04-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Hajj: Mlango Wa Ihraam Na Yanayohusiana Nayo

 

بُلُوغُ الْمَرام

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتَابُ اَلْحَجِّ

 

Kitabu Cha Hajj

 

بَابُ اَلْإِحْرَامِ وَمَا يَتَعَلَّقُ بِهِ

 

04-Mlango Wa Ihraam Na Yanayohusiana Nayo

 

 

 

 

593.

عَنْ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {مَا أَهَلَّ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏إِلَّا مِنْ عِنْدِ اَلْمَسْجِدِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kamwe hakupaza sauti katika Talbiyah isipokuwa alipo toka Msikitini (Dhul-Hulayfah).”[1] [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

594.

وَعَنْ خَلَّادِ بْنِ اَلسَّائِبِ عَنْ أَبِيهِ ‏ رضى الله عنه‏ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏قَالَ:{أَتَانِي جِبْرِيلُ، فَأَمَرَنِي أَنْ آمُرَ أَصْحَابِي أَنْ يَرْفَعُوا أَصْوَاتَهُمْ بِالْإِهْلَالِ} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ، وَصَحَّحَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ، وَابْنُ حِبَّانَ

Kutoka kwa Khallaad[2] bin As-Saaib kutoka kwa baba yake[3] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Jibriyl alikuja kwangu akaniamrisha niwaamrishe Swahaba zangu kupaza sauti[4] zao katika kutamka Talbiyah.”[5] [Imetolewa na Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad) na akaisahihisha At-Tirmidhiy na Ibn Hibbaan]

 

 

 

595.

وَعَنْ زَيْدِ بْنِ ثَابِتٍ رضى الله عنه {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم ‏تَجَرَّدَ لِإِهْلَالِهِ وَاغْتَسَلَ} رَوَاهُ اَلتِّرْمِذِيُّ وَحَسَّنَهُ

Kutoka kwa Zayd bin Thaabit (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alivua nguo zake (za kawaida) ili avae Ihraam zake na akaoga.”[6] [Imetolewa na At-Tirmidhiy na akaiita Hasan]

 

 

 

596.

وَعَنْ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا: {أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏سُئِلَ: مَا يَلْبَسُ اَلْمُحْرِمُ مِنْ اَلثِّيَابِ؟ فَقَالَ: "لَا تَلْبَسُوا الْقُمُصَ، وَلَا اَلْعَمَائِمَ، وَلَا السَّرَاوِيلَاتِ، وَلَا اَلْبَرَانِسَ، وَلَا اَلْخِفَافَ، إِلَّا أَحَدٌ لَا يَجِدُ اَلنَّعْلَيْنِ فَلْيَلْبَسْ اَلْخُفَّيْنِ وَلْيَقْطَعْهُمَا أَسْفَلَ مِنَ اَلْكَعْبَيْنِ، وَلَا تَلْبَسُوا شَيْئًا مِنْ اَلثِّيَابِ مَسَّهُ اَلزَّعْفَرَانُ وَلَا اَلْوَرْسُ"} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ وَاللَّفْظُ لِمُسْلِمٍ

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliulizwa mwenye kuhirimia anavaa nguo gani?[7] Akasema: Asivae shati, kilemba, suruali, vazi lenye vifuniko vya kichwa, wala viatu, isipokuwa kama mtu hawezi kupata ndala na akalazimika kuvaa viatu mbapo ni lazima avikate chini ya tindi ya mguu na asivae nguo zenye kutiwa rangi ya zaafarani (Manjano) au Wars.”[8] [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Muslim]

 

 

 

597.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {كُنْتُ أُطَيِّبُ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏لِإِحْرَامِهِ قَبْلَ أَنْ يُحْرِمَ، وَلِحِلِّهِ قَبْلَ أَنْ يَطُوفَ بِالْبَيْتِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Nilikuwa ninampaka manukato[9] Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kwa ajili ya Ihraam yake[10] kabla hajaivaa, na baada ya kuivua, kabla hajatufu Nyumba (hajaizunguka Ka’bah).” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

598.

وَعَنْ عُثْمَانَ بْنِ عَفَّانَ رضى الله عنه ‏ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏قَالَ:{لَا يَنْكِحُ اَلْمُحْرِمُ، وَلَا يُنْكِحُ، وَلَا يَخْطُبُ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Aliye katika Ihraam asioe, wala asimuozeshe mtu[11], wala asichumbie.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

599.

