyo wajuzi zaidi wa mambo ya dunia yenu”.

 

 

Hivyo haipaswi kuchukulia kwamba tiba iliyonakiliwa kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka Hadiyth zake kuwa ndio Shariy’ah, kwani hakuna ushahidi wa hilo, isipokuwa ikiwa itatumika kwa namna ya kutabaruku na ukweli wa makusudio ya ki-iymaan. Hivyo patatokea manufaa makubwa na sio katika tiba ya hali ya kawaida.”

 

 

Al-Qaadhwiy ‘Iyaadhw amesema katika kitabu chake: “Ash-Shifaa Bita’riyf Huquwqil-Mustwafaa.” (2/183-185):

 

 

Faswl: “Ama hali zake katika mambo ya kidunia; sisi tunayaweka katika namna iliyotangulia, itikadi, kauli, na kitendo; ama kiitikadi ni, mtu anaweza kuwa anayaelewa mambo ya kidunia kwa upande mmoja lakini kikadhihiri kingine tofauti. Au akawa ana shaka ya jambo lenyewe au akadhania tofauti na mambo ya ki-Shariy’ah (kisha akataja Hadiyth ya mtende) na haya ndiyo tuliyothibitisha katika aliyoelezea kwa nafsi yake katika mambo ya kidunia na kudhani kwake katika hali zake na siyo kwa upande wa jitihada zake katika Shariy’ah au Sunnah alizoziweka mambo haya na mengine kama hayo ni katika mambo ya dunia yasio na uhusiano na elimu ya Dini wala itikadi yake au mafundisho yake kama yanajuzu kwa yale tuliyoyataja. Kwa haya hayapunguzi hadhi yake, haya ni mambo ya kimazowea mtu aliyefanya majaribio anayajua na kuweza kutilia hima na kuyashughulikia.”

 

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amejawa na mambo ya elimu za Ar-Rubuwbiyyah (Uola) na amesheheni elimu za Shariy’ah. Akili yake inazingatia maslahi ya ummah ya kidini na ya kidunia, lakini hii ni kwa baadhi ya mambo tu na inajuzu kwa mambo yaliyo nadra ambayo ili uweze kuyafikia ni kufanya ufuatiliaji wa makini katika kulinda dunia na kufanya uzalishaji na kuwekeza, sio katika mengi yanayoruhusu upuuzi wa kughafilika.

 

 

Imepokewa kwa wingi kwa njia ya ‘Tawaatur’ kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika ujuzi wa mambo ya dunia na undani wa maslahi yake ya kidunia na ya kisiasa ya makundi ya watu wake kwa namna ambayo ni muujiza kwa wana Aadam kama ilivyotanabahishwa kwetu kwenye mlango wa miujiza yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye kitabu hiki.”

Wote wanaokuja baada ya kauli hizo mbili huwa wanarudia kitu hicho hicho, na sio nje ya hayo waliyosema.

 

 

Yafuatayo ni majibu ya kauli hizo:

 

 

1. Tiba ya Nabiy inatokana na Wahyi na chimbuko la Unabiy na upevu wa akili, miongoni mwa hoja za mlango huu.

 

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ ﴿٣﴾

Na wala hatamki kwa hawaa.

 

إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ ﴿٤﴾

Hayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa.

 

عَلَّمَهُ شَدِيدُ الْقُوَىٰ ﴿٥﴾

Amemfunza (Jibriyl) mwenye nguvu shadidi. [An-Najm: 3-5]

 

 

Kauli Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ ﴿٣﴾

Na wala hatamki kwa hawaa. [An-Najm: 3]

 

 

Kwa mujibu wa lugha ni kila linalotokea kwenye kinywa cha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) miongoni mwa kauli. Ziwe ni kauli zote zinazohusiana na mambo ya Dini au kidunia, vyote hivyo ni Wahyi kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) hakuna nafasi ya kukosea, au kuteleza kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ ﴿٤﴾

Hayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa. [An-Najm: 4]

 

 

Haya ndio madhhab ya watu wa Hadiyth.  Kwa mfano kwenye Swahiyh Al-Bukhaariy: ‘Baab As-Su’uwtw’, ‘Baab Ayyu Saa’ah Yuhtajam’, ‘Baab Al-Hijamah fis-Safar’, ‘Baab Al-Hijaamah Minash-Shaqiyqah wasw-Swudaa’ah’,   

 

 

Hii yote ni milango ya tiba na katika “As-Sunan” Utakuta sura mahsusi za tiba.

