103-Aayah Na Mafunzo: Macho Hayamzunguki Allaah Bali Yeye Anayazunguka Macho Yote

 

Aayah Na Mafunzo

 

www.alhidaaya.com

 

Al-An’aam 103

 

103-Suala La ‘Aqiydah: Macho Hayamzunguki Allaah (سبحانه وتعالى)  

Bali Yeye Anayazunguka Macho Yote

 

 

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ ﴿١٠٣﴾

Macho hayamzunguki (hayamdiriki) bali Yeye Anayazunguka macho yote, Naye Ni Mwenye Kudabiri mambo kwa ulatifu, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. (6:103).

 

 

 

Mafunzo:

 

Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) Hakumuona Allaah (سبحانه وتعالى):

 

  

Masruwq  (رضي الله عنه)  amehadithia kwamba: Nilimwambia ‘Aaishah (رضي الله عنها) : Ee Mama! Je Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake? Akasema: Hayo uliyoyasema yamefanya nywele zangu zisimame kunisisimka mwili! Tambua kwamba mtu akikutajia mambo matatu yafuatayo basi yeye ni muongo! Atakayesema kwamba Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) amemuona Rabb wake, kisha akasoma:

 

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ ﴿١٠٣﴾

Macho hayamzunguki (hayamdiriki) bali Yeye Anayazunguka macho yote, Naye Ni Mwenye Kudabiri mambo kwa ulatifu, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. (6:103).

 

Na akasoma pia:

 

وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُكَلِّمَهُ اللَّـهُ إِلَّا وَحْيًا أَوْ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ أَوْ يُرْسِلَ رَسُولًا فَيُوحِيَ بِإِذْنِهِ مَا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ عَلِيٌّ حَكِيمٌ﴿٥١﴾

Na wala haikuwa kwa mtu yeyote kwamba Allaah Amsemeze isipokuwa kwa Wahy au kutoka nyuma ya kizuizi, au Hutuma Mjumbe, kisha Anamfunulia Wahy Ayatakayo kwa Idhini Yake. Hakika Yeye Ni Mwenye ‘Uluwa, Mwenye Hikmah wa yote. (42:51).

 

 

Kisha akaendelea kusema: Na atakayesema kwamba Nabiy anajua yatakayotokea kesho basi ni muongo. Kisha Akasoma:

 

وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا ۖ

Na nafsi yoyote haijui nini itachuma kesho, na nafsi yoyote haijui itafia katika ardhi gani.  (31:34).

 

 

Kisha akasema: Na atakayesema kuwa Nabiy ameficha aliyofunuliwa Wahyi (na maamrisho) basi ni muongo! Kisha akasoma:

 

يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ ۖ وَإِن لَّمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ ۚ  

Ee Rasuli! Balighisha yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Rabb wako. Na usipofanya, basi utakuwa hukubalighisha ujumbe Wake.  

(5:67).

 

 

Kisha akasema: Lakini Nabiy alimuona Jibriyl katika umbile lake khalisi mara mbili. [Al-Bukhaariy]

 

 

Kwa upande mwengine Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amesema: Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Allaah, na akasema kuwa Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake mara mbili. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]  

 

Al-Haafidhw, Ibn Hajar amesema: “Maelezo ya Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) yamekuja katika hali ya kutodhibitiwa (hayaelezi kama Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake kwa macho yake au vipi) wakati kauli za Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها)  na wenziwe zimedhibitiwa kwa kusema Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) hakumuona Allaah “Kwa macho yake.” Tunaweza kuunganisha kauli hizo mbili kwa kusema Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها)  alikataa muono “Kwa macho yake” na kauli ya Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kuwa ni kamuona kiroho.” [Fat-hul-Baariy, 8/608]  

 

 

Na Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kwa riwaaya nyingine  alisema kuwa Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake wakati akiwa katika usingizi, na hii ni ndoto ya kweli. Na kauli ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها)  inakataa, na kwamba Rasuli hakumuona Rabb wake wakati yeye akiwa macho, lakini kauli hiyo haikatazi kuwa  Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake akiwa usingizini Alichokana hapa ni kuwa Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) hakumuona Allaah kwa macho yake meupe, akiwa macho.  

 

Wale ambao wanao msimamo kuwa Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake kwa macho yake meupe wanaleta Hadiyth dhaifu. Hakuna Hadiyth Swahiyh ambayo inaeleza ya kuwa Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake kwa macho yake akiwa macho. Wenye msimamo huo wanaleta Hadiyth ya At-Tirmidhiy ambayo Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) anasema kuwa Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake. ‘Ikrimah alimuuliza: “Vipi Aayah ambayo inasema:

 

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ

Macho hayamzunguki (hayamdiriki) bali Yeye Anayazunguka macho yote

 

 

Alijibu, kuwa ni wakati tu Allaah amezungukwa na Nuru, lakini Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake mara mbili. “Hadiyth hii ni dhaifu.”

 

Kwa hali hiyo, hakuna mgongano wa kauli, na Allaah Anajua zaidi [Sharh ya Uswuwl Al-I’itiqaad cha Al-Laalika’iy, (93/512), As-Sunnah (1/181) na Swifaat Al-Maqdisiy ukurasa (109-111]   

 

Hapa kunathibitishwa kuwa Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) hakumuona Rabb wake wakati alipopelekwa Al-Israa Wal Mi’raaj, na hii ndio ‘Aqiydah ya Ahlus-Sunnah wal- Jamaa’ah kuwa Allaah Haonekani duniani, kinyume na ‘Aqiydah ya Masufi wanaoamini kuwa Allaah Anaonekana duniani kwa kuegemeza tukio hilo la Al-Israa Wal Mi’raaj.

 

Kadhaalika, Aayah hiyo vilevile haikanushi kuonekana Allaah Qiyaamah, bali Qiyaamah Allaah Ataonekana katika kisimamo cha Qiyaamah katika Jannah (Peponi) kwa dalili nyingi kutoka katika Qur-aan na Sunnah, kinyume na ‘Aqiydah ya makundi potofu yanayoamini kuwa Allaah Hatoonekana Aakhirah.

 

 

Share