10-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Swalaah: Mlango Wa Swalaah Ya Jamaa Na Uimaamu
بُلُوغُ الْمَرام
Buluwgh Al-Maraam
كِتَابُ اَلصَّلَاةِ
Kitabu Cha Swalaah
بَابُ صَلَاةِ اَلْجَمَاعَةِ وَالْإِمَامَةِ
10- Mlango Wa Swalaah Ya Jamaa Na Uimaamu1
315.
عَنْ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا; أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {صَلَاةُ اَلْجَمَاعَةِ أَفْضَلُ مِنْ صَلَاةِ اَلْفَذِّ بِسَبْعٍ وَعِشْرِينَ دَرَجَةً} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
وَلَهُمَا عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ: {بِخَمْسٍ وَعِشْرِينَ جُزْءًا}
وَكَذَا لِلْبُخَارِيِّ: عَنْ أَبِي سَعِيدٍ، وَقَالَ: "دَرَجَةً "
Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Swalaah ya Jamaa ina fadhila zaidi kuliko ya peke yake kwa daraja ishirini na saba[1].” [Al-Bukhaariy, Muslim]
Nao (Al-Bukhaariy na Muslim) tena wamepokea Hadiyth ya Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ): “Kwa mafungu ishirini na tano.”
Kadhalika Al-Bukhaariy amepokea Hadiyth ya Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy, amesema: “...daraja…”
316.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {وَاَلَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَقَدْ هَمَمْتُ أَنْ آمُرَ بِحَطَبٍ فَيُحْتَطَبَ، ثُمَّ آمُرَ بِالصَّلَاةِ فَيُؤَذَّنَ لَهَا، ثُمَّ آمُرَ رَجُلًا فَيَؤُمَّ اَلنَّاسَ، ثُمَّ أُخَالِفُ إِلَى رِجَالٍ لَا يَشْهَدُونَ اَلصَّلَاةَ، فَأُحَرِّقَ عَلَيْهِمْ بُيُوتَهُمْ، وَاَلَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَوْ يَعْلَمُ أَحَدُهُمْ أَنَّهُ يَجِدُ عَرْقًا سَمِينًا أَوْ مِرْمَاتَيْنِ حَسَنَتَيْنِ لَشَهِدَ اَلْعِشَاءَ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ وَاللَّفْظُ لِلْبُخَارِيِّ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Naapa kwa Ambaye nafsi yangu imo Mkononi Mwake, nimetamani kuamuru kukusanywa kuni, kisha kuamrisha kwa Swalaah kuadhiniwe, kisha nimuamrishe mtu mmoja aongoze watu, kisha niwaendee watu wasiohudhuria Swalaah nichome[2] nyumba zao. Naapa kwa Ambaye Nafsi yangu ipo Mikononi Mwake, angejua mmoja wao atapata mfupa ulionona au miguu mizuri ya kondoo angehudhuria Swalaah ya ‘Ishaa.” [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Al-Bukhaariy]
317.
وَعَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم { أَثْقَلُ اَلصَّلَاةِ عَلَى اَلْمُنَافِقِينَ: صَلَاةُ اَلْعِشَاءِ، وَصَلَاةُ اَلْفَجْرِ، وَلَوْ يَعْلَمُونَ مَا فِيهِمَا لَأَتَوْهُمَا وَلَوْ حَبْوًا} مُتَّفَقٌ عَلَيْه
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) tena amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Swalaah nzito zaidi kwa wanafiki[3] ni ‘Ishaa na Alfajiri, na laiti wangalijua yaliyomo humo, wangeziendea, hata kwa kutambaa kwa magoti.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
318.
وَعَنْهُ قَالَ: {أَتَى اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم رَجُلٌ أَعْمَى فَقَالَ: يَا رَسُولَ اَللَّهِ! لَيْسَ لِي قَائِدٌ يَقُودُنِي إِلَى اَلْمَسْجِدِ، فَرَخَّصَ لَهُ، فَلَمَّا وَلَّى دَعَاهُ، فَقَالَ: "هَلْ تَسْمَعُ اَلنِّدَاءَ بِالصَّلَاةِ؟" قَالَ: نَعَمْ. قَالَ: "فَأَجِبْ"} رَوَاهُ مُسْلِم
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema tena: “Mtu kipofu[4] alikuja kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Mimi sina mwongozaji anayeniongoza Msikitini. Na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akamruhusu (kuswali nyumbani). Kisha mtu yule alipogeuka kwenda zake Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimuuliza: “Je, unaisikia Adhana?” Akasema: “Ndiyo.” Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akamuambia: “Basi itikia.” [Imetolewa na Muslim]
319.
