13-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Swalaah: Mlango Wa Swalaatul-Khawf (Swalaah Kipindi Cha Ya Khofu)

 

بُلُوغُ الْمَرام

 

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتَابُ اَلصَّلَاةِ

 

Kitabu Cha Swalaah

 

بَابُ صَلَاةِ اَلْخَوْفِ

 

13-Mlango Wa Swalaatul-Khawf (Swalaah Ya Kipindi Cha Khofu)

 

 

 

 

 

379.

عَنْ صَالِحِ بْنِ خَوَّاتٍ، {عَمَّنْ صَلَّى مَعَ رَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  يَوْمَ ذَاتِ اَلرِّقَاعِ صَلَاةَ اَلْخَوْفِ: أَنَّ طَائِفَةً صَلَّتْ مَعَهُ وَطَائِفَةٌ وِجَاهَ اَلْعَدُوِّ، فَصَلَّى بِاَلَّذِينَ مَعَهُ رَكْعَةً، ثُمَّ ثَبَتَ قَائِمًا وَأَتَمُّوا لِأَنْفُسِهِمْ، ثُمَّ اِنْصَرَفُوا فَصَفُّوا وِجَاهَ اَلْعَدُوِّ، وَجَاءَتِ اَلطَّائِفَةُ اَلْأُخْرَى، فَصَلَّى بِهِمْ اَلرَّكْعَةَ اَلَّتِي بَقِيَتْ، ثُمَّ ثَبَتَ جَالِسًا وَأَتَمُّوا لِأَنْفُسِهِمْ، ثُمَّ سَلَّمَ بِهِمْ}  مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَهَذَا لَفْظُ مُسْلِمٍ 

وَوَقَعَ فِي "اَلْمَعْرِفَةِ" لِابْنِ مَنْدَهْ، عَنْ صَالِحِ بْنِ خَوَّاتٍ، عَنْ أَبِيهِ 

Kutoka kwa Swaalih bin Khawwaat[1] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kwa upokezi wa mtu aliyeswali pamoja na Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) Swalaatul-Khawf (Swalaah ya Khofu) katika vita vya Dhaat Ar-Riqaa’i[2]: “Kuwa kundi la jeshi lilijipanga safu moja pamoja naye, na kundi jingine mkabala na maadui. Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akaswalisha kundi lililokuwa pamoja naye Rakaa moja, kisha akabaki amesimama wima wakati wanamalizia Swalaah yao wenyewe. Wakaondoka na wakapanga safu mkabala na maadui, na kundi jingine la jeshi likaja. Akawaswalisha Rakaa iliyobaki ya Swalaah yake, kisha akabakia ameketi wakati wao wakimalizia Swalaah yao kisha akatoa nao Salaam.”[3] [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Muslim]

 

Na katika mapokezi ya Al Ma’rifah ya Ibn Mandah kutoka kwa Swaalih bin Khawwaat kutoka kwa babaake.

 

 

 

380.

وَعَنِ ابْنِ عُمَرَ قَالَ: {غَزَوْتُ مَعَ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم  قِبَلَ نَجْدٍ، فَوَازَيْنَا اَلْعَدُوَّ، فَصَافَفْنَاهُمْ، فَقَامَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  يُصَلِّي بِنَا، فَقَامَتْ طَائِفَةٌ مَعَهُ، وَأَقْبَلَتْ طَائِفَةٌ عَلَى اَلْعَدُوِّ، وَرَكَعَ بِمَنْ مَعَهُ، وَسَجَدَ سَجْدَتَيْنِ، ثُمَّ انْصَرَفُوا مَكَانَ اَلطَّائِفَةِ الَّتِي لَمْ تُصَلِّ فَجَاءُوا، فَرَكَعَ بِهِمْ رَكْعَةً، وَسَجَدَ سَجْدَتَيْنِ، ثُمَّ سَلَّمَ، فَقَامَ كُلُّ وَاحِدٍ مِنْهُمْ، فَرَكَعَ لِنَفْسِهِ رَكْعَةً، وَسَجَدَ سَجْدَتَيْنِ}  مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَهَذَا لَفْظُ اَلْبُخَارِيِّ 

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Nilikwenda vitani pamoja na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) huko Najd[4], tulipofika mbele ya adui tulijipanga msitari tukiwakabili, akasimama Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akatuswalisha. Kundi moja likasimama pamoja naye kundi jingine limesimama mkabala na adui. Akawaswalisha Rakaa moja waliokuwa pamoja naye na akasujudu Sijdah mbili. Kisha wakaondoka wakaenda mahali pa kundi lililokuwa bado halijaswali. Wakaja na akawaswalisha Rakaa moja na akasujudu Sijdah mbili. Kisha akatoa Salaam. Kila mmoja akasimama na kuswali peke yake Rakaa moja na kusujudu Sijdah mbili.[5] [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Al-Bukhaariy]

 

 

 

381.

