10-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo: Du’aa Ya Mwenye Swawm Hairejeshwi

 

Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo

 

10-Du’aa Ya Mwenye Swawm Hairejeshwi

 

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ قَالَ قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((ثَلاثَةٌ لا تُرَدُّ دَعْوَتُهُمْ الإِمَامُ الْعَادِلُ وَالصَّائِمُ حِينَ يُفْطِرُ وَدَعْوَةُ الْمَظْلُومِ )) 

Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  akisema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: ((Watatu du’aa zao hazirejeshwi: Imaam (kiongozi)  mtenda haki, mwenye Swawm wakati anapofungua, na du’aa ya aliyedhulumiwa)) [Imesimuliwa na At-Tirmidhiy Hadiyth nambari (2525), na Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Swahihy At-Tirmidhiy Hadiyth nambari (2050)]

 

 

Mafunzo:

 

 

Hadiyth hii tukufu ni dalili ya kuwa mwenye Swawm anatakiwa akitumie kitambo cha wakati wa kufungua Swawm yake kwa kuomba du’aa ya kheri, kwani wakati huo du’aa hujibiwa.

 

 

Bora zaidi cha kusema wakati huo ni yale yaliyopokelewa na ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) aliyesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alikuwa anapofungua Swawm alikuwa Anasema:

(( ذَهَبَ الظَّمَأُ وَابْتَلَّتْ الْعُرُوقُ وَثَبَتَ الأَجْرُ إِنْ شَاءَ اللَّهُ )) 

((Kiu kimeondoka, mishipa imelowana, na ujira umethibiti In Shaa Allaah)). [Imesimuliwa na Abuu Daawuwd (2357). Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Hasan katika Swahiyh Abiy Daawuwd (2066)]

 

 

Hivyo basi, mwenye Swawm anapoomba wakati huu, anatakikana ahudhurishe moyo wake na awe na yakini kwamba Allaah ('Azza wa Jalla)  Atamwitikia du’aa yake hiyo, kwani huo ni wakati wa udhalili na unyenyekevu mkubwa Kwake Subhaanahu wa Ta’aalaa. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Hadiyth nyingine:

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ ، قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وسلم: ((إِنَّ لِلَّهِ تَبَارَكَ وَتَعَالَى عُتَقَاءَ فِي كُلِّ يَوْمٍ وَلَيْلَةٍ)) يَعْنِي: فِي َمَضَانَ وَإِنَّ لِكُلِّ مُسْلِمٍ فِي كُلِّ يَوْمٍ وَلَيْلَةٍ دَعْوَةً مُسْتَجَابَةً)) 

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Ana watu wa kuwaacha huru na moto kila siku na usiku, na kila mja kati yao ana dua inayojibiwa)) [Imesimuliwa na Ahmad (7401). Na Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Swahihy Al-Jaami’i (2169), Swahiyh At-Targhiyb Wat-Tarhiyb (1002)]

 

 

Na kwa vile hilo la kuachwa huru limethibitishwa na Hadiyth hii, inakuwa ni vizuri zaidi pia mfungaji Swawm aombe kuachwa huru na moto, kwani hakuna mafanikio makubwa kama mtu kuwekwa mbali na moto wa Jahannam.

 

 

Hivyo basi, atakayemwomba Mola wake wakati huo wa kufungua swawm yake kwa moyo safi na maombi halali ya ki-Shariy’ah, na wala kisiwepo kizuizi cha kukubaliwa du’aa kama mlo wa haramu na kadhalika, mbali na kuwa ni mwenye kuwajibika kwa maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake,  basi Allaah ('Azza wa Jalla)  Huijibu du’aa yake moja kwa moja.

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametaja kuhusu kuomba ‘duaa mubashara baada ya Aayah za kuhusu Ramadhwaan na Swiyaam, kwamba Anamtaqabalia mja Wake pindi anapomuomba du’aa ikiwa atamwamini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama Anavyosema:

 

 

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ ﴿١٨٦﴾

Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu (kwa ujuzi); Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [Al-Baqarah: 186]

 

 

Kingine anachotakiwa mfungaji wa Swawm kushikamana nacho wakati wa swawm yake, ni kukithirisha kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika kipindi chote cha mchana, kwani swawm humfanya awe karibu zaidi na Allaah ('Azza wa Jalla) na wakati anapokuja kumwomba wakati wa kufungua Swawm, Allaah (‘Azza wa Jalla) Anakuwa Ashajikurubisha zaidi naye.

 

 

 

 

 

 

 

 

Share