وَعَنْ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا، عَنْ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {مَنْ سَمِعَ اَلنِّدَاءَ فَلَمْ يَأْتِ فَلَا صَلَاةَ لَهُ إِلَّا مِنْ عُذْرٍ} رَوَاهُ اِبْنُ مَاجَهْ، وَاَلدَّارَقُطْنِيُّ، وَابْنُ حِبَّانَ، وَالْحَاكِمُ، وَإِسْنَادُهُ عَلَى شَرْطِ مُسْلِمٍ، لَكِنْ رَجَّحَ بَعْضُهُمْ وَقْفَه
Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mwenye kusikia[5] Adhana asije, hana Swalaah isipokuwa kwa udhuru.” [Imetolewa na Ibn Maajah, Ad-Daaraqutwniy, Ibn Hibbaan na Al-Haakim. Isnaad yake ni kwa sharti la Muslim, lakini baadhi ya wapokezi wa Hadiyth waliipa daraja la Mawquwf]
320.
وَعَنْ يَزِيدَ بْنِ اَلْأَسْوَدِ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ {أَنَّهُ صَلَّى مَعَ رَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم صَلَاةَ اَلصُّبْحِ، فَلَمَّا صَلَّى رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم إِذَا هُوَ بِرَجُلَيْنِ لَمْ يُصَلِّيَا، فَدَعَا بِهِمَا، فَجِيءَ بِهِمَا تَرْعَدُ فَرَائِصُهُمَا، فَقَالَ لَهُمَا: "مَا مَنَعَكُمَا أَنْ تُصَلِّيَا مَعَنَا؟" قَالَا: قَدْ صَلَّيْنَا فِي رِحَالِنَا. قَالَ: "فَلَا تَفْعَلَا، إِذَا صَلَّيْتُمَا فِي رِحَالِكُمْ، ثُمَّ أَدْرَكْتُمْ اَلْإِمَامَ وَلَمْ يُصَلِّ، فَصَلِّيَا مَعَهُ، فَإِنَّهَا لَكُمْ نَافِلَةٌ"} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَاللَّفْظُ لَهُ، وَالثَّلَاثَةُ، وَصَحَّحَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ، وَابْنُ حِبَّان
Kutoka kwa Yaziyd bin Al-Aswad[6] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) alisema kuwa: “Yeye aliswali Swalaah ya Fajr pamoja na Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipomaliza kuswali, aliwaona watu wawili ambao hawakuswali pamoja naye. Akaamrisha waletwe, na wakaletwa huku wakitetemeka[7] (kwa uoga). Akawauliza: “Jambo gani lilowazuia msiswali pamoja nasi?” Wakasema: “Tumeswali majumbani mwetu.” Akasema: “Msifanye hivyo, mkiswali majumbani mwenu, kisha mkaja Msikitini wakati Imaam hajamaliza kuswalisha watu, swalini pamoja naye, na hiyo itakuwa ni Swalaah ya Sunnah kwenu.” [Imetolewa na Ahmad, na tamshi hili ni lake, na Ath-Thalaathah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd) na akaisahihisha At-Tirmidhiy na Ibn Hibbaan]
321.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {إِنَّمَا جُعِلَ اَلْإِمَامُ لِيُؤْتَمَّ بِهِ، فَإِذَا كَبَّرَ فَكَبِّرُوا، وَلَا تُكَبِّرُوا حَتَّى يُكَبِّرَ، وَإِذَا رَكَعَ فَارْكَعُوا، وَلَا تَرْكَعُوا حَتَّى يَرْكَعَ، وَإِذَا قَالَ سَمِعَ اَللَّهُ لِمَنْ حَمِدَهُ، فَقُولُوا: اَللَّهُمَّ رَبَّنَا لَكَ اَلْحَمْدُ، وَإِذَا سَجَدَ فَاسْجُدُوا، وَلَا تَسْجُدُوا حَتَّى يَسْجُدَ، وَإِذَا صَلَّى قَائِمًا فَصَلُّوا قِيَامًا، وَإِذَا صَلَّى قَاعِدًا فَصَلُّوا قُعُودًا أَجْمَعِينَ} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ، وَهَذَا لَفْظُهُ وَأَصْلُهُ فِي اَلصَّحِيحَيْن
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Hakika Imaam amefanywa ili afuatwe, kwa hivyo akipiga Takbiyra nanyi pigeni, lakini nyie msipige Takbiyra hadi yeye apige. Na akirukuu nanyi mrukuu, wala msirukuu hadi amerukuu. Imaam akisema:
سَمِعَ اَللَّهُ لِمَنْ حَمِدَهُ
“Sami’a-Allaahu liman hamidah” (Allaah Amemsikia aliyemhimidi),
Semeni:
اَللَّهُمَّ رَبَّنَا لَكَ اَلْحَمْدُ
“Allaahumma Rabbanaa Lakal-Hamd.” (Ee Allaah! Rabb wetu, ni Zako Wewe Himd).
