01-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Swiyaam
بُلُوغُ الْمَرام
Buluwgh Al-Maraam
كِتَابُ اَلصِّيَامِ
05-Kitabu Cha Swiyaam[1]
527.
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {لَا تَقَدَّمُوا رَمَضَانَ بِصَوْمِ يَوْمٍ وَلَا يَوْمَيْنِ، إِلَّا رَجُلٌ كَانَ يَصُومُ صَوْمًا، فَلْيَصُمْهُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Msitangulie Ramadhwaan kwa Swawm siku moja au mbili[2] isipokuwa mtu alikuwa ana Swawm basi afunge.”[3] [Al-Bukhaariy, Muslim]
528.
وَعَنْ عَمَّارِ بْنِ يَاسِرٍ رضى الله عنه قَالَ: {مَنْ صَامَ اَلْيَوْمَ اَلَّذِي يُشَكُّ فِيهِ فَقَدْ عَصَى أَبَا اَلْقَاسِمِ صلى الله عليه وسلم} وَذَكَرَهُ اَلْبُخَارِيُّ تَعْلِيقًا، وَوَصَلَهُ اَلْخَمْسَةُ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ خُزَيْمَةَ، وَابْنُ حِبَّانَ
Kutoka kwa ‘Ammaar bin Yaasir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Mwenye kufunga siku ambayo inatiliwa mashaka,[4] atakuwa amemuasi Abul-Qaasim (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ).” [Al-Bukhaariy aliitaja kuwa ni Mu’allaq, lakini Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad) waliifuatilia Hadiyth hii kuwa ni Mawsuwl, na akaisahihisha Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan]
529.
وَعَنِ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَقُولُ: {إِذَا رَأَيْتُمُوهُ فَصُومُوا، وَإِذَا رَأَيْتُمُوهُ فَأَفْطِرُوا، فَإِنْ غُمَّ عَلَيْكُمْ فَاقْدُرُوا لَهُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
وَلِمُسْلِمٍ: {فَإِنْ أُغْمِيَ عَلَيْكُمْ فَاقْدُرُوا لَهُ ثَلَاثِينَ}
وَلِلْبُخَارِيِّ: {فَأَكْمِلُوا اَلْعِدَّةَ ثَلَاثِينَ}
وَلَهُ فِي حَدِيثِ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه {فَأَكْمِلُوا عِدَّةَ شَعْبَانَ ثَلَاثِينَ}
Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema Nilimsikia Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akisema: “Mkiuona mwezi mpya fungeni, na msifungue hadi mmeuona. Lakini ikiwa anga ina mawingu, basi ukadirieni.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
Na Muslim amesema: “Ikiwa kuna mawingu, basi hesabuni siku thelathini (ambapo mwezi sharti uandame).”
Na Al-Bukhaariy amesema: “Kamilisheni hesabu siku thelathini.”
Naye amenukuu Hadiyth ya Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) kuwa: “Kamilisheni hesabu ya siku thelathini[5] za mwezi wa Sha’baan.”
530.
وَعَنِ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {تَرَاءَى اَلنَّاسُ اَلْهِلَالَ، فَأَخْبَرْتُ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم أَنِّي رَأَيْتُهُ، فَصَامَ، وَأَمَرَ اَلنَّاسَ بِصِيَامِهِ} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ، وَالْحَاكِمُ
Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Watu waliuona mwezi mwandamo, nikamuarifu Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kuwa nimeuona. Kwa hivyo yeye akafunga na akawaamrisha watu wafunge.”[6] [Imetolewa na Abuu Daawuwd, na wakaisahihisha Ibn Hibbaan na Al-Haakim]
531.
وَعَنِ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا أَنَّ أَعْرَابِيًّا جَاءَ إِلَى اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ: {إِنِّي رَأَيْتُ اَلْهِلَالَ، فَقَالَ: " أَتَشْهَدُ أَنْ لَا إِلَهَ إِلَّا اَللَّهُ ؟ " قَالَ: نَعَمْ. قَالَ: " أَتَشْهَدُ أَنَّ مُحَمَّدًا رَسُولُ اَللَّهِ ؟ " قَالَ: نَعَمْ. قَالَ: " فَأَذِّنْ فِي اَلنَّاسِ يَا بِلَالُ أَنْ يَصُومُوا غَدًا"} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ خُزَيْمَةَ، وَابْنُ حِبَّانَ وَرَجَّحَ النَّسَائِيُّ إِرْسَالَهُ
Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema Bedui mmoja alikuja kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akamuambia: “Nimeona mwezi, Akasema: “Unashahadia kuwa hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah?” Akasema “Ndiyo.” Akasema: “Unashahadia pia kuwa Muhammad ni Rasuli wa Allaah?” Akasema: “Ndiyo.” Akasema: Bilaal! Watangazie watu wafunge kesho.” [Imetolewa na Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad) na akaisahihisha Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan, na An-Nasaaiy aliipa daraja ya Mursal]
532.
