02-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Swiyaam: Mlango Wa Swawm Za Sunnah, Na Siku Zilizokatazwa Swawm
بُلُوغُ الْمَرام
Buluwgh Al-Maraam
كِتَابُ اَلصِّيَامِ
Kitabu Cha Swawm
بَابُ صَوْمُ اَلتَّطَوُّعِ وَمَا نُهِيَ عَنْ صَوْمِهِ
02-Mlango Wa Swawm Za Sunnah, Na Siku Zilizokatazwa Swawm
552.
عَنْ أَبِي قَتَادَةَ اَلْأَنْصَارِيِّ رضى الله عنه {أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم سُئِلَ عَنْ صَوْمِ يَوْمِ عَرَفَةَ. قَالَ: " يُكَفِّرُ اَلسَّنَةَ اَلْمَاضِيَةَ وَالْبَاقِيَةَ "، وَسُئِلَ عَنْ صِيَامِ يَوْمِ عَاشُورَاءَ. قَالَ: " يُكَفِّرُ اَلسَّنَةَ اَلْمَاضِيَةَ " وَسُئِلَ عَنْ صَوْمِ يَوْمِ اَلِاثْنَيْنِ، قَالَ: " ذَاكَ يَوْمٌ وُلِدْتُ فِيهِ، وَبُعِثْتُ فِيهِ، أَوْ أُنْزِلَ عَلَيَّ فِيهِ "} رَوَاهُ مُسْلِمٌ
Kutoka kwa Abuu Qataadah Al-Answaariy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliulizwa kuhusu Swawm ya siku ya ‘Arafah akasema: “Hufuta madhambi ya mwaka uliopita na unaobakia.” Akaulizwa kuhusu Swawm ya siku ya ‘Aashuwraa akasema: “Inafuta madhambi ya mwaka uliopita.” Akaulizwa kuhusu Swawm ya siku za Jumatatu, akasema: “Hiyo ni siku niliyozaliwa na siku niliyopewa Unabiy na ni siku niliyoteremshiwa Qur-aan.”[1] [Imetolewa na Muslim]
553.
وَعَنْ أَبِي أَيُّوبَ اَلْأَنْصَارِيِّ رضى الله عنه أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {مَنْ صَامَ رَمَضَانَ، ثُمَّ أَتْبَعَهُ سِتًّا مِنْ شَوَّالٍ كَانَ كَصِيَامِ اَلدَّهْرِ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ
Kutoka kwa Abuu Ayyuwb Al-Answaariyy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mwenye kufunga Ramadhwaan, kisha akafuatishia siku sita za mwezi Shawwaal,[2] huwa kama Swiyaam ya mwaka mzima.” [Imetolewa na Muslim]
554.
وَعَنْ أَبِي سَعِيدٍ اَلْخُدْرِيِّ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {مَا مِنْ عَبْدٍ يَصُومُ يَوْمًا فِي سَبِيلِ اَللَّهِ إِلَّا بَاعَدَ اَللَّهُ بِذَلِكَ اَلْيَوْمِ عَنْ وَجْهِهِ اَلنَّارَ سَبْعِينَ خَرِيفًا} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَّفْظُ لِمُسْلِمٍ
Kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Hakuna mja yoyote anayefunga siku moja katika njia ya Allaah isipokuwa Allaah Atamuweka mbali na moto miaka sabini elfu kwa sababu ya siku hiyo.” [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Muslim][3]
555.
وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَصُومُ حَتَّى نَقُولَ لَا يُفْطِرُ، وَيُفْطِرُ حَتَّى نَقُولَ لَا يَصُومُ، وَمَا رَأَيْتُ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم اِسْتَكْمَلَ صِيَامَ شَهْرٍ قَطُّ إِلَّا رَمَضَانَ، وَمَا رَأَيْتُهُ فِي شَهْرٍ أَكْثَرَ مِنْهُ صِيَامًا فِي شَعْبَانَ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَّفْظُ لِمُسْلِمٍ
Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema kuwa: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akifunga hadi tunasema kuwa hatofungua; na anakula hadi tunasema hatofunga. Sikuwahi kumuona Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) anafunga mwezi mzima bila kufungua isipokuwa mwezi wa Ramadhwaan tu, na sikumuona anafunga sana katika mwezi wowote zaidi ya Sha’baan.” [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Muslim]
556.