Na akisujudu, nanyi msujudu, wala msisujudu hadi amesujudu. Akiswali akiwa amesimama nanyi simameni, na akiswali huku amekaa, nanyi swalini huku mmekaa.[8]” [Imetolewa na Abuu Daawuwd, na hili ni tamshi lake, na chanzo chake kimo katika Swahiyhayn (Al-Bukhaariy na Muslim)]
322.
وَعَنْ أَبِي سَعِيدٍ اَلْخُدْرِيِّ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {رَأَى فِي أَصْحَابِهِ تَأَخُّرًا. فَقَالَ: "تَقَدَّمُوا فَائْتَمُّوا بِي، وَلْيَأْتَمَّ بِكُمْ مَنْ بَعْدَكُمْ"} رَوَاهُ مُسْلِم
Kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesimulia kuwa: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipoona Maswahaba zake wanachelewa, alisema: “Njooni mbele na mnifuate, na wale wa nyuma wawafuate nyinyi.”[9] [Imetolewa na Muslim]
323.
وَعَنْ زَيْدِ بْنِ ثَابِتٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ: {اِحْتَجَرَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم حُجْرَةً بِخَصَفَةٍ، فَصَلَّى فِيهَا، فَتَتَبَّعَ إِلَيْهِ رِجَالٌ، وَجَاءُوا يُصَلُّونَ بِصَلَاتِهِ...} اَلْحَدِيثَ، وَفِيهِ: {أَفْضَلُ صَلَاةِ اَلْمَرْءِ فِي بَيْتِهِ إِلَّا اَلْمَكْتُوبَةَ} مُتَّفَقٌ عَلَيْه
Kutoka kwa Zayd bin Thaabit (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alitengeneza mswala akaswali ndani yake. Watu wakamfuata na wakawa wanaswali nyuma yake…”[10] Msimuliaji aliitaja Hadiyth yote na ina maneno: “Swalaah bora ya mtu ni (anayoiswali) nyumbani kwake isipokuwa Swalaah ya faradhi.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
324.
وَعَنْ جَابِرٍ قَالَ: {صَلَّى مُعَاذٌ بِأَصْحَابِهِ اَلْعِشَاءَ، فَطَوَّلَ عَلَيْهِمْ، فَقَالَ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم: "أَتُرِيدُ أَنْ تَكُونَ يَا مُعَاذُ فَتَّانًا؟ إِذَا أَمَمْتَ اَلنَّاسَ فَاقْرَأْ: بِالشَّمْسِ وَضُحَاهَا، وَ: سَبِّحْ اِسْمَ رَبِّكَ اَلْأَعْلَى، وَ: اِقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ، وَاللَّيْلِ إِذَا يَغْشَى"} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَّفْظُ لِمُسْلِمٍ
Kutoka kwa Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Mu’aadh aliwaswalisha Maswahaba wenziwe Swalaah ya ‘Ishaa na akawarefushia Swalaah. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akamuambia: “Ee Mu’aadh! Unataka uwe Fattaan[11]? Ukiswalisha watu[12] soma:
وَالشَّمْسِ وَضُحَاهَا[13]
na
سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى[14]
na
اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ[15]
na
وَاللَّيْلِ إِذَا يَغْشَىٰ[16]
[Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Muslim[17]]
325.
وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا فِي قِصَّةِ صَلَاةِ رَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم بِالنَّاسِ، وَهُوَ مَرِيضٌ قَالَتْ: {فَجَاءَ حَتَّى جَلَسَ عَنْ يَسَارِ أَبِي بَكْرٍ، فَكَانَ يُصَلِّي بِالنَّاسِ جَالِسًا وَأَبُو بَكْرٍ قَائِمًا، يَقْتَدِي أَبُو بَكْرٍ بِصَلَاةِ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم وَيَقْتَدِي اَلنَّاسُ بِصَلَاةِ أَبِي بَكْرٍ} مُتَّفَقٌ عَلَيْه
Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema kuhusu Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kuswalisha watu wakati akiwa mgonjwa. Amesema: “Alikuja na akaketi upande wa kushoto wa Abuu Bakr (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ). Akawa anaswalisha watu huku amekaa na Abuu Bakr amesimama. Abuu Bakr alikuwa anamfuata Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) na watu wanafuata Swalaah ya Abuu Bakr.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
326.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {إِذَا أَمَّ أَحَدُكُمْ اَلنَّاسَ فَلْيُخَفِّفْ، فَإِنَّ فِيهِمْ اَلصَّغِيرَ وَالْكَبِيرَ وَالضَّعِيفَ وَذَا اَلْحَاجَةِ، فَإِذَا صَلَّى وَحْدَهُ فَلْيُصَلِّ كَيْفَ شَاءَ} مُتَّفَقٌ عَلَيْه
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mmoja wenu atakaposwalisha watu, afupishe, kwani miongoni mwao wapo watoto, wazee, wadhoofu, na wenye shida. Lakini akiwa anaswali peke yake, na aswali kadiri anavyotaka.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
327.
