158-Aayah Na Mafunzo: Miongoni Mwa Alama Kuu Za Qiyaamah Kuchomoza Jua Magharibi Ad-Dajjaal Mnyama Mkubwa Kuongea

 

Aayah Na Mafunzo

 

www.alhidaaya.com

 

Al-An’aam 158

 

158-Miongoni Mwa Alama  Kuu Za Qiyaamah

Kuchomoza Jua Magharibi Ad-Dajjaal Mnyama Mkubwa Kuongea

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 

هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا أَن تَأْتِيَهُمُ الْمَلَائِكَةُ أَوْ يَأْتِيَ رَبُّكَ أَوْ يَأْتِيَ بَعْضُ آيَاتِ رَبِّكَ ۗ يَوْمَ يَأْتِي بَعْضُ آيَاتِ رَبِّكَ لَا يَنفَعُ نَفْسًا إِيمَانُهَا لَمْ تَكُنْ آمَنَتْ مِن قَبْلُ أَوْ كَسَبَتْ فِي إِيمَانِهَا خَيْرًا ۗ قُلِ انتَظِرُوا إِنَّا مُنتَظِرُونَ ﴿١٥٨﴾

Je, wanangojea nini isipokuwa Malaika wawafikie (kuwatoa roho), au Awafikie Rabb wako (kuwahukumu), au ziwajie baadhi ya Aayaat za Rabb wako? Siku zitakapokuja baadhi ya Alama (za Qiyaamah) za Rabb wako haitoifaa nafsi iymaan yake, ikiwa haikuamini kabla au haikuchuma katika Iymaan yake kheri yoyote. Sema: Ngojeeni hakika nasi tunangojea. [Al-An'aam: 158]

 

Mafunzo:

 

Aayah hii tukufu imetaja kuwa kutatokea alama kabla ya kusimama Qiyaamah; alama ambazo wale wasioamini kabla ya kutokea alama hizo, watakapotaka kuamini, basi Iymaan zao hazitawafaa lolote kwa kuwa hawatakubaliwa kuamini kwao. Mifano ya hayo ni jua kuchomoza kutoka upande wa Magharibi badala ya kuchomoza kutoka Mashariki kwa Hadiyth ifuatayo:

 

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayetubu kabla ya kuchomoza jua upande wa Magharibi, Allaah Atamkubalia tawbah yake.” [Muslim]

 

Na pia: Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Matatu yakitokea, basi nafsi haitofaa iymaan yake tena ikiwa haikuamini kabla au haikuchuma kheri yoyote; kuchomoza jua upande wa Magharibi, kutokeza kwa Ad-Dajjaal, na mnyama mkubwa wa ardhi (atakyesemesha watu).” [Ibn Jariyr na Ahmad].

 

Na Hadiyth ifuatayo imetaja alama zote kumi:

 

Amesimulia Hudhayfah Bin Asiyd (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa chumbani nasi tulikuwa chini yake, akachungulia na kutuuliza:   “Mnajadiliana nini?” Tukasema: (Tunajadili kuhusu) Saa (Qiyaamah). Hapo akasema: Saa (Qiyaamah) hakitatokea mpaka zionekane Alama (au Ishara) kumi: Kudidimia kwa Mashariki na Magharibi, Kudidimia Bara la Arabu, Moshi, (Masiyh) Ad-Dajjaal, Mnyama mwitu mkubwa wa ardhi (atakayewasemesha watu), Ya-ajuwj na Ma-ajuwj,  Kuchomoza jua upande wa Magharibi,   Moto utakaotokea  upande wa chini ya ‘Aden utakaowasukuma watu (kufikia Ardhi ya Mkusanyiko).”  Shu'bah   amesema na amenihadithia   ‘Abdul-‘Aziyz bin Rufa’y kutoka kwa Abiy Atw-Twufayl kutoka kwa Abiy Sariyhah Hadiyth kama hiyo  ila Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) hakuitaja (alama ya kumi) lakini alisema kuwa katika kumi, mojawapo ni kuteremka Nabiy ‘Iysaa  bin Maryam alayhi  (عليه السلام)  na katika riwaaya nyengine ni: Upepo mkali utakaowaendesha watu na kutupwa   baharini. [Muslim]

 

 

Na ‘Ulamaa wametaja alama hizo kubwa kumi ingawa wamekhitilafiana katika mpangilio wake na kuzitaja kwake nazo ni:

 

-Kuja kwa Mahdi.

-Kutokeza kwa Masiyh Ad-Dajjaal.

-Kuteremka kwa Nabiy ‘Iysaa na (عليه السّلام).

-Kuchomoza kwa Yaajuwj na Maajuwj.

-Ka’bah kubomolewa na kutoka Moshi.

-Kutoweka Qur-aan nyoyoni mwa Waumini na Miswahafu.

-Jua kuchomoza Magharibi.

-Kutokeza mnyama mkubwa atakayewasemesha watu.

-Mididimizo mitatu ya ardhi: Mdidimizo wa Mashariki, Magharibi na katika Jaziyrah ya Arabia.

-Moto utakaotoka kutoka Yemen utawapeleka watu kufika katika Ardhi ya Mkusanyiko.

 

 

 

 

 

 

 

   

 

 

 

 

Share