وَعَنْ حَفْصَةَ أُمِّ اَلْمُؤْمِنِينَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا، عَنِ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {مَنْ لَمْ يُبَيِّتِ اَلصِّيَامَ قَبْلَ اَلْفَجْرِ فَلَا صِيَامَ لَهُ} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ، وَمَالَ النَّسَائِيُّ وَاَلتِّرْمِذِيُّ إِلَى تَرْجِيحِ وَقْفِهِ، وَصَحَّحَهُ مَرْفُوعًا اِبْنُ خُزَيْمَةَ وَابْنُ حِبَّانَ
وَلِلدَّارَقُطْنِيِّ: {لَا صِيَامَ لِمَنْ لَمْ يَفْرِضْهُ مِنَ اَللَّيْلِ}
Kutoka kwa Hafswah[7] Ummul Mu-uminiyna (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Asiyelaza niyyah[8] kabla ya alfajiri hana Swawm.”[9] [Imetolewa na Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad), At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy wakaisahihisha na kuipa daraja la Mawquwf. Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan wakaipa daraja la Marfuw’]
Na Ad-Daaraqutwniyy amesema: “Hana Swawm ambaye hakuifaradhisha tangu usiku.”
533.
وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {دَخَلَ عَلَيَّ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم ذَاتَ يَوْمٍ. فَقَالَ: " هَلْ عِنْدَكُمْ شَيْءٌ ؟ " قُلْنَا: لَا. قَالَ: " فَإِنِّي إِذًا صَائِمٌ " ثُمَّ أَتَانَا يَوْمًا آخَرَ، فَقُلْنَا: أُهْدِيَ لَنَا حَيْسٌ، فَقَالَ: " أَرِينِيهِ، فَلَقَدْ أَصْبَحْتُ صَائِمًا " فَأَكَلَ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ
Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliingia kwangu siku moja akasema: “Una kitu chochote cha kula?” Tukasema: “Hapana.” Na akasema (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ): “Basi mie ninafunga leo.”[10] Kisha akanitembelea siku nyingine nami nikamuambia kuwa nimepewa zawadi ya Hays[11], Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Hebu nionyeshe, kwani nimeamka nikiwa na Swawm.” Kisha Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akala.”[12] [Imetolewa na Muslim]
534.
وَعَنْ سَهْلِ بْنِ سَعْدٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا، أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {لَا يَزَالُ اَلنَّاسُ بِخَيْرٍ مَا عَجَّلُوا اَلْفِطْرَ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
وَلِلتِّرْمِذِيِّ: مِنْ حَدِيثِ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه عَنِ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {قَالَ اَللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ أَحَبُّ عِبَادِي إِلَيَّ أَعْجَلُهُمْ فِطْرًا}
Kutoka kwa Sahl bin Sa’d (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Watu wataendelea kuwa katika khayr ilimradi wanaharakisha kufuturu.”[13] [Al-Bukhaariy, Muslim]
Na katika At-Tirmidhiy kwa upokezi wa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Allaah amesema Mja Nimpendaye sana kati ya waja Wangu ni anayeharakisha kufuturu.”
535.
وَعَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {تَسَحَّرُوا فَإِنَّ فِي اَلسَّحُورِ بَرَكَةً} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
Kutoka kwa Anas bin Maalik (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Kuleni sahuwr (daku) kwani katika sahuwr kuna Baraka.”[14] [Al-Bukhaariy, Muslim]
536.