وَعَنْ عَمْرِو بْنِ سَلَمَةَ قَالَ: قَالَ أَبِي: {جِئْتُكُمْ مِنْ عِنْدِ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم حَقًّا. قَالَ: "فَإِذَا حَضَرَتْ اَلصَّلَاةُ فَلْيُؤَذِّنْ أَحَدُكُمْ، وَلْيَؤُمَّكُمْ أَكْثَرُكُمْ قُرْآنًا"، قَالَ: فَنَظَرُوا فَلَمْ يَكُنْ أَحَدٌ أَكْثَرَ قُرْآنًا مِنِّي، فَقَدَّمُونِي، وَأَنَا اِبْنُ سِتٍّ أَوْ سَبْعِ سِنِينَ} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيُّ، وَأَبُو دَاوُدَ، وَالنَّسَائِيّ
Kutoka kwa ‘Amr bin Salamah[18] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: Baba yangu amesema: “Nimekuleteeni haki kutoka kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kwa hivyo wakati wa Swalaah ukiwadia, mmoja wenu aadhini, na mmoja wenu na aliyehifadhi Qur-aan kuliko wote awe Imaam.” ‘Amr akaendelea kusema: Wakaangalia lakini hakuwepo mtu aliyejua Qur-aan kuliko mimi.[19]. Wakanitanguliza nami nikiwa na umri wa miaka sita au saba tu. ”[20] [Imetolewa na Al-Bukhaariy, Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy]
328.
وَعَنْ اِبْنِ مَسْعُودٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {يَؤُمُّ اَلْقَوْمَ أَقْرَؤُهُمْ لِكِتَابِ اَللَّهِ، فَإِنْ كَانُوا فِي اَلْقِرَاءَةِ سَوَاءً فَأَعْلَمُهُمْ بِالسُّنَّةِ، فَإِنْ كَانُوا فِي اَلسُّنَّةِ سَوَاءً فَأَقْدَمُهُمْ هِجْرَةً، فَإِنْ كَانُوا فِي اَلْهِجْرَةِ سَوَاءً فَأَقْدَمُهُمْ سِلْمًا وَفِي رِوَايَةٍ: سِنًّا وَلَا يَؤُمَّنَّ اَلرَّجُلُ اَلرَّجُلَ فِي سُلْطَانِهِ، وَلَا يَقْعُدْ فِي بَيْتِهِ عَلَى تَكْرِمَتِهِ إِلَّا بِإِذْنِهِ".} رَوَاهُ مُسْلِم
وَلِابْنِ مَاجَهْ: مِنْ حَدِيثِ جَابِرٍ: {وَلَا تَؤُمَّنَّ اِمْرَأَةٌ رَجُلًا، وَلَا أَعْرَابِيٌّ مُهَاجِرًا، وَلَا فَاجِرٌ مُؤْمِنًا.} وَإِسْنَادُهُ وَاه
Kutoka kwa Ibn Mas-‘uwd (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema kuwa: “Anaswalisha watu msomaji wao zaidi wa Qur-aan. Ikiwa wako sawa katika usomaji, basi anayejua Sunnah zaidi, na ikiwa wako sawa katika Sunnah basi mtu aliyetangulia Hijrah[21], na kama wako sawa katika uhamiaji basi aliyetangulia kusilimu.”
Na katika mapokezi mengine: “Kwa umri.” Na mtu asiswalishe mtu aliyekaa katika milki yake au asikae nyumbani kwa mwenyeji wake penye nafasi ya heshima isipokuwa kwa ruhusa yake.” [Imetolewa na Muslim]
Na Ibn Maajah amepokea kutokana na Hadiyth ya Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ): “Mwanamke asimswalishe kamwe mwanamume, wala Bedui (Mwarabu wa jangwani) asimswalishe mhamiaji, na muovu asimswalishe Muumini.” [Isnaad yake ni Waahin (Dhaifu sana)]
329.
وَعَنْ أَنَسٍ، عَنْ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {رُصُّوا صُفُوفَكُمْ، وَقَارِبُوا بَيْنَهَا، وَحَاذُوا بِالْأَعْنَاقِ.} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ، وَالنَّسَائِيُّ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ
Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Pangeni safu zenu na karibieni baina yake[22], na muwe shingo kwa shingo.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy, na akaisahihisha Ibn Hibbaan]
330.
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم { خَيْرُ صُفُوفِ اَلرِّجَالِ أَوَّلُهَا، وَشَرُّهَا آخِرُهَا، وَخَيْرُ صُفُوفِ اَلنِّسَاءِ آخِرُهَا، وَشَرُّهَا أَوَّلُهَا} رَوَاهُ مُسْلِم
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Safu bora kwa wanaume ni ya kwanza, na mbaya zaidi ni ya mwisho; na kwa mwanamke safu bora zaidi ni ya mwisho na mbaya zaidi ni ya mwanzo.” [Imetolewa na Muslim]
331.
