01-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Hajj: Mlango Wa Fadhila Zake Na Ubainisho Wa Wale Waliofaradhishiwa

 

بُلُوغُ الْمَرام

Buluwgh Al-Maraam

 

 

كِتَابُ اَلْحَجِّ

Kitabu Cha Hajj

 

 

بَابُ فَضْلِهِ وَبَيَانِ مَنْ فُرِضَ عَلَيْهِ

01-Mlango Wa Fadhila Zake Na Ubainisho Wa Wale Waliofaradhishiwa

 

 

 

 

 

579.

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ ‏ رضى الله عنه ‏ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏قَالَ: {اَلْعُمْرَةُ إِلَى اَلْعُمْرَةِ كَفَّارَةٌ لِمَا بَيْنَهُمَا، وَالْحَجُّ اَلْمَبْرُورُ لَيْسَ لَهُ جَزَاءٌ إِلَّا اَلْجَنَّةَ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “’Umrah mpaka ‘Umrah ni kafara ya madhambi yatendwayo baina yake. Hajjun-Mabruwr (Hijjah iliyokubaliwa) haina malipo isipokuwa Jannah.”[1] [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

580.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {قُلْتُ: يَا رَسُولَ اَللَّهِ! عَلَى اَلنِّسَاءِ جِهَادٌ  ؟ قَالَ: " نَعَمْ، عَلَيْهِنَّ جِهَادٌ لَا قِتَالَ فِيهِ: اَلْحَجُّ، وَالْعُمْرَةُ "} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَابْنُ مَاجَهْ وَاللَّفْظُ لَهُ، وَإِسْنَادُهُ صَحِيحٌ ‏ وَأَصْلُهُ فِي اَلصَّحِيحِ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Nilisema: Ee Rasuli wa Allaah! Je Jihaad ni lazima kwa wanawake?” Akasema: “Ndiyo, Jihaad isiyonasibisha mapigano ni lazima kwao, hiyo ni Hijjah na ‘Umrah.”[2] [Imetolewa na Ahmad na Ibn Maajah, na tamshi hili ni la Ibn Maajah, Isnaad yake ni imara, na chanzo chake ni Swahiyh Al-Bukhaariy]

 

 

 

581.

وَعَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اَللَّهِ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {أَتَى اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم ‏أَعْرَابِيٌّ.‏ فَقَالَ: يَا رَسُولَ اَللَّهِ! أَخْبِرْنِي عَنْ اَلْعُمْرَةِ، أَوَاجِبَةٌ هِيَ ؟ فَقَالَ: " لَا.‏ وَأَنْ تَعْتَمِرَ خَيْرٌ لَكَ "} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَاَلتِّرْمِذِيُّ، وَالرَّاجِحُ وَقْفُهُ

وَأَخْرَجَهُ اِبْنُ عَدِيٍّ مِنْ وَجْهٍ آخَرَ ضَعِيفٍ ‏ عَنْ جَابِرٍ مَرْفُوعًا: {اَلْحَجُّ وَالْعُمْرَةُ فَرِيضَتَانِ}

Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdullaah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Bedui mmoja alikuja kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Niambie juu ya ‘Umrah, je ni lazima?”[3] Akasema: “Hapana, lakini ukifanya ni bora kwako.” [Imetolewa na Ahmad na At-Tirmidhiy. Imeamuliwa kuwa ni Mawquwf]

Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Hijjah na ‘Umrah ni faradhi mbili.” [Imetolewa na Ibn ‘Adiyy kuwa ni dhaifu]

 

 

 

582.

وَعَنْ أَنَسٍ رضى الله عنه‏ قَالَ: {قِيلَ يَا رَسُولَ اَللَّهِ، مَا اَلسَّبِيلُ ؟ قَالَ: " اَلزَّادُ وَالرَّاحِلَةُ "} رَوَاهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ وَصَحَّحَهُ اَلْحَاكِمُ، وَالرَّاجِحُ إِرْسَالُهُ

وَأَخْرَجَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ مِنْ حَدِيثِ اِبْنِ عُمَرَ أَيْضًا، وَفِي إِسْنَادِهِ ضَعْفٌ

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: Ilisemwa: “Ee Rasuli wa Allaah! Nini maana ya As-Sabiyl?”[4] Akasema: “Chakula na kipando.” [Imetolewa na Ad-Daaraqutwniyy na akaisahihisha Al-Haakim, na imeitwa Mursal]

Na tafsiri ya At-Tirmidhiy kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) ni sawa na hiyo, lakini ina udhaifu wa upokezi wake.