وَعَنْ أَبِي ذَرٍّ رضى الله عنه قَالَ: {أَمَرَنَا رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم أَنْ نَصُومَ مِنْ اَلشَّهْرِ ثَلَاثَةَ أَيَّامٍ: ثَلَاثَ عَشْرَةَ، وَأَرْبَعَ عَشْرَةَ وَخَمْسَ عَشْرَةَ} رَوَاهُ النَّسَائِيُّ، وَاَلتِّرْمِذِيُّ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ
Kutoka kwa Abuu Dharri (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alituamrisha Swawm siku tatu kila mwezi, siku ya kumi na tatu na kumi na nne na kumi na tano.”[4] [Imetolewa na An-Nasaaiy na At-Tirmidhiy na akaisahihisha Ibn Hibbaan]
557.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {لَا يَحِلُّ لِلْمَرْأَةِ أَنْ تَصُومَ وَزَوْجُهَا شَاهِدٌ إِلَّا بِإِذْنِهِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَّفْظُ لِلْبُخَارِيِّ .
وَزَادَ أَبُو دَاوُدَ: {غَيْرَ رَمَضَانَ}
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Si halali kwa mwanamke kufunga (Swawm ya khiari wakati) mume wake yupo, bila idhini yake.”[5] [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Al-Bukhaariy]
Na Abuu Daawuwd Akaongezea: “Swawm ambayo si ya Ramadhwaan.”
558.
وَعَنْ أَبِي سَعِيدٍ اَلْخُدْرِيِّ رضى الله عنه {أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم نَهَى عَنْ صِيَامِ يَوْمَيْنِ: يَوْمِ اَلْفِطْرِ وَيَوْمِ اَلنَّحْرِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
Kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikataza watu kufunga siku mbili hizi: siku ya ‘Iydul-Fitwr na siku ya ‘Iydul-Adhwhaa.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
559.
وَعَنْ نُبَيْشَةَ اَلْهُذَلِيِّ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {أَيَّامُ اَلتَّشْرِيقِ أَيَّامُ أَكْلٍ وَشُرْبٍ، وَذِكْرٍ لِلَّهِ عَزَّ وَجَلَّ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ
Kutoka kwa Nubayshah Al-Hudhaliyy[6] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Siku za At-Tashriyq[7] ni siku za kula, kunywa na za kumdhukuru Allaah (عزّ وجلّ).” [Imetolewa na Muslim]
560.
وَعَنْ عَائِشَةَ وَابْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمْ قَالَا: {لَمْ يُرَخَّصْ فِي أَيَّامِ اَلتَّشْرِيقِ أَنْ يُصَمْنَ إِلَّا لِمَنْ لَمْ يَجِدِ اَلْهَدْيَ} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيُّ
Kutoka kwa ‘Aaishah na Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) wamesema: “Hakuna aliyeruhusiwa Swawm siku za At-Tashriyq, isipokuwa yule mtu asiyekuwa na uwezo wa Al-Hadya (mnyama wa kafara).” [Imetolewa na Al-Bukhaariy]
561.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه عَنِ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {لَا تَخْتَصُّوا لَيْلَةَ اَلْجُمُعَةِ بِقِيَامٍ مِنْ بَيْنِ اَللَّيَالِي، وَلَا تَخْتَصُّوا يَوْمَ اَلْجُمُعَةِ بِصِيَامٍ مِنْ بَيْنِ اَلْأَيَّامِ، إِلَّا أَنْ يَكُونَ فِي صَوْمٍ يَصُومُهُ أَحَدُكُمْ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Msiufanye usiku wa Ijumaa miongoni mwa nyusiku nyenginezo kuwa makhsusi kwa Qiyaam (kusimama kuswali), na msiifanye siku ya Ijumaa miongoni mwa siku kuwa makhsusi kwa Swiyaam isipokuwa iwe ni Swawm anayofunga mmoja wenu.” [Imetolewa na Muslim]
562.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {لَا يَصُومَنَّ أَحَدُكُمْ يَوْمَ اَلْجُمُعَةِ، إِلَّا أَنْ يَصُومَ يَوْمًا قَبْلَهُ، أَوْ يَوْمًا بَعْدَهُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Yeyote kati yenu asifunge siku ya Ijumaa[8] isipokuwa ikiwa anaifunga pamoja na siku kabla yake au siku baada yake.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
563.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {إِذَا اِنْتَصَفَ شَعْبَانَ فَلَا تَصُومُوا} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ، وَاسْتَنْكَرَهُ أَحْمَدُ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mwezi wa Sha’baan ukifikia nusu, msifunge.”[9] [Imetolewa na Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad) Ahmad hakuiafiki]
564.
