043-Aayah Na Mafunzo: Waumini Kulipana Kisasi Na Kuondosheana Mafundo Ya Nyoyo Kabla Ya Kuingizwa Jannah Na Watashukuru Kuhidiwa Na Allaah
Aayah Na Mafunzo
Al-Araaf 43
043-Waumini Kulipana Kisasi Na Kuondosheana Mafundo Ya Nyoyo
Kabla Ya Kuingizwa Jannah
Na Watashukuru Kuhidiwa Na Allaah
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَنَزَعْنَا مَا فِي صُدُورِهِم مِّنْ غِلٍّ تَجْرِي مِن تَحْتِهِمُ الْأَنْهَارُ ۖ وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي هَدَانَا لِهَـٰذَا وَمَا كُنَّا لِنَهْتَدِيَ لَوْلَا أَنْ هَدَانَا اللَّـهُ ۖ لَقَدْ جَاءَتْ رُسُلُ رَبِّنَا بِالْحَقِّ ۖ وَنُودُوا أَن تِلْكُمُ الْجَنَّةُ أُورِثْتُمُوهَا بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٤٣﴾
Na Tutaondosha mizizi ya mafundo ya kinyongo yaliyomo vifuani mwao itapita chini yao mito. Na watasema: AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah), Ambaye Ametuongoza kwa haya, na tusingelikuwa wenye kuhidika kama Allaah Asingetuongoza. Kwa yakini wamekuja Rusuli wa Rabb wetu na haki. Na wataitwa (kuambiwa): Hii ndiyo Jannah mliyorithishwa kwa sababu ya yale mliyokuwa mnayatenda. [Al-A'raaf: 43]
Mafunzo:
Qantwarah Daraja Baina Ya Jannah Na Moto Ambalo Waumini Watalipana Kisasi Na Kuondoshewa Mafundo Na Vinyongo Baina Yao.
Amesimulia Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه) : Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Baada ya Waumini kuokolewa na moto, watazuiliwa wangojee katika Qantwarah (daraja) baina ya Jannah na moto. Kisha watahojiwa kuhusu dhulma zote walizotendeana duniani. Watakapotakaswa (madhambi yao kuhukumiwa) watapewa ruhusa kuingia Jannah. Naapa kwa Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake, kila mtu atatambua makazi yake Jannah kuliko anavyotambua makazi yake ya duniani.” [Al-Bukhaariy]
Shukurani Za Watu Kuingia Jannah Na Majuto Kuingia Motoni:
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) : Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Kila mmoja katika watu wa Jannah ataona sehemu yake ya kikao chake cha motoni atasema: Ingekuwa Allaah Hakunihidi! Basi itakuwa ndio shukurani yake. Na kila mtu wa motoni ataona sehemu yake ya kikao Jannah atasema: Ingekuwa Allaah Kanihidi! Basi huwa ndio majuto yake.” [An-Nasaaiy]