Imaam Akiswalisha Haingii Katika Mihraab
SWALI:
Assalamu aleikum. Amma baad. mimi nina tashwishi kuhusu na hali ya baadhi ya misikiti yalivyo. ninapozuru hayo misikiti ninaona kuwa imamu huwa haingii kwenye mihrabu je ndugu itanisaidiaje kuhusu hili jambo ambalo ni geni kwa wengi? Shukran
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani kwa swali lako nyeti kama hilo kuhusu uswalishaji wa Imaam ambaye amewashangaza kwa hilo la kuswalisha kwake nje ya Mihraab. Ni kweli jambo kama hilo litaonekana geni kwa wengi haswa katika Afrika Mashariki hata nchi nyingi za Bara Asia.
Tufahamu kuwa jambo hilo si geni katika Dini yetu ya Uislamu. Msikiti wa kwanza wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Madiynah haukuwa na Mihraab bali sehemu ya Qiblah kulikuwa na ishara tu. Huu ndio mtindo ambao utatumika sana haswa Bara Ulaya kwa watu kukodisha majumba kwa sababu ya Swalah na hivyo huwa hakuwezekani kujenga Mihraab. Msikiti huo ulibaki katika hali huyo mpaka akafariki Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na hali hiyo ikaendelea kwa Makhalifa wake na hadi baada ya Maswahaba.
Baadaye ndio Mihraab ilianzishwa na kuwepo mpaka sasa.
Baadhi ya Maulamaa wamesema ni jambo ambalo halikuwepo katika wakati wa Mtume, na hivyo halifai. Wengine wakasema si vibaya kwa kuwa ni kielelezo cha Qiblah mradi tu isiwe inafanana na Mihraab ambayo inawekwa na wakiristo kwenye makanisa yao.
Jambo hilo halifai litushughulishe sana kwani kuswalisha kwa Imaam akiwa katika Mihraab si katika nguzo wala Sunnah ya Swalah. Akiswalisha ndani ya Mihraab Swalah inakubaliwa na akiswalisha nje pia Swalah yake na yenu inakubaliwa.
Wakiweza watu kujenga misikiti ambayo haina Mihraab na kukawekwa alama tu mbele au mchoro wa kujulisha Qiblah basi ni bora zaidi ili kufanana na msikiti wakati wa zama za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam na Makhalifa wake (Radhiya Allaahu 'anhum).
Allaah Aliyetukuka Atupatie tawfiki katika kufuata maagizo yake na yale ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Atufanye ni wenye kufanikiwa katika Nyumba mbili.
Na Allaah Anajua zaidi