03-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Twahaarah:Mlango Wa Kuondosha Najisi Na Ubainifu Wake
بلُوغُ الْمَرام
Buluwgh Al-Maraam
كِتابُ الطَّهارَة
Kitabu Cha Twahaarah
بَابُ إِزَالَةِ اَلنَّجَاسَةِ وَبَيَانِهَا
03-Mlango Wa Kuondosha Najisi Na Ubainifu Wake
22.
عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ رضى الله عنه قَالَ: سُئِلَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم عَنْ اَلْخَمْرِ تُتَّخَذُ خَلًّا؟ قَالَ: { لَا} أَخْرَجَهُ مُسْلِم ٌ
Kutoka kwa Anas bin Maalik (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliulizwa kuhusu kutengeneza siki kutokana na mvinyo. Akasema: “Hapana[1].” [Imetolewa na Muslim]
23.
وَعَنْهُ قَالَ: لَمَّا كَانَ يَوْمُ خَيْبَرَ، أَمَرَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم أَبَا طَلْحَةَ، فَنَادَى: {إِنَّ اَللَّهَ وَرَسُولَهُ يَنْهَيَانِكُمْ عَنْ لُحُومِ اَلْحُمُرِ اَلْأَهْلِيَّةِ، فَإِنَّهَا رِجْسٌ } مُتَّفَقٌ عَلَيْه ِ
Kutoka kwa Anas bin Maalik (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: Katika siku ya Khaybar, Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimuamrisha Abuu Twalhah[2] kutangaza: “Hakika Allaah na Rasuli Wake wamekukatazeni kula nyama ya punda vihongwe kwa kuwa ni najisi.[3]” [Al-Bukhaariy, Muslim]
24.
وَعَنْ عَمْرِو بْنِ خَارِجَةَ رضى الله عنه قَالَ: {خَطَبَنَا رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم بِمِنًى وَهُوَ عَلَى رَاحِلَتِهِ، وَلُعَابُهَا يَسِيلُ عَلَى كَتِفَيَّ } أَخْرَجَهُ أَحْمَدُ وَاَلتِّرْمِذِيُّ وَصَحَّحَه ُ
Kutoka kwa ‘Amr bin Khaarijah[4] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alitukhutubia kule Minna huku akiwa juu ya kipando chake, na mate yake yanachuruzika mabegani[5] mwangu.” [Imetolewa na Ahmad na ameisahihisha At-Tirmidhiy]
25.
وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: { كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَغْسِلُ اَلْمَنِيَّ، ثُمَّ يَخْرُجُ إِلَى اَلصَّلَاةِ فِي ذَلِكَ اَلثَّوْبِ وَأَنَا أَنْظُرُ إِلَى أَثَرِ اَلْغُسْلِ فِيهِ } مُتَّفَقٌ عَلَيْه ِ
وَلِمُسْلِمٍ: { لَقَدْ كُنْتُ أَفْرُكُهُ مِنْ ثَوْبٍ رَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَرْكًا، فَيُصَلِّي فِيهِ }
وَفِي لَفْظٍ لَهُ: { لَقَدْ كُنْتُ أَحُكُّهُ يَابِسًا بِظُفُرِي مِنْ ثَوْبِهِ }
Kutoka kwa ‘Aaishah[6] (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akiosha manii[7], na kisha alikuwa akielekea katika Swalaah na nguo hiyo, nami nilikuwa naona mabaki ya athari za maosho ndani yake.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
Na katika Muslim: “Nilikuwa nikikwangua (manii) kutoka kwenye nguo ya Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) mkwanguo na huswali na nguo hiyo.”
Na katika riwaayah nyengine ya Muslim: “Mimi (‘Aaishah) nilikuwa nayakwangua kwa kucha yangu hali ya kuwa yamekauka.”
26.
وَعَنْ أَبِي اَلسَّمْحِ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم { يُغْسَلُ مِنْ بَوْلِ اَلْجَارِيَةِ، وَيُرَشُّ مِنْ بَوْلِ اَلْغُلَامِ} أَخْرَجَهُ أَبُو دَاوُدَ وَالنَّسَائِيُّ وَصَحَّحَهُ اَلْحَاكِم ُ
Kutoka kwa Abuu As-Samh[8] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mkojo wa mtoto mchanga wa kike uoshwe, na mkojo wa mtoto wa kiume unyunyiziwe maji[9].” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy na ameisahihisha Al-Haakim]
27.