 

 

 

583.

وَعَنْ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا، {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم ‏لَقِيَ رَكْبًا بِالرَّوْحَاءِ فَقَالَ: " مَنِ اَلْقَوْمُ ؟ " قَالُوا: اَلْمُسْلِمُونَ.‏ فَقَالُوا: مَنْ أَنْتَ ؟ قَالَ: " رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏" فَرَفَعَتْ إِلَيْهِ اِمْرَأَةٌ صَبِيًّا.‏ فَقَالَتْ: أَلِهَذَا حَجٌّ ؟ قَالَ: " نَعَمْ: وَلَكِ أَجْرٌ "} رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikutana na wasafiri kule Ar-Rawhaa akasema: “Ninyi ni nani?” Wakasema: “Ni Waislam.” Wakasema: “Wewe ni nani?” Akasema: “Mimi ni Rasuli wa Allaah.” Kisha mwanamke mmoja akamnyanyua mtoto wa kiume akamsogezea na kusema:  “Je huyu ana Hijjah?” Akasema: “Ndiyo na wewe utapata thawabu.”[5] [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

584.

وَعَنْهُ قَالَ: {كَانَ اَلْفَضْلُ بْنُ عَبَّاسٍ رَدِيفَ رَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏.‏ فَجَاءَتِ اِمْرَأَةٌ مَنْ خَثْعَمَ، فَجَعَلَ اَلْفَضْلُ يَنْظُرُ إِلَيْهَا وَتَنْظُرُ إِلَيْهِ، وَجَعَلَ اَلنَّبِيُّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏يَصْرِفُ وَجْهَ اَلْفَضْلِ إِلَى اَلشِّقِّ اَلْآخَرِ.‏ فَقَالَتْ: يَا رَسُولَ اَللَّهِ، إِنَّ فَرِيضَةَ اَللَّهِ عَلَى عِبَادِهِ فِي اَلْحَجِّ أَدْرَكَتْ أَبِي شَيْخًا كَبِيرًا، لَا يَثْبُتُ عَلَى اَلرَّاحِلَةِ، أَفَأَحُجُّ عَنْهُ ؟ قَالَ: " نَعَمْ " وَذَلِكَ فِي حَجَّةِ اَلْوَدَاعِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَفْظُ لِلْبُخَارِيِّ

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema tena: “Al-Fadhwl bin ‘Abbaas[6] alikuwa amepanda mnyama nyuma ya Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ). Mwanamke wa Khath-am alikuja na Al-Fadhwl akawa anamtazama, naye akawa anamtazama. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akageuza uso wa Al-Fadhwl upande mwingine. Kisha yule mwanamke akasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Amri ya Allaah kuwa waja Wake wafanye Hijjah imekuja na baba yangu ni mzee mno hawezi kukaa sawa sawa juu ya ngamia. Je, mimi naweza kufanya Hijjah kwa niaba yake?” Akasema: “Ndiyo.”[7] Hiyo ilikuwa katika Hijjatul-Wadaa’ (Hijjah ya kuaga).” [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Al-Bukhaariy]

 

 

 

585.

وَعَنْهُ: {أَنَّ اِمْرَأَةً مِنْ جُهَيْنَةَ جَاءَتْ إِلَى اَلنَّبِيِّ‏ صلى الله عليه وسلم ‏فَقَالَتْ: إِنَّ أُمِّي نَذَرَتْ أَنْ تَحُجَّ، فَلَمْ تَحُجَّ حَتَّى مَاتَتْ، أَفَأَحُجُّ عَنْهَا ؟ قَالَ: " نَعَمْ "، حُجِّي عَنْهَا، أَرَأَيْتِ لَوْ كَانَ عَلَى أُمِّكِ دَيْنٌ، أَكُنْتِ قَاضِيَتَهُ ؟ اِقْضُوا اَللَّهَ، فَاَللَّهُ أَحَقُّ بِالْوَفَاءِ} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيُّ

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema tena: “Mwanamke mmoja wa Juhaynah alikuja kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Mama yangu aliweka nadhiri kuhiji na hakuhiji, mpaka akafariki. Je, naweza kuhiji kwa niaba yake?” Akasema: “Ndiyo nenda kafanye Hijjah kwa niaba yake. Hebu niambie, je iwapo mama yako alikuwa na deni kwa mtu, ungemlipia? Basi lipa deni la mama yako kwa Allaah, kwani Allaah Anastahiki zaidi kulipwa deni alilokopwa Yeye.”[8] [Imetolewa na Al-Bukhaariy]

 

 

 

586.

وَعَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏{أَيُّمَا صَبِيٍّ حَجَّ، ثُمَّ بَلَغَ اَلْحِنْثَ، فَعَلَيْهِ  أَنْ يَحُجَّ  حَجَّةً أُخْرَى، وَأَيُّمَا عَبْدٍ حَجَّ، ثُمَّ أُعْتِقَ، فَعَلَيْهِ  أَنْ يَحُجَّ  حَجَّةً أُخْرَى} رَوَاهُ اِبْنُ أَبِي شَيْبَةَ، وَالْبَيْهَقِيُّ وَرِجَالُهُ ثِقَاتٌ، إِلَّا أَنَّهُ اِخْتُلِفَ فِي رَفْعِهِ، وَالْمَحْفُوظُ أَنَّهُ مَوْقُوفٌ

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema tena Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Endapo mtoto mdogo anafanya Hijjah na baadae anafikia baleghe, ni lazima ahiji tena. Na iwapo mtumwa anafanya Hijjah na baadae anaachwa huru, lazima afanye Hijjah nyingine.” [Imetolewa na Ibn Abuu Shaybah na Al-Bayhaqiyy, na mlolongo wa wapokezi wake ni wa kutegemewa; lakini wametofautiana kama Hadiyth hii ni Marfuw’. Hata hivyo imekubalika kuwa ni Mawquwf]

 

 

 

587.

وَعَنْهُ: سَمِعْتُ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏يَخْطُبُ يَقُولُ: {" لَا يَخْلُوَنَّ رَجُلٌ بِاِمْرَأَةٍ إِلَّا وَمَعَهَا ذُو مَحْرَمٍ، وَلَا تُسَافِرُ اَلْمَرْأَةُ إِلَّا مَعَ ذِي مَحْرَمٍ " فَقَامَ رَجُلٌ، فَقَالَ: يَا رَسُولَ اَللَّهِ، إِنَّ اِمْرَأَتِي خَرَجَتْ حَاجَّةً، وَإِنِّي اِكْتُتِبْتُ فِي غَزْوَةِ كَذَا وَكَذَا، قَالَ: " اِنْطَلِقْ، فَحُجَّ مَعَ اِمْرَأَتِكَ "} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَّفْظُ لِمُسْلِمٍ

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema Nilimsikia Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akihutubia na kusema: “Mwanamume asikae faragha na mwanamke isipokuwa pamoja na mahram[9] wake. Na mwanamke asisafiri isipokuwa pamoja na mahram.” Mtu mmoja alisimama akasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Mke wangu anaazimia kuenda kuhiji, na mimi nimeandikiwa kuenda vita kadha wa kadha.” Akasema: “Nenda kahiji pamoja na mkeo.” [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Muslim]

 

 

 

588.

وَعَنْهُ: {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم ‏سَمِعَ رَجُلًا يَقُولُ: لَبَّيْكَ عَنْ شُبْرُمَةَ، قَالَ: " مَنْ شُبْرُمَةُ ؟ " قَالَ: أَخٌ  لِي، أَوْ قَرِيبٌ لِي، قَالَ: " حَجَجْتَ عَنْ نَفْسِكَ ؟ " قَالَ: لَا.‏ قَالَ: "حُجَّ عَنْ نَفْسِكَ، ثُمَّ حُجَّ عَنْ شُبْرُمَةَ "} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ، وَابْنُ مَاجَهْ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ، وَالرَّاجِحُ عِنْدَ أَحْمَدَ وَقْفُهُ

Kutoka kwa Ibn ‘Abbas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema tena kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimsikia mtu akisema: “Labbayka[10] kwa niaba ya Shubrumah.” Akasema: “Shubrumah ndiyo nani?” Akasema: “Ni kaka yangu.” Akasema: “Umeshahiji kwa ajili ya nafasi yako?” Akasema: “Hapana.” Hapo akasema: “Basi wewe hiji kwa ajili ya nafsi yako mwenyewe kisha utahiji kwa niaba ya Shubrumah.”[11] [Imetolewa na Abuu Daawuwd na Ibn Maajah, na akaisahihisha Ibn Hibbaan, na Ahmad aliihesabu kuwa ni Mawquwf]

 

 

 

589.

