17-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Swalaah: Mlango Wa Adabu Za Mavazi
بُلُوغُ الْمَرام
Buluwgh Al-Maraam
كِتَابُ اَلصَّلَاةِ
Kitabu Cha Swalaah
بَابُ اَللِّبَاسِ
17-Mlango Wa Adabu Za Mavazi
415.
عَنْ أَبِي عَامِرٍ اَلْأَشْعَرِيِّ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {لَيَكُونَنَّ مِنْ أُمَّتِي أَقْوَامٌ يَسْتَحِلُّونَ اَلْحِرَ وَالْحَرِيرَ} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ، وَأَصْلُهُ فِي اَلْبُخَارِيِّ
Kutoka kwa Abuu ‘Aamir Al-Ash’ariyy[1] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Kutakuwepo miongoni mwa ummah wangu watu watakaohalalisha zinaa pamoja na hariri.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na chanzo chake[2] kimo katika Al-Bukhaariy]
416.
وَعَنْ حُذَيْفَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ: {نَهَى اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم أَنْ نَشْرَبَ فِي آنِيَةِ اَلذَّهَبِ وَالْفِضَّةِ، وَأَنْ نَأْكُلَ فِيهَا، وَعَنْ لُبْسِ اَلْحَرِيرِ وَالدِّيبَاجِ، وَأَنْ نَجْلِسَ عَلَيْهِ} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيُّ
Kutoka kwa Khudhayfah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) ametukataza kunywa katika vyombo vya dhahabu na fedha, na kula humo na kuvaa hariri na ad-diybaaj (vitambaa vya hariri vya vito na vilotariziwa kwa dhahabu na fedha) na kukaa juu yake.” [Imetolewa na Al-Bukhaariy]
417.
وَعَنْ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ: {نَهَى اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم عَنْ لُبْسِ اَلْحَرِيرِ إِلَّا مَوْضِعَ إِصْبَعَيْنِ، أَوْ ثَلَاثٍ، أَوْ أَرْبَعٍ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَّفْظُ لِمُسْلِمٍ
Kutoka kwa ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amekataza kuvaa hariri isipokuwa sehemu ya vidole viwili, vitatu au vinne.”[3] [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Muslim]
418.
وَعَنْ أَنَسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم {رَخَّصَ لِعَبْدِ اَلرَّحْمَنِ بْنِ عَوْفٍ، وَالزُّبَيْرِ فِي قَمِيصِ اَلْحَرِيرِ، فِي سَفَرٍ، مِنْ حَكَّةٍ كَانَتْ بِهِمَا} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliwaruhusu ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf na Az-Zubayr[4] wavae kanzu za hariri katika safari kwa sababu ya upele wa kuwashwa ngozi waliokuwa nao.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
419.
وَعَنْ عَلِيٍّ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ قَالَ:{كَسَانِي اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم حُلَّةً سِيَرَاءَ، فَخَرَجْتُ فِيهَا، فَرَأَيْتُ اَلْغَضَبَ فِي وَجْهِهِ، فَشَقَقْتُهَا بَيْنَ نِسَائِي} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَهَذَا لَفْظُ مُسْلِمٍ
Kutoka kwa ‘Aliy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alinipa mie juba lenye mistari[5] yenye hariri, halafu nikalivaa, nikaona ghadhabu usoni mwake, nililikatakata (na kuligawa) baina ya ahli zangu wanawake.” [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Muslim]
420.
وَعَنْ أَبِي مُوسَى رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {أُحِلَّ اَلذَّهَبُ وَالْحَرِيرُ لِإِنَاثِ أُمَّتِي، وَحُرِّمَ عَلَى ذُكُورِهِمْ.} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَالنَّسَائِيُّ، وَاَلتِّرْمِذِيُّ وَصَحَّحَهُ
Kutoka kwa Abuu Muwsaa (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Dhahabu na hariri vimeruhusiwa kwa wanawake wa Ummah wangu, na vimekatazwa kwa wanaume wao.” [Imetolewa na Ahmad, An-Nisaaiy na At-Tirmidhiy, naye aliisahihisha]
421.
وَعَنْ عِمْرَانَ بْنِ حُصَيْنٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا; أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {إِنَّ اَللَّهَ يُحِبُّ إِذَا أَنْعَمَ عَلَى عَبْدٍ أَنْ يَرَى أَثَرَ نِعْمَتِهِ عَلَيْهِ} رَوَاهُ اَلْبَيْهَقِيُّ
Kutoka kwa ‘Imraan bin Huswayn (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Allaah Anapomneemesha mja Wake hupenda kuona athari ya neema yake juu yake.”[6] [Imetolewa na Al-Bayhaqiyy]
422.
وَعَنْ عَلِيٍّ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم { نَهَى عَنْ لُبْسِ الْقَسِيِّ وَالْمُعَصْفَرِ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ
Kutoka kwa ‘Aliy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amekataza kuvaa hariri na nguo zenye rangi ya zaafarani. [Imetolewa na Muslim]
423.
وَعَنْ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ عَمْرِوٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا، قَالَ: {رَأَى عَلَيَّ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم ثَوْبَيْنِ مُعَصْفَرَيْنِ، فَقَالَ: "أُمُّكَ أَمَرَتْكَ بِهَذَا؟"} رَوَاهُ مُسْلِمٌ
Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amr (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliniona mimi nikiwa nimevaa nguo mbili za rangi ya zaafarani, akasema: “Mama yako ndiye aliyekuamrisha ufanye hivi?”[7] [Imetolewa na Muslim]
424.
