Kuanza Swafu Ya Nyuma Kwa Kumvuta Mtu Wa Mbele Katika Swalaah Ya Jamaa
Kuanza Swafu Ya Nyuma Kwa Kumvuta Mtu Wa Mbele Katika Swalaah Ya Jamaa
SWALI
Vipi kama mtu amechelewa ktk swala ya jamaa na akakuta waumini wenzake wakiendelea na jamaa na swafu ya mbele imejaa, na ilimbidi anzishe swafu ingine,je lazima amvute mtu aliembele yake? Na asipofanya kuna madhambi?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Zimekuja Hadiyth mbalimbali kuonyesha kutokufaa na makatazo ya Maamuma kusimama nyuma ya swafu peke yake. Kama atafanya hivyo kwa makusudi basi hana Swalaah mtu huyo, kwa kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomuelezea yule mtu aliyesimama nyuma ya swafu peke yake: “Isaliti Swalaah yako, kwani hakuna Swalaah kwa mtu aliye pekee nyuma ya swafu” [Ibn Maajah na Imaam Ahmad kwa Isnadi iliyo Hasan].
Pia, Imepokewa kwa Waabisah kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona mtu akiswali peke yake katika swafu, alimuamuru aswali tena. [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah].
Na katika Hadiyth nyengine, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu mtu anayeswali nyuma ya swafu peke yake. Akajibu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) “Atarudia Swalaah yake”. [Imaam Ahmad]
Shaykh Al-Albaaniy anasema: “Ikiwa zitasihi Hadiyth kuhusu hilo (ameona kuwa kuna baadhi hazikusihi), basi makusudio ni kuwa mtu asiswali peke yake na hali kuna nafasi hata ya kujibana kwenye swafu, kwa hiyo mtu ajitahidi kujipenyeza kwenye swafu kwani swafu nyingi za siku hizi Misikitini zina mapengo mengi. Na akishindwa kupata nafasi kabisa basi anaweza kuswali peke yake kwenye swafu ya nyuma na Swalaah yake itakuwa ni sahihi kabisa.’’
Shaykh ametoa mifano pia kuwa kuna baadhi ya watu walio na tabia ya kuswali katika maeneo fulani Msikitini na hawajali swafu, kama baadhi ya waadhini kuswali maeneo ya karibu na mlango. Na hao ndio hizo Hadiyth zimewakusudia na si wale wanaojitahidi kutafuta nafasi za kujibana na wakakosa.
Shaykhul-Islami Ibn Taymiyyah anaeleza, “Ikiwa mtu ameingia Msikitini akajaribu kuunga swafu ya mbele yake na ikawa imejaa hakuna nafasi kabisa, na akawa hakuna aliyekuja kujiunga naye, basi ataswali peke yake kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) hamkalifishi mja kwa kile asichokuwa na uwezo nacho.”
Ama ilivyozoeleka ya kuja kwenye swafu ya nyuma akiwa peke yake na kumgusa mtu wa mbele yake amuunge, hayo pamoja na kuwa yanahitaji ushahidi wa kufanya hivyo, pia ni mambo yanayoleta tashwishi katika Swalaah na kuvuruga khushuu za wengine.
Na Allah Anajua zaidi