040-Aayah Na Mafunzo: Anayemkadhibisha Allaah Na Aayaat Zake Hatofunguliwa Milango Ya Mbingu Mpaka Ngamia Aingie Katika Tundu Ya Sindao
Aayah Na Mafunzo
Al-A’raaf 40
040-Anayemkadhibisha Allaah Na Aayaat Zake Hatofunguliwa Milango Ya Mbingu Mpaka Ngamia Aingie Katika Tundu Ya Sindao
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَاسْتَكْبَرُوا عَنْهَا لَا تُفَتَّحُ لَهُمْ أَبْوَابُ السَّمَاءِ وَلَا يَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ حَتَّىٰ يَلِجَ الْجَمَلُ فِي سَمِّ الْخِيَاطِ ۚ وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُجْرِمِينَ ﴿٤٠﴾
Hakika wale waliokadhibisha Aayaat Zetu na wakazifanyia kiburi, hawatofunguliwa kamwe milango ya mbingu na wala hawatoingia Jannah mpaka ngamia aingie katika tundu ya sindano. Na hivyo ndivyo Tunavyowalipa wakhalifu. (7:40).
Mafunzo:
Mustahili Kwa Waliokufuru Kuingia Janna (Peponi) Kama Vile Mustahili Ngamia Kuingia Katika Tundu Ya Sindano:
Allaah (سبحانه وتعالى) Anatoa mifano mbali mbali katika Qur-aan; mifano yenye Hikmah, mafundisho na mazingatio kwa wenye kutafakari. Rejea Ibraahiym (14:24-25), Al-Kahf (18:54), Al-Hajj (22:73), Al-‘Ankabuwt (29:43), Ar-Ruwm (30:58) na kwengineko kwingi katika Qur-aan. Na katika Sunnah hali kadhaalika Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amepiga mifano mingi mmojawapo ni kuhusu Swalaah tano jinsi zinavyomsafisha mtu na madhambi:
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mnaonaje kungekuwa na mto mlangoni mwa mmoja wenu na akaoga mara tano kwa siku, je, atabakiwa na tone la uchafu (mwilini mwake)?” Wakasema: “Hatabakiwa na tone la uchafu.” Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: ”Basi hivyo ni mfano wa Swalaah tano ambazo Allaah Anafuta madhambi kwazo.” [Al-Bukhaariy na Muslim]
Sharh (Ufafanuzi) Ya Aayah:
Imaam Bin Baaz (رحمه الله) amesema alipoulizwa kuhusu Aayah hii:
إِنَّ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَاسْتَكْبَرُوا عَنْهَا لَا تُفَتَّحُ لَهُمْ أَبْوَابُ السَّمَاءِ وَلَا يَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ حَتَّىٰ يَلِجَ الْجَمَلُ فِي سَمِّ الْخِيَاطِ ۚ وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُجْرِمِينَ ﴿٤٠﴾
Hakika wale waliokadhibisha Aayaat Zetu na wakazifanyia kiburi, hawatofunguliwa kamwe milango ya mbingu na wala hawatoingia Jannah mpaka ngamia aingie katika tundu ya sindano. Na hivyo ndivyo Tunavyowalipa wakhalifu. (7:40).
“Ni dhahiri kuwa mwenye kukadhibisha Aayaat za Allaah akatakabari kufuata haki, hivyo ndivyo itakavyokuwa hali yake, haitopanda roho yake mbinguni, bali itarudishwa ardhini katika mwili wake aadhibishwe kaburini mwake. Kisha atahamishwa motoni, tunamuomba Allaah Al-‘Aafiyah. Kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى) kuhusu Fir’awn:
النَّارُ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا غُدُوًّا وَعَشِيًّا ۖ وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ أَدْخِلُوا آلَ فِرْعَوْنَ أَشَدَّ الْعَذَابِ﴿٤٦﴾
Wanadhihirishiwa moto asubuhi na jioni, na Siku itakayosimama Saa (itasemwa): Waingizeni watu wa Fir’awn katika adhabu kali kabisa. [Ghaafir 40:46]
Hivyo ndivyo hali ya wengineo, kila atakayetakabari na haki na asifuate Mwongozo, haitofunguliwa milango ya mbingu wala hazirudishwi roho zao mbinguni wala kwa Allaah (عزّ وجلّ) bali itarudi roho yake katika mwili wake muovu na ataadhibiwa kaburini mwake pamoja na adhabu ya moto Siku ya Qiyaamah. Tunamuomba Allaah Al-‘Aafiyah. Na pia hawatoingia Jannah kamwe. Ndipo Allaah (سبحانه وتعالى) Anabainisha kuwa hatoingia kamwe Jannah mpaka iwezekane ngamia aingie katika tundu ya sindano. Na inajulikana wazi kuwa ngamia hawezi kuingia kamwe katika tundu ya sindano! Na lilokusudiwa hapa ni jambo hili kuwa mustahili aingie Jannah kama vile ilivyokuwa mustahili ngamia aingie katika tundu ya sindano, kutokana na kufru zao na upotofu wao, ni mustahili kuingia Jannah bali wao wataingia motoni milele. Tunamuomba Allaah Al-‘Aafiyah.” [Fataawa Ibn Baaz]