وَعَنْ أَبِي قَتَادَةَ اَلْأَنْصَارِيِّ ‏ رضى الله عنه {فِي قِصَّةِ صَيْدِهِ اَلْحِمَارَ اَلْوَحْشِيَّ، وَهُوَ غَيْرُ مُحْرِمٍ، قَالَ: فَقَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏لِأَصْحَابِهِ، وَكَانُوا مُحْرِمِينَ: " هَلْ مِنْكُمْ أَحَدٌ أَمَرَهُ أَوْ أَشَارَ إِلَيْهِ بِشَيْءٍ ؟ " قَالُوا: لَا.‏ قَالَ: " فَكُلُوا مَا بَقِيَ مِنْ لَحْمِهِ "} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Abuu Qataadah Al-Answaariy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Kuhusu Hadiyth ya yeye kuwinda pundamilia na hakuwa katika hali ya Ihraam, Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliwauliza Maswahaba wake waliokuwa katika hali ya Ihraam kuwa: “Kuna yeyote kati yenu amependekeza au ameashiria chochote kwake kuhusu kuwinda?” Wakasema: “Hapana.” Akasema: “Kuleni nyama yake iliyobakia.”[12] [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

600.

وَعَنْ اَلصَّعْبِ بْنِ جَثَّامَةَ اَللَّيْثِيِّ رضى الله عنه {أَنَّهُ أَهْدَى لِرَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏حِمَارًا وَحْشِيًّا، وَهُوَ بِالْأَبْوَاءِ، أَوْ بِوَدَّانَ، فَرَدَّهُ عَلَيْهِ، وَقَالَ: " إِنَّا لَمْ نَرُدَّهُ عَلَيْكَ إِلَّا أَنَّا حُرُمٌ "} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Asw-Swa’b bin Jath-thaamah Al-Laythiyy[13] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa: “Alimpa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) nyama ya pundamilia[14] alipokuwa Al-Abwaa au Waddaan, akaikataa na kusema: “Tulikataa kwa sababu tulikuwa katika Ihraam.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

601.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏{خَمْسٌ مِنَ اَلدَّوَابِّ كُلُّهُنَّ فَاسِقٌ، يُقْتَلْنَ فِي اَلْحِلِّ وَ اَلْحَرَمِ: اَلْغُرَابُ، وَالْحِدَأَةُ، وَالْعَقْرَبُ، وَالْفَأْرَةُ، وَالْكَلْبُ اَلْعَقُورُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Kuna viumbe watano wana madhara, na vinaweza kuuliwa nje au ndani ya maeneo matukufu: (a) Kunguru (b) Kipanga, (c) ‘Nge, (d) Panya na (e) mbwa anayeuma watu.”[15] [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

602.

وَعَنِ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا، أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم ‏{اِحْتَجَمَ وَهُوَ مُحْرِمٌ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ): “Alifanya hijaamah (kuumikwa) wakati akiwa katika hali ya Ihraam.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

603.

وَعَنْ كَعْبِ بْنِ عُجْرَةَ رضى الله عنه ‏ قَالَ: {حُمِلْتُ إِلَى رَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏وَالْقَمْلُ يَتَنَاثَرُ عَلَى وَجْهِي، فَقَالَ: " مَا كُنْتُ أَرَى اَلْوَجَعَ بَلَغَ بِكَ مَا أَرَى، تَجِدُ شَاةً ؟ قُلْتُ: لَا.‏ قَالَ: " فَصُمْ ثَلَاثَةَ أَيَّامٍ، أَوْ أَطْعِمْ سِتَّةَ مَسَاكِينَ، لِكُلِّ مِسْكِينٍ نِصْفُ صَاعٍ "} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Ka’b bin ‘Ujrah[16] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nilichukuliwa mpaka kwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) na chawa walikuwa wakipuputika usoni mwangu. Akasema: “Sikujua kuwa uchungu umekuathiri kama ninavyoona sasa, unaweza kutoa kafara ya mbuzi?” Nikasema: “Hapana.” Akasema: “Funga Swawm siku tatu au walishe maskini sita kila masikini nusu pishi.”[17] [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

