160-Aayah Na Mafunzo: Mja Akitia Niyyah Kutenda Jema Analipwa Moja, Akitimiza Analipwa Mara Kumi, Ovu Haliandikiwi Mpaka Alitende Na Huhesabiwa Moja
Aayah Na Mafunzo
Al-An’aam 160
160-Miongoni Mwa Rahma Za Allaah Ni Kwamba Mja Akitia Niyyah Kutenda Jema Analipwa Moja Na Akitimiza Analipwa Mara Kumi Na Ovu Haliandikiwi Mpaka Alitende Na Huhesabiwa Moja
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا ۖ وَمَن جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَلَا يُجْزَىٰ إِلَّا مِثْلَهَا وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿١٦٠﴾
Atakayekuja na ‘amali njema basi atapata (thawabu) kumi mfano wake. Na Atakayekuja na ovu basi hatolipwa ila mfano wake, nao hawatodhulumiwa. [Al-An'aam: 160]
Mafunzo:
Rahmah Ya Allaah (سبحانه وتعالى) Kwa Waumini Kuongezewa Thawabu Mara Kumi Kwa ‘Amali Njema Moja Na Kuandikiwa Dhambi Moja Tu Kwa Tendo Ovu:
Ukitia niyyah kutenda amali moja lakini ukawa hukujaaliwa kuitenda utaandikiwa moja. Utakapoweza kuitenda utalipwa mara kumi yake.
Ukitia niyyah kutenda uovu haitoandikwa kwanza kwa kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Anampa mja muhula ajirudi ili asitende uovu au dhambi. Na atakapolitenda basi ataandikiwa dhambi moja.
Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah Ameandika mema na mabaya, kisha Akayabainisha, basi atakayetia niyyah kutenda jema kisha asilifanye, ataandikiwa jema moja kamili. Atakapofanya hima na akalitenda, ataandikiwa mema kumi hadi kuzidi mia saba na ziada nyingi. Na atakayetia niyyah kufanya kitendo kibaya kisha asikifanye, ataandikiwa jema moja kamili. Atakapokifanya, ataandikiwa dhambi moja.” [Al-Bukhaariy na Muslim]