وَعَنْ سَلْمَانَ بْنِ عَامِرٍ اَلضَّبِّيِّ رضى الله عنه عَنِ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {إِذَا أَفْطَرَ أَحَدُكُمْ فَلْيُفْطِرْ عَلَى تَمْرٍ، فَإِنْ لَمْ يَجِدْ فَلْيُفْطِرْ عَلَى مَاءٍ، فَإِنَّهُ طَهُورٌ} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ خُزَيْمَةَ وَابْنُ حِبَّانَ وَالْحَاكِمُ
Kutoka kwa Salmaan bin ‘Aamir Adhw-Dhwabbiyy[15] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Endapo mmoja wenu anafuturu, afuturu kwa tende, asipopata (tende), basi kwa maji,[16] kwani maji yanatakasa.” [Imetolewa na Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad), akaisahihisha Ibn Khuzaymah, Ibn Hibbaan na Al-Haakim]
537.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه قَالَ: {نَهَى رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم عَنِ اَلْوِصَالِ، فَقَالَ رَجُلٌ مِنَ اَلْمُسْلِمِينَ: فَإِنَّكَ يَا رَسُولَ اَللَّهِ تُوَاصِلُ ؟ قَالَ: " وَأَيُّكُمْ مِثْلِي ؟ إِنِّي أَبِيتُ يُطْعِمُنِي رَبِّي وَيَسْقِينِي". فَلَمَّا أَبَوْا أَنْ يَنْتَهُوا عَنِ اَلْوِصَالِ وَاصَلَ بِهِمْ يَوْمًا، ثُمَّ يَوْمًا، ثُمَّ رَأَوُا اَلْهِلَالَ، فَقَالَ: " لَوْ تَأَخَّرَ اَلْهِلَالُ لَزِدْتُكُمْ " كَالْمُنَكِّلِ لَهُمْ حِينَ أَبَوْا أَنْ يَنْتَهُوا} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikataza kufunga Swawm mfululizo,[17] akasema mtu mmoja: “Wewe hufunga mfululi’zo Ee Rasuli wa Allaah! Akasema: “Nani kati yenu yuko kama Mimi? Wakati wa usiku Rabb Wangu Hunilisha na Kuninywesha. Walipokataa wakataka kuendelea kufunga mfululizo, alifunga pamoja nao kwa siku moja na kisha siku moja tena, kisha wakaona mwezi, Akasema: “Mwezi ungechelewa, ningewazidishia”. Alielekea kutaka kuwaadhibu walipokataa kusitisha.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
538.
وَعَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {مَنْ لَمْ يَدَعْ قَوْلَ اَلزُّورِ وَالْعَمَلَ بِهِ، وَالْجَهْلَ، فَلَيْسَ لِلَّهِ حَاجَةٌ فِي أَنْ يَدَعَ طَعَامَهُ وَشَرَابَهُ} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيُّ، وَأَبُو دَاوُدَ وَاللَّفْظُ لَهُ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Iwapo mtu hatoacha uongo[18] na matendo yake na ujinga, Allaah Hana haja mtu huyo aache chakula chake na kinywaji chake.” [Imetolewa na Al-Bukhaariy, na Abuu Daawuwd, na tamshi hili ni lake]
539.
وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم يُقَبِّلُ وَهُوَ صَائِمٌ، وَيُبَاشِرُ وَهُوَ صَائِمٌ، وَلَكِنَّهُ أَمْلَكُكُمْ لِإِرْبِهِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَّفْظُ لِمُسْلِمٍ
وَزَادَ فِي رِوَايَةٍ: {فِي رَمَضَانَ}
Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema kuwa: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa anabusu[19] na kukumbatia huku akiwa katika Swawm, lakini yeye anamiliki zaidi matamanio yake kuliko nyinyi.”[20] [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Muslim]
Na katika Riwaayah ya Muslim inasema: “Katika Ramadhwaan”
540.
وَعَنِ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا، {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم اِحْتَجَمَ وَهُوَ مُحْرِمٌ، وَاحْتَجَمَ وَهُوَ صَائِمٌ} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيُّ
Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliumikwa wakati amevaa Ihraam (wakati wa Hajj au ‘Umrah), na aliumikwa akiwa na Swawm.” [Imetolewa na Al-Bukhaariy]
541.
وَعَنْ شَدَّادِ بْنِ أَوْسٍ رضى الله عنه {أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم أَتَى عَلَى رَجُلٍ بِالْبَقِيعِ وَهُوَ يَحْتَجِمُ فِي رَمَضَانَ. فَقَالَ: " أَفْطَرَ اَلْحَاجِمُ وَالْمَحْجُومُ "} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ إِلَّا اَلتِّرْمِذِيَّ، وَصَحَّحَهُ أَحْمَدُ، وَابْنُ خُزَيْمَةَ، وَابْنُ حِبَّانَ
Kutoka kwa Shaddaad bin Aws[21] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikutana na mtu Al-Baqiy’ aliyekuwa anaumikwa ndani ya mwezi wa Ramadhwaan, akasema: “Amefungua Swawm aliyeumika na aliyeumikwa wote wamebatilisha Swawm zao.”[22] [Imetolewa na Al-Khamsah (An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad) isipokuwa At-Tirmidhiy, na wakaisahihisha Ahmad, Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan]
542.
وَعَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ رضى الله عنه قَالَ: {أَوَّلُ مَا كُرِهَتِ اَلْحِجَامَةُ لِلصَّائِمِ ، أَنَّ جَعْفَرَ بْنَ أَبِي طَالِبٍ اِحْتَجَمَ وَهُوَ صَائِمٌ، فَمَرَّ بِهِ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ: " أَفْطَرَ هَذَانِ "، ثُمَّ رَخَّصَ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم بَعْدُ فِي اَلْحِجَامَةِ لِلصَّائِمِ، وَكَانَ أَنَسٌ يَحْتَجِمُ وَهُوَ صَائِمٌ} رَوَاهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ وَقَوَّاهُ
Kutoka kwa Anas bin Maalik (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Mwanzo kukatazwa kuumika kwa mwenye Swawm ilikuwa hivi: Ja’far bin Abiy Twaalib alikwenda kuumikwa wakati akiwa ana Swawm, na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipomuona akasema: “Wote wawili hawa wamebatilisha Swawm zawo.” Baadaye Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akaruhusu mtu aweza kuumikwa wakati ana Swawm. Anas alikuwa akienda kuumikwa wakati ana Swawm.” [Imetolewa na Ad-Daaraqutwniy na akaipa nguvu]
543.
وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا، {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم اِكْتَحَلَ فِي رَمَضَانَ، وَهُوَ صَائِمٌ} رَوَاهُ اِبْنُ مَاجَهْ بِإِسْنَادٍ ضَعِيفٍ
قَالَ اَلتِّرْمِذِيُّ: لَا يَصِحُّ فِيهِ شَيْءٌ
Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alitia Kuhl[23] ndani ya Ramadhwaan akiwa ana Swawm.” [Imetolewa na Ibn Maajah kwa Isnaad dhaifu]
Na amesema At-Tirmidhiy: “Hakuna lolote katika maudhui haya lililo Swahiyh.”
544.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {مَنْ نَسِيَ وَهُوَ صَائِمٌ، فَأَكَلَ أَوْ شَرِبَ، فَلْيُتِمَّ صَوْمَهُ، فَإِنَّمَا أَطْعَمَهُ اَللَّهُ وَسَقَاهُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
وَلِلْحَاكِمِ: {مَنْ أَفْطَرَ فِي رَمَضَانَ نَاسِيًا فَلَا قَضَاءَ عَلَيْهِ وَلَا كَفَّارَةَ} وَهُوَ صَحِيحٌ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mtu yeyote anayesahau wakati yumo katika Swawm, akala au akanywa kitu, basi akamilishe Swawm yake, kwani Allaah Amemlisha na Kumnywesha yeye.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
Na Al-Haakim amesema: “Mtu yeyote anayefungua Swawm yake kwa kusahau, hana haja ya kulipa Swawm hiyo wala kafara.”[24] [Usimulizi huo ni Swahiyh]
545.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {مَنْ ذَرَعَهُ اَلْقَيْءُ فَلَا قَضَاءَ عَلَيْهِ، وَمَنْ اسْتَقَاءَ فَعَلَيْهِ اَلْقَضَاءُ} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ وَأَعَلَّهُ أَحْمَدُ وَقَوَّاهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Endapo mtu atajiwa ghafla na kutapika huku yumo ndani ya Swawm, hana haja ya kulipa, na mwenye kujitapisha atalazimika kulipa.”[25] [Imetolewa na Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad) na Ahmad aliiona ina dosari, na Ad-Daaraqutwniyy aliipa nguvu]
546.
وَعَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اَللَّهِ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا، {أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم خَرَجَ عَامَ اَلْفَتْحِ إِلَى مَكَّةَ فِي رَمَضَانَ، فَصَامَ حَتَّى بَلَغَ كُرَاعَ الْغَمِيمِ، فَصَامَ اَلنَّاسُ، ثُمَّ دَعَا بِقَدَحٍ مِنْ مَاءٍ فَرَفَعَهُ، حَتَّى نَظَرَ اَلنَّاسُ إِلَيْهِ، ثُمَّ شَرِبَ، فَقِيلَ لَهُ بَعْدَ ذَلِكَ: إِنَّ بَعْضَ اَلنَّاسِ قَدْ صَامَ. قَالَ: "أُولَئِكَ اَلْعُصَاةُ، أُولَئِكَ اَلْعُصَاةُ"}
وَفِي لَفْظٍ: {فَقِيلَ لَهُ: إِنَّ اَلنَّاسَ قَدْ شَقَّ عَلَيْهِمُ اَلصِّيَامُ، وَإِنَّمَا يَنْظُرُونَ فِيمَا فَعَلْتَ، فَدَعَا بِقَدَحٍ مِنْ مَاءٍ بَعْدَ اَلْعَصْرِ، فَشَرِبَ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ
Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdullaah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ): “Aliondoka kuenda Makkah wakati wa Ramadhwaan mwaka wa kuiteka Makkah, na yeye na watu walifunga hadi alipofika Kuraa’ Al-Ghamiym. Kisha akaomba kikombe cha maji akakiinua juu mpaka watu wakakitazama ndipo akanywa.[26] Aliambiwa baadaye kuwa watu waliendelea kufunga akasema: “Hao ni waasi, hao ni waasi.”[27]
Tafsiri nyingine inasema: “Watu wanaona ugumu kufunga na wanangojea utakalofanya wewe.” Hapo akaitisha kikombe cha maji, baada ya Swalaah ya alasiri, akanywa. [Imetolewa na Muslim]
547.
وَعَنْ حَمْزَةَ بْنِ عَمْرٍو الْأَسْلَمِيِّ رِضَى اَللَّهُ عَنْهُ ، أَنَّهُ قَالَ: {يَا رَسُولَ اَللَّهِ! أَجِدُ بِي قُوَّةً عَلَى اَلصِّيَامِ فِي اَلسَّفَرِ، فَهَلْ عَلَيَّ جُنَاحٌ ؟ فَقَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم " هِيَ رُخْصَةٌ مِنَ اَللَّهِ، فَمَنْ أَخَذَ بِهَا فَحَسَنٌ، وَمَنْ أَحَبَّ أَنْ يَصُومَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِ "} رَوَاهُ مُسْلِمٌ وَأَصْلُهُ فِي " اَلْمُتَّفَقِ " مِنْ حَدِيثِ عَائِشَةَ ، {أَنَّ حَمْزَةَ بْنَ عَمْرٍو سَأَلَ}
Kutoka kwa Hamzah bin ‘Amr Al-Aslamiyy[28] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Aliuliza Ee Rasuli wa Allaah! Mimi najiona nina nguvu za kutosha za Swiyaam nikiwa safarini, je nitapata dhambi? Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Hiyo ni ruhsa toka kwa Allaah, na kila atakayeitekeleza atakuwa kafanya vizuri, lakini iwapo mtu yeyote atapenda kufunga, hana dhambi.” [Imetolewa na Muslim na chanzo chake kimo katika Al-Bukhaariy na Muslim kutoka katika ripoti ya ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) ambayo Hamzah bin ‘Amr aliiulizia]
548.
وَعَنِ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {رُخِّصَ لِلشَّيْخِ اَلْكَبِيرِ أَنْ يُفْطِرَ، وَيُطْعِمَ عَنْ كُلِّ يَوْمٍ مِسْكِينًا، وَلَا قَضَاءَ عَلَيْهِ} رَوَاهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ، وَالْحَاكِمُ، وَصَحَّحَاهُ
Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Mzee anaruhusiwa kula katika mwezi wa Ramadhwaan na kulisha maskini kila siku, na hailipi.”[29] [Imetolewa na Ad-Daaraqutwniy na Al-Haakim ambao pia waliithibitisha]
549.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه قَالَ: {جَاءَ رَجُلٌ إِلَى اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ: هَلَكْتُ يَا رَسُولَ اَللَّهِ. قَالَ: " وَمَا أَهْلَكَكَ ؟ " قَالَ: وَقَعْتُ عَلَى اِمْرَأَتِي فِي رَمَضَانَ، فَقَالَ: " هَلْ تَجِدُ مَا تَعْتِقُ رَقَبَةً ؟ " قَالَ: لَا. قَالَ: " فَهَلْ تَسْتَطِيعُ أَنْ تَصُومَ شَهْرَيْنِ مُتَتَابِعَيْنِ ؟ " قَالَ: لَا. قَالَ: " فَهَلْ تَجِدُ مَا تُطْعِمُ سِتِّينَ مِسْكِينًا ؟ " قَالَ: لَا، ثُمَّ جَلَسَ، فَأُتِي اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم بِعَرَقٍ فِيهِ تَمْرٌ. فَقَالَ: " تَصَدَّقْ بِهَذَا "، فَقَالَ: أَعَلَى أَفْقَرَ مِنَّا ؟ فَمَا بَيْنَ لَابَتَيْهَا أَهْلُ بَيْتٍ أَحْوَجُ إِلَيْهِ مِنَّا، فَضَحِكَ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم حَتَّى بَدَتْ أَنْيَابُهُ، ثُمَّ قَالَ: "اذْهَبْ فَأَطْعِمْهُ أَهْلَكَ "} رَوَاهُ اَلسَّبْعَةُ، وَاللَّفْظُ لِمُسْلِمٍ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Mtu mmoja[30] alikuja kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “ Ee Rasuli wa Allaah! Nimeangamia.” Akasema: “Kitu gani kilichokuangamiza?” Akasema: “Nimemuingilia mke wangu ndani ya Swawm ya Ramadhwaan.” Akasema: “Je unaweza kupata mtumwa wa kumuacha huru?” Akasema: “Hapana.” Akasema tena: “Unaweza kufunga miezi miwili mfululizo?” Akasema: “Hapana.” Akasema tena: “Je unaweza kuwapa chakula maskini sitini?” Akasema: “Hapana.” Kisha akakaa chini. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akaletewa ‘Araq[31] moja lenye tende. Akasema: “Litoe hili Swadaqah.” Akasema: “Je kuna maskini kuliko sisi? Hakuna familia iliyo masikini kuliko yangu kati ya milima hii miwili ya Al-Madiynah.” Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akacheka hadi magego yake yakaonekana, na akasema: “Nenda ukailishe familia yako[32] kwa hizo.”[33] [Imetolewa na As-Sab’ah (Al-Bukhaariy, Muslim, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad) na tamshi hili ni la Muslim]
550.
وَعَنْ عَائِشَةَ وَأُمِّ سَلَمَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم كَانَ يُصْبِحُ جُنُبًا مِنْ جِمَاعٍ، ثُمَّ يَغْتَسِلُ وَيَصُومُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
زَادَ مُسْلِمٌ فِي حَدِيثِ أُمِّ سَلَمَةَ: وَ لَا يَقْضِي
Kutoka kwa ‘Aaishah na Ummu Salamah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) wamesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akiamka alfajiri[34] akiwa katika hali ya janaba, kisha alikuwa akifanya ghuslu (kuoga josho) na kufunga.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
Na akaongezea Muslim katika usimulizi wa Ummu Salamah kuwa: “wala halipi.”
551.
وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا، أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {مَنْ مَاتَ وَعَلَيْهِ صِيَامٌ صَامَ عَنْهُ وَلِيُّهُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Endapo atakayefariki na deni la Swawm, Waliy wake amfungie.”[35] [Al-Bukhaariy, Muslim]
[1] Maana ye neno Swiyaam na Swawm ni “kusitisha” na “kujizuia”. Kwa mujibu wa Istilaahi za Shariy’ah, inamaanisha kujizuia kula, kunywa, na ngono, kuanzia alfajiri hadi machweo ya jua, huku ukiwa na niyyah thabiti ya kutekeleza amri ya Allaah (سبحانه وتعالى). Swawm ni moja ya nguzo tano za Uislaam. Ukiikataa nguzo hii, wewe siyo Muislam, na ukiikwepa, wewe ni muasi. Swawm iliamrishwa kuwa ni lazima mnamo mwaka wa 2 A.H.
[2] Hadiyth hii inatufundisha kuwa kule kufunga siku moja kabla ya kuja kwa Ramadhwaan, kama wanavyofanya baadhi ya watu wasiojua, imekatazwa
[3] Endapo mtu ana desturi ya kufunga siku fulani maalumu, na siku hiyo ikaangukia kuwa siku moja kabla ya Ramadhwaan, anaruhusiwa mtu huyo kufunga siku hiyo.
[4] Endapo mwezi wa Ramadhwaan haukuonekana mnamo tarehe 29 ya Sha’baan kwa sababu anga ilikuwa na vumbi au mawingu, ubora mtu akamilishe siku thelathini za Sha’baan ndipo aanze Swiyaam. Kuanza Swiyaam kwa kudhani tu mwezi wa Ramadhwaan unaweza kuwa ulionekana mnamo tarehe 29 ya Sha’baan, kumekatazwa.
[5] Hii inatufunza kwamba usianze kufunga hadi baada ya kuuona mwandamo wa mwezi.
[6] Hii inatufunza kuwa hata shahidi mmoja tu anatosha kutangazwa mwanzo wa mfungo, lakini kuutangaza mwandamo wa mwezi wa ‘Iyd (mfungo mosi) wanahitajika mashahidi wawili, kanuni hii imeafikwa kwa pamoja.