 

 

2. Ijtihaad ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) sio sawa na Ijtihaad ya wengine miongoni mwa Wanazuoni kwa sababu hakiri kufanyike kosa kamwe iwe kosa hilo ni katika mambo ya kidini au kidunia.

 

 

Huenda mtu atasema: Kwa kuwa Sunnah ni Wahy kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) basi inapingana na kusema kuwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni mujtahid, kwa mujibu wa wale wanaosema hivyo.

 

 

Jibu: Mas-ala ya Ijtihaad ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni mas-ala ya kiusuli yenye khilafu ndani yake. Lakini wanazuoni wengi wa elimu ya kiusuli wameshika kauli ya kwamba inajuzu kutokea ijtihaad kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kiakili na ki-Shariy’ah.[1]

 

 

Hapana kinachozuia kutokea hilo isipokuwa kwa uelewa wa watu wasiweze kufahamu haki, wameshindwa kuunganisha taarifa za ki-Shariy’ah zilizo sahihi. Kwani katika mas-ala haya kuna fumbo, wanaweza kulifungua waliozama kupekua katika fani hii nayo ni:

 

 

1. Ijtihaad yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inashika nafasi ya Wahy.

 

 

2. Ijtihaad yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) si sawa na ya mtu mwingine.

 

 

Al-‘Allaamah Ash-Shawkaaniy (Rahimahu Allaah) amesema katika “Irshaad Al-Fuhuwl” (uk 256) akijibu kauli ya waliosema kuwa: “Katika Ijtihaad kuna kusibu na kukosea.” Akajibu (Rahimahu Allaah): “Imekwishajibiwa suala hilo kwamba Ijtihaad yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) haihukumiwi sawa na Ijtihaad na mtu mwingine. Kwa mtu mwingine hayo ni sawa, kwani sio lazima kwake kumfuata.

 

 

Na akasema Al-‘Allaamah i bin Sultwaan Muhammad Al-Qaariy  katika ‘Mirqaat Al-Mafaatiyh Sharh Mishkaat Al-Maswaabiyh’  (1/237). “Kisha aliyesema kuwa (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) (Swala Allahu ‘Alayhi Wasallam) alikuwa mujtahid, Ijtihaad yake inachukua daraja ya Wahy, kwani hakosei, na akikosea husahihishwa na hii hali haipo kwa yeyote asiyekuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Na kabla ya wanazuoni hao wawili Al-Imaam Ash-Shaatwibiy amehakiki mas-ala haya kwa kina na kudhibiti vema akasema (Rahimahu Allaah) katika kitabu ‘Al-Muwafaqaat’ (4/21): “Kwani Hadiyth ima ni Wahyi kutoka Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) au ni Ijtihaad ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inazingatiwa kuwa inatokana na kitabu cha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Sunnah zake. Na katika makadirio yote hayo ya aina mbili ni muhali kuwepo kwa mgongano na kitabu cha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hazungumzi kwa matamanio ya nafsi yake, bali ni Wahyi anaoshushiwa, ikiwa itasemwa kuwa (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anaweza kukosea, basi kosa hilo kamwe hatalikiri, lazima atarejea katika njia yenye kusibu.”

 

 

Kauli yangu (mwandishi) Hii ndio kweli, na sahihi, kwani matukio sahihi yanathibitisha hili na udhibiti huu madhubuti. Jitihada za Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) zilipatikana kama katika mateka wa vita vya Badri na katika kumpuuza kipofu, ‘Amru bn Ummi Makhtuwm (Radhwiya Allaahu 'anhu) na kuwapa ruhusa waliobaki nyumbani wasiende vitani. Basi ni haraka sana Wahy unashuka kumsahihisha na kumuonesha haki na kuwaongoza wafuasi wake.

 

 

Kwa hiyo khilafu kati ya pande mbili hizi ni ya lafudhi tu; kwani matokeo yake ni mamoja kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakiri yaani hadumu katika kufanya kosa, kwani yeye ameridhiwa kutokosea, yaani hatulii na kosa na hapitishi muda katika kosa. Kwa sababu anahifadhiwa na maasi. Hivyo ndivyo inayokuwa mambo ya Sunnah kama alivyosema Ash-Shaatwiby katika “Al-Muwafaqaat” (4/80) kuwa: “Yote aliyoyaeleza Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) yapo kama alivyoeleza, ni kweli tupu. Kauli zake pia zilizoelezwa kuhusu yeye ni za kutegemewa iwe zina msingi wa kiutekelezaji wa Shariy’ah au hapana, kadhalika ikiwa akiweka hukumu ya Shariy’ah, ameamrisha, au kukataza basi huwa kama alivyosema (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni sawa kati ya haya ikiwa ameelezwa na Malaika kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na yaliyopenyezwa moyoni mwake au njozi alizoziota ni kumulika mambo yaliyojificha kwa namna inayovunja kanuni za kawaida ni muujiza, au vyovyote iwavyo, vyote hivyo vitazingatiwa na kuwekewa msingi katika itikadi na matendo yote kwa sababu Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anaungwa mkono na sifa ya  “Iswmah” kuwa na hatamki kwa matashi ya nafsi yake.”

