14-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Swalaah: Mlango Wa Swalaatul-'Iydayni (Swalaah Za ‘Iyd Mbili)

بُلُوغُ الْمَرام

 

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتَابُ اَلصَّلَاةِ

 

Kitabu Cha Swalaah

 

بَابُ صَلَاةِ اَلْعِيدَيْنِ

14-Mlango Wa Swalaatul-‘Iydayni (Swalaah Za ‘IydMbili)[1]

 

 

 

385.

عَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم { الْفِطْرُ يَوْمَ يُفْطِرُ اَلنَّاسُ، وَالْأَضْحَى يَوْمَ يُضَحِّي اَلنَّاسُ} رَوَاهُ اَلتِّرْمِذِيُّ 

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Al-Fitwr ni siku ambapo watu wanakula. Na Al-Adhwhaa ni siku ambapo watu wanachinja.”[2] [Imetolewa na At-Tirmidhiy]

 

 

 

386.

وَعَنْ أَبِي عُمَيْرِ بْنِ أَنَسٍ، عَنْ عُمُومَةٍ لَهُ مِنَ اَلصَّحَابَةِ، {أَنَّ رَكْبًا جَاءُوا، فَشَهِدُوا أَنَّهُمْ رَأَوُا الْهِلَالَ بِالْأَمْسِ، فَأَمَرَهُمْ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم  أَنْ يُفْطِرُوا، وَإِذَا أَصْبَحُوا يَغْدُوا إِلَى مُصَلَّاهُمْ} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَأَبُو دَاوُدَ وَهَذَا لَفْظُهُ وَإِسْنَادُهُ صَحِيحٌ 

Kutoka kwa Abuu ‘Umayr bin Anas[3] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kwa upokezi wa maami zake miongoni mwa Maswahaba: “Msafara ulikuja wakashuhudia kuwa wao wameona mwezi mwandamo jana. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akawaamrisha kula (waache Swawm) na asubuhi waende mahali pa kuswalia.”[4] [Imetolewa na Ahmad na Abuu Daawuwd, na tamshi hili ni la Abuu Daawuwd, na Isnaad zake ni Swahiyh]

 

 

 

387.

وَعَنْ أَنَسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ:{كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  لَا يَغْدُو يَوْمَ اَلْفِطْرِ حَتَّى يَأْكُلَ تَمَرَاتٍ} أَخْرَجَهُ اَلْبُخَارِيُّ

وَفِي رِوَايَةٍ مُعَلَّقَةٍ وَوَصَلَهَا أَحْمَدُ: وَيَأْكُلُهُنَّ أَفْرَادًا 

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa hatoki siku ya ‘Iyd Al-Fitwr isipokuwa mpaka ale tende.” [Imetolewa na Al-Bukhaariy]

 

Na katika mapokezi mengine ni Mu’allaq lakini imeunganishwa na Ahmad: “...Na alikuwa akila moja moja Witr.”

 

 

 

388.

وَعَنِ ابْنِ بُرَيْدَةَ، عَنْ أَبِيهِ قَالَ:{كَانَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم  لَا يَخْرُجُ يَوْمَ اَلْفِطْرِ حَتَّى يَطْعَمَ، وَلَا يَطْعَمُ يَوْمَ اَلْأَضْحَى حَتَّى يُصَلِّيَ} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَاَلتِّرْمِذِيُّ، وَصَحَّحَهُ ابْنُ حِبَّانَ 

Kutoka kwa Ibn Buraydah amesema kutoka kwa baba yake kuwa amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa hatoki siku ya ‘Iyd isipokuwa mpaka ale, wala hali kitu siku ya ‘Iyd ya kuchinja[5] mpaka aswali.” [Imetolewa na Ahmad na At-Tirmidhiy na akaisahihisha Ibn Hibbaan]

 

 

 

389.

وَعَنْ أُمِّ عَطِيَّةَ قَالَتْ:{أُمِرْنَا أَنْ نُخْرِجَ اَلْعَوَاتِقَ، وَالْحُيَّضَ فِي الْعِيدَيْنِ; يَشْهَدْنَ الْخَيْرَ وَدَعْوَةَ اَلْمُسْلِمِينَ، وَيَعْتَزِلُ اَلْحُيَّضُ اَلْمُصَلَّى} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ 

Kutoka kwa Ummu ‘Atwiyyah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Tumeamrishwa[6] siku za ‘Iyd mbili (‘Iydul Fitwr na ‘Iydul Adhwhaa) tuwatoe wasichana na wenye hedhi ili wahudhuriye kheri na du’aa ya Waislamu, isipokuwa wanawake wenye hedhi waepuke mahala pa kuswalia.”[7] [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

390.