[7] Hafswah alikuwa binti wa ‘Umar bin Al-Khatwaab (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) na akaolewa na Khunays bin Hudhaafah As-Sahmi aliyehama naye kwenda Al-Madiynah. Alipokufa baada ya Badr, Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akamuoa mnamo mwaka wa 3 A.H. Alifariki mnamo mwezi Sha’baan mwaka wa 45 A.H akiwa na umri wa miaka 60.
[8] Moja ya masharti ya Swawm ni niyyah. Kwa hivyo kila mtu sharti aweke niyyah ya Swawm kabla ya alfajiri.
[9] Kila mtu ni lazima aweke niyyah ya kufunga kabla ya alfajiri, hasa akiwa anafunga Swawm ya faradhi (ya lazima). Lakini akiwa anafunga Swawm ya Nafl (ya khiari), inatosha kuweka niyyah hata kabla ya saa sita mchana.
[10] Hadiyth hii inatufunza kuwa, niyyah ya kufunga Swawm ya khiari si lazima iwekwe kabla ya Alfajiri, bali niyyah inaweza kuwekwa hata mchana.
[11] Hays ni mchanganyiko wa tende na samli.
[12] Hadiyth hii inatufunza kwamba, Swawm ya khiari inaweza kusitishwa bila sababu yoyote.
[13] Mtu akiwa na hakika kabisa juu ya machweo ya jua, lazima asikawie kufuturu, kwani kuchelewa kufuturu ni desturi ya Mayahudi na Manaswara.
[14] Mayahudi na Wakristo hawana desturi hii ya kula sahuwr (daku). Muslim ameipokea kuwa: “Kula sahuwr ndio tofauti kati yetu na Ahl-al-Kitaab (watu wa kitabu).” Hii inasahilisha Swawm na pia inaleta thawabu zaidi.
[15] Salmaan bin ‘Aamir Adhw-Dhwabbiyy ndiye Ibn Aws bin Hujr bin ‘Amr bin Al-Haarith Adhw-Dhwabbiyy, alikuwa ni Swahaba aliyelowea Basra, na alikuwa mtu mzee wakati wa uhai wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), aliishi hadi kwenye ukhalifa wa Mu’aawiyah, na inasemekana kuwa aliuliwa katika vita vya Al-Jamaal akiwa na umri wa miaka 100. Pia inasemekana kuwa hakuna Swahaba mwingine yoyote kutoka Adhw-Dwabbi isipokuwa yeye.
[16] Kitu kizuri kuliko vyote vya kufungulia Swawm ni tende mbichi, tende kavu, kisha maji, chumvi.
[17] Neno la kiarabu Wiswaal hutumika kwa mtu ambaye hafungui Swawm yake jioni bali anaendelea kufunga mfululizo hadi siku ya pili bila kula wala kunywa katikati. Aina hii ya kufunga Swawm imekatazwa.
[18] Madhumuni ya kufunga Swawm ni kwamba, mtu ajifunze kujidhibiti mwenyewe. Lengo na azma ya kufunga Swawm linapoteza maana iwapo mtu anashindwa kujifunza hilo.
[19] Haijakatazwa kumbusu mkeo au kumkumbatia wakati wa kufunga Swawm, kwani tendo hilo tu halibatilishi Swawm.
[20] ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) anapendekeza kuwa watu wajiepushe kufanya hayo (kubusu na kukumbatia wake/waume), asije mtu akateleza na kubatilisha Swawm yake.
[21] Shaddaad bin Aws ndiye Abuu Ya’laa Al-Answaariy An-Najaariy Al-Madaniy, mpwa wa Hassan bin Thaabit. Alikuwa msomi na mwenye subira sana. Alifia Sham mnamo mwaka 58 A.H. akiwa na umri wa miaka 75.
[22] Hadiyth iliyopita (540) imeruhusu kuumikwa (kunyonywa damu kitabibu) hata kama ni ndani ya Ramadhwaan wakati mtu ana Swawm. Inaelekea kuwa kuna kutofautiana hapa, lakini hakuna. Hadiyth hii iliyosimuliwa na Shaddaad bin Aws imefutwa kwa sababu Shaddaad aliwasili Makkah baada ya mwaka wa kutekwa Makkah. Lakini ‘Abdullaah bin ‘Abbaas alisimulia kuwa hayo hayo yalitokea mnamo mwaka wa Hajjatul-Wadaa’ (Hijjah ya mwisho aliyoitekeleza Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kabla hajafariki). Ama kuhusu uhalali wake, kuumika hakubatilishi Swawm kwa mujibu wa ‘Ulamaa walio wengi; lakini kuumika hakupendezi kwa kuwa kuumikwa kunaweza kusababisha udhoofu ambao nao unaweza kupelekea mtu kuvunja Swawm yake. Lakini iwapo mtu ana nguvu za kutosha kuhimili ulegevu au kusinzia kunakoweza kusababishwa na kuumikwa, basi hiyo nasaha ya kuumikwa kutopendeza haiwi na maana.