 

 

Kauli yangu: Katika masuala ya kuoanisha mitende kunajibu linaloleta mwanga basi usahihi wake ni huu:

 

 

Imaam Muslim, (15/116 Nawawiy) Ibn Maajah (2470) na Ahmad (1/162) kutoka kwa As-Simaak: Kwamba amemsikia Muwsaa bin Twalhah Ibn ‘Ubaydillaah akihadithia kutoka kwa Baba yake akisema: Nimepita pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa watu wakiwa juu ya mitende akasema: “Hawa wanafanya nini?” wakasema: “Wanaoanisha (wanaunganisha) dume na jike basi inazaa”. Akasema: “Sidhani kama inafaa kitu kufanya hivyo” Wakaeleza hivyo, wakaacha, akaelezwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hivyo akasema: “Ikiwa inawafaa, basi na wafanye, kwani mimi hakika nilidhani, msinichukulie kwa dhana, lakini nikiwahadithieni jambo kutoka kwa Allaah lichukueni, kwani mimi sitomsingizia urongo Allaah (‘Azza wa Jalla).”

 

 

Na imepokewa na Muslim (15/117) kutoka katika Hadiyth ya Raafi’ bin Khudayj amesema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia Madiynah wakiwa wanaunganisha mitende dume na jike. Na wanasema wanaweka uzazi katika tende, akawauliza kwa kusema: “Mnafanya nini?” Wakasema: “Tulikuwa tukifanya hivi mazowea yetu.” Akasema: “Msingefanya hivyo huenda ingekuwa bora.” Wakaacha ikapungua (kuzaa). Akasema: Wakaeleza hilo kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Akasema: “Hakika mimi ni mtu, nikikuamrisheni jambo katika Dini yenu lichukueni, na nikikwambieni jambo katika maoni yangu basi hakika mimi ni mtu.”

 

 

Ikrimah akasema: Au mfano wa hivi. Amesema Al-Ma’qiriy[2] “Yakapungua kuzaa hakutia shaka[3]

 

 

Imepokewa na Muslim (15/117 Nawawiy), Ibn Maajah (2471) na Ahmad (6/123) kutoka kwa Hammad kuwa Thaabit ametuhadithia kutoka kwa Maalik Ibn Anas na Hishaam Ibn ‘Urwah kutoka kwa baba yake kutoka kwa ‘Aaishah; kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amepita kwa watu wakiunganisha mitende dume na jike akasema: “Msingefanya, ingefaa.” Akatoka akawapitia akasema: “Mitende yenu ina hali gani.” Wakasema: “Ulisema hivi.” Akasema: “Ninyi ni wajuzi zaidi wa mambo ya dunia yenu.”

 

Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alielezea fikra yake na pia dhana yake, hivyo ndivyo ilivyokuwa kama ilivyobainishwa na riwaayah zilizo Swahiyh; hivyo basi taarifa hiyo sio katika mlango wa Ijtihaad yake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo anaiona kuwa ni Shariy’ah ikiwa hivyo inapasa kuitimiza kwa kuifanyia kazi, hakuthibitisha kosa.

 

 

Imaam An-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema katika, “Sharh–Swahiyh Muslim: (15/116-117): “Wanazuoni wamesema kuhusu kauli yake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) “Katika maoni yangu” yaani: Katika mambo ya dunia na maisha yake na sio katika Shariy’ah. Ama aliyoyasema kwa Ijtihaad yake, na akayaona kuwa ni Shariy’ah hayo yanapasa kutendewa kazi na sio kuunganisha mitende katika fungu hilo bali ni katika aina ya yale yaliyotajwa kabla huko nyuma pamoja na kuwa lafudhi ya “Ar-Ra-yi” ameitamka Ikrimah katika maana, kwa kuwa alisema mwishoni mwa Hadiyth. Amesema Ikrimah: ‘Au maneno kama haya’, hakueleza tamko la Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa hakika.

 

 

‘Ulamaa wamesema: Kauli hii haikuwa khabari bali ni dhana kama alivyoibainisha katika riwaayah hizi.