وَعَنْ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {صَلَّيْتُ مَعَ رَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ذَاتَ لَيْلَةٍ، فَقُمْتُ عَنْ يَسَارِهِ، فَأَخَذَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم بِرَأْسِي مِنْ وَرَائِي، فَجَعَلَنِي عَنْ يَمِينِهِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْه
Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Niliswali pamoja na Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) usiku mmoja, nikasimama kushoto kwake, Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akanishika kisogoni[23] na akaniweka upande wake wa kulia.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
332.
وَعَنْ أَنَسٍ قَالَ: {صَلَّى رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَقُمْتُ وَيَتِيمٌ خَلْفَهُ، وَأُمُّ سُلَيْمٍ خَلْفَنَا} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَّفْظُ لِلْبُخَارِيّ
Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliswali nikasimama mimi na yatima[24] nyuma yake, na Ummu Sulaym nyuma yetu[25].” [Al-Bukhaariy, Muslim, na tamshi hili ni la Al-Bukhaariy]
333.
وَعَنْ أَبِي بَكْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ{ أَنَّهُ اِنْتَهَى إِلَى اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم وَهُوَ رَاكِعٌ، فَرَكَعَ قَبْلَ أَنْ يَصِلَ إِلَى اَلصَّفِّ، فَقَالَ لَهُ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم زَادَكَ اَللَّهُ حِرْصًا وَلَا تَعُدْ} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيُّ
وَزَادَ أَبُو دَاوُدَ فِيهِ: {فَرَكَعَ دُونَ اَلصَّفِّ، ثُمَّ مَشَى إِلَى اَلصَّفِّ}
Kutoka kwa Abuu Bakr (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) kwamba alikwenda kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akiwa anarukuu. Akarukuu kabla hajakuta safu. Akamtajia hayo Nabiy , (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) hapo akamuambia: “Allaah Akuongezee himma, lakini usirudie.[26]” [Imetolewa na Al-Bukhaariy]
Na Abuu Daawuwd akaongezea: “Alirukuu kabla hata ya kuifikia safu, kisha akatembea hadi kwenye safu.”
334.
وَعَنْ وَابِصَةَ بْنِ مَعْبَدٍ اَلْجُهَنِيِّ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم { رَأَى رَجُلًا يُصَلِّي خَلْفَ اَلصَّفِّ وَحْدَهُ، فَأَمَرَهُ أَنْ يُعِيدَ اَلصَّلَاةَ} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَأَبُو دَاوُدَ، وَاَلتِّرْمِذِيُّ وَحَسَّنَهُ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ
وَلَهُ عَنْ طَلْقٍ {لَا صَلَاةَ لِمُنْفَرِدٍ خَلْفَ اَلصَّفِّ}
وَزَادَ اَلطَّبَرَانِيُّ مِنْ حَدِيثِ وَابِصَةَ: {أَلَا دَخَلْتَ مَعَهُمْ أَوْ اِجْتَرَرْتَ رَجُلًا؟ }
Kutoka kwa Waabiswah bin Ma’bad[27] Al-Juhaniyy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimuona mtu mmoja anaswali peke yake nyuma ya safu, na akamuamrisha arudie kuswali.” [Imetolewa na Ahmad, Abuu Daawuwd, na At-Tirmidhiy naye akaipa daraja la Hasan, Ibn Hibbaan akaipa daraja la Swahiyh]
Naye (Ibn Hibbaan) amepokea Hadiyth ya Twalq bin ‘Aliy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ): “Hakuna Swalaah ya mtu peke yake nyuma ya safu.[28]”
Na akaongezea Atw-Twabaraaniyy kwenye usimulizi wa Waabiswah: “Kwa nini hukujiunga nao au kumvuta mtu (ajiunge nawe?).”
335.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ عَنْ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {إِذَا سَمِعْتُمْ اَلْإِقَامَةَ فَامْشُوا إِلَى اَلصَّلَاةِ، وَعَلَيْكُمْ اَلسَّكِينَةُ وَالْوَقَارُ، وَلَا تُسْرِعُوا، فَمَا أَدْرَكْتُمْ فَصَلُّوا، وَمَا فَاتَكُمْ فَأَتِمُّوا} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَّفْظُ لِلْبُخَارِيِّ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mkisikia Iqaamah, nendeni kuswali kwa utulivu na taadhima, na msifanye haraka, na swalini sehemu yoyote ya Swalaah mtakayoiwahi[29], kisha timizeni sehemu iliyokupiteni." [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Al-Bukhaariy]
336.
