15-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo: Fadhila Za Swalaah Ya Taraawiyh
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
15-Fadhila Za Swalaah Ya Taraawiyh
عَنْ أَبِي سَلَمَةَ بْنِ عَبْدِ الرَّحْمَنِ ، أَنَّهُ سَأَلَ عَائِشَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا : كَيْفَ كَانَتْ صَلاَةُ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي رَمَضَانَ ؟ قَالَتْ : " مَا كَانَ يَزِيدُ فِي رَمَضَانَ وَلاَ فِي غَيْرِهِ عَلَى إِحْدَى عَشْرَةَ رَكْعَةً ، يُصَلِّي أَرْبَعَ رَكَعَاتٍ ، فَلاَ تَسْأَلْ عَنْ حُسْنِهِنَّ وَطُولِهِنَّ ، ثُمَّ يُصَلِّي أَرْبَعًا ، فَلاَ تَسْأَلْ عَنْ حُسْنِهِنَّ وَطُولِهِنَّ ، ثُمَّ يُصَلِّي ثَلاَثًا ، فَقُلْتُ : يَا رَسُولَ اللَّهِ تَنَامُ قَبْلَ أَنْ تُوتِرَ؟ قَالَ : ( تَنَامُ عَيْنِي وَلاَ يَنَامُ قَلْبِي ) .
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Salamah bin ‘Abdir-Rahmaan (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba kamuuliza ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa): Vipi ilikuwa Swalaah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Ramadhwaan? Akasema: “Hakuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akizidisha katika Ramadhwaan wala katika miezi mingineyo zaidi ya rakaa kumi na moja. Anaswali nne, usiulize umakinifu na urefu wa rakaa hizo. Kisha anaswali nne, usiulize umakinifu na urefu wa rakaa hizo, halafu anaswali tatu)) [Al-Bukhaariy, Muslim]
Mafunzo:
Swalaah ya Taraawiyh ni Swalaah inayoswaliwa kwa jamaa katika mwezi wa Ramadhwaan. Inaweza pia kuswaliwa na mtu peke kama hakupata nafasi ya kuswali jamaa na wenzake.
Imeitwa kwa jina hili la Taraawiyh kutokana na neno ترويحة ambalo wingi wake ni تراويح , kwa kuwa Maswahaba walikuwa wakipumzika kidogo kati ya kila tasliym mbili, yaani kila baada ya rakaa nne.
Na kwa mujibu wa Hadiyth hii ya Mama wa Waumini‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa), ni kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali rakaa kumi na moja tu. Lakini kitendo hiki cha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakidulishi kuwa ni lazima ziwe rakaa hizo hizo kumi na moja, bali zinaweza kupungua chini ya hapo kwa mujibu wa hali ya mtu, au zikazidi kwa mujibu wa nguvu na utashi wa mwenye kuiswali. Anaweza kuswali rakaa 36 kama ilivyo kwa dhehebu la Imaam Maalik.
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Taraawiyh jamaa na Maswahaba wake kwa muda wa siku tatu tu. Haya yanaelezwa na Mama wa Wuamini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) aliposema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Msikitini. Watu wengi wakaswali pamoja naye. Kisha akaswali usiku uliofuata, na watu wakazidi kuwa wengi zaidi. Kisha usiku wa tatu walijumuika, lakini yeye hakutoka kuswali nao. Asubuhi ilipopambazuka aliwaambia: ((Niliona mlichokifanya. Hakuna kilichonizuia kutoka niwajieni isipokuwa nilichelea kufaradhiwa juu yenu)) [Al-Bukhaariy]
Na baada ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kufariki, ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliifufua Sunnah hii.
Imepokelewa toka kwa Abdur-Rahmaan bin Abdil-Qaariy akisema: “Nilitoka pamoja na ‘Umar bin Al–Khattwaab usiku mmoja wa Ramadhwaan kwenda Msikitini. Tukakuta watu wamezagaa wakiswali. Mwingine anaswali peke yake, na mwingine anaswali na watu kidogo. Umar akasema: “Naona ingelikuwa bora zaidi kama ningeliwakusanya hawa wakaswalishwa na Imaam mmoja.” Halafu akaazimia na akawakusanya waswalishwe na Ubayya bin Ka’ab. Kisha nikatoka naye usiku mwingine, na watu wanaswalishwa na Imaam mmoja. Umar akasema: “Bid‘ah njema hii.”
Makusudio ya bid‘ah hapa kwa mujibu wa kauli ya ‘Umar, ni bid‘ah ya kilugha na si bid‘ah ya kiistilahi. Ni Sunnah aliyoiasisi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kisha ‘Umar akaifufua. Anatuambia:
عَلَيْكُمْ بِسُنَّتِي وَسُنَّةِ الْخُلَفَاءِ الرَّاشِدِينَ الْمَهْدِيِّينَ عَضُّوا عَلَيْهَا بِالنَّوَاجِذِ وَإِيَّاكُمْ وَمُحْدَثَاتِ الأُمُورِ فَإِنَّ كُلَّ بِدْعَةٌ ضَلاَلَةٌ)) رواه أبو داوود والترمذي وقال حديث حسن صحيح
(Shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa waongofu, waliohidika zishikilieni kwa magego [mambo yao]. Na tahadharini na mambo yenye kuzushwa, kwani kila uzushi ni upotovu)) [Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy, na amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh].
Swalaah hii ya Taraawiyh Waislamu wengi hufanya pupa ya kuiswali. Lakini baadhi yao, huiswali kwa spidi ya hali ya juu bila khushuw’ (utulivu, unyenyekevu) wala khudhwu’ (utiifu, kujisalimisha kikamilifu kiakili na moyo) almuradi kumaliza. Hawa wana hatari ya kukosa thawabu kubwa na kukosa mafanikio Aliyoyagusia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) yatokanayo na khushuw’ na khudhuw’ ndani ya Swalaah. Anatuambia:
قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١﴾
Kwa yakini wamefaulu Waumini.
الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ ﴿٢﴾
Ambao katika Swalaah zao huwa wananyenyekea. [Al-Muuminuwn: 1-2]