172-Aayah Na Mafunzo: Ahadi Ya Alastu Waliyoahidiana Viumbe Na Allaah Katika Hali Ya Fitwrah Kumtii Na Kutokumshirikisha
Aayah Na Mafunzo
Al-A’raaf 172
172-Ahadi Ya Alastu Walioahidi Viumbe Kwa Allaah (سبحانه وتعالى) Kumtii
Na Kutokumshirikisha
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَإِذْ أَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِي آدَمَ مِن ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَأَشْهَدَهُمْ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ أَلَسْتُ بِرَبِّكُمْ ۖ قَالُوا بَلَىٰ ۛ شَهِدْنَا ۛ أَن تَقُولُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَـٰذَا غَافِلِينَ ﴿١٧٢﴾
Na pindi Rabb wako Alipowaleta wana wa Aadam kutoka migongoni mwao kizazi chao, Akawashuhudisha juu ya nafsi zao, Je, Mimi siye Rabb wenu? Wakasema: Ndio bila shaka, tumeshuhudia! (Allaah Akawaambia): Msije kusema Siku ya Qiyaamah: hakika sisi tulikuwa tumeghafilika nayo haya.
أَوْ تَقُولُوا إِنَّمَا أَشْرَكَ آبَاؤُنَا مِن قَبْلُ وَكُنَّا ذُرِّيَّةً مِّن بَعْدِهِمْ ۖ أَفَتُهْلِكُنَا بِمَا فَعَلَ الْمُبْطِلُونَ ﴿١٧٣﴾
Au mkasema: Hakika baba zetu ndio walioshirikisha kabla, nasi tulikuwa kizazi baada yao. Basi Utatuangamiza kwa yale waliyoyafanya wabatilifu? [Al-A'raaf: 172-173]
Mafunzo:
Ahadi ya “Alastu” ni ile ambayo viumbe vyote viliahidi kwa Allaah (سبحانه وتعالى) kutokumshirikisha na kumtii Amri Zake. Ahadi hiyo waliichukua viumbe kabla ya kuzaliwa kwao wakati roho zao zimeshaumbwa. Kwa kuwa kuna uhai miwili na mauti mawili kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى) katika Swurah Ghaafir 40:10-11) na (Al-Baqarah 2:28):
كَيْفَ تَكْفُرُونَ بِاللَّـهِ وَكُنتُمْ أَمْوَاتًا فَأَحْيَاكُمْ ۖ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يُحْيِيكُمْ ثُمَّ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٢٨﴾
Vipi mnamkufuru Allaah na hali mlikuwa wafu Akakuhuisheni, kisha Atakufisheni, kisha Atakuhuisheni, kisha Kwake mtarejeshwa [Al-Baqarah (2: 28)]
Na pia:
قَالُوا رَبَّنَا أَمَتَّنَا اثْنَتَيْنِ وَأَحْيَيْتَنَا اثْنَتَيْنِ فَاعْتَرَفْنَا بِذُنُوبِنَا فَهَلْ إِلَىٰ خُرُوجٍ مِّن سَبِيلٍ﴿١١﴾
Watasema: Rabb wetu! Umetufisha mara mbili na Umetuhuisha mara mbili, na tumekiri madhambi yetu. Basi je, kuna njia ya kutoka? [Ghaafir: 11]
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) : Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakuna kizazi kinachozaliwa (mtoto mchanga) isipokuwa anazaliwa katika 'fitwrah' kisha wazazi wake (humbadilisha na) humuingiza katika dini ya Uyahudi, au Unaswara au Umajusi, kama mfano mnyama mwenye pembe anavyomzaa mnyama mwenye pembe kama yeye, je, mtahisi kuwa hana pembe?” Kisha Abuu Hurayrah akasema: Someni mkipenda: (Kauli ya Allaah):
ۚ فِطْرَتَ اللَّـهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا ۚ لَا تَبْدِيلَ لِخَلْقِ اللَّـهِ ۚ
(Shikamana na) Umbile la asili la kumpwekesha Allaah Alilowaumbia watu. Hakuna kubadilisha Uumbaji wa Allaah. (Ar-Ruwm 30:30). [Al-Bukhaariy na Muslim]
Maana ya Fitwrah: Umbile la asili la Tawhiyd (Kumpwekesha Allaah bila ya kumshirikisha). Ahadi hiyo waliahidi viumbe kabla ya kuzalilwa kwao.
Rejea pia Ar-Ruwm (30:30)