وَعَنِ ابْنِ عُمَرَ:{كَانَ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم  وَأَبُو بَكْرٍ، وَعُمَرُ: يُصَلُّونَ الْعِيدَيْنِ قَبْلَ اَلْخُطْبَةِ}  مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ 

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), Abuu Bakr na ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) walikuwa wakiswali ‘Iyd kabla ya Khutbah.”[8] [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

391.

وَعَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ: {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم  صَلَّى يَوْمَ اَلْعِيدِ رَكْعَتَيْنِ، لَمْ يُصَلِّ قَبْلَهَا وَلَا بَعْدَهَا}  أَخْرَجَهُ اَلسَّبْعَةُ 

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliswali Rakaa mbili[9] siku ya ‘Iyd na hakuswali kabla wala baada yake.”[10] [Imetolewa na As-Sab’ah (Al-Bukhaariy, Muslim, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad)]

 

 

 

392.

وَعَنْهُ: {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم  صَلَّى اَلْعِيدَ بِلَا أَذَانٍ، وَلَا إِقَامَةٍ} أَخْرَجَهُ أَبُو دَاوُدَ  . وَأَصْلُهُ فِي اَلْبُخَارِيِّ 

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema tena: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliswali ‘Iyd bila Adhana wala Iqaamah.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na chanzo chake ni katika Al-Bukhaariy]

 

 

 

393.

وَعَنْ أَبِي سَعِيدٍ قَالَ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  لَا يُصَلِّي قَبْلَ اَلْعِيدِ شَيْئًا، فَإِذَا رَجَعَ إِلَى مَنْزِلِهِ صَلَّى رَكْعَتَيْنِ}  رَوَاهُ اِبْنُ مَاجَهْ بِإِسْنَادٍ حَسَنٍ 

Kutoka kwa Abuu Sa’iyd (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) hakuswali kamwe Swalaah yoyote kabla ya Swalaah ya ‘Iyd, lakini aliporejea nyumbani alikuwa anaswali Rakaa mbili.” [Imetolewa na Ibn Maajah kupitia mlolongo mzuri wa wapokezi]

 

 

 

394.

وَعَنْهُ قَالَ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  يَخْرُجُ يَوْمَ اَلْفِطْرِ وَالْأَضْحَى إِلَى اَلْمُصَلَّى، وَأَوَّلُ شَيْءٍ يَبْدَأُ بِهِ اَلصَّلَاةُ، ثُمَّ يَنْصَرِفُ فَيَقُومُ مُقَابِلَ اَلنَّاسِ وَالنَّاسُ عَلَى صُفُوفِهِمْ فَيَعِظُهُمْ وَيَأْمُرُهُمْ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Abuu Sa’iyd (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema tena kuwa: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa anatokea siku ya Fitwr na siku ya Al-Adhwhaa, mpaka mahala pa kuswalia, na jambo la mwanzo alilofanya ni kuswali. Alipomaliza, alisimama wima kuwakabili watu walioketi chini katika safu zao. Kisha aliwakhutubia na kuwaamrisha.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

395.

وَعَنْ عَمْرِوِ بْنِ شُعَيْبٍ عَنْ أَبِيهِ عَنْ جَدِّهِ قَالَ: قَالَ نَبِيُّ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {اَلتَّكْبِيرُ فِي اَلْفِطْرِ سَبْعٌ فِي اَلْأُولَى وَخَمْسٌ فِي اَلْآخِرَةِ، وَالْقِرَاءَةُ بَعْدَهُمَا كِلْتَيْهِمَا} أَخْرَجَهُ أَبُو دَاوُدَ  وَنَقَلَ اَلتِّرْمِذِيُّ عَنِ اَلْبُخَارِيِّ تَصْحِيحَهُ 

Kutoka kwa ‘Amr bin Shu’ayb amesema kutoka kwa baba yake, naye kutoka kwa babu yake, amesema: Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Takbiyr katika Swalaah ya ‘Iydul Fitwr ni saba katika Rakaa ya kwanza[11], na tano katika Rakaa ya pili. Na kisomo (cha Qur-aan) katika zote mbili ni baada yake (Takbiyra).” [Imetolewa na Abuu Daawuwd, na At-Tirmidhiy aliisahihisha kutoka kwa Al-Bukhaariy]

 

 

 

396.