 

 

Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyah amesema katika Majmuw’ Al-Fataawa (18-12): “….yeye hakuwakataza kupandiliza uzazi wa mitende lakini wao walikosea katika dhana yao kuwa aliwakataza; kama alivyokosea aliyekosea kudhania kuwa uzi mweupe na uzi mweusi ni ile kamba nyeupe na nyeusi”.

 

 

3. Tiba ni katika matendo ya watu mukallafiyna (wenye kubebeshwa amri na makatazo ya Dini) ama Shariy’ah safi imekuja kudhibiti matendo ya mukallafiyna na kuyahukumu kwa kubainisha aliyowajibisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Shariy’ah na aliyoyakataza na anayopendelewa na yanayochukiwa au yanayojuzishwa kufanywa na hizi ndizo hukumu tano za Takliyf; matendo yote ya watu mukallafiyna hayatoki nje ya mambo hayo matano.

 

 

Kwa sababu hiyo zimekuja Hadiyth zinazoamrisha kujitibu, na Hadiyth zinazoelezea baadhi ya madawa, na zingine zinaharamisha fungu lingine n.k.

 

 

4. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameteremsha maradhi na dawa; waliojua wamejua na wasio jua hawakujua, na kuhusu mambo ya dawa yaliomo katika Sunnah ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni katika maelimisho ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَلَّمَهُ شَدِيدُ الْقُوَىٰ ﴿٥﴾

Amemfunza (Jibriyl) mwenye nguvu shadidi. [an-Najm: 5]

 

Na kwa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakupata elimu kwa mwengine asiyekuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwani wapinga haki wangetia shaka:

 

وَمَا كُنتَ تَتْلُو مِن قَبْلِهِ مِن كِتَابٍ وَلَا تَخُطُّهُ بِيَمِينِكَ ۖ إِذًا لَّارْتَابَ الْمُبْطِلُونَ ﴿٤٨﴾

Na wala hukuwa (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) ukisoma kabla yake kitabu chochote, na wala hukukiandika kwa mkono wako wa kuume, kwani basi hapo wangetilia shaka wabatilifu. [Al-‘Ankabuwt: 48]

 

 

5. Taarifa za kitaalamu na kitiba zinazokuja katika Sunnah zina dalili za nguvu zilizoungwa mkono na sayansi ya enzi hizi. Na tiba mpya imetilia mkazo na kuweka hoja ya wazi kabisa haina shaka yoyote. Wala haina kificho: kuwa Aliyemfunulia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni Rabb wa walimwengu (Subhaanahu wa Ta'aalaa).    

 

 

6. Zimepokewa Hadiyth zilizokata shauri kuwa Twibbun-Nabawiy ni Wahyi kutoka kwa Allaah; katika Swahiyh Al-Bukhaariy kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu): Kwamba mtu mmoja alimjia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ndugu yangu analalamika maumivu ya tumbo. Akasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Mnyweshe asali.” Akamjia mara nyingine akamwambia: "Mnyweshe asali.” Kisha akamjia mara ya tatu akamwambia: "Mnyweshe asali.” Kisha akamjia akasema “Nimefanya.” Akasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Kasema kweli Allaah na tumbo la ndugu yako limeongopa! Mnyweshe asali!” Akamnywesha, akapona.

 

 

Imaam Ibn Al-Qayyim Al-Jawziyyah (Rahimahu Allaah) amesema: “Maelekezo ya dawa hiyo aliyomuelekeza Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ilikuwa ni kusafisha tumbo lililojaa, hivyo akamuamuru kunywa asali ili kuondoa mabaki ya vyakula yaliyo jikusanya katika maeneo ya tumbo la chakula na utumbo. Kwa sababu asali hufanya kazi ya kutakasa na kuondosha mabaki ya chakula. Alikuwa ana tatizo la maada zenye kuteleza zinazozuia chakula kutulia tumboni kutokana na hali yake ya utelezi. Tumbo la chakula lina chamvaa kama ya taulo, hivyo basi ikishikamana na vitu vya kuteleza ambavyo vimeganda kwenye tumbo, huliharibu pia na huharibu chakula. Hivyo dawa yake ni kisafisho cha mchanganyo huo, na asali ni katika dawa bora sana ya kutibia maradhi hayo. Na hasa inapochanganywa na maji ya moto.

