03-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Swiyaam: Mlango Wa Al-I’tikaaf Na Qiyaam: Kisimamo cha Swalaah Za Usiku Wa Ramadhwaan

 

بُلُوغُ الْمَرام

Buluwgh Al-Maraam

 

 

كِتَابُ اَلصِّيَامِ

Kitabu Cha Swawm

 

 

بَابُ اَلِاعْتِكَافِ وَقِيَامِ رَمَضَانَ

03-Mlango Wa Al-I’tikaaf Na Qiyaam: Kisimamo cha Swalaah Za Usiku Wa Ramadhwaan

 

 

 

 

 

 

568.

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {مَنْ قَامَ رَمَضَانَ إِيمَانًا وَاحْتِسَابًا، غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mwenye kusimama katika mwezi wa Ramadhwaan[1] kwa Iymaan na kutaraji malipo[2] ataghufuriwa dhambi zake zilizotangulia.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

569.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم إِذَا دَخَلَ اَلْعَشْرُ أَيْ: اَلْعَشْرُ اَلْأَخِيرُ مِنْ رَمَضَانَ شَدَّ مِئْزَرَهُ، وَأَحْيَا لَيْلَهُ، وَأَيْقَظَ أَهْلَهُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Siku kumi za mwisho wa Ramadhwaan zilipoingia, Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alijifunga mkanda wake na alikesha usiku wake na aliiamsha familia yake.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

570.

وَعَنْهَا: {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم كَانَ يَعْتَكِفُ اَلْعَشْرَ اَلْأَوَاخِرَ مِنْ رَمَضَانَ، حَتَّى تَوَفَّاهُ اَللَّهُ، ثُمَّ اعْتَكَفَ أَزْوَاجُهُ مِنْ بَعْدِهِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema tena kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akikaa I’tikaaf siku kumi za mwisho za Ramadhwaan mpaka alipofishwa na Allaah (عزّ وجلّ)  kisha wakeze wakakaa I’tikaaf baada yake.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

571.

وَعَنْهَا قَالَتْ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم إِذَا أَرَادَ أَنْ يَعْتَكِفَ صَلَّى اَلْفَجْرَ، ثُمَّ دَخَلَ مُعْتَكَفَهُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema kuwa: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa anapotaka kukaa I’tikaaf anaswali Alfajiri kisha anaingia I’tikaaf yake.”[3] [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

572.

وَعَنْهَا قَالَتْ: {إِنْ كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم لَيُدْخِلُ عَلَيَّ رَأْسَهُ وَهُوَ فِي اَلْمَسْجِدِ فَأُرَجِّلُهُ، وَكَانَ لَا يَدْخُلُ اَلْبَيْتَ إِلَّا لِحَاجَةٍ، إِذَا كَانَ مُعْتَكِفًا} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَّفْظُ لِلْبُخَارِيِّ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akiweka kichwa chake katika chumba changu wakati alipokuwa Msikitini, nami nikawa namchana nywele zake Msikitini, na alikuwa haingii nyumbani isipokuwa kwa haja tu anapokuwa kwenye I’tikaaf.”[4] [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Al-Bukhaariy]

 

 

 

573.

وَعَنْهَا قَالَتْ: {اَلسُّنَّةُ عَلَى اَلْمُعْتَكِفِ أَنْ لَا يَعُودَ مَرِيضًا، وَلَا يَشْهَدَ جِنَازَةً، وَلَا يَمَسَّ امْرَأَةً، وَلَا يُبَاشِرَهَا، وَلَا يَخْرُجَ لِحَاجَةٍ، إِلَّا لِمَا لَا بُدَّ لَهُ مِنْهُ، وَلَا اعْتِكَافَ إِلَّا بِصَوْمٍ وَلَا اعْتِكَافَ إِلَّا فِي مَسْجِدٍ جَامِعٍ} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ، وَلَا بَأْسَ بِرِجَالِهِ، إِلَّا أَنَّ اَلرَّاجِحَ وَقْفُ آخِرِهِ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Ni Sunnah kwa mwenye kukaa I’tikaaf asiende kumzuru mgonjwa, wala kuenda mazikoni, na asimuingilie wala kumkumbatia mwanamke,[5] au kutoka kwa haja yoyote ila asiyo budi nayo, iwe dharura muhimu sana kwake. Hakuna I’tikaaf ila kwa Swawm na hakuna I’tikaaf ila ndani ya Msikiti wa jamaa.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd kwa upokezi sahihi, lakini huhesabika Mawquwd]

 

 

 

574.