وَعَنْهُ قَالَ: خَطَبَنَا رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏فَقَالَ: {" إِنَّ اَللَّهَ كَتَبَ عَلَيْكُمُ اَلْحَجَّ " فَقَامَ اَلْأَقْرَعُ بْنُ حَابِسٍ فَقَالَ: أَفِي كَلِّ عَامٍ يَا رَسُولَ اَللَّهِ ؟ قَالَ: " لَوْ قُلْتُهَا لَوَجَبَتْ، اَلْحَجُّ مَرَّةٌ، فَمَا زَادَ فَهُوَ تَطَوُّعٌ "} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ، غَيْرَ اَلتِّرْمِذِيِّ

وَأَصْلُهُ فِي مُسْلِمٍ مِنْ حَدِيثِ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alituhutubia na akasema: “Allaah Amekufaradhishieni Hijjah.” Al-Aqra’ bin Haabis[12] akasimama na akasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Hiyo ifanyike kila mwaka?” Akasema: “Ningekuambia kuwa itekelezwe kila mwaka ingekuwa lazima. Hijjah ni mara moja, na ziada ni khiari.” [Imetolewa na Al-Khamsah (An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad) isipokuwa At-Tirmidhiy, na chanzo chake ni Swahiyh Muslim kutoka katika Hadiyth ya Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ)]

 

[1] Hakuna siku maalumu iliyoagizwa kufanya ‘Umrah, bali inaweza kufanywa wakati wowote mtu anaopenda. Hajj Mabruwr (Hijjah kubwa iliyokubaliwa) ni ile inayofanywa na mtu mwenye niyyah njema ya ikhlaasw, na mwaminifu, na ‘ibaadah zake zote zimefanywa kikamilifu na kisahihi kabisa, na ambayo matokeo yake humfanya Haji (anayehiji) atake zaidi uadilifu na utendaji sahihi.

[2] Hii inatufahamisha kwamba hakuna ulazima wa wanawake kujiunga au kushiriki katika Jihaad ya kupigana kwenye viwanja vya vita. Hadiyth hii inatufahamisha kuwa, kwa kufanya Hajj wanawake wanastahiki thawabu za Jihaad.

[3] Kiistilahi, ‘Umrah ni “ziara”. Kwa mujibu wa istilahi za ki-shariy’ah, inamaanisha: “Ukiwa katika hali ya Ihraam, uizunguke Ka’bah (utufu), uswali Rakaa mbili kuelekea Maqaam ya Ibraahiym, unywe maji ya zamzam, utembee baina ya Asw-Swafaa na Al-Marwaa, na upunguze au unyoe kabisa nywele.” Kuna tofauti ya maoni ya kuwa ‘Umrah ni waajib au laa. Wanazuoni wengine wanaihesabu kuwa Mustahabb (iliyopendekezwa). Allaah Anajua zaidi.

[4] Allaah Anasema katika Qur-aan kuwa, Hijjah ni lazima kwa wale wenye uwezo kuenda kuhiji. Mtu mmoja akamuuliza Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ): “Nini maana ya neno As-Sabiyl? (njia)” Naye Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akajibu: “Maana yake ni gharama za safari na za kukimu familia ya mtu aendae kuhiji, na upatikanaji wa njia ya usafiri. Haya yote akiwa nayo, mtu huyo analazimika kuenda kuhiji. Lakini gharama zote hizi lazima asizipate kwa kukopa, yaani asibaki na deni, kwani akiwa na deni kwa mtu mwingine halazimiki kufanya Hijjah. Watu wanaoishi pale pale Makkah hawana lile sharti la kuwa na njia ya usafiri.

[5] Hadiyth hii inatufahamisha kuwa, thawabu za tendo jema alitendalo mtoto mdogo huwafikia wazazi wake. Pia inatufahamisha kuwa, kuhusu kufanya ‘ibaadah za Hijjah watoto wadogo wanatawaliwa na shariy’ah zile zile za mama yao, yaani Ihraam ya mama yao inakuwa ndiyo Ihraam yao na wao; na kukimbia kwa mama yao huwa ndiyo kukimbia kwao. Na iwapo mtoto kaifanya Hajj kabla hajabaleghe, atalazimika kufanya Hajj nyingine akisha kubaleghe, ilimradi ana pesa za kutosha kulipia gharama zake na za njia ya usafiri wake.