 

 

Na katika kuendelea kunywa asali kuna maana kubwa nzuri sana, nayo, ni kwamba dawa yoyote inabidi iwe na kiwango kulingana na hali ya ugonjwa wenyewe ulivyo, ikiwa chini ya kiwango haiwezi kutibu kabisa na ikivuka kiasi hudhoofisha nguvu, hapo basi husababisha madhara mengine. Alipomuamrisha kumpa asali alimnywesha kiasi kisichotosha kupambana na ule ugonjwa na wala lengo halikutimia, alipomjulisha akajua alichomnywesha hakikufikia kiwango kinachohitajika na lengo linakuwa halifikiwi. Alipoendelea kurudiarudia kwenda kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamsisitizia kurejea matumizi ya asali ili ifikie kiasi kinachoweza kupambana na maradhi. Alipokunywa asali tena na tena, kulingana na ugonjwa wake, akapona kwa idhini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

 

Kuzingatia viwango na aina ya dawa na matibabu yanayotolewa na nguvu ya ugonjwa ni katika misingi mikubwa ya tiba.

 

 

Kauli yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) “Allaah amesema kweli na tumbo la ndugu yako limeongopa.“ Ni ishara ya uhakika wa kufaa kwa dawa hii, na kwamba ugonjwa uliendelea kuwapo sio kwa dosari ya dawa, lakini kwa uongo wa tumbo na wingi wa maada mbovu ndani mwake, hapo ndipo alipomuamuru kurudia matibabu kulingana na hali ya tatizo lilivyo.

 

Tiba ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) sio sawa na tiba za matabibu wengine. Kwani tiba ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni yakini haina shaka, ni ya ki-Ilaah (Allaah), chanzo chake ni Wahyi na dirisha la Unabii na ukamilifu wa akili.

 

 

Na tiba nyingine sana huwa ni dhana, na kuthibitishwa dhana hizo kwa majaribio, na sio jambo la kukanusha kwamba Twibbun-Nabawiy haifai kwa baadhi ya watu kutonufaika nayo; bali wameweza kunufaika wengi, kwani hunufaika na tiba ya ki-Nabii yule anayeipokea kwa kuikubali na kuamini kuwa ataweza kupona kwa tiba hiyo.

 

Hii Qur-aan mathalan ambayo ni shifaa kwa maradhi ya nyoyo ikiwa haikupokelewa kwa namna inayostahiki kupokelewa, basi nyoyo hazitapona kamwe kwa dawa yake, bali maradhi ya wanafiki yanaongezeka juu ya maradhi yao, na tiba ya miili inaponya wapi? Basi Twibbnu-Nabawiy haiendani na miili isipokuwa iwe mizuri, kama ilivyokuwa tiba ya Qur-aan haiwiani isipokuwa na Roho nzuri safi na nyoyo zilizo hai. Watu kupuuza tiba ya ki-Nabii, ni sawa kwamba wamepuuza tiba ya Qur-aan ambayo ndio tiba yenye kufaa. Hiyo sio kwa sababu ya dosari katika dawa lakini ni kutokana na ubaya wa hali ya mazingira na ufisadi wa mahali, na kutoikubali tiba hiyo. WabiLLaah At-Tawfiyq .”

 

 

7. Kwa hiyo, Imaam Ibn Al-Qayyim Al-Jawaziyyah (Rahimahu Allaah) ameelezea sana kuhusu kadhia hii, na ameweza kuweka hoja madhubuti na kulifafanua kikamilifu. Na baadhi ya hayo aliyosema: - “Basi hizi ni fusuli zenye kufaa katika mwongozo wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika tiba aliyojitibia, na kuielekeza kwa wengine, tunaelezea hekima kubwa zinazohemeza akili za matabibu na kushindwa kuzifikia na mlinganisho wa tiba zao sawa na watu walioshindwa.” [ukurasa wa 35]

 

 

“Nasi tunasema: Kuna jambo lingine hapa. Kuwa mfano wa matabibu bingwa na wanaoshindwa kufikia mfano wao, hili wamekiri matabibu wao bora kabisa wenye ujuzi wa tiba, wapo wanaosema: “Ni majaribio” na wengine wanasema: “Ni il-hamu, njozi, na mabunio yenye kusibu.” Na kati yao wapo wanaosema: “Tiba nyingi zimechukuliwa kwa wanyama.” Kama tunavyoshuhudia paka anapokula wadudu wenye sumu, hukimbilia kwenye taa na kuramba mafuta kujitibia kama nyoka walivyoonekana anapotoka chini ya ardhi, na macho yao yana giza hivyo huelekea majani ya mmea uitwao, Ar-Raaziyanij na kupitisha macho yao kwenye majani hayo. Pia kama ilivyo kwa ndege wanapopatwa na hali ya kutatizika kiafya hujitibu kwa maji ya bahari na mifano ya hayo, mengi yametajwa katika taaluma ya tiba.