وَعَنْ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا، أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {لَيْسَ عَلَى اَلْمُعْتَكِفِ صِيَامٌ إِلَّا أَنْ يَجْعَلَهُ عَلَى نَفْسِهِ} رَوَاهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ وَالْحَاكِمُ، وَالرَّاجِحُ وَقْفُهُ أَيْضًا

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Swiyaam si lazima[6] kwa mwenye kukaa I’tikaaf Msikitini siku kumi za mwisho wa Ramadhwaan isipokuwa kama yeye mwenyewe anataka.”[7] [Imetolewa na Ad-Daaraqutwniyy na Al-Haakim, pia ni Mawquwf]

 

 

 

575.

وَعَنْ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا: {أَنَّ رِجَالاً مِنْ أَصْحَابِ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم أُرُوا لَيْلَةَ اَلْقَدْرِ فِي اَلْمَنَامِ، فِي اَلسَّبْعِ اَلْأَوَاخِرِ، فَقَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم "أَرَى‏ رُؤْيَاكُمْ قَدْ تَوَاطَأَتْ فِي اَلسَّبْعِ اَلْأَوَاخِرِ، فَمَنْ كَانَ مُتَحَرِّيَهَا فَلْيَتَحَرَّهَا فِي اَلسَّبْعِ اَلْأَوَاخِرِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Baadhi ya Maswahaba wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) waliona katika ndoto Laylatul-Qadr mnamo usiku wa saba wa mwisho wa Ramadhwaan. Kwa hivyo Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Naona ndoto zenu zinaafikiana na usiku wa saba wa mwisho, kwa hivyo mtu anayeitafuta aitafute mnamo siku saba za mwisho.”[8] [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

576.

وَعَنْ مُعَاوِيَةَ بْنَ أَبِي سُفْيَانَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا، عَنْ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ: { لَيْلَةُ سَبْعٍ وَعِشْرِينَ} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ، وَالرَّاجِحُ وَقْفُهُ‏ .‏

وَقَدْ اِخْتُلِفَ فِي تَعْيِينِهَا عَلَى أَرْبَعِينَ قَوْلًا أَوْرَدْتُهَا فِي " فَتْحِ اَلْبَارِي "

Kutoka kwa Mu’aawiyah bin Abiy Sufyaan (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa kuhusu Laylatul Qadr, Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Ni usiku wa ishirini na saba.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na ni Mawquwf]

 

 

 

577.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {قُلْتُ يَا رَسُولَ اَللَّهِ : أَرَأَيْتَ إِنْ عَلِمْتُ أَيَّ لَيْلَةٍ لَيْلَةُ اَلْقَدْرِ، مَا أَقُولُ فِيهَا ؟ قَالَ: " قُولِي: اَللَّهُمَّ إِنَّكَ عَفُوٌّ تُحِبُّ اَلْعَفْوَ فَاعْفُ عَنِّي "} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ، غَيْرَ أَبِي دَاوُدَ، وَصَحَّحَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ، وَالْحَاكِمُ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Mimi nilisema: Ee Rasuli wa Allaah! Unaonaje, nikiwa najua Laylatul-Qadr inaangukia usiku gani,[9] niseme nini?” Akasema: Sema:

اَللَّهُمَّ إِنَّكَ عَفُوٌّ تُحِبُّ اَلْعَفْوَ فَاعْفُ عَنِّي

Allaahumma Innaka ‘Afuwwun Tuhibul-‘Afwa Fa’fu ‘Anniy

 

Ee Allaah! Hakia Wewe ni Msamehevu na Unapenda kusamehe, kwa hivyo nisamehe mimi.” [Imetolewa na Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Ibn Maajah, Ahmad) isipokuwa Abuu Daawuwd, na akaisahihisha At-Tirmidhiy na Al-Haakim]

 

 

 

578.

