16-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Swalaah: Mlango Wa Swalaatul-Istisqaa (Swalaah Ya Mvua)

 

بُلُوغُ الْمَرام

 

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتَابُ اَلصَّلَاةِ

 

Kitabu Cha Swalaah

 

 

بَابُ صَلَاةِ اَلِاسْتِسْقَاءِ

16-Mlango Wa Swalaatul-Istisqaa[1] (Swalaah Ya Mvua)

 

 

 

 

 

406.

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {خَرَجَ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم  مُتَوَاضِعًا، مُتَبَذِّلًا، مُتَخَشِّعًا، مُتَرَسِّلًا، مُتَضَرِّعًا، فَصَلَّى رَكْعَتَيْنِ، كَمَا يُصَلِّي فِي اَلْعِيدِ، لَمْ يَخْطُبْ خُطْبَتَكُمْ هَذِهِ} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ، وَصَحَّحَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ، وَأَبُو عَوَانَةَ، وَابْنُ حِبَّانَ 

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alitoka (kwenda kuswali Swalaah ya kuomba mvua) huku akiwa mnyonge, amevaa nguo duni na katika hali ya udhalili na mnyenyekevu, anaomba du’aa. Akaswali Rakaa mbili kama za Swalaah ya ‘Iyd,[2] lakini hakukhutubu kama khutbah yenu hii.”[3] [Imetolewa na Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad) na wakaisahihisha At-Tirmidhiy, Abuu ‘Awaanah na Ibn Hibbaan]

 

 

 

407.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {شَكَا اَلنَّاسُ إِلَى رَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  قُحُوطَ الْمَطَرِ، فَأَمَرَ بِمِنْبَرٍ، فَوُضِعَ لَهُ فِي اَلْمُصَلَّى، وَوَعَدَ اَلنَّاسَ يَوْمًا يَخْرُجُونَ فِيهِ، فَخَرَجَ حِينَ بَدَا حَاجِبُ اَلشَّمْسِ، فَقَعَدَ عَلَى اَلْمِنْبَرِ، فَكَبَّرَ وَحَمِدَ اَللَّهَ، ثُمَّ قَالَ: "إِنَّكُمْ شَكَوْتُمْ جَدَبَ دِيَارِكُمْ، وَقَدْ أَمَرَكُمْ اَللَّهُ أَنْ تَدْعُوَهُ، وَوَعَدَكُمْ أَنْ يَسْتَجِيبَ لَكُمْ، ثُمَّ قَالَ: اَلْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ اَلْعَالَمِينَ، اَلرَّحْمَنِ اَلرَّحِيمِ، مَالِكِ يَوْمِ اَلدِّينِ، لَا إِلَهَ إِلَّا اَللَّهُ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ، اَللَّهُمَّ أَنْتَ اَللَّهُ، لَا إِلَهَ إِلَّا أَنْتَ، أَنْتَ اَلْغَنِيُّ وَنَحْنُ اَلْفُقَرَاءُ، أَنْزِلْ عَلَيْنَا الْغَيْثَ، وَاجْعَلْ مَا أَنْزَلْتَ قُوَّةً وَبَلَاغًا إِلَى حِينٍ" ثُمَّ رَفَعَ يَدَيْهِ، فَلَمْ يَزَلْ حَتَّى رُئِيَ بَيَاضُ إِبِطَيْهِ، ثُمَّ حَوَّلَ إِلَى اَلنَّاسِ ظَهْرَهُ، وَقَلَبَ رِدَاءَهُ، وَهُوَ رَافِعٌ يَدَيْهِ، ثُمَّ أَقْبِلَ عَلَى اَلنَّاسِ وَنَزَلَ، وَصَلَّى رَكْعَتَيْنِ، فَأَنْشَأَ اَللَّهُ سَحَابَةً، فَرَعَدَتْ، وَبَرَقَتْ، ثُمَّ أَمْطَرَتْ} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ وَقَالَ: "غَرِيبٌ، وَإِسْنَادُهُ جَيِّدٌ"

وَقِصَّةُ اَلتَّحْوِيلِ فِي "اَلصَّحِيحِ" مِنْ: حَدِيثِ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ زَيْدٍ، وَفِيهِ: {فَتَوَجَّهَ إِلَى اَلْقِبْلَةِ، يَدْعُو، ثُمَّ صَلَّى رَكْعَتَيْنِ، جَهَرَ فِيهِمَا بِالْقِرَاءَةِ}

وَلِلدَّارَقُطْنِيِّ مِنْ مُرْسَلِ أَبِي جَعْفَرٍ اَلْبَاقِرِ: وَحَوَّلَ رِدَاءَهُ؛ لِيَتَحَوَّلَ اَلْقَحْطُ 

