09-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo:Swawm Na Qur-aan Zitamuombea Mja Ash-Shafaa’ah Siku Ya Qiyaamah

 

Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo

 

09-Swawm Na Qur-aan Zitamuombea Mja Ash-Shafaa’ah Siku Ya Qiyaamah

 

 

 

وعَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ : ((الصِّيَامُ وَالْقُرْآنُ يَشْفَعَانِ لِلْعَبْدِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ يَقُولُ الصِّيَامُ أَيْ رَبِّ مَنَعْتُهُ الطَّعَامَ وَالشَّهَوَاتِ بِالنَّهَارِ فَشَفِّعْنِي فِيهِ وَيَقُولُ الْقُرْآنُ مَنَعْتُهُ النَّوْمَ بِاللَّيْلِ فَشَفِّعْنِي فِيهِ قَالَ فَيُشَفَّعَانِ))  

Imepokelewa toka kwa Abdullaah bin ‘Amr (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Swiyaam na Qur-aan zitamwombea shafaa’ah (uombezi) mja Siku ya Qiyaamah. Swawm itasema: “Nilimzuia chakula na matamanio yake mchana, basi Niwezeshe nimwombee shafaa’ah. Na Qur-aan itasema: Nilimzuia usingizi usiku, basi Niwezeshe nimwombee shafaa’ah. Akasema, basi vitaomba shafaa’ah)) [Ahmad ni Hadiyth Swahiyh taz Swahiyh Al-Jaami’ (3882)]

 

 

Mafunzo:

 

Mwenye Swawm anatakiwa akithirishe kusoma Qur-aan Tukufu katika masiku haya ya barakah na hususan usiku kwa mujibu wa Hadiyth hii tukufu ambapo Qur-aan wakati inalilia shafaa’ah (uombezi) toka kwa Allaah ('Azza wa Jalla) inaeleza: “Nilikuwa nikimzuia asilale usingizi usiku. Alikuwa halali kwa ajili ya kunisoma mimi.”  Na hii ni pengine kwa kuwa Qur-aan yenyewe iliteremshwa wakati wa usiku, usiku wa Laylatul-Qadr ambao ‘amali zake ni bora kuliko za miezi 1000. Mtu anaposoma Qur-aan usiku, tadaburi yake inakuwa ni kubwa zaidi, na moyo unakuwa umetulia kwa kuwa akili yake haishughulishwi na jambo lolote kinyume na mchana wakati wa pilikapilika nyingi za kutafuta riziki.

 

 

Imethibiti kwamba Jibriyl ('Alayhis-Salaam) alikuwa akikutana na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kila usiku wa Ramadhwaan na kumsomesha Qur-aan Tukufu.

 

 

‏ ‏عَنْ ‏ ‏ابْنِ عَبَّاسٍ ‏ ‏قَالَ ‏ ‏كَانَ رَسُولُ اللَّهِ ‏ ‏صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ‏ ‏أَجْوَدَ النَّاسِ وَكَانَ أَجْوَدُ مَا يَكُونُ فِي رَمَضَانَ حِينَ يَلْقَاهُ ‏ ‏جِبْرِيلُ ‏ ‏وَكَانَ يَلْقَاهُ فِي كُلِّ لَيْلَةٍ مِنْ رَمَضَانَ فَيُدَارِسُهُ الْقُرْآنَ  

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abaaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni mbora (mwenye matendo mema) wa watu, lakini alikuwa mbora  zaidi katika Ramadhwaan kwa sababu Jibriyl alikuwa akimjia kila usiku wa Ramadhwaan akimfundisha Qur-aan))  [Al-Bukhaariy]  

 

Na tukio hili linatufidisha kuwa inapendeza kusoma zaidi Qur-aan, kuifasiri na kuisomesha kama inavyofanyika kwenye Misikiti yetu mingi.

 

Ash-Shafaa’ah ni nini?

 

Shafaa’ah ni mtu kumwombea mtu mwingine apatiwe manufaa au aondoshewe adhabu.