وَعَنْ أَسْمَاءَ بِنْتِ أَبِي بَكْرٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم قَالَ فِي دَمِ اَلْحَيْضِ يُصِيبُ اَلثَّوْبَ: { تَحُتُّهُ ثُمَّ تَقْرُصُهُ بِالْمَاءِ ثُمَّ تَنْضَحُهُ ثُمَّ تُصَلِّي فِيهِ } مُتَّفَقٌ عَلَيْه ِ
Kutoka kwa Asmaa’ bint Abiy Bakar[10] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) kwamba Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema kuhusu damu ya hedhi inayodondokea nguo: “Aikwangue, aifikiche na maji, na kisha aioshe, na kisha aswali na nguo hiyo.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
28.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه قَالَ: قَالَتْ خَوْلَةُ: { يَا رَسُولَ اَللَّهِ، فَإِنْ لَمْ يَذْهَبْ اَلدَّمُ، قَالَ: "يَكْفِيكِ اَلْمَاءُ، وَلَا يَضُرُّكِ أَثَرُهُ" } أَخْرَجَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ وَسَنَدُهُ ضَعِيف ٌ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: Khawlah[11] aliuliza: “Ee Rasuli wa Allaah! Je, endapo alama ya damu haitatoweka?” Akasema: “Maji yanakutosha, na athari yake haitokuathiri chochote.” [Imetolewa na At-Tirmidhiy, na Isnaad yake ni dhaifu]
[1] Kutengeneza siki kwa kuongeza vitu kwenye mvinyo kumekatazwa.
[2] Abuu Twalhah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) ndiye Zayd bin Sahl bin Al-Aswad bin Haraam Al-Answaar An-Najaar, ambaye alikuwa ni mmoja wa Swahaba waandamizi. Alihudhuria Bay’atul-‘Aqabah na vita vyote.
Alipigana kishujaa wakati wa Vita Vya Uhud na akamhami Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) mpaka mkono wake ukapooza. Pia aliua watu ishirini katika Vita Vya Hunayn. Akijulikana kwa Abuu Twalha Al-Answaawiry na alikuwa ni mume wa Ummu Sulaym ambaye alitaka mahari yake yawe ni kusilimu kwake. Wawili hawa walikuwa wakarimu mno na wenye iymaan za hali ya juu. Walikuwa na visa vizuri vyenye mafunzo na vya kusisimua, na hata kisa chake kimoja cha kupokea wageni kilikuwa ni sababu ya kuteremshwa kauli ya Allaah (عز وجل):وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ۚ
Na wanawapendelea kuliko nafsi zao japokuwa wao wenyewe wanahitaji. [Al-Hashr: 9]
Alifariki mwaka 34 au 51 A.H.
[3] Hadiyth hii ni dalili kuwa nyama ya punda vihongwe ni haraam.
[4] ‘Amr ndiye ‘Amr bin Kharija bin Al-Muntafiq Al-Asad. Alikuwa rafiki wa Abuu Sufyaan. Anahesabika kuwa alitokana na ukoo wa Al-Ash’ar. Yeye ni miongoni mwa Swahaba waliolowea Sham, na Hadiyth yake iliripotiwa na watu wa Basra.
[5] Kutoka katika Hadiyth hii tunatambua kuwa mate ya mnyama ambaye ni halaal (kuliwa) ni masafi. Hadiyth hii iliafikiwa na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ).
[6] ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) ni binti wa Abuu Bakar Asw-Swiddiyq (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) aliyeolewa na Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) miaka miwili kabla ya Hijrah (kuhama) mnamo mwezi wa Shawwaal, lakini akaanza kuishi naye mnamo mwaka wa 1 A.H wakati akiwa na umri wa miaka 9. Alikuwa msomi sana na aliripoti Hadiyth nyingi. Alifariki mnamo tarehe 17 mwezi wa Ramadhwaan mwaka 57 au 58 A.H. Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) alimswalia Swalaah ya Janaazah, na akazikwa Al-Baq’.
[7] Kuna kutofautiana maoni kuhusu manii ya mwana Aadam, kama ni safi au siyo safi. Wanazuoni wengine wanayahesabu kama mate au makamasi, na kwa mujibu wa wengine ni lazima kuyaosha. Kundi hilo la kwanza linatoa sababu yake katika Hadiyth ya kuwa huwa yanakwanguliwa yakikauka, na kundi la pili linatoa sababu yake kutoka kwenye Hadiyth ya kuyaosha. Kwa hakika manii ni najsi, na lazima yasafishwe kwa kuyaosha, kuyakwangua au kuyapangusa. (Tazama kitabu cha Niyl Al-Awtwaar cha Imaam Shawkaaniy).
[8] Abuu As-Samh jina lake halisi ni Iyyaad. Alikuwa ni mtumwa aliyeachwa huru na akawa mtumishi wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ). Ibn Abdil-Barr alisema aliripotiwa kwamba alipotea na hakuna anayejua alifia wapi au lini.
[9] Hii inamaanisha kuwa ipo tofauti baina ya mkojo wa msichana na mvulana. Katika wakati wa kunyonya, mkojo wa mvulana ni msafi zaidi kuliko mkojo wa msichana.
[10] ‘Asmaa ni Mama wa ‘Abdullaah bin Az-Zubayr na ni dada mkubwa wa ‘Aaishah. Alisilimu mapema sana kule Makkah na akahamia Madiynah. Alifariki chini ya mwezi mmoja baada ya kuuliwa mwanawe Ibn Az-Zubayr mnamo mwaka 73 A.H akiwa na umri wa miaka 100, nab ado hakung’oa jino hata moja wala kuharibika akili kwa uzee.
[11] Khawlah bint Yaasir alikuwa Swahaba, na Abu Salamah bin ‘Abdir-Rahmaan alisimulia Hadiyth hiyo kutoka kwake.