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Watu walimlalamikia Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) uhaba wa mvua. Kwa hivyo akaamrisha ijengwe Mimbar, akawekewa hapo Al-Muswallaa, na akaagana na watu siku watakayotoka watu kuja hapo. Akatoka jua lilipoanza kudhihiri. Akakaa juu ya Mimbar, akapiga Takbiyra na akamhimidi Allaah, akasema: Hakika nyinyi mmelalamikia ukame wa maskani zenu, Allaah Amekuamrisheni mumuombe Yeye na Amekuahidini kuwa Atakujibuni. Kisha akasema:  “AlhamduliLLaah, Rabb wa ulimwengu, Ar-Rahmaan,  Mwenye kurehemu, Mfalme wa siku ya malipo, hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah, Hufanya Alitakalo. Ee Allaah! Wewe ni Allaah hapana mwabudiwa wa haki ila Wewe, Wewe ni Mkwasi, nasi ni mafukara. Tuteremshie mvua na Ukifanye Utakachotuteremshia kiwe nguvu na chenye kutufikisha mpaka muda (wa mwisho).” Akanyanyua mikono,[4] na akawa anazidi kuinyanyua hadi weupe wa kwapa zake unaonekana. Kisha akawapa mgongo watu, na akageuza ridaa (juba) yake ya juu huku mikono yake kainyanyua juu. Akawageukia watu, akashuka akawaswalisha Rakaa mbili. Kisha Allaah Akaanzisha wingu, radi na umeme, kisha ikanyesha mvua.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd, ambaye aliipa daraja la Ghaarib, na Isnaad yake ni nzuri]

Kisa cha kugeuza nguo kimetajwa katika Swahiyh Al-Bukhaariy kutokana na usimulizi wa ‘Abdullaah bin Zayd, na kinasema: “(Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ)) alielekea Qiblah huku akiomba du’aa, akaswalisha Rakaa mbili na akasoma kwa sauti.”

 

Na Ad-Daaraqutwniyy alisimulia vivyo hivyo katika Hadiyth Mursal iliyosimuliwa na Abuu Ja’far Al-Baaqir[5]: “(Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ)) aligeuza ridaa (juba) yake ili ukame ugeuke.”

 

 

 

408.

 وَعَنْ أَنَسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  {أَنَّ رَجُلًا دَخَلَ اَلْمَسْجِدَ يَوْمَ اَلْجُمُعَةِ، وَالنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم   قَائِمٌ يَخْطُبُ. فَقَالَ: يَا رَسُولَ اَللَّهِ، هَلَكَتِ اَلْأَمْوَالُ، وَانْقَطَعَتِ اَلسُّبُلُ، فَادْعُ اَللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ يُغِيثُنَا، فَرَفَعَ يَدَيْهِ، ثُمَّ قَالَ: "اَللَّهُمَّ أَغِثْنَا، اَللَّهُمَّ أَغِثْنَا..." فَذَكَرَ اَلْحَدِيثَ، وَفِيهِ اَلدُّعَاءُ بِإِمْسَاكِهَا} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ 

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Mtu aliingia Msikitini katika siku ya Ijumaa huku Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akiwa amesimama akikhutubia. Akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Mali imeangamia na njia zimekatika, basi muombe Allaah (عزّ وجلّ)  Atuletee mvua. (Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ)) akainua mikono yake, akasema: Ee Allaah! (Tuteremshie mvua), Ee Allaah! Tuteremshie mvua.” Msimulizi akataja Hadiyth yote, ndani yake kuna du’aa za kuzuia mvua.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

409.

وَعَنْ أَنَسٍ; {أَنَّ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  كَانَ إِذَا قَحِطُوا يَسْتَسْقِي بِالْعَبَّاسِ بْنِ عَبْدِ اَلْمُطَّلِبِ. وَقَالَ: اَللَّهُمَّ إِنَّا كُنَّا نَسْتَسْقِي إِلَيْكَ بِنَبِيِّنَا فَتَسْقِينَا، وَإِنَّا نَتَوَسَّلُ إِلَيْكَ بِعَمِّ نَبِيِّنَا فَاسْقِنَا، فَيُسْقَوْنَ} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيُّ

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) tena amesema: “Walikuwa walipofikwa na ukame, ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) alikuwa akiomba mvua[6] kwa Al-‘Abbaas bin ‘Abd Al-Mutwallib[7] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ), naye akasema: Ee Allaah! Tulikuwa tukikuomba kwa Nabiy wetu, na Ukatuteremshia maji. Sasa tunakuomba kwa Ammi wa Nabiy wetu. Kwa hivyo tunakuomba mvua. Wakawa wanateremshiwa mvua.” [Imetolewa na Al-Bukhaariy]

 

 

 

410.