604.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: {لَمَّا فَتَحَ اَللَّهُ عَلَى رَسُولِهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏مَكَّةَ، قَامَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏فِي اَلنَّاسِ، فَحَمِدَ اَللَّهَ وَأَثْنَى عَلَيْهِ، ثُمَّ قَالَ: " إِنَّ اَللَّهَ حَبَسَ عَنْ مَكَّةَ اَلْفِيلَ، وَسَلَّطَ عَلَيْهَا رَسُولَهُ وَالْمُؤْمِنِينَ، وَإِنَّهَا لَمْ تَحِلَّ لِأَحَدٍ كَانَ قَبْلِي، وَإِنَّمَا أُحِلَّتْ لِي سَاعَةٌ مِنْ نَهَارٍ، وَإِنَّهَا لَنْ تَحِلَّ لِأَحَدٍ بَعْدِي، فَلَا يُنَفَّرُ صَيْدُهَا، وَلَا يُخْتَلَى شَوْكُهَا، وَلَا تَحِلُّ سَاقِطَتُهَا إِلَّا لِمُنْشِدٍ، وَمَنْ قُتِلَ لَهُ قَتِيلٌ فَهُوَ بِخَيْرِ اَلنَّظَرَيْنِ " فَقَالَ اَلْعَبَّاسُ: إِلَّا اَلْإِذْخِرَ، يَا رَسُولَ اَللَّهِ، فَإِنَّا نَجْعَلُهُ فِي قُبُورِنَا وَبُيُوتِنَا، فَقَالَ: " إِلَّا اَلْإِذْخِرَ "} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Allaah alipompa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) ushindi wa Makkah, Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alisimama akamhimidi na kumtukuza Allaah kisha akasema: “Allaah Alizuia tembo[18] asiingie Makkah, na Akampa uwezo Rasuli Wake na Waumini wa kushinda. Kupigana ndani yake hakukuruhusiwa kwa mtu yeyote kabla yangu, lakini imeruhusiwa kwangu saa moja ya mchana, na haitoruhusiwa kwa yeyote baada yangu. Wanyama wake hawatumbuliwa, miiba yake haitakatwa, si halali kuokota kinachoangukia ila kwa yule anayekitangaza,[19] na mwenye kuuwawa mtu wake ana chaguo zuri kati ya zaidi kati ya mawili hayo.”[20] Al-‘Abbaas akasema: “Isipokuwa mti uitwao Al-Idkhir Ee Rasuli wa Allaah! Kwa sababu tunautumia katika makaburi na nyumba zetu.” Naye akasema: “Isipokuwa Al-Idkhir.”[21] [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

605.

وَعَنْ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ زَيْدِ بْنِ عَاصِمٍ ‏ رضى الله عنه ‏ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏قَالَ: {إِنَّ إِبْرَاهِيمَ حَرَّمَ مَكَّةَ وَدَعَا لِأَهْلِهَا، وَإِنِّي حَرَّمْتُ اَلْمَدِينَةَ كَمَا حَرَّمَ إِبْرَاهِيمُ مَكَّةَ، وَإِنِّي دَعَوْتُ فِي صَاعِهَا وَمُدِّهَا بِمِثْلَيْ‏ مَا دَعَا‏ إِبْرَاهِيمُ لِأَهْلِ مَكَّةَ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin Zayd bin ‘Aaswim (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Kuwa Ibraahiym alitangaza Makkah kuwa ni tukufu,[22] na kawaombea du’aa watu wake, na mimi naitangaza Al-Madiynah kuwa ni tukufu kama Ibraahiym alivyoitangaza Makkah kuwa ni tukufu, na mimi ninaomba katika pishi na kibaba (ibarikiwe), mara mbili zaidi kuliko Ibraahiym alivyowaombea watu wa Makkah.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

606.

وَعَنْ عَلِيِّ بْنِ أَبِي طَالِبٍ رضى الله عنه‏ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏{اَلْمَدِينَةُ حَرَمٌ مَا بَيْنَ عَيْرٍ إِلَى ثَوْرٍ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa ‘Aliy bin Abuu Twaalib (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Al-Madiynah ni tukufu kutoka ‘Ayr hadi Thawr.”[23] [Imetolewa na Muslim]

 

[1] Hadiyth hii inadhihirisha Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliingia katika Ihraam ima kule Baida au karibu na mti. Pia tunafahamishwa kuwa kuingia katika Ihraam kabla ya kufika katika Miyqaat kumekatazwa. Hii inapinga maoni ya wengine wanaosema ni sawa kuingia katika hali ya Ihraam kabla.