وَعَنْ أَبِي وَاقِدٍ اللَّيْثِيِّ قَالَ: {كَانَ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم  يَقْرَأُ فِي اَلْأَضْحَى وَالْفِطْرِ بِـ (ق)، وَ (اقْتَرَبَتْ) } أَخْرَجَهُ مُسْلِمٌ 

Kutoka kwa Abuu Waaqid Al-Laythiyy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa anasoma katika ‘Iydul Adhwhaa na ‘Iyd Al-Fitwr

ق[12]

na,

اقْتَرَبَتِ[13]

  [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

397.

وَعَنْ جَابِرٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  إِذَا كَانَ يَوْمُ اَلْعِيدِ خَالَفَ اَلطَّرِيقَ} أَخْرَجَهُ اَلْبُخَارِيُّ

وَلِأَبِي دَاوُدَ: عَنِ ابْنِ عُمَرَ، نَحْوُهُ 

Kutoka kwa Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Ilipofika siku ya ‘Iyd, Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akibadilisha njia[14]”. [Imetolewa na Al-Bukhaariy]

 

Naye Abuu Daawuwd amepokea Hadiyth kama hiyo kutoka kwa ‘Umar.

 

 

 

398.

وَعَنْ أَنَسٍ قَالَ: {قَدِمَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  اَلْمَدِينَةَ، وَلَهُمْ يَوْمَانِ يَلْعَبُونَ فِيهِمَا. فَقَالَ: "قَدْ أَبْدَلَكُمُ اَللَّهُ بِهِمَا خَيْرًا مِنْهُمَا: يَوْمَ اَلْأَضْحَى، وَيَوْمَ اَلْفِطْرِ} أَخْرَجَهُ أَبُو دَاوُدَ، وَالنَّسَائِيُّ بِإِسْنَادٍ صَحِيحٍ 

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuja Al-Madiynah, watu wakiwa na siku mbili wacheza michezo ndani yake (kusherehekea). Akasema: “Allaah Amewabadilishieni kilicho bora zaidi, siku ya Al-Adhwhaa (kuchinja) na siku ya Al-Fitwr (kufungua Swawm).” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy kwa Isnaad Swahiyh]

 

 

 

399.

وَعَنْ عَلِيٍّ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ: {مِنَ اَلسُّنَّةِ أَنْ يَخْرُجَ إِلَى اَلْعِيدِ مَاشِيًا} رَوَاهُ اَلتِّرْمِذِيُّ، وَحَسَّنَهُ

Kutoka kwa ‘Aliy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Ni miongoni mwa Sunnah kwenda kwa kuswali ‘Iyd kwa miguu.” [Imetolewa na At-Tirmidhiy na akaopa daraja la Hasan]

 

 

 

400.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ{  أَنَّهُمْ أَصَابَهُمْ مَطَرٌ فِي يَوْمِ عِيدٍ. فَصَلَّى بِهِمْ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم  صَلَاةَ اَلْعِيدِ فِي اَلْمَسْجِدِ}  رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ بِإِسْنَادٍ لَيِّنٍ 

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Mvua ilinyesha siku ya ‘Iyd, kwa hivyo Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akawaswalisha watu ‘Iyd ndani ya Msikiti.”[15] [Imetolewa na Abuu Daawuwd kwa Isnaad layyin (dhaifu)]

 

[1] Swalaah za Iyd mbili ni Sunnah Muakkadah (Sunnah iliyosisitizwa). Wanazuoni wengine huzitekeleza hizo kama Fardwh Kifaayah (Faradhi ya kutoshelezana). Na wengine wanasema hizo ni Fardhw ‘Ayn (wajibu wa binafsi ambayo ni sharti utekelezwe na kila mtu). Rai ya  mwanzo ndio inaonekana ni ya nguvu.

 

[2] Hadiyth hii inadhihirisha kuwa, ili kuiadhimisha ‘Iydul-Fitwr na ‘Iydul-Adhwhaa kwa Swalaah inahitajika kuswaliwa na ummati wa watu kwa amri ya kiongozi Muislamu. Kama mtu anauona mwezi mchanga wa Shawwaal na watu hawamuamini, basi mtu huyo hawezi kuacha Swawm wala kuswali ‘Iyd hiyo pekee. Anaweza kufanya hivyo pale tu ambapo Waislamu wengine wameshiriki.

 

[3] Jina la Abuu ‘Umayr ni ‘Abdullaah bin Anas bin Maalik Al-Answaariyy, naye alikuwa ndiye mtoto mkubwa kuliko wote. Alikuwa wa kutegemewa wa daraja la nne, na alikuwa mmoja wa Taabi’iyn. Aliishi muda mrefu baada ya babake.