وَعَنْ أَنَسٍ قَالَ: {أَصَابَنَا وَنَحْنُ مَعَ رَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم   مَطَرٌ قَالَ: فَحَسَرَ ثَوْبَهُ، حَتَّى أَصَابَهُ مِنَ اَلْمَطَرِ، وَقَالَ: "إِنَّهُ حَدِيثُ عَهْدٍ بِرَبِّهِ"} رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Tulipata mvua wakati tulipokuwa pamoja na Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), akafunua nguo yake hadi akapata mvua ikamnyeshea na akasema: Imetoka sasa hivi kutoka kwa Rabb wake.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

411.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا; أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم   كَانَ إِذَا رَأَى اَلْمَطَرَ قَالَ: {اَللَّهُمَّ صَيِّبًا نَافِعًا} أَخْرَجَاهُ 

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema kuwa: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipoona mvua alikuwa akisema: Ee Allah! Tumiminie mvua yenye manufaa.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

412.

وَعَنْ سَعْدٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم   دَعَا فِي اَلِاسْتِسْقَاءِ: {اَللَّهُمَّ جَلِّلْنَا سَحَابًا، كَثِيفًا، قَصِيفًا، دَلُوقًا، ضَحُوكًا، تُمْطِرُنَا مِنْهُ رَذَاذًا، قِطْقِطًا، سَجْلًا، يَا ذَا اَلْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ} رَوَاهُ أَبُو عَوَانَةَ فِي "صَحِيحِهِ

Kutoka kwa Sa’d (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliomba mvua inyeshe[8]: Ee Allaah! Tufunike kwa mawingu mazito mengi, yenye ngurumo, ya kuteleza, na yenye umeme na kutokea humo Utushushie mvua ya kumwagika na ya manyunyu. Ee Mwenye Ujalali na Utukufu.” [Imetolewa na Abuu ‘Awaanah katika Swahiyh yake]

 

 

 

413.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم   قَالَ: {خَرَجَ سُلَيْمَانُ عَلَيْهِ اَلسَّلَامُ يَسْتَسْقِي، فَرَأَى نَمْلَةً مُسْتَلْقِيَةً عَلَى ظَهْرِهَا رَافِعَةً قَوَائِمَهَا إِلَى اَلسَّمَاءِ تَقُولُ: اَللَّهُمَّ إِنَّا خَلْقٌ مِنْ خَلْقِكَ، لَيْسَ بِنَا غِنًى عَنْ سُقْيَاكَ، فَقَالَ: ارْجِعُوا لَقَدْ سُقِيتُمْ بِدَعْوَةِ غَيْرِكُمْ} رَوَاهُ أَحْمَدُ وَصَحَّحَهُ اَلْحَاكِمُ 

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Sulaymaan (عَلَيْهِ اَلسَّلَامُ) alitoka kuenda kuomba mvua, akamuona sisimizi amelala chali huku amenyanyua miguu yake mbinguni akisema:[9] “Ee Allaah! Sisi ni miongoni mwa viumbe Wako, na hatuwezi kuishi bila mvua Yako.” Akasema (kuwaambia Maswahaba): “Rudini, kwani mumenyeshewewa kwa du’aa za wengine.” [Imetolewa na Ahmad na akaisahihisha Al-Haakim]

 

 

 

414.

وَعَنْ أَنَسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم   اسْتَسْقَى فَأَشَارَ بِظَهْرِ كَفَّيْهِ إِلَى اَلسَّمَاءِ} أَخْرَجَهُ مُسْلِمٌ 

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliomba mvua, akaashiria kwa nyuma ya viganja[10] vyake kuelekea angani.” [Imetolewa na Muslim]

 

[1] Maana ya kifasihi ya Istisqaa ni “Kutafuta au kuomba maji.” Katika lugha ya ki Shariy’ah, hutumika kuuswalisha mkusanyiko maalumu ambamo du’aa huombwa ya kuomba mvua.  Ziko aina tatu za Istisqaa: (a) Adnaa (ndogo kuliko zote), (b) Awsatw (ya kati), (c) A’alaa (kubwa kuliko zote). Adnaa inamaanisha maombi ya mdomo tu. Awsatw ni maombi ya mdomo katika jamaa baada ya kuswali Swalaah ya Faradhi.   A’alaa inahitaji Swalaah maalumu ya jamaa kuomba mvua. Mchakato sahihi wa kuswali Istisqaa ni kuswali Rakaa mbili. Kisomo kiwe kwa sauti kubwa, kikifuatiwa na Khutbah mbili, na mwishowe du’aa iombwe kwa kuelekea Qiblah.

[2] Kuna tofauti ya idadi na mfululizo wa kutamka Takbiyra kati ya Swalaah ya ‘Iyd na Swalaah ya Istisqaa. Khutbah ni sharti ifuatie Swalaah ya Istisqaa, kwa namna ile ile kama katika Swalaah ya ‘Iyd.