 

 

Ni umbali gani wa tiba ya namna hii na ile tiba itokanayo na Wahyi ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anamfunulia Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kumjulisha yanayofaa na yale yenye madhara mlingano wa tiba hizo kwa Wahyi huu, ni sawa na kulinganisha elimu mbali mbali walizokuja nazo Manabii.

 

 

Bali zipo dawa ziponyazo maradhi ambazo madaktari wakubwa wameshindwa kuzigundua. Kadhalika utaalamu wao haukuweza kufikia huko wala majaribio na vipimo vyao havikuweza kugundua. Ni maradhi ya nyoyo, ya kiroho, moyo madhubuti, imani na kutawakali kwa Allaah na kumkimbilia, kujitupa Kwake, kujivunjavunja, mbele yake, kujidhalilisha kabisa, na unyenyekevu wa hali ya juu, moyo wa utayari kutoa, kuomba, kutubia, kuomba maghfirah,  kuwafanyia ihsaan viumbe, kuwasaidia wenye mahitaji, kuwafariji wenye shida; kwani dawa hizi mataifa yamezijaribu, katika dini, mila na desturi zao mbalimbali wakaona dawa hizo zimetia fora kuliko ujuzi wa wataalamu bobezi wa tiba na kuliko hata majaribio na vipimo vyao.

 

 

Kwa kweli sisi tumefanyia majaribio jambo hili, katika mambo mengi. Tukaona linaleta matokeo ambayo dawa za kihisia haziwezi kuyaleta bali tiba hizo huwa sawa na tiba za atw-twarqiyyah (makuhani) mbele ya matabibu. Na jambo hili linakwenda kwa mujibu wa kanuni ya hekima ya ki-Ilaah (Allaah) na halitoki nje ya hapo, lakini sababu ziko tofauti, wakati moyo umeungana na Rabb wa walimwengu, Muumba wa maradhi na dawa, Mwendesha maumbile na kuyageuza Atakavyo, Allaah Ana dawa nyinginezo mbali na ambazo mtu mwenye moyo usioshikamana na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) huteseka. Inajulikana kuwa Roho zinapokuwa na nguvu, na nafsi na maumbile ya mtu yakawa na nguvu, husaidiana kuondosha na kushinda maradhi. Vipi isikubalike kwa mwenye hali na nafsi yenye nguvu, na moyo wake ukajawa na furaha kwa kuwa karibu na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Muumba wake na mtoa maliwazo, na kumpenda, kufurahia kumdhukuru na kuelekeza nguvu zake zote Kwake. Na kuzikusanya na kumtaka Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) msaada Wake. Pia kutawakali Kwake. Hayo kwa ajili hiyo ni dawa kubwa na kuwajibisha pia kuondosha maumivu, moja kwa moja. Hakanushi haya ila mjinga wa watu kupindukia. Asiyeona mbele, mwenye nafsi nzito aliye mbali na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na ukweli wa ki mwana Aadam. Tutataja In Shaa Allaah sababu ya Suwratul Al-Faatihah kuweza kuondosha ugonjwa wa kung’atwa, kwa yule aliyejitibu kwayo baada ya kung’atwa akasimama mzima kabisa” [Uk 41-43].

 

 

“Tutaongeza ufafanuzi wa hili wakati wa kuelezea matibabu kwa njia ya ruqyah na Al-‘Awdh (kinga) ya ki-Nabiy, dhikri na du’aa, na kufanya kheri mbali mbali. Na tutabainisha tiba ya matabibu mbele ya tiba ya ki-Nabiy ni sawa na tiba ya atw-tarqiyyah (makuhani) na wanaoshindwa kwenye tiba zao. Kama wabobezi na viongozi wao walivyokiri hivyo. Tutabainisha kuwa tabia ya mwana Aadam ni yenye kuathirika sana na Roho, na kwamba nguvu za Al-‘Awdh (kujinga), ruqyah na du’aa, ziko juu kuliko nguvu za madawa, hadi kufikia kubadilisha nguvu za sumu kali zenye uwezo wa kuuwa”  [Uk 77].