وَعَنْ أُبَيِّ بْنِ كَعْبٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم { صَلَاةُ اَلرَّجُلِ مَعَ اَلرَّجُلِ أَزْكَى مِنْ صَلَاتِهِ وَحْدَهُ، وَصَلَاتُهُ مَعَ اَلرَّجُلَيْنِ أَزْكَى مِنْ صَلَاتِهِ مَعَ اَلرَّجُلِ، وَمَا كَانَ أَكْثَرَ فَهُوَ أَحَبُّ إِلَى اَللَّهِ} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ، وَالنَّسَائِيُّ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّان
Kutoka kwa ‘Ubayy bin Ka’b (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Swalaah ya mtu anayoiswali pamoja na mtu mwingine ni bora zaidi kuliko anayoswali peke yake. Na Swalaah ya mtu anaiswali pamoja na watu wawili ni bora zaidi kuliko anayoswali na mtu mmoja; na Swalaah inapokuwa na watu wengi zaidi humpendeza zaidi Allaah (عزّ وجلّ).” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy na akaisahihisha Ibn Hibbaan]
337.
وَعَنْ أُمِّ وَرَقَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا، {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم أَمَرَهَا أَنْ تَؤُمَّ أَهْلَ دَارِهَا} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ خُزَيْمَةَ
Kutoka kwa Ummu Waraqah[30] (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimuamrisha Ummu Waraqah awaswalishe watu wa nyumba yake.”[31] [Imetolewa na Abuu Daawuwd na akaisahihisha Ibn Khuzaymah]
338.
وَعَنْ أَنَسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ; {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم اِسْتَخْلَفَ اِبْنَ أُمِّ مَكْتُومٍ، يَؤُمُّ اَلنَّاسَ، وَهُوَ أَعْمَى} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَأَبُو دَاوُد
وَنَحْوُهُ لِابْنِ حِبَّانَ: عَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا
Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesimulia kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimteua Ibn Ummu Maktuwm (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) aswalishe, alipokuwa hayupo, naye (Ibn Ummu Maktuwm) alikuwa kipofu.[32]” [Imetolewa na Ahmad na Abuu Daawuwd]
Ibn Hibbaan pia amepokea Hadiyth kama hiyo, kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا)
339.
وَعَنْ اِبْنِ عُمَرَ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم { صَلُّوا عَلَى مَنْ قَالَ: لَا إِلَهَ إِلَّا اَللَّهُ، وَصَلُّوا خَلْفَ مَنْ قَالَ: لَا إِلَهَ إِلَّا اَللَّهُ} رَوَاهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ بِإِسْنَادٍ ضَعِيفٍ
Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mswalieni mtu aliyetamka (aliyesilimu) Laa ilaaha illa Allaah (hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah) na swalini nyuma ya mtu aliyesema: Laa ilaaha illa Allaah.”[33] [Imetolewa na Ad-Daaraqutwniyy kwa Isnaad dhaifu]
340.
وَعَنْ عَلِيٍّ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم { إِذَا أَتَى أَحَدُكُمْ اَلصَّلَاةَ وَالْإِمَامُ عَلَى حَالٍ، فَلْيَصْنَعْ كَمَا يَصْنَعُ اَلْإِمَامُ} رَوَاهُ اَلتِّرْمِذِيُّ بِإِسْنَادٍ ضَعِيفٍ
Kutoka kwa ‘Aliy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mmoja wenu akiingia katika Swalaah, na Imaam yuko katika kitendo fulani, basi afanye anavyofanya Imaam.” [Imetolewa na At-Tirmidhiy kwa Isnaad dhaifu]
[1] Katika simulizi zinazofuata, thawabu zimeripotiwa kuwa ni kubwa mara ishirini na tano. Inategemeana na hali ya huyo anayeswali. Mtu mwenye hadhi ya juu hupata mara ishirini na saba zaidi, na yule mwenye hadhi ya chini hupata mara ishirini na tano tu zaidi.
[2] Tunaarifiwa katika Hadiyth hii kwamba, kuswali katika jamaa ni Fardhw ‘Ayn (wajibu wa binafsi). Ingelikuwa ni Fardhw Kifaaya (wajibu wa wengi) au Sunnah Muakkadah (iliyosisitizwa), Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) asingetumia maneno makali vile kwa watu wasiohudhuria Swalaah za Jamaa.
[3] Neno hilo “unafiki” hapa limetumika kuhusu unafiki wa matendo na siyo unafiki wa uaminifu, kwani mnafiki ni mtu asiyeamini moyoni mwake, na huenda Msikitini kwa ajili ya kujionyesha tu kwa watu.
[4] Mtu huyo asiyeona hakuwa mwengine bali ni ‘Abdullaah bin Ummi Maktuwm. Baada ya amri hiyo ya Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akienda kuswali Msikitini kila mara hadi akateuliwa kuwa Muadhini. Kwa kuwa hata walemavu wanaamrishwa wahudhurie Swalaah ya Jamaa Msikitini, je wale wasiohudhuria Swalaah za jamaa bila kisingizio chochote? Swalaah ya mlemavu inakubalika iswaliwe nyumbani, lakini yeye pia hazipati thawabu za jamaa.