وَعَنْ أَبِي سَعِيدٍ اَلْخُدْرِيِّ رضى الله عنه  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم : {لَا تُشَدُّ اَلرِّحَالُ إِلَّا إِلَى ثَلَاثَةِ مَسَاجِدَ: اَلْمَسْجِدِ اَلْحَرَامِ، وَمَسْجِدِي هَذَا، وَالْمَسْجِدِ اَلْأَقْصَى} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Msifunge safari isipokuwa ya Misikiti mitatu: Al-Masjid Al-Haraam (Makkah), Msikiti wangu na Al-Masjid Al-Aqswaa.”[10] [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

[1] Qiyaam ni kuswali Swalaah za khiari katika usiku.  Katika mwezi wa  Ramadhwaan, Swalaah inayoswaliwa baada ya ‘Ishaa inajulikana kwa Taraawiyh. Kwa kuswali Swalaah hizi, mtu hughufuriwa dhambi zake zote zilizopita, ilimradi mtu huyo ana Iymaan kamili juu ya ahadi ya Allaah (عزّ وجلّ) kuhusu malipo yake.

[2] Inamaanisha kuwa hayo yasifanywe kwa ajili ya riyaa (kujionyesha). Iwapo mtu hafanyi kwa riyaa, basi ataghufuriwa madhambi yake madogomadogo yote. Wanazuoni wengine wanasema kughufuriwa huko  kuna masharti ataghufuriwa mtu ikiwa tu anayo ‘Aqiydah (Iymaan) thabiti.

[3] Kwa mujibu wa Hadiyth hii, wanawake pia wanafaa kukaa I’tikaaf (kujitenga na kukaa faragha Msikitini kuswali na kumdhukuru Allaah (عزّ وجلّ)  mnamo siku 10 za mwisho za Ramadhwaan).  Lakini wanawake lazima iwe shariy’ah inamruhusu kukaa I’tikaaf.   

[4] Hapa “shida (Haja)” inamaanisha kuenda haja ndogo au kubwa.

[5] Hapa kumgusa mwanamke kunamaanisha kukutana naye kimwili, tendo linalobatilisha I’tikaaf. Vinginevyo, kumgusa tu mwanamke hakukatazwi.

[6] Inamaanisha siku zile za kawaida, zisizokuwa za Ramadhwaan.

[7] Mtu anayefanya I’tikaaf siyo lazima afunge Swawm, ila kama yeye kaapa kufunga.

[8] Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Umar kupitia kwa Swahiyhayn yasema mtu aitafute Laylatul-Qadr masiku kumi ya mwisho. Vinginevyo aitafute masiku saba ya mwisho, khususani masiku ya Witr kama ya tarehe ishirini na moja, ishirini na tatu, ishirini na tano, ishirini na saba, na tarehe ishirini na tisa.

[9] Maoni ya wengi kuhusu Laylatul-Qadr ni kwamba, usiku huu huangukia usiku wa 10 wa mwisho ya Ramadhwaan, khususan katika usiku wa Witr, na hubadilika kila Ramadhwaan. Usiku huo huweza kutokea mnamo tarehe 21, 23, 25, n.k. haiwezi kusemwa kwa hakika kabisa, kwa kuwa siku hiyo imegubikwa na siri, ndivyo Hadiyth zinavyoelezea.

[10] Kama ilivyotajwa katika Hadiyth ya hapo nyuma, kuwa I’tikaaf ni sharti iwe Msikitini kutokana na kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

وَلَا تُبَاشِرُوهُنَّ وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ ۗ

Na wala msiwaingilie hali ya kuwa nyinyi wenye kukaa i’tikaaf Misikitini. [Al-Baqarah: 186]

 

Hadiyth hii pia inatuambia kuwa hairuhusiwi kuenda kutembea popote kwa madhumuni ya kupatia thawabu isipokuwa Misikiti hii mitatu ambayo ina fadhila zake. Mtu akienda katika Msikiti wa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), basi na apate fadhila za kulizuru kaburi la Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ).   

Share