Ramadhwaan: Uzushi Wa Adhkaar Baada Ya Kila Rakaa Za Swalaah Ya Taraawiyh
Uzushi Wa Adhkaar Baada Ya Kila Rakaa Za Swalaah Ya Taraawiyh
SWALI LA KWANZA:
Assalam Aleikum.amma baad nina maswala machache kuhusu Ramadhwaan na yalyomo ndani yake.
1.je kunao adhkar ambazo mtume Salla Allahu alayhi wa sallam alizileta baada ya kila rakaa mbili za taraweeeh ambayo inasomwa hivi: "Ashadu anlaaillaha ila allah nastaghfiru Allah nasalukajannatu wanaudhubika minanari” (mara 3) "Allahuma Innaka Afuwwun tuhibulafwaa faafuanna" (mara 3) hii nyiradi nina isikia katika kila kipindi cha swala watu wakileta kwa sauti. Je ina juzu?
SWALI LA PILI:
Assalamu Alaikum,
Ndugu waislamu naomba kuuliza, Je iliwahi kuthibiti enzi za Nabiy kwa mwezi wa Ramadhwaani kila baada ya swala kuleta adhkar kama hizi za sasa (Ash-hada alaa ilaa hailallah,ya Rabbi nastaghfiru llah,nas-alu kaljana na kuendelea)?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hayo ni bid’ah (uzushi) kwa sababu:
Kwanza: Hakuna dalili kama Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akileta adhkaar yoyote kila baada ya Rakaa mbili katika Swalaah ya Taraawiyh. Kufanya hivyo itakuwa ni kinyume na mafunzo ya Sunnah na hivyo itakuwa ni bid'ah (uzushi).
Bid'ah hii imeenea mno katika Misikiti na baadhi ya Misikiti huweka hata mabango yaliyoandikwa Adhkaar hizo kwa ajili ya watu waihifadhi ili wasiome katika mapumziko hayo. Hivyo inatupasa tuepukane na bid'ah kama hizo na tufuate mafunzo Sahihi ya Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Nayo ni kwamba unapomaliza kabisa Swalaah ya Qiyaamul-Layl ambayo kwa jina lingine ni Taraawiyh au Tahajjud, ambazo zinamalizwa kwa Swalaah ya Witr, unatakiwa usome ifuatavyo na huwa ndio mwisho wa Swalaah kabisa.
سُـبْحانَ المَلِكِ القُدّوس
Subhaanal-Malikil-Qudduws
"Ametakasika Mfalme Mtakatifu"
(mara tatu na mara ya mwisho unavuta kwa sauti na kusema)
ربِّ الملائكةِ والرّوح
Rabbul-Malaaikati War-Ruwh
"Rabb wa Malaika na wa Jibriyl"
Pili: Ni bi’dah kusoma adhkaar au du’aa au aina yoyote ya adhkaar kwa sauti na mkusanyiko wa watu. Kwa maelezo zaidi bonyeza viungo vifuatavyo upate faida:
Kusoma Uradi Kwa Pamoja Kila Mwezi Kwa Kukusanyika Inafaa?
Na Allaah Anajua zaidi.