[5] Hadiyth hii inadhihirisha kwamba, ni waajib kwa kwa anayesikia Adhana kuitikia kwa kuwenda kuswali Jamaa Msikitini. Hakuna kisingizio cha kutokwenda kuswali jamaa madamu tu kasikia Adhana. Miongoni mwa nyudhuru zinazokubalika mtu asiende Msikitini kuswali Jamaaa, ni kimbunga, mvua, njaa kali sana, kwenda haja kubwa, kukojoa, kuugua maradhi n.k.
[6] Yaziyd bin Al-Aswad ndiye Jaabir As-Sawaaiy Al-‘Aamiriy, ambaye alikuwa sahiba wa Maquraysh. Alikuwa ni Swahaba aliyeishi Twaaif, na hii ndiyo Hadiyth pekee kutoka kwake kupitia kwa mwanawe Jaabir.
[7] Miili yao ilianza kusisimka kwa sababu ya woga kutokana na haiba ya Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), kama ambavyo hutokea kwa sababu ya mshituko wa woga.
[8] Shariy’ah hii sasa imefutwa. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliswalisha watu huku kaketi chini kwa sababu ya maradhi yake (ambayo ndiyo yaliyomuua), ambapo Maamuma (wafuasi) wake waliswali huku wamesimama wima kama ilivyo kawaida.
[9] Hadiyth hii inaweza kunukuliwa kuwa ndiyo ushahidi wa Maamuma ambao wanaweza kumuona Imaam lakini hawawezi kumsikia. Maamuma kama hao lazima wafuate Maamuma mwengine walio mbele yao. Pia inatufundisha kuwa msitari wa mbele kabisa ndiyo mbora, na mtu sharti afuate kuujaza huo kwanza ikiwezekana, na kwamba msitari wa pili usiwe mbali na msitari wa kwanza, na halikadhalika msitari wa kwanza usiwe mbali na Imaam.
[10] Hadiyth hii inaonyesha kuwa, ikiwa upo ukuta au kitenganisho au umbali fulani kati ya Imaam na Maamuma, Swalaah itabakia kuwa halali. Watu wengine hawaafiki maneno yote ya Hadiyth hii, lakini usahihi wake unatosha kuwashawishi watu hao.
[11] Inamaanisha: “Kwa kukirefusha kisomo unataka kuwatesa watu unaowaswalisha, na kwa hivyo unawakatisha tamaa wasiwe wanahudhuria Swalaah za Jamaa?”
[12] Hadiyth hii inatufundisha kwamba, Imaam asirefushe kisomo chake ndani ya Swalaah asiwakere Maamuma wake, wasije kuiepuka Swalaah ya Jamaa. Hadiyth nyingine inayoifuatia hii inatoa sababu za kutorefusha kisomo, lakini pia kisifupishwe kwa kiasi cha Maamuma kushindwa hata kukamilisha kisomo chake au Swalaah yake. Njia iliyo sahihi ni kuswalisha kwa namna ya wastani kwa mujibu wa Sunnah ya Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ)
[13] [Ash-Sams (91)]
[14] [Al-A’laa (87)]
[15] [Al-‘Alaq (96)]
[16] [Al-Layl: (92)]
[17] Hadiyth nyingine inaripoti kwamba, Mu’aadh alikuwa kwanza anaswali nyuma ya Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), kisha anaswali Nafl (Swalaah ya khiari, ya Sunnah), na kisha alikuwa anakwenda kuswalisha katika Msikiti mwingine. Hii inaonyesha kuwa, mtu anaweza kuswali Swalaah yake ya faradhi nyuma ya Imaam anayeswali Swalaah yake ya Nafl.
[18] ‘Amr bin Salamah ndiye Abu Yaziyd au Abuu Burayd. Alikuja na baba yake kwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ). Inasemekana pia kuwa hakuja na baba yake. Alikuwa katika kabila la Jarum, na akawa anaishi Basra.
[19] Hadiyth hii inaeleza kuwa, mtu anayestahili zaidi kuliko wengine wote kuwa Imaam ni yule anayejua Shari’a zaidi kuliko wote. Ikiwa watu wawili wana ujuzi sawa, yule ambaye ni mwenye taqwa zaidi ndiye awe Imaam. Vigezo hivyo pia vimetajwa katika usimulizi wa Ibn Mas-‘uwd.
[20] Hadiyth hii inaonyesha kuwa mtoto ambaye bado hajabaleghe anaweza kumswalisha mtu mkubwa au kundi la watu wakubwa iwapo anatokezea kuwa mjuzi zaidi kuliko wale wakubwa kwenye mambo ya Shariy’ah.
[21] Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na Maswahaba walipohamia Madiynah kutoka Makkah.