 

[4] Hii inathibitisha kuwa ikiwa mwezi haujaonekana mnamo tarehe 29 ya mwezi wa Ramadhwaan, lakini siku inayofuata taarifa za kuthibitisha kuona mwezi zikifika, Swawm sharti isitishwe pale pale. Iwapo uthibitisho huo utafika kabla ya wakati wa Zawaal (Jua linapogeuka), Swalaah ya ‘Iyd ni sharti iswaliwe siku ile ile. Lakini ikiwa uthibitisho umefika baada ya wakati wa Zawaal basi ‘Iyd sharti iswaliwe asubuhi siku inayofuata.

 

[5] Hadiyth hii inatufunza kuwa ni Sunnah watu kula kitu fulani kabla ya kuswali ‘Iydul-Fitwr na kula baada ya ‘Iydul-Adhwhaa. Hakijapendekezwa chakula chochote maalumu, lakini kwa kuzingatia mwenendo wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), bora kula tende.

 

[6] Hadiyth hii inatufunza kuwa ni ubora wanawake waende kwenye Muswalla wa ‘Iyd na wakaswali kule pamoja na wanaume. Upendeleo huo wanapewa wanawake ili nao pia washiriki katika du’aa pamoja na Baraka za siku kuu hiyo.

 

[7] Watu wengine wanaifasiri Hadiyth hii kwamba upendeleo huu ulikuwa kwa siku zile za mwanzo mwanzo tu ili uwingi wa Ummah wa Waislam uonekane mkubwa sana, lakini wanadai kuwa, rukhsa ile kwa wanawake kuja nje ilifutwa baadaye. Lakini kuijibu hoja yao uzuri, yatosheleza kunukuu Hadiyth iliyosimuliwa na ‘Abdullaah bin ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) ambayo inasema, hata baada ya kuiteka Makkah yeye aliwaona wanawake wakienda katika Muswalla wa ‘Iyd.

 

[8] Kwa mujibu wa Sunnah, Khutbah hutolewa baada ya kuswali, na hakuna kutofautiana maoni juu ya hili. Katika enzi za Baniy Umayyah, Marwaan alileta uzushi kwamba Khutbah itolewe kabla ya kuswali, lakini desturi hiyo haina nafasi katika Uislam.

 

[9] Iwapo mtu atashindwa kuunga nyuma ya Imaam katika Swalaah ya ‘Iyd, akaswali pekee, basi Imaam Ahmad na Ath-Thawriy wana rai kwamba aswali Rakaa nne. Wanazuoni wengine wanaona kwamba aswali Rakkaa mbili. Ama Imaam Abuu Haniyfah ana rai kwamba mtu anaweza kuchagua kati ya kuswali Swalaah ya ‘Iyd iliyompita kama ni Rakaa mbili au nne [Rejea Fathul-‘Allaam (2/521)] 

 

 

[10] Kusiswaliwe Naafil (Swalaah ya Sunnah, ya khiari) kabla wala baada ya Swalaah ya ‘Iyd katika mahala pa kuswalia ‘Iyd. Lakini mtu anaweza kuswali Sunnah nyumbani.

 

[11] Kuna tofauti ya maoni miongoni mwa Wanazuoni juu ya ripoti kumi kuhusu hizi Takbiyra zaidi mbili. Mchakato sahihi ni huo uliosimuliwa katika Hadiyth hii. Watu wengine wanaegemea katika Hadiyth iliyosimuliwa na Ibn Mas-‘uwd (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) kuwa baki ya Takbiyratul-Iftitaah (ya kufungulia Swalaah),  na Takbiyratur-Rukuwu’ (ya kurukuu) zipo Takbiyra nyenginezo sita; tatu za kutamka ndani ya Rakaa ya kwanza kabla ya kisomo, na tatu zingine za kutamka ndani ya Rakaa ya pili baada ya kisomo. Kwa usahihi, Hadiyth iliyosimuliwa na Ibn Mas-‘uwd si ya kutegemewa.

 

[12] Qaaf (50)

 

[13] Al-Qamar: (54)

 

[14] Yaani kama alipokua akienda kuswali ‘Iyd alifuata njia hii, basi aliporudi kutoka huko alirudi kwa njia nyingine, kwa sababu mahala mbalimbali hizo zitashuhudia  upitaji njia kuenda kuswali, na hadhi ya Uislam itakuwa juu.

 

[15] Hadiyth hii inathibitisha kuwa itokeapo ugumu kuswalia Muswalla wa ‘Iyd (Pahala pa kuswalia ‘Iyd), ni rukhsa kuswali ‘Iyd ndani ya Msikiti.

 

 

Share