058-Aayah Na Mfunzo: Mfano Wa Uongofu Na ‘Ilmu Kulingana Na Ardhi Yenye Rutuba Na Isiyokuwa Na Rutuba
Aayah Na Mafunzo
Al-A’raaf 58
058-
Mfano Wa Uongofu Na ‘Ilmu Kulingana Na Ardhi Yenye RutubaNa Isiyokuwa Na Rutuba
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَالْبَلَدُ الطَّيِّبُ يَخْرُجُ نَبَاتُهُ بِإِذْنِ رَبِّهِ ۖ وَالَّذِي خَبُثَ لَا يَخْرُجُ إِلَّا نَكِدًا ۚ كَذَٰلِكَ نُصَرِّفُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَشْكُرُونَ ﴿٥٨﴾
Na nchi nzuri mimea yake hutoka kwa idhini ya Rabb wake. Na ile ambayo ni mbaya haitoki ila kwa uadimu. Hivyo ndivyo Tunavyosarifu namna kwa namna ishara na dalili kwa watu wanaoshukuru. [Al-A'raaf: 58]
Mafunzo:
Amesimulia Abuu Muwsaa Al-Ash-‘ariyy (رضي الله عنه) : Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mfano wa uongofu na ‘Ilmu ambayo Allaah Amenituma kufikisha ni kama mvua kubwa inayoanguka juu ya ardhi, baadhi yake (hufikia) katika ardhi yenye rutuba ikanyonya maji ya mvua na ikaleta mimea na majani kwa wingi. Na baadhi yake (ardhi) ikawa nzito na ikazuia maji ya mvua (kupenya katika ardhi), na Allaah Akawanemeesha watu kutokana nayo, na wakaitumia kwa kunywa, kunyweshea wanyama wao na kwa ajili ya umwagiliaji na kilimo kwenye ardhi hiyo. Na baadhi yake ikawa si yenye rutuba ambayo haikuweza kukamata maji wala kutoa mimea (hivyo ardhi hiyo haikutoa faida yoyote). (Ardhi) Ya mwanzo ni mfano wa mtu anayetambua Dini ya Allaah na akapata faida (kutokana na ‘Ilmu) ambayo Allaah Ameishusha kupitia kwangu (Manabii na ‘Ulamaa) na akaisomesha kwa wengine. (Ardhi) Ya mwisho ni mfano wa yule mtu asiyejali na hafuati Uongofu wa Allaah Alioushusha kupitia kwangu (Ni mfano wa hiyo ardhi isiyo na rutuba).” [Al-Bukhaariy]