[22] Imeripotiwa katika Swahiyh mbili kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliwakhutubia watu huku uso wake umewaelekea wao, na akawaamrisha wanyooshe safu (misitari) zao vinginevyo Allaah (عزّ وجلّ) Atafanya kutopatana ndani ya nyoyo zenu. Msimuliaji anasema aliwaona watu wanaoswali jamaa walikuwa wakisogezeana vifundo vya miguu na mikono yao karibu karibu. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alisema huku akimuapia Allaah (عزّ وجلّ) kuwa iwapo safu za ndani ya Swalaah zinaacha mapengo, anaweza kumuona shaytwaan mle. Pamoja na hii, zipo Hadiyth nyingi zinazozungumzia mpangilio wa safu katika Swalaah.
[23] Safu ya mwisho ya wanaume ni mbaya kwa sababu kwa kuwa imenyimwa fadhila za kuwa katika safu ya kwanza. Safu ya mwisho kuliko zote kwa mwanamke ndio bora zaidi kwa sababu iko mbali zaidi kuweza kuchanganyika na wanaume. Lakini iwapo jamaa ni ya wanawake watupu na Swalaah hiyo ya jamaa inaswalishwa na mwanamke, basi kanuni hiyo hiyo inahusika kwa wanawake pia, yaani safu ya kwanza ya wanawake hao ni bora zaidi kuliko safu ya mwisho sawa sawa na wanaume.
[24] Hukmu ni kwamba, wanaume sharti wapange safu kwanza, kisha watoto na kisha wanawake. Endapo yupo mwanamme mmoja na mtoto mmoja, basi wote wawili wasimame safu moja.
[25] Mwanamke mmoja tu anaruhusiwa aswali nyuma ya safu ya mwisho ya wanaume kukiwa hakuna mwanamke mwingine wa kuungana naye.
[26] Maana yake ni kuwa: “Allaah (عزّ وجلّ) na Aongeze shauku au himma yako ya kufanya matendo ya uadilifu, lakini tendo hilo lisikiuke mipaka.”
[27] Waabiswah bin Ma’bad ndiye Answaar kutoka katika ukoo wa Asad bin Khuzaymah. Alipewa jina la utani la Abuu Qirswaafah. Kwanza aliishi Kufa, kisha akahamia Al-Hira na akafariki mnamo mwaka 90 A.H.
[28] Kama Swalaah ya mtu anayeswali peke yake nyuma ya safu inakubalika au laa ni suala lenye kutofautiana na linalohitaji majadiliano zaidi. Ukweli ni kuwa mtu asiswali kwa kusimama peke yake wakati Swalaah ya Jamaa inaendelea.
[29] Nukta nyingine yenye kutofautiana ni kama sehemu ya Swalaah iliyobakia anayoiswali mtu nyuma ya Imaam katika Swalaah ya jamaa, ihesabike kuwa ni sehemu ya mwanzo ya Swalaah au kama ihesabike kuwa ni sehemu ya mwisho.
[30] Umm Waraqah huyu ndiye Bint Nawfal, au Bint ‘Abdillaah bin Al-Haarith bin ‘Uwaymr Al-Answaariyyah. Alikusanya Qur-aan na akamuomba Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amruhusu ashiriki katika vita vya Badr. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akimzuru na akimwita “Shahidi”. Aliuliwa na watumwa wake wa kiume na wa kike kwa kumziba pumzi na nguo. Kisha wakakimbia, lakini walikamatwa na wakauliwa kwa amri ya ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ)
[31] Hadiyth hii inaeleza kuwa inaruhusiwa kwa mwanamke kuswalisha. Ni ukweli uliothibitishwa kuwa ‘Aaishah na Ummu Salamah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) waliwahi kuswalisha. Imaam Shawkaan alisema kuwa, mwanamke akiswalisha, asisimame peke yake mbele ya safu, bali naye asimame ndani ya safu. Iwapo katika Maamuma wake wamo wanaume pia, basi ni sharti wawe Mahaarim (wasioweza kuwaoa). Mwanamke hawezi hadhara ya watu ambao kuna watu wageni au watu wasio mahaarim wake.
[32] Hadiyth hii inaweka wazi kabisa kuwa kipofu asiyeona anafaa kuswalisha. Wanazuoni wengine huafiki hili, lakini hiyo ni kinyume cha desturi. Wanazuoni wengine husema kuwa, pakiwepo Mwanazuoni mwenye uwezo kamili wa kuona, si sahihi kumuomba Mwanazuoni asiyeona kuswalisha na oni hili ni batili pia. Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimuamuamrisha ‘Abdallaah bin Umm Maktwum (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) pamoja na kutoona kwake aswalishe kiasi cha mara kumi na tatu.
[33] Nukta inayodhihirishwa hapa ni kuwa, inaruhusiwa kuswali nyuma ya mtu anayepuuza kutekeleza mambo ya waajib. Lakini mtu kama huyo asiteuliwe kamwe kuwa Imaam, yaani asipewe kazi ya kuswalisha.