وَعَنْ أَسْمَاءَ بِنْتِ أَبِي بَكْرٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا {أَنَّهَا أَخْرَجَتْ جُبَّةَ رَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم مَكْفُوفَةَ اَلْجَيْبِ وَالْكُمَّيْنِ وَالْفَرْجَيْنِ، بِالدِّيبَاجِ} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ
وَأَصْلُهُ فِي "مُسْلِمٍ"، وَزَادَ: {كَانَتْ عِنْدَ عَائِشَةَ حَتَّى قُبِضَتْ، فَقَبَضْتُهَا، وَكَانَ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم يَلْبَسُهَا، فَنَحْنُ نَغْسِلُهَا لِلْمَرْضَى نَسْتَشْفِي بِهَا}
وَزَادَ اَلْبُخَارِيُّ فِي "اَلْأَدَبِ اَلْمُفْرَدِ". {وَكَانَ يَلْبَسُهَا لِلْوَفْدِ وَالْجُمُعَةِ}
Kutoka kwa Asmaa bint Abiy Bakr (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa: “Yeye alilitoa joho la Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) lililokuwa limedariziwa kwa hariri nzito mifukoni, mikononi na sehemu mbili zilizo wazi.”[8] [Imetolewa na Abuu Daawuwd]
Na chanzo chake kimo katika Swahiyh Muslim na kina nyongeza: “Lilikuwa kwa ‘Aaishah hadi alipokufa, nikalichukua mimi. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akilivaa, nasi tulikuwa tukiliosha kwa ajili ya wagonjwa waliokuwa wakilitumia kwa kuponywa nalo.”
Na Al-Bukhaariy aliongezea katika kitabu Adab Al-Mufrad[9]: “Alikuwa akilivaa kwa ajili ya wageni[10] na siku za Ijumaa.” [Imetolewa na Muslim]
[1] Abuu ‘Aamir Al-Ash’ariyy ndiye anayeitwa ‘Abdullaah bin Haaniy au ‘Ubayd bin Wahaab. Alikuwa ni Swahaba aliyelowea Sham, na alikuwa wakati wa utawala wa ‘Abdul Maalik bin Marwaan.
[2] Inamaanisha kwamba, watakuwa wakivaa mavazi ya hariri na watakuwa wanatenda zinaa kwa wingi sana ikiwa vitu hivi havitaharamishwa.
[3] Uvaaji wa mavazi ya hariri umekatazwa kwa wanaume. Hata hivyo inaruhusiwa kwa wanaume kuvaa vazi lenye msitari usiozidi sentimita tano hadi kumi. Lakini inaruhusiwa kwa mwanaume kuvaa vazi la hariri iwapo ana maradhi ya kuwashwa ngozi yaani eczema, n.k., au iwapo anashambuliwa na chawa. Kwa kuwa mavazi ya hariri humsaidia mtu anayeumwa magonjwa kama hayo, wanaruhusiwa kuendelea kuyatumia mpaka wapone.
[4] Az-Zubayr hyu ndiye Az-Zubayr bin Al-‘Awwaam bin Khuwaylid bin Asad Al-Qurayshiy Al-Asad, ambaye Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimwita mwenyewe kuwa ni mfuasi mtiifu wake. Ni mtoto wa Swafiyyah bint Abdil-Muttwalib shangazi yake Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Zubayr ni miongoni mwa Maswahaba kumi waliobashiriwa Jannah. Alikuwa ni miongoni mwa mashujaa katika vita vya Kiislamu. Alifariki mwaka 36H baada ya kurejea kutoka vita vya Al-Jamal.
[5] Vazi hili alipewa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) na Mfalme wa jimbo la Aila. Lilikuwa na taraza (nakshi) za nyuzi za dhahabu na hariri.
[6] Hii inaweka wazi kwamba, kula chakula kizuri na kuvaa nguo nzuri sio dhidi ya taqwa. Kwa mujibu wa Hadiyth kwamba Allaah (عزّ وجلّ) Anapenda uzuri na usafi. Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hatoingia Jannah ambaye moyoni mwake mna kiburi uzito wa chembe (au sisimizi)). Mtu mmoja akauliza: “Mtu hupenda nguo yake iwe nzuri na viatu vyake viwe vizuri [itakuwaje?]” Akasema: ((Hakika Allaah ni Mzuri Anapenda Uzuri. Kiburi ni kukataa haki na kudharau watu)). [Muslim]
[7] Hadiyth yote inasema hivi: “’Abdullaah bin ‘Amr (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) alimuomba ruhusa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kuenda kuliosha lile vazi. Jibu lake (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikanusha, na akamuamrisha alichome, ambayo bila shaka ni adhabu.”
[8] Diybaaj ni hariri nzito iliyotariziwa kwa dhahabu.
[9] Hili ndilo jina la kitabu kilichoandikwa na Imaam Al-Bukhaariy.
[10] Hii inathibitisha kuwa, kuvaa mavazi mazuri inaruhusiwa siku za Ijumaa, na katika ‘Iyd zote mbili, na katika hadhara za watu.