[3] Maneno yale yasemayo, “Hakutoa aina yako ya Khutbah” inaashiria kuwa haikuwa Khutbah yake ndefu na ya kuchosha. Shah Waliyullaah katika kitabu chake ‘Hujjatullaahil-Baalighah’ amesema kuwa ziko njia nyingi za Istisqaa ambazo zimehusishwa na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ). Njia nzuri kuliko zote ambazo watu wanaweza kuzifuata ni kuwa watu wote wakusanyike msituni na Imaam; wawe wamevaa nguo za marapurapu, na wamuombe Allaah (عزّ وجلّ) huku wakilia machozi na nyoyo zilizojaa huzuni. Kisha Imaam aswalishe Swalaah yenye Rakaa mbili kwa kisomo cha sauti kubwa. Baada ya Swalaah, Imaam atoe Khutbah, kwa kumuomba Allaah (عزّ وجلّ) wakati uso wake umeelekea Qiblah, na kisha ageuze ridaa (juba) lake ndani nje.

[4] Kwa hivyo tunafahamishwa kuwa, katika Swalaah ya Istisqaa, du’aa zisomwe huku mikono imenyanyuliwa juu. Imaam An-Nawawi amekusanya Hadiyth ishirini juu ya jambo hili. Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesimulia kuwa hakuwahi kamwe kumuona Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akinyanyua mikono yake katika du’aa zozote isipokuwa hizo za Istisqaa. Hii inadhihirisha ukweli kwamba hakuwahi kumuona Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akinyanyua mikono yake juu sana katika Swalaah yoyote ile isipokuwa hiyo ya Istisqaa.

[5] Abuu Ja’far Al-Baaqir ndiye Muhamaad Al-Baaqir bin ‘Aliy Zainul-‘Aabidiyn bin Husayn bin ‘Aliy bin Abiy Twaalib, Aliitwa Baaqir kwa ajili ya ‘Ilmu au ujuzi wake mpana. Alizaliwa mnamo mwaka 56 A.H. na akafa mnamo mwaka 117 A.H. akiwa na umri wa miaka 63, na akazikwa Al-Baqi’.

[6] Hadiyth hii inadhihirisha  kwamba, inafaa kuwataka watu wenye taqwa walio hai watuombee du’aa za Istisqaa, na wala siyo watu waliokwisha kufa. Watu wengi wanaamini kuwa du’aa zinaweza kuombwa kupitia kwa wafu, kwa kuwafanya wao wawe mapitio. Hivi ni kumshirikisha Allaah (عزّ وجلّ). Ingekuwa ni sahihi kuomba kwa kupitia wafu, ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) asingemuomba ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) kuwaombea du’aa badala ya Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ).

[7] Al-‘Abbaas bin Abd Al-Mutwallib ndiye Ammi yake Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) na alipewa jina la Abul-Fadhwl. Alikuwa ndiye anayewapa maji mahujaji Makkah na ujenzi wa Ka’bah. Alihudhuria Bay’atul-‘Aqabah (mkataba ‘Aqabah) kuhakikisha Maanswaar walikuwa waaminifu na wakweli katika ahadi zao, alikuwa hajawa Muislam hadi wakati ule. Alikamatwa pamoja na makafiri katika vita vya Badr, akasilimu kabla ya kuiteka Makkah, naye alishiriki kuiteka, alisimama imara katika vita vya Hunayn. Alikufa mwezi wa Rajab au Ramadhwaan mwaka 32 A.H. na akazikwa Al-Baqi’.

 

[8] Du’aa nyingi kuhusu Istisqaa zimeripotiwa kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), na hii ni mojawapo.

[9] Mtindo wa kuwachukua wanyama katika Swalaah ya Istisqaa imethibitishwa kupitia Hadiyth hii. Kwa kuwa Allaah pengine Anaweza kuzikubali du’aa zao.

[10] Wanazuoni wanasema, iwapo du’aa itaombwa ili kupata Baraka za Allaah, mtu sharti anyanyue mikono yake kuomba du’aa kama kawaida (viganja viwe vinamwelekea huyo muombaji du’aa katika Swalaah hiyo). Lakini ikiwa du’aa inaombwa kuliepusha jambo ovu, mnyanyuo wa mikono sharti ugeuzwe (mikono inyanyuliwe, na viganja vikielekea nje). Inaelekea kuwa Allaah Ageuze ile hali. Kule kugeuza ridaa (juba) ndani kuwe nje pia kunamaanisha hivyo hivyo; na hali kadhalika tendo la kuelekeza nyuma ya viganja nje inaashiria ni kuomba Allaah Ayasogeze mawingu chini (yakiwa yamejaa maji).

 

 

Share