 

 

“Kwa ujumla: Tiba ya kawaida mbele ya tiba ya ki-Nabiy ni sawa tiba ya atw-twarqiyyah (makuhani) kulinganisha na tiba zao, bali chini ya hapo, na tofauti kati yake na Manabii ni kubwa na kubwa zaidi kuliko tofauti kati yake na atw-twarqiyyah (makuhani) kwa mtu asiyejua kipimo chake, imekudhihirikia mkataba wa udugu uliopo kati ya hikma na shariy’ah, na kuwa kimoja hakigongani na kingine, na Allaah Humhidi Amtakaye  katika lililo sahihi, na humfungulia kwa atakayedumu katika kugonga mlango kumpa taufiki ya kila mlango, na Yeye (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  ni Mwenye neema isiyo na ukomo na hoja yenye umbuji. [uk 238]”

 

 

“Na imetangulia kuwa: Tiba ya matabibu kulingana na tiba ya ki-Nabiy ipo chini kwa kiasi cha tiba ya atw-twarqiyyah (makuhani) na wasioweza kulinganisha na tiba ya Manabii; na ya kuwa kati ya yanayoshushwa katika Wahyi na yale ya majaribio na unaweza kupima tofauti iliyopo ni kubwa.

 

 

Walau kuwa wajinga wale wamepata dawa yenye andiko kutoka kwa baadhi ya Mayahudi na Manaswara na washirikina (miongoni mwa matabibu): ili waipokee kwa kukubali na kujisalimisha kwayo, wala wasisimame katika jaribio lake.

 

 

Naam: Sisi hatupingi kuwa ada, mazoea yana taathira yake katika kumfanya mtu anufaike na dawa au kutonufaika nayo; kwa Yule aliyezoea dawa pamoja na chakula: Basi itamnufaisha zaidi na itamfaa kuliko yule ambaye hajaizoea. Bali huenda hawezi kunufaika nayo yule ambaye hajaizoea.

 

 

Maneno ya madaktari bingwa ingawa katika hali zote bila ya upekee, basi ni kutokana na mazingira na nyakati, na mahali, na ada za watu na ikiwa maneno yao yanalenga hali maalum, maneno yao na ujuzi wao hauna dosari, basi vipi atiwe kasoro mkweli aliyesadikiwa (Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)? Lakini nafsi za wana Aadam zimeundwa kwa ujahili na dhulma, ila kwa yule atakayepata msaada wa Allaah kwa iymaan na kupata nuru ya mwongozo.” [Uk 442].

 

 

“Tumeleta kiasi cha kufaa kabisa katika jumla yenye kunufaisha miongoni mwa sehemu za za tiba ya kielimu na kimatendo, yamkini mtu hawezi kuona kwengine mambo haya ila ndani ya kitabu hiki. Na umekuonesha ukaribu wa tiba hiyo na Shariy’ah. Na kwamba Twibbun-Nabawiy uwiano wa tiba ya matibabu ya utaalamu wa kawaida ni kiwango cha chini kuliko uwiano wa kati yao na wale wanaowashinda.

 

 

Mambo hayo ni zaidi ya ulivyotaja ukubwa wake ni zaidi mno, na kiasi ulichokielezea ni kidogo tu. Na mtu ambaye hajapata busara ya upambanuzi wa mambo, hajaruzukiwa neema ya namna hiyo, waelewe tu, ile tofauti kubwa iliyopo kati ya nguvu inayoungwa mkono na Wahyi kutoka kwa Allaah, tofauti kabisa na elimu ya watu wasiokuwa Manabii.

 

 

Huenda msemaji akasema tu: “Kuna uhusiano gani wa mwongozo wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na mlango huu wa tiba, na kutaja nguvu za madawa, na kanuni za tiba na uangalizi wa mambo ya afya?”

 

 

Hapo tatizo litakuwa kwa huyo msemaji ambaye ana upungufu wa kuelewa yale aliyokuja nayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwani hayana mengine zaidi ya haya, kwa mwenye ujuzi sahihi wa ujumbe wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Kwa atakayefahamu yale aliyokuja nayo Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na mwongozo wake, na dalili kuhusu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na uelewa mzuri kuhusu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):  Hii ni neema ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Humneemesha Amtakaye katika waja wake.

 

 

Tumekufahamisha misingi mitatu ya tiba katika Qur-a’an. Vipi ikanushwe kufaa kwa Shariy’ah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyetumwa kwa maslahi ya kidunia na Aakhirah. Na hili ni jambo la maslahi ya miji pia ustawi wa viwiliwili kama vile inavyokusanya ustawi wa nyoyo bali pia mwongozo wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) unaelekeza kutunza afya ya mwili, kwa namna zote. Ama upambanuzi wake unategemea akili sahhi, maumbile safi, kwa njia ya qiyasi, tanbihi, na ishara, kama ilivyo sana katika matawi ya ki-Fiqhi. Wala usiwe katika kundi la wale ambao hukifanyia uadui asichokijua.

