14-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo: Thawabu Za Kumfuturisha Mwenye Swawm

 

Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo

 

14-Thawabu Za Kumfuturisha Mwenye Swawm

 

 

 

 

عن زيد بن خالد رضي الله عنه قال: قال رسول  صلى الله عليه وسلم: ((مَنْ فَطَّرَ صَائِمًا كَانَ لَهُ مِثْلُ أَجْرِهِ غَيْرَ أَنَّهُ لَا يَنْقُصُ مِنْ أَجْرِ الصَّائِمِ شَيْئًا )) أخرجه أحمد والنسائي وصححه الألبان

Imepokelewa kutoka kwa Zayd bin Khaalid (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallaam) amesema: ((Atakayemfuturisha aliyefunga atapata ujira (wa Swawm) kama ujira wake bila ya kupungua chochote katika ujira wa yule aliyefunga)) [Ahmad, An-Nasaaiy – Ameipa daraja ya Swahiyh Shaykh Al-Albaaniy]

 

 

Mafunzo:

 

 

Hadiyth hii inatuonyesha fadhila ya kumfuturisha mwenye Swawm na ujira mkubwa unaopatikana ambao ni sawa na mfungaji anayefuturishwa. Jambo hili waliLlaahil-Hamd linafanywa na Waislamu wengi wenye uwezo. Kuna baadhi yao huleta vyakula vya futari Misikitini ikiwa ni pamoja na mlo kamili kwa ajili ya wenye kuswali. Kuna wengine huleta na kugawa tende kwa wafungaji, na kuna wengine hata maji tu, kila mtu kwa mujibu wa uwezo wake na hali yake.

 

 

Isitoshe, kuna ada nzuri iliyotanda kwenye baadhi ya nchi zetu. Majirani hupelekeana futari kila mtu kwa mujibu wa kile alichokiandaa angalau kidogo. Kwa ada hii, utakuta majirani hupata futari za aina tofauti tofauti, na hili bila shaka linazidisha mapenzi na roho ya ushirikiano zaidi kati ya majirani. Na hapa kila mmoja hujipatia fungu lake la thawabu bila kumpunguzia thawabu mwingine.

 

Kufuturisha kunakuwa pia vile vile kwa njia ya kutoa pesa, au kuwagaiwa wafungaji vifurushi vya unga, sukari, mafuta, tambi na kadhalika kama inavyofanyika katika baadhi ya nchi. Katika baadhi ya nchi pia, utakuta watu wanazunguka na magari yao wakati wa kabla ya adhana ya Swalaah ya Magharib, wakiwatafuta walio majiani ambao wamechelewa kufika majumbani mwao, na kuwagaiwa milo ya futari iliyofungwa vizuri.

 

Katika nchi nyingine, kuna matajiri ambao huweka mahema ya kuwafuturisha wafungaji kwa muda wa mwezi mzima, na futari huwa ni ya hali ya juu inayomfanya aliyefuturishwa kutoka hapo akiwa ameridhika kabisa. Hili ni jambo la kushukuriwa na kuombewa du’aa.

 

Haya yote yanaingia ndani ya wigo huu wa kheri ambao Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ndio mtoaji zaidi kuliko miezi mingine yote.

 

Na huenda kinachowapa chachu Waislamu kuwa na pupa ya kuwafuturisha nduguzo Waislamu, ni pale wanapoikumbuka neema ya Allaah ('Azza wa Jalla)  kwao ya kumiliki hicho wanachokitoa kwa nduguzo katika mwezi huu wa kheri na Baraka, na kuwezeshwa kufunga.

 

Kukutana Swawm na kulisha masikini kunakuwa na msukumo zaidi kwa Mwislamu kufutiwa makosa yake na kulindwa na moto wa Jahannam likiongezewa hili na Qiyaamul-Layl (kisimamo cha usiku kuswali). Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Mu’aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu 'anhu):

 

أَلَا أَدُلُّكَ عَلَى أَبْوَابِ الْخَيْرِ ؟ الصَّوْمُ جُنَّةٌ، وَالصَّدَقَةُ تُطْفِئُ الْخَطِيئَةَ كَمَا يُطْفِئُ الْمَاءُ النَّارَ، وَصَلَاةُ الرَّجُلِ فِي جَوْفِ اللَّيْلِ، ثُمَّ تَلَا: ((تَتَجَافَى جُنُوبُهُمْ عَنْ الْمَضَاجِعِ...))  حَتَّى بَلَغَ  ((يَعْمَلُونَ))

((Je, nikuonyeshe milango ya kheri? Swawm ni kinga, Swadaqah inazima makosa kama maji yanavyozima moto, na Swalaah ya mtu usiku mpevu)). Kisha akasoma:   

 تَتَجَافَىٰ جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ  

Mbavu zao zinatengana na vitanda …. Mpaka akafikia:

  يَعْمَلُونَ  

wakiyatenda.     [Imesimuliwa na At Tirmidhiy. Amesema ni Hadiyth Hasan – Aayah ni Suwrah As-Sajdah: 16-17]

 

 

Cha muhimu zaidi kuchunga katika ‘amali hii ya kheri ya kuwafuturisha wafungaji, ni kujiepusha na ufujaji, israfu na riyaa. Chakula kipikwe kwa mujibu wa idadi ya watu, na ikiwa kitabaki basi kihifadhiwe na kitumike siku inayofuatia. Allaah ('Azza wa Jalla) Anatuambia:

 

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ ﴿٣١﴾

Na kuleni na kunyweni; na wala msifanye israfu. Hakika Yeye (Allaah) Hapendi wanaofanya israfu [Al-A’raaf: 31]

 

 

Anatuambia tena:

 

إِنَّ الْمُبَذِّرِينَ كَانُوا إِخْوَانَ الشَّيَاطِينِ ۖ وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِرَبِّهِ كَفُورًا ﴿٢٧﴾

Hakika wabadhirifu wamekuwa ni ndugu wa mashaytwaan, na shaytwaan amekuwa ni mwingi wa kumkufuru Rabb wake.  [Al-Israa: 27]

 

 

 

 

 

Share