055-Aayah Na Mafunzo: Adabu Za Kuomba Du’aa: Kwa Unyenyekevu, Kwa Siri, Kwa Sauti Ndogo, Kwa Khofu Na Matumaini
Aayah Na Mafunzo
Al-A’raaf 55 Na 56
055-Miongoni Mwa Adabu Za Kuomba Du’aa: Kwa Unyenyekevu, Kwa Siri, Kwa Sauti Ndogo, Kwa Khofu Na Matumaini
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
ادْعُوا رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ ﴿٥٥﴾
Muombeni Rabb wenu kwa unyenyekevu na kwa siri, hakika Yeye Hapendi wenye kupindukia mipaka.
وَلَا تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ بَعْدَ إِصْلَاحِهَا وَادْعُوهُ خَوْفًا وَطَمَعًا ۚ إِنَّ رَحْمَتَ اللَّـهِ قَرِيبٌ مِّنَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٥٦﴾
Na wala msifanye ufisadi katika ardhi baada ya (Allaah) kuitengeneza sawa, na muombeni kwa khofu na matumaini. Hakika Rahmah ya Allaah iko karibu na wafanyao ihsaan. [Al-A’raaf: 55-56]
Mafunzo:
Miongoni Mwa Adabu Za Kuomba Du’aa:
Aayah hii Al-A’raaf (55) na inayofuatia (56) zimetajwa baadhi ya adabu za kuomba Du’aa nazo ni: Kuomba kwa unyenyekevu, kwa Siri, kwa sauti ndogo, kwa khofu na matumaini .
عَنْ أَبِي مُوسَى الأَشْعَرِيِّ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) قَالَ: كُنَّا مَعَ رَسُولِ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) فَكُنَّا إِذَا أَشْرَفْنَا عَلَى وَادٍ هَلَّلْنَا وَكَبَّرْنَا. ارْتَفَعَتْ أَصْوَاتُنَا فَقَالَ النَّبِيُّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم)َ: ((يَا أَيُّهَا النَّاسُ ارْبَعُوا عَلَى أَنْفُسِكُمْ فَإِنَّكُمْ لاَ تَدْعُونَ أَصَمَّ ولاَ غَائِبًا إِنَّهُ مَعَكُمْ ، إِنَّهُ سَمِيعٌ قَرِيبٌ تَبَارَكَ اسْمُهُ وَتَعَالَى جَدُّهُ))
Amesimulia Abu Muwsaa Al-Ash’ariyy (رضي الله عنه): Tulikuwa pamoja na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na tukawa kila tukipanda bonde, tunafanya tahliyl (Laa Ilaaha Illa-Allaah), na tunaleta takbiyr (Allaahu Akbar). Zikapanda sauti zetu, na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Enyi watu, zihurumieni nafsi zenu, kwani hamumwombi kiziwi wala asiyekuwepo, hakika Yeye Yupo nanyi (kwa Ujuzi Wake), hakika Yeye Ni Mwenye Kusikia yote, Yupo Karibu, Limebarikika Jina Lake na Umetukuka Ujalali Wake.” [Al-Bukhaariy]
Rejea pia tanbihi (2:186).