 

Basi ambaye ataruzukiwa ufahamu wa kitabu cha Allaah na Sunnah ya Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mtu wa namna hiyo angeweza kutosheka kabisa, na akaacha maneno mengine yasiyokuwa hayo na angetoa elimu zote sahihi kutoka humo.

 

Elimu zote zimo katika kumjua Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na viumbe Wake. Na hili limeachwa kwa Rusuli (Swalaawatu Allaahi ‘alayhim wa salaam) kwani wao wana ujuzi zaidi. Hii linajulikana tu kwa mjuzi wa tiba sahihi na Shariy’ah ambaye anaweza kulinganisha kati ya pande mbili. Na kuona upande upi ulio bora.

 

 

Na tiba ya wafuasi wa Manabii: ni yenye kufaa zaidi kuliko tiba ya wengine.  Na tiba ya aliyewafuata ambaye ni mwisho wa Manabii na bwana wao na Imaam wao; Muhammad bin ‘Abdillaah (Swalawaatu-Allaahi Wa Salaamuhu ‘alayhi wa ‘alayhim) ni tiba kamili na sahihi na yenye manufaa zaidi.    

 

 

Na hayafahamu haya isipokuwa yule anayejua tiba ya watu wasiokuwa wao, kisha akapima kati yao, na hapo basi hudhihiri tofauti yao.  Nao ni ummah sahihi zaidi kwa maumbile ya fitwrah na akili, na wenye elimu kubwa zaidi na wa karibu zaidi katika haki; kwani wao ni wabora kwa Allaah katika watu wa ummah mbali mbali, kama ambavyo Rasuli wao ni bora zaidi kuliko Rusuli wengineo, na elimu ambayo amepewa, uvumilivu na hekima ni jambo ambalo hakuna mfano wake na kulinganisha na wengine.

 

Imaam Ahmad amepokea katika Musnad Hadiyth ya Bahz bin Hakiym, kutoka kwa Baba yake, kutoka kwa Babu yake (Radhwiya Allaahu) amesema: “Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Nyinyi mnatoshea mataifa sabini, nyinyi ni wa bora wao na watukufu zaidi kwa Allaah.” 

 

Basi imejitokeza athari ya utukufu wake kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika elimu zao na akili zao na maumbile yao, hao wamedhihirishiwa elimu za ummah zilizotangulia na akili matendo na daraja zao.  Kwa hivyo wakazidi elimu upole na akili kuongeza katika ile elimu na upole na hekima alizowapa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa wingi mno. Kwa ajili hiyo ikawazidishia elimu, uvumilivu na utambuzi kwa yale ambayo Allaah Aliwapa katika elimu na uvumilivu.

 

Na hili lilipelekea tabia ya kidamu ni yao, ya umanjano ni ya Mayahudi, na kibalghamu kwa Manaswara na kwa ajili hiyo kwa Manaswara imezidi hali ya upumbavu, uchache wa kufahamu na utambuzi. Na kwa Mayahudi imezidi huzuni, majonzi na unyonge. Kwa Waislamu imezidi, akili, ushujaa, ufahamu kunusuru na furaha.

 

Na hizi ni siri na hakika ambazo atakayejua kiasi chake ni mwenye ufahamu mzuri na umakini wa ubongo, na wingi wa elimu yake, na kujua hali walizo nazo watu. WabiLLaah At-Tawfiyq.” [(Uk 499-501)]

 

Ama baada ya hayo. Basi yanayofuatia ni Fusuli zenye manufaa kutoka katika mwongozo wake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika tiba ambayo amejitibia akawaelekeza wengine na tutabainisha hekima ya kuwashangaza watu na kushindwa kuifikia, tiba zao mbele ya tiba ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni sawa na tiba ya wengine wenye kushindwa kufikia tiba zao (hao matabibu wa kawaida). Basi tunasema tukiwa tunamuomba msaada Allaah na kutafuta hila na nguvu kutoka Kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):   

 

 

 

 

[1] Angalia ‘Al-Musawwadah fiy Uswuwl Fiqhi cha Ibn Taymiyyah (uk 451-452) na Irshaad Al-Fuhuwl cha Ash-Shawkaany (uk 255-256).

 

[2]  Huyu Ahmad bin Ja’far Al-Ma’qiriy

[3] Kwa umakini huu wenye kushangaza Hadiyth nyingi za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) zimenukuliwa, hivyo mpokezi akitia shaka, au akapokea kwa maana basi ataeleza hilo ili kile kinachonukuliwa kifahamike.

 

Share