وَعَنِ اَلصَّمَّاءِ بِنْتِ بُسْرٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {لَا تَصُومُوا يَوْمَ اَلسَّبْتِ، إِلَّا فِيمَا اِفْتُرِضَ عَلَيْكُمْ، فَإِنْ لَمْ يَجِدْ أَحَدُكُمْ إِلَّا لِحَاءَ عِنَبٍ، أَوْ عُودَ شَجَرَةٍ فَلْيَمْضُغْهَا} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ، وَرِجَالُهُ ثِقَاتٌ، إِلَّا أَنَّهُ مُضْطَرِبٌ
وَقَدْ أَنْكَرَهُ مَالِكٌ
وَقَالَ أَبُو دَاوُدَ: هُوَ مَنْسُوخٌ
Kutoka kwa Asw-Swammaai bint Busr[10] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Msifunge siku ya Jumamosi isipokuwa katika mliofaradhishwa, na iwapo mmoja wenu hakupata isipokuwa punje ya zabibu au kijiti cha mti basi na akitafune.”[11] [Imetolewa na Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad), wapokezi wake wanaaminika, lakini ni Mudhwtwarib (inababaisha)]
Maalik hakuiafiki
Na Abuu Daawuwd amesema: “Hii ni mansuwkh (imefutwa)”
565.
وَعَنْ أُمِّ سَلَمَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا، {أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم كَانَ أَكْثَرَ مَا يَصُومُ مِنَ اَلْأَيَّامِ يَوْمُ اَلسَّبْتِ، وَيَوْمُ اَلْأَحَدِ، وَكَانَ يَقُولُ: " إِنَّهُمَا يَوْمَا عِيدٍ لِلْمُشْرِكِينَ، وَأَنَا أُرِيدُ أَنْ أُخَالِفَهُمْ "} أَخْرَجَهُ النَّسَائِيُّ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ خُزَيْمَةَ، وَهَذَا لَفْظُهُ
Kutoka kwa Ummu Salamah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akifunga zaidi siku ya Jumamosi na Jumapili, na alikuwa akisema: “Hizo ni siku za sikukuu za washirikina, nami nataka kutofautiana nao.” [Imetolewa na An-Nasaaiy, na akaisahihisha Ibn Khuzaymah, na hii ni tafsiri yake]
566.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم {نَهَى عَنْ صَوْمِ يَوْمِ عَرَفَةَ بِعَرَفَةَ} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ غَيْرَ اَلتِّرْمِذِيِّ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ خُزَيْمَةَ، وَالْحَاكِمُ، وَاسْتَنْكَرَهُ الْعُقَيْلِيُّ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikataza Swawm siku ya ‘Arafah ndani ya ‘Arafah.”[12] [Imetolewa na Al-Khamsah (An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad) isipokuwa At-Tirmidhiy, na akaisahihisha Ibn Khuzaymah na Al-Haakim, na hakuiafiki Al-‘Uqayliyy]
567.
وَعَنْ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ عَمْرِوٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم {لَا صَامَ مَنْ صَامَ اَلْأَبَدَ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
وَلِمُسْلِمٍ عَنْ أَبِي قَتَادَةَ بِلَفْظِ: {لَا صَامَ وَلَا أَفْطَرَ}
Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amr (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Hakufunga Swawm anayefunga milele”[13] [Al-Bukhaariy, Muslim]
Na Muslim ameandika Hadiyth ya Abuu Qataadah ikiwa na tamshi: “Hakufunga Swawm wala hakula.”
[1] Hii inamaanisha kuwa dhambi ndogo hufutwa kwa sababu ya Swawm, lakini dhambi kubwa hufutwa kwa kutubu tu. Ama kuhusu haki za watu, madeni na wajibu wa kipesa, kuhusiana na mdaiwa, kusamehewa kunategemea matakwa ya watu wanaomdai. ‘Arafah ni jina la siku ya 9 ya mwezi wa Dhul-Hijjah (Mfungo tatu au mwezi wa kumi na mbili wa Kiislam), na ‘Aashuwraa ni siku ya 10 ya mwezi Muharram (Mfungo nne au mwezi wa kwanza wa Kiislam). Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipenda kufunga siku za Jumatatu, lakini hakuelezea juu ya thawabu zake.
[2] Endapo siku 30 za Ramadhwaan zitaunganishwa na siku 6 za kufunga mwezi wa Shawwaal ambayo inaifanya jumla iwe ni siku 36. Kwa mujibu wa Shariy’ah kila jema linalipwa mara kumi. Kwa hivyo tukizidisha siku 36 kwa mara 10 tutapata 360, namba ambayo ni sawa na siku za mwaka mmoja. Wanazuoni wengine wanasema siku hizo 6 za kufunga katika mwezi wa Shawwaal ni sharti zifungwe mfululizo mara baada ya Ramadhwaan. Wengine wanasema inatosha kuzifunga siku zote 6 ndani ya mwezi Shawwaal kwa mpangilio wowote, ama mfululizo au ukajiwekea siku za kufungua baada ya kufunga siku moja. Rai hii ya pili inachukuliwa kuwa sahihi zaidi. Kadhalika Swawm ya Shawwaal hutekelezwa baada ya kukamilisha funga kamili ya Ramadhwaan na kama kuna siku iliyopita basi ifungwe kulipwa kabla ya kuanza Sita za Shawwaal.