[6] Al-Fadhwl bin ‘Abbaas alikuwa binami wa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), na mama yake alikuwa Umm Fadhwl Lubaabah Al-Kubraa bint Al-Haarith Al-Hilaaliyyah. Al-Fadhwl alikuwa mzuri wa sura. Alikuwa imara pamoja na Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) katika vita vya Hunayn, na alihudhuria uoshaji wa mwili wa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ). Alikuwa ndiye mwana wa kwanza wa Al-‘Abbaas. Alikwenda kwenye Jihaad kule Shaam, na yasemekana kuwa alikufa kwa tauni iitwayo “Amwas” kule Jordan mnamo mwaka wa 18 A.H. Pia inasemekana kuwa alikufa shahidi kule Yarmuk au kule Damascus akiwa amevaa deraya ya Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ).

[7] Hijjah huwa ni ya lazima kwa mtu aliyekuwa na pesa za kutosha kuenda kuhiji, njia yake inakuwa wazi na salama, anapata idhini ya serikali yake, na anayo njia ya usafiri pia. Na ikiwa mtu huyu ana afya imara, ni lazima aende Hijjah yeye mwenyewe, na kumpeleka mtu mwingine akamfanyie Hijjah yake haitokubaliwa. Iwapo mtu anakuwa mzee mno kujiweza au anaugua ugonjwa mkubwa mno ambao haielekei kupona, inaruhusiwa amtume mtu kuenda kuhiji kwa niaba yake kwa kumpa pesa, na atimize wajibu wake wa Hijjah kwa njia hiyo. Lakini ni sharti kuwa, huyo mtu anayetumwa kuenda kumhijia huyo asiyejiweza awe alikwisha kuhiji yeye mwenyewe kabla ya kutumwa.

[8] Hadiyth hii inatuarifu kuwa, iwapo atakufa mtu ambaye kuhiji kulikuwa lazima kwake alipokuwa hai, basi ni lazima mrithi wake ahiji kwa niaba yake, bila kujali kama aliacha wasia kuhusu hii Hijjah au la. Halikadhalika katika matendo mengine ya ‘ibaadah kama Swawm na Zakaah. (Rejea Ahkaam Al-Janaaiz, cha Shaykh Al-Albaaniy, ukurasa (168-178) kwa maelezo zaidi).

[9] Tunafahamishwa kwamba mwanamume na mwanamke ambao hawajuani wasikutane faragha. Mwanamke asiende safari yoyote, iwe ndefu au fupi, iwe kwa sababu za kidini au kwa dharura, isipokuwa awe na mume wake au Mahram  wake. Mahram ni mtu ambaye asiyeweza kumuoa mwanamke huyo.

[10] “Labbayka Allaahumma Labbayka” maana yake ni “Ninaitikia mwito Wako Ee Allaah!” maneno yarudiwayo kusemwa kwa sauti (wanaume) na wanawake (kimya kimya) baada ya kuingia katika Ihraam mpaka kufikia Makkah kwa ajili ya Twawaaf (kwa mwenye kutekeleza ‘Umrah). Kisha wanapoingia tena Ihraam kwa ajili ya taratibu za Hajj ambayo inaanza tarehe 8 mwezi wa Hajj.

[11] Hii inatufahamisha kuwa, kama mtu hajahiji kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, haruhusiwi kumhijia mwingine, hata ikiwa ana nguvu ya aina gani (nguvu za kiwiliwili na kifedha) ya kutekeleza Hijjah yake mwenyewe. Maimaam wengi wanaafiki maoni haya.

[12] Al-Aqra’ bin Haabis alikuwa Tamiymiy aliyekuwa katika ujumbe wa Banuw Tamiym uliomzuru Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) baada ya kutekwa Makkah. Alikuwa miongoni mwa Mu’allafati Quluwbuhum (ambao nyoyo zao zilizoezwa kwa ajili ya Uislam, na kwa hivyo wakapewa Swadaqah ili wabakie imara katika Uislam). Alikuwa anaheshimika sana katika Jaahiliyyah. Alikufa wakati wa Ukhalifa wa ‘Umar.

Share