[23] Kuhl ni chombo kinachotumiwa kwenye nyusi na kope kwa madhumuni ya kujiremba au kitabibu.
[24] Hii inatujulisha kuwa, kula au kunywa kwa kusahau, hakubatilishi Swawm. Na mtu hana haja ya kuilipa Swawm hiyo wala kuilipia fidia.
[25] Kuna tofauti ya maoni juu ya kama kutapika kunabatilisha Swawm au laa. Rai inayoelekea kuwa sahihi na ina mantiki ni kuwa, iwapo kutapika huko kumetokea kwenyewe, Swawm ni halali, lakini ikiwa ni kwa maksudi Swawm hubatilika.
[26] Inaruhusiwa Swawm wakati wa safari, lakini ni bora zaidi kutofunga. Endapo mtu atahisi kachoka sana wakati wa safari, anaruhusiwa kufungua. Anaweza kulipa kwa kufunga baadaye, lakini halazimiki kufidia au kutubu.
[27] Kwa kawaida inaruhusiwa Swawm kwa mtu akiwa safarini. Wale watu waliokuwa hawakufungua alipofungua Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) waliitwa hawana utii kwa sababu kuwa, kwa vile Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alifungua Swawm yake, wao ni nani waendelee na Swawm? Utii unahitaji utekelezaji wa kikamilifu kabisa wa amri za Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ). Maswahaba zake walidhani kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliwaamrisha kwa kufungua Swawm yake kwa sababu aliwaonea huruma wao Maswahaba, vinginevyo Maswahaba zake wasingesita kamwe kufuata atakavyo.
[28] Hamzah bin ‘Amr Al-Aslamiyy alikuwa Swahaba aliyehesabika kutoka Al-Hijaaz. Aliitwa jina la utani Abuu Muhammad au Abuu Swaalih. Mwanawe Muhammad na ‘Aaishah, Mama wa Waumini walipokea Hadiyth hii kutoka kwake. Alikufa mnamo mwaka wa 61 A.H. akiwa na umri wa miaka 80.
[29] Mzee ambaye hawezi Swawm anaweza kulipia upungufu huu kwa kutoa fidia. Halikadhalika mtu mgonjwa asiyejiweza ambaye haelekei kupona karibuni, anaweza kutoa fidia. Fidia ni kutolewa chakula mara mbili kwa maskini. Pia fidia ya kukosa kufunga Swawm kwa siku moja ni hiyo hiyo.
[30] Huyo aliyemuendea Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) ni Salama bin Sakhr.
[31] ‘Araq ni kapu lenye pishi moja ya tende.
[32] Hii inatufahamisha kwamba, endapo mtu ni maskini sana, anaweza kuilisha familia yake yeye mwenyewe kwa kafara yake mwenyewe. Wanazuoni wengu hawaiafiki Hadiyth hii na wanadai kuwa siyo kweli. Wengine wanaihesabu Hadiyth hii kuwa ni agizo maalumu alilopewa bwana huyo mahususi. Lakini maoni yote hayo hayana ushahidi.
[33] Hadiyth hii inatufahamisha kwamba, mwanamke hastahili kutozwa kafara (kafara au fidia ya kosa). Wengi wa Wanazuoni hawaafiki. Kanuni itumikayo ya kuwa, iwapo mme na mke wote walikubaliana kukutana kimwili, basi wote wawili wanastahili kulipa kafara. Lakini ikiwa mme ndiye aliyemlazimisha mke kukutana naye kimwili, basi mme ndiye anayestahili kafara siyo mke.
[34] Iwapo mme atakutana kimwili na mkewe usiku wa Ramadhwaan, lazima aoge asubuhi akiwa ana wasaa wa kutosha na kisha afunge.
[35] Endapo mtu atakufa kabla hajatimiza wajibu wake wa Swiyaam, warithi wake lazima wafunge siku hizo kwa niaba ya aliyefariki ndipo aliyefariki atasamehewa deni lake la Swiyaam.