[3] Swawm kwa ajili ya Allaah (سبحانه وتعالى) kunaweza kumaanisha kuwa mtu anafunga huku yumo katika uwanja wa vita vya Jihaad. Inaweza pia kumaanisha mfungo wa khiari (Sunnah).
[4] Siku hizo tatu zinaitwa Ayyaamul-biydhw (Masiku meupe), mwanga wa angani unaangaza (kwa sababu ya mwezi mpevu) usiku kucha.
[5] Mwanamke kakatazwa Swiyaam za Sunnah bila ruhusa ya mumewe. Hata kama atataka kufunga siku za fardhi alizozikosa ni sharti aombe ruhusa.
[6] Nubayshah Al-Hudhaliyy ndiye Abuu Twariyf Nubayshah bin ‘Abdillaah bin ‘Amr bin ‘Itaab Al-Hudhali. Huyu ni Swahaba ambaye ana Hadiyth kumi na moja. Alilowea Basra na aliitwa Nubayshah mkarimu.
[7] Siku za Tashriyq ni siku kumi na moja na kumi na mbili na kumi na tatu ya mwezi wa Dhul-Hijjah. Imekatazwa Swiyaam katika siku hizi. Mtu anayehiji anaweza kufunga katika siku hizo iwapo kashindwa kupata mnyama wa kuchinja kama kafara. Watu wengine hawana ruhusa ya kufunga siku hizo. Pia imekatazwa kufunga siku za ‘Iyd zote mbili (ya Fitwr na Adhwhaa), iwe ni Swawm ya khiari au ya kulipia Swiyaam za fardhi.
[8] Imekatazwa Swawm siku ya Ijumaa peke yake. Katazo hili ni makhususi la kumsudia mtu anayefunga siku ya Ijumaa kwa kuamini kuwa atapata thawabu zaidi kwa kufunga siku hii.
[9] Mtu anaweza kufunga ilimradi awe analipa Swawm ya faradhi, au Swawm zinazohesabika kuwa ni za Waajib (za lazima). Lakini Swiyaam za khiari zimekatazwa asije mtu akachoshwa au akadhoofishwa mno kiasi cha kuifanya Swawm ya Ramadhwaan inayokuja iwe nzito kwake.
[10] Asw-Swammaai bint Busr alikuwa ni Buhaiya au Bahima bint Busr. Alikuwa Swahaba wa kutoka ukoo wa Mazin. Ikisemekana kuwa ni dada wa au shangazi wa ‘Abdullaah bin Busr.
[11] Kwa kuwa Jumamosi ina umuhimu maalumu kwa Mayahudi na wao hufunga katika siku hii, tunatakiwa tuwe tofauti nao, na kwa kuwa Swawm hiyo inavyofanana na ya Mayahudi, Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amekataza kuichagua Jumamosi peke yake kwa Swawm. Lakini Ummu Salamah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) anasimulia kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akifunga Jumamosi pamoja na Jumapili. Kwa kuwa siku ya Jumamosi ni sikukuu kwa Mayahudi, Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alifunga siku hii ili kuharibu kawaida ya Mayahudi na kuongeza thawabu zake, alifunga siku ya Jumapili pia.
[12] Kwa mtu ambaye yumo katika tendo la kuhiji, imekatazwa Swawm siku ya ‘Arafah kwa vile mtu analazimika kukabiliana na taabu na mihangaiko migumu siku hiyo. Kwa hiyo Swawm siku hii atachoka na kudhoofu sana ambako kutapelekea kushindwa kuyafanya uzuri matendo mengine ya Hajj (Hijjah). Watu wengine wote wasiokuwa katika mchakato wa kuhiji siku ile wao hawakatazwi kufunga Swawm siku ile, na kwa yakini Swawm siku ile kwao kuna umuhimu na thawabu nyingi sana.
[13] Watu wengine wasiojua, hung’ang’ania kufunga Swawm mfululizo bila kuacha hata siku moja. Hadiyth hii inadhihirisha kuwa desturi hii imekatazwa. Wengi wa Wanazuoni wanaamini kuwa desturi hii ya kufunga Swawm kila siku milele kwa sababu hii inamdhoofisha mtu kwa hivyo inakuwa kikwazo kwa harakati zake za kidini na kidunia. Hadiyth nyingine inasema mtu anadaiwa au ana deni kwa afya yake na uhai wa mwili wake unahitaji mtu kujipa mapumziko mara kwa mara. Hata Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akifunga siku moja na anafungua siku nyingine.