[2] Khallaad ndiye Khallaad bin As-Saaib bin Khallaad bin Suwayd Al-Answaar Al-Khazraj, ambaye alikuwa Taabi’iy aliyetegemewa sana wa kizazi cha tatu.

[3] Babake Khallaad ni Swahaba aliyepewa jina la utani la Abuu Sahla. Alihudhuria vita vya Badr na akawa gavana wa Mu’aawiyah huko Yaman. Inasemekana pia kuwa ‘Umar alimpeleka kule Yaman. Alikufa mnamo mwaka wa 71 A.H.

[4] Hadiyth hii inatufahamisha kuwa ni lazima kutamka Talbiyah kwa sauti kubwa. Kuhusu wanawake ‘Ulamaa wengi wanaona kuwa waitamke Talbiyah kwa sauti ya chini.  

[5] Talbiyah ni kutamka:

 

لَبَّيْكَ اللَّهُمَّ لَبَّيْكَ ، لَبَّيْكَ لاَ شَرِيكَ لَكَ لَبَّيْكَ ، إِنَّ الْحَمْدَ ، وَالنِّعْمَةَ ، لَكَ وَالْمُلْكَ ، لاَ شَرِيكَ لَكَ

Labbayka-Allaahumma Labbayk. Labbayka laa shariyka Laka Labbayk. Innal-Hamda Wan-Ni'imata Laka wal-Mulk laa shariyka Lak.

"Nimekuitikia Ee Allaah nimekuitika, nimekuitika Huna mshirika nimekuitika, hakika Himdi na Neema na Ufalme ni Vyako Huna mshirika."

 

 

[6] Hii inatufahamisha kua kuoga kwa ajili ya kuingia katika Ihraam ni Sunnah.

[7] Nguo zote hizi zikishavuliwa, nguo pekee za kuvaa ni shuka mbili ambazo ndiyo nguo za Ihraam yenyewe. Mwanamke anaweza kufunika kichwa chake kwa ushungi, lakini asifunike uso wake kwa ushungi.

[8] Manukato yenye rangi ya manjano.

[9] Kupitia Hadiyth hii inadhihirisha kuwa, manukato yanaweza kupakwa katika mwili wa hujaji kabla hajaingia katika Ihraam, na si ubaya kama mwili wake utaendelea kunukia hata baada ya kuingia katika Ihraam. Pia inaruhusiwa tena kupaka mwili manukato kabla ya Twawaaful-Widaa’i (Twawaaf ya kuaga).

[10] Hali ya kuwania kutekeleza Hijjah na ‘Umrah.

[11] Mtu ambaye yumo katika hali ya Ihraam haruhusiwi kufungisha ndoa ya mwanamume au mwanamke au yake mwenyewe au kwa niaba ya mtu mwingine.

[12] Tukio hili lilitokea mnamo mwaka wa Mkataba wa Al-Hudaybiyah. Kama mtu Halal (yaani mtu ambaye hayumo katika hali ya Ihraam) anawinda mnyama kwa niyyah ya kumpa Muhrim, au kwa njia yoyote ile Muhrim alijisaidia yeye mwenyewe kuwinda, anakatazwa kula nyama ya mnyama aliyewindwa hivyo. Inaruhusiwa pale tu ambapo mnyama huyo amewindwa na au kwa niaba ya mtu Halal, bila kusaidiwa na kwa ridhaa ya Muhrim.

[13] Asw-Swa’b bin Jath-thaamah Al-Laythiyy aliishi kule Waddaan na Al-Abwaa na Hadiyth yake ilitajwa na watu wa Al-Hijaaz. Alikuwa katika Ukhalifa wa Abuu Bakar au wa ‘Uthmaan.

[14] Hii inatuarifu kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikula nyama ya mnyama aliyewindwa akiwa katika Ihraam kwa kuwa Sa’b aliwinda kwa niyyah ya kumpa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ).