وَعَنْ جَابِرٍ قَالَ: {شَهِدْتُ مَعَ رَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  صَلَاةَ اَلْخَوْفِ، فَصَفَّنَا صَفَّيْنِ: صَفٌّ خَلْفَ رَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  وَالْعَدُوُّ بَيْنَنَا وَبَيْنَ اَلْقِبْلَةِ، فَكَبَّرَ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم  وَكَبَّرْنَا جَمِيعًا، ثُمَّ رَكَعَ وَرَكَعْنَا جَمِيعًا، ثُمَّ رَفَعَ رَأْسَهُ مِنَ اَلرُّكُوعِ وَرَفَعْنَا جَمِيعًا، ثُمَّ اِنْحَدَرَ بِالسُّجُودِ وَالصَّفُّ اَلَّذِي يَلِيهِ، وَقَامَ اَلصَّفُّ اَلْمُؤَخَّرُ فِي نَحْرِ اَلْعَدُوِّ، فَلَمَّا قَضَى اَلسُّجُودَ، قَامَ اَلصَّفُّ اَلَّذِي يَلِيهِ...}  فَذَكَرَ اَلْحَدِيثَ

وَفِي رِوَايَةٍ: {ثُمَّ سَجَدَ وَسَجَدَ مَعَهُ اَلصَّفُّ اَلْأَوَّلُ، فَلَمَّا قَامُوا سَجَدَ اَلصَّفُّ اَلثَّانِي، ثُمَّ تَأَخَّرَ اَلصَّفُّ اَلْأَوَّلِ وَتَقَدَّمَ اَلصَّفُّ اَلثَّانِي...}  فَذَكَرَ مِثْلَهُ

وَفِي آخِرِهِ: {ثُمَّ سَلَّمَ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم  وَسَلَّمْنَا جَمِيعًا}  رَوَاهُ مُسْلِمٌ 

وَلِأَبِي دَاوُدَ: عَنْ أَبِي عَيَّاشٍ الزُّرَقِيِّ مِثْلُهُ، وَزَادَ: {أَنَّهَا كَانَتْ بِعُسْفَانَ}  

وَلِلنَّسَائِيِّ مِنْ وَجْهٍ آخَرَ عَنْ جَابِرٍ {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم  صَلَّى بِطَائِفَةٍ مِنْ أَصْحَابِهِ رَكْعَتَيْنِ، ثُمَّ سَلَّمَ، ثُمَّ صَلَّى بِآخَرِينَ أَيْضًا رَكْعَتَيْنِ، ثُمَّ سَلَّمَ}

وَمِثْلُهُ لِأَبِي دَاوُدَ، عَنْ أَبِي بَكْرَةَ 

Kutoka kwa Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nilihudhuria Swalaatul-Khawf (Swalaah ya Khofu) pamoja na Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ). Tulijipanga safu mbili. Safu nyuma yake na maadui wakiwa baina yetu na Qiblah. Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akapiga Takbiyr nasi sote tukaitamka, kisha akarukuu na sisi sote tukarukuu, kisha akanyanyua kichwa chake baada ya kurukuu na sisi sote tukanyanyua vichwa vyetu, kisha akateremka kusujudu pamoja na safu iliyokuwa karibu yake wakati safu ya nyuma imesimama mkabala na adui. (Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ)) alipomaliza kusujudu ikasimama safu iliyo karibu yake...” akaitaja Hadiyth yote mfano wake.”[6] [Imetolewa na Muslim]

 

Na katika mapokezi mengine: “...kisha safu ya kwanza ikasujudu pamoja naye, waliposimama, ikasujudu safu ya pili, halafu safu ya kwanza ikaenda nyuma na safu ya pili ikaenda mbele.” Hadiyth ikatajwa kama hiyo iliyotangulia.

 

Na mwisho wake inaeleza: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akatoa Salaam, kisha nasi sote tukatoa Salaam.” [Imetolewa na Muslim]

 

Abuu Daawuwd amepokea Hadiyth kama hiyo kutoka kwa Abuu ‘Ayyaash Az-Zuraqiyy[7] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) akaongezea: “Ilikuwa Usfaan.[8]

 

An-Nasaaiy amepokea kwa njia nyingine kutoka Hadiyth ya Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliswalisha kundi la Maswahaba wake Rakaa mbili, kisha akatoa Salaam, kisha akaswalisha kundi jingine Rakaa mbili, kisha akatoa Salaam.”

 

Hadiyth kama hiyo imepokewa na Abuu Daawuwd kutoka kwa Abuu Bakr.

 

 

 

382.

 وَعَنْ حُذَيْفَةَ: {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم  صَلَّى صَلَاةَ اَلْخَوْفِ بِهَؤُلَاءِ رَكْعَةً، وَبِهَؤُلَاءِ رَكْعَةً، وَلَمْ يَقْضُوا} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَأَبُو دَاوُدَ، وَالنَّسَائِيُّ، وَصَحَّحَهُ ابْنُ حِبَّانَ 

وَمِثْلُهُ عِنْدَ ابْنِ خُزَيْمَةَ: عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ 

Kutoka kwa Khudhayfah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliswali Swalaatul-Khawf (Swalaah ya Khofu) kwa kuswalisha hawa Rakaa moja na hawa (kundi jingine) Rakaa moja, na hawakukidhi (kulipa).” [Imetolewa na Ahmad, Abu Daawuwd na An-Nasaaiy, na akaisahihisha Ibn Hibbaan]

 

Mfano wa Hadiyth hiyo ameipokea Ibn Khuzaymah kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا)

 

 

 

383.

وَعَنِ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم { صَلَاةُ اَلْخَوْفِ رَكْعَةٌ عَلَى أَيِّ وَجْهٍ كَانَ}  رَوَاهُ اَلْبَزَّارُ بِإِسْنَادٍ ضَعِيفٍ 

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Swalaatul-Khawf (Swalaah  ya Khofu) ni Rakaa moja, kwa njia yoyote iwayo.” [Imetolewa na Al-Bazzaar kwa Isnaad dhaifu[9]]

 

 

 

384.

وَعَنْهُ مَرْفُوعًا: {لَيْسَ فِي صَلَاةِ اَلْخَوْفِ سَهْوٌ} أَخْرَجَهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ بِإِسْنَادٍ ضَعِيفٍ

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) tena katika Hadiyth Marfuw’ amesema: “Katika Swalaatul-Khawf (Swalaah ya Khofu) hakuna (Sijdah ya) kusahau.” [Imetolewa na Ad-Daaraqutwniyy kwa Isnaad dhaifu]

 

[1] Swaalih bin Khawwaat ndiye Swaalih bin Khawwaat bin Jaabir bin An-Nu’maan Al-Answaariyy Al-Madaniy. Alikuwa ni mmoja wa Maswahaba maarufu, na Ahaadiyth zake zina usahihi wa hali ya juu.

[2] Dhaati Ar-Riqaa’ inaweza kutafsiriwa kuwa ni “iliyo na misitari au milia”. Waislamu walikuwa wana ufukara wa hali ya juu sana, na walikuwa wanatembea pekupeku, bila kuvaa viatu. Miguu yao ikipata malengelenge, walikuwa wakiifungiliza kwa marapurapu ya nguo chakavu. Kwa hivyo vita hivi vikaja kujulikana kama ni vita vya Dhaati Ar-Riqaa’.

[3] Hadiyth hii inaeleza kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliswalisha Swalaah moja yenye Rakaa mbili, na Hadiyth ya pili inasema aliswalisha Swalaah mbili za Rakaa mbili kila moja kwa makundi mawili tofauti. Kwa kuwa kuswalisha Swalaah mbili kumetajwa, hakuna tofauti ya maoni juu yake. Uhakika wa mambo ni kwamba, katika Swalaatul-Khawf  (Swalaah ya Khofu) kama mbinu za vita zimezingatiwa. Imethibitishwa kwamba Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akitumia aina mbalimbali za kuswali wakati wa vita. Ibn Hazam alirejea au alizitaja namna kumi na nne mbalimbali za kuswali, kulingana na mahitaji au mazingira ya wakati ule. Wakati mwingine Swalaah ilikuwa ndefu, na wakati mwingine inakuwa fupi. Mara nyingine mtindo mmoja, na mara nyingine mtindo mwingine. Jina la Swahaba wa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) huyo lilitajwa kuwa ni Sahl bin Abuu Hathmah.

[4] Najd ni jina la sehemu ya Rasi ya Arabuni ambako kuna nyanda za juu za milima.

[5] Kutokana na Hadiyth hii, inaelekea kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliswalisha Rakaa moja kwa kila moja ya makundi mawili tofauti, wakati kila kundi liliswali Rakaa nyingine moja peke yake. Inaelekea kuwa hali hii inaafikiana na Aayah za Qur-aan [An-Nisaa (4: 102-103)]

[6] Sehemu iliyobaki ya Hadiyth inaeleza: “...safu ya nyuma ikaenda chini kusujudu kisha wakasimama. Halafu safu ya nyuma ikaenda mbele na safu ya mbele ikarudi nyuma. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akarukuu nasi sote tukarukuu, akanyanyua kichwa chake baada ya kurukuu na sisi sote tukanyanyua vichwa vyetu. Kisha yeye na safu ya karibu yake lakini ilikuwa nyuma katika Rakaa ya kwanza wakasujudu, wakati safu ya nyuma imesimama mkabala na adui. Kisha Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) na safu iliyokuwa karibu naye walipomaliza kusujudu, safu ya nyuma nao wakaenda chini kusujudu. Kisha Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akatoa Salaam, nasi sote tukafanya hivyo.” Mwisho wa Hadiyth.

[7] Abuu ‘Ayyaash ndiye Zayd bin Thaabit, ambaye ni Answaariyy na Zuraqiyy. Kundi la Waislamu limeripoti Hadiyth kutoka kwake na alikufa baada ya mwaka 40 A.H.

[8] ‘Usfaan ni pahala ambapo pako Nanzil (takribani sawa na safari ya siku mbili) kutoka Makkah.

[9] Hadiyth hii imewafanya wengine waamue kwamba ipo Rakaa moja tu kwa wote Maamuma na Imaam pia. Kwa hivyo Sufyaan anafuata vivyo hivyo.

 

 

Share