 

Na shafaa’ah iliyothibiti inagawanyika vigawanyo viwili:

 

Ya kwanza ni Shafaa’ah jumuishi, na hii ni ile ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atawapa idhini baadhi ya waja Wake wema Awatakao kuwaombea wengine. Shafaa’ah hii watapewa Manabii, Wasadikishaji, Mashuhadaa na watu wema. Hawa watawaombea shafaa’ah Waislamu walioko motoni ili watolewe toka humo.

 

 

Ya pili ni shafaa’ah mahsusi kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Shafaa’ah hii ijulikanayo kama الشفاعة العظمى ni ile ambayo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ataiomba ili mambo yafunguke kutokana na hali ngumu kabisa ya kisimamo cha Siku ya Qiyaamah. Na hii ni baada ya watu kwenda kwa Manabii Aadam, Nuwh, Ibraahiym, Muwsaa na Iysas (‘Alayhimus-salaam) ili wamwombe Allaah ('Azza wa Jalla) mambo yafunguke, na wote hao wakatoa nyudhuru. Kisha wataelekea kwa kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) naye atasujudu, na atamwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) mambo yafunguke, nayo yatafunguka. Hadiyth kama ilivyokuja ni ifuatayo:

 

عَنْ أَنَسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ:  يَجْتَمِعُ الْمُؤْمِنُونَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فَيَقُولُونَ: لَوْ اسْتَشْفَعْنَا إِلَى رَبِّنَا،  فَيَأْتُونَ آدَمَ فَيَقُولُونَ: أَنْتَ أَبُو النَّاسِ خَلَقَكَ اللَّهُ بِيَدِهِ وَأَسْجَدَ لَكَ مَلَائِكَتَهُ وَعَلَّمَكَ أَسْمَاءَ كُلِّ شَيْءٍ فَاشْفَعْ لَنَا عِنْدَ رَبِّكَ حَتَّى يُرِيحَنَا مِنْ مَكَانِنَا هَذَا.  فَيَقُولُ: لَسْتُ هُنَاكُمْ وَيَذْكُرُ ذَنْبَهُ فَيَسْتَحِي ، ائْتُوا نُوحًا فَإِنَّهُ أَوَّلُ رَسُولٍ بَعَثَهُ اللَّهُ إِلَى أَهْلِ الْأَرْضِ،   فَيَأْتُونَهُ فَيَقُولُ لَسْتُ هُنَاكُمْ وَيَذْكُرُ سُؤَالَهُ رَبَّهُ مَا لَيْسَ لَهُ بِهِ عِلْمٌ. فَيَسْتَحِي فَيَقُولُ: ائْتُوا خَلِيلَ الرَّحْمَنِ فَيَأْتُونَهُ فَيَقُولُ: لَسْتُ هُنَاكُمْ،  ائْتُوا مُوسَى عَبْدًا كَلَّمَهُ اللَّهُ وَأَعْطَاهُ التَّوْرَاةَ.  فَيَأْتُونَهُ فَيَقُولُ: لَسْتُ هُنَاكُمْ وَيَذْكُرُ قَتْلَ النَّفْسِ بِغَيْرِ نَفْسٍ فَيَسْتَحِي مِنْ رَبِّهِ فَيَقُولُ: ائْتُوا عِيسَى عَبْدَ اللَّهِ وَرَسُولَهُ وَكَلِمَةَ اللَّهِ وَرُوحَهُ فَيَقُولُ: لَسْتُ هُنَاكُمْ ،  ائْتُوا مُحَمَّدًا صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَبْدًا غَفَرَ اللَّهُ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ وَمَا تَأَخَّرَ،  فَيَأْتُونِي،  فَأَنْطَلِقُ حَتَّى أَسْتَأْذِنَ عَلَى رَبِّي فَيُؤْذَنَ لِي ،  فَإِذَا رَأَيْتُ رَبِّي وَقَعْتُ سَاجِدًا فَيَدَعُنِي مَا شَاءَ اللَّهُ ثُمَّ يُقَالُ: ارْفَعْ رَأْسَكَ وَسَلْ تُعْطَهْ،  وَقُلْ يُسْمَعْ   وَاشْفَعْ تُشَفَّعْ،  فَأَرْفَعُ رَأْسِي فَأَحْمَدُهُ بِتَحْمِيدٍ يُعَلِّمُنِيهِ ثُمَّ أَشْفَعُ فَيَحُدُّ لِي حَدًّا فَأُدْخِلُهُمْ الْجَنَّةَ.  ثُمَّ أَعُودُ إِلَيْهِ فَإِذَا رَأَيْتُ رَبِّي مِثْلَهُ ثُمَّ أَشْفَعُ فَيَحُدُّ لِي حَدًّا فَأُدْخِلُهُمْ الْجَنَّةَ.  ثُمَّ أَعُودُ الرَّابِعَةَ فَأَقُولُ: مَا بَقِيَ فِي النَّارِ إِلَّا مَنْ حَبَسَهُ الْقُرْآنُ وَوَجَبَ عَلَيْهِ الْخُلُودُ)) البخاري،  مسلم، مالك،    الترمذي وابن ماجه

 Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Watakusanyika Waumini Siku ya Qiyaamah na Watasema: Lau tungetafuta kuombewa shafaa’ah kwa Rabb wetu! Watakwenda kwa Aadam na watasema: Wewe ndio baba wa watu, Amekuumba Allaah kwa Mkono Wake na Akaamrisha Malaika wakusujudie, na Akakufundisha majina ya vitu vyote, basi tuombee kwa Rabb wako ili Atupe faraja kutokana na sehemu yetu hii? Atasema: Mimi siwezi kufanya mnaloomba! Na atakumbuka makosa yake na ataona hayaa, atasema: Mfuateni Nuwh, hakika yeye ndiye Rasuli wa kwanza Aliyemtuma Allaah kwa watu ardhini. Watamfuata. Naye atasema: Siwezi kufanya mnaloomba! Na atakumbuka kumuomba kwake Allaah kwa jambo asilokuwa na ujuzi nalo.  Naye ataona hayaa na atasema: Nendeni kwa Khaliylur-Rahmaan. Watakwenda kwa Ibraahiym. Naye atawaambia: Siwezi kufanya mnaloomba! Nendeni kwa Muwsaa mja ambaye Allaah Alizungumza naye na Akampa Tawraat. Muwsaa atasema: Siwezi kufanya mnaloomba!  Atakumbuka kuwa aliwahi kumuua mtu bila ya haki na ataona hayaa kwa Rabb wake.  Atasema: Nendeni kwa ‘Iysaa kwani ni mja wa Allaah na Rasuli Wake na neno Lake na Roho Yake. Naye atasema: Siwezi kufanya mnaloomba! Nendeni kwa Muhammad, ni mja aliyefutiwa makosa yaliyotangulia na yajayo. Watakuja kwangu na nitakwenda kwa Rabb wangu kumuomba idhini (ya maombi), nitapewa idhini. Nitakapomuona Rabb wangu nitasujudu na Ataniacha hivyo hivyo mpaka Atakavyo. Kisha itasemwa: Inua kichwa chako na omba utapewa! Na sema yatasikilizwa (uyasemayo)! Na omba shafaa‘ah utapewa! Nitainua kichwa changu na nitamhimidi kwa Himdi Zake Atakazonifundisha, kisha nitaomba na Atanikubalia idadi kubwa ya watu, nitawaingiza Jannah. Kisha nitarudi tena Kwake. Nitakapomuona Rabb wangu, nitafanya kama mara ya kwanza, kisha nitaomba na Atanikubalia idadi kubwa ya watu nitawaingiza Jannah. Kisha nitarejea mara ya tatu, kisha nitarudi mara ya nne kisha nitasema: Hakuna watu waliobakia motoni isipokuwa Qur-aan imewazuia na watawajibika kubakia humo.” [Al-Bukhaariy, Muslim, Maalik, At-Tirmidhiy na Ibn Maajah]

 

 

Na hii ndio ijulikanayo kama المقام المحمود ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amemwahidi Aliposema:

 

وَمِنَ اللَّيْلِ فَتَهَجَّدْ بِهِ نَافِلَةً لَّكَ عَسَىٰ أَن يَبْعَثَكَ رَبُّكَ مَقَامًا مَّحْمُودًا ﴿٧٩﴾

Na katika usiku, amka uswali (tahajjud) kuisoma (Qur-aan); ni ziada ya Sunnah kwako Asaa Rabb wako Akakuinua cheo kinachosifika. [Al-Israa: 79]

 

 

 

 

Share