[15] Kuwaua wanyama hao watano hata wakiwa wamo ndani ya eneo la Msikiti Mtukufu siyo vibaya. Halikadhalika, mtu akiwaua hao wakati yumo katika hali ya Ihraam na yumo ndani ya eneo la Msikiti Mtukufu, hapati adhabu yoyote (kama kutoa kafara ya mnyama au Swadaqah). Kwa kunukuu Hadiyth au tukio hili la mwanzo, Wanazuoni wengine wamekuwa wakiruhusu kuuliwa kwa wanyama wote Haraam (yaani wanyama ambao kuliwa nyama yake kumekatazwa katika Uislam), na hawataji adhabu yoyote kwa mtu kuwaua hao. Inapotokea Muhrim anamuua mnyama baada ya kumshambulia, hapati adhabu yoyote.

[16] Ka’b bin ‘Ujrah alikuwa Swahaba maarufu kutoka katika kabila la Al-Bali, na alikuwa rafiki wa Answaar. Alilowea Kufa na akafia Al-Madiynah mnamo mwaka wa 51 A.H. akiwa na umri wa miaka 75.

[17] Hii inatuarifu kuwa Muhrim analazimika kulipa fidya, hata kama kanyoa kichwa chake kwa sababu maalumu. Na fidya zipo aina tatu: (a) Atoe kafara ya mnyama (b) Afunge Swawm siku tatu (c) Awalishe maskini sita au atoe kilo moja ya nafaka kama Swadaqah kwa kila mtu. Endapo akiwa na uwezo wa kutoa kafara ya mnyama, basi haruhusiwi kutoa fidya hizo mbili za mwisho. Ikiwa hana pesa za kutosha kutoa kafara atachagua moja kati ya haya mawili: (i) Ima afunge Swawm, au (ii) Awalishe maskini.

[18] Hadiyth hii imesimuliwa katika Qur-aan (105: 1-5). Imesemwa kuwa Abraha Al-Athram alipokuwa mfalme wa Manaswara wa Yaman, aliishambulia Makkah kwa jeshi la tembo wengi, kwa lengo la kuibomoa Ka’bah. Maqurayshi hawakuweza kumkabili, kwa hivyo waliondoka Makkah na wakakimbilia mbali. Allaah (سبحانه وتعالى)  Akawatuma makundi ya ndege wana vijiwe vidogo mdomoni mwao na kwenye makucha yao. Kila aliyeangukiwa na vijiwe hivi, kwa nguvu za mateso Aliyoyatuma Allaah (سبحانه وتعالى) aliteketea. Abraha, pamoja na majeshi yake yaliyokuwa yakiunguruma wakaishia kuangamizwa. Na hivyo ndivyo Allaah (عزّ وجلّ)  Alivyoiokoa Nyumba Yake (Ka’bah) isibomolewe.

[19] Hii inamaanisha kuwa iwapo mtu ataokota kitu kitachoanguka au kupotea mle kwa niyyah ya kukichukua yeye mwenyewe, imekatazwa. Lakini akikiokota kwa niyyah ya kutangaza ili kirejeshwe kwa mwenye kukimiliki kihalali, hiyo imeruhusiwa.

[20] Yaani atachagua kati ya haya mawili: (a) Ima atakubali apewe diya (pesa za damu, au malipo kwa kuuliwa mtu wake). (b) Au anaweza kuchagua kulipiza kwa kumuua muuaji yaani kuchukua Qiswaasw (kisasi)

[21] Al-Idkhir ni aina ya majani yanayotumika katika mchakato wa kuyeyusha metali. Hayo hulazwa juu ya mapaa na sakafuni ndani ya majumba, na pia hupandwa makaburini pia.

[22] Nabiy Ibraahiym   (عليه السلام)      aliitangaza Makkah kuwa ni patukufu, na aliwaombea watu wake waweze kujikimu. Naye Nabiy Muhammad (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) pia aliitangaza Al-Madiynah kuwa ni tukufu na akawaombea watu wake waweze kujikimu.

[23] ‘Ayr na Thawr ni milima miwili inayoizunguka Al-Madiynah. ‘Ayr ni mlima maarufu ulioko kusini mwa Al-Madiynah na kusini Magharibi ya Msikiti wa Qubaa. Watu wengine wameelewa vibaya kwamba mlima wa Thawr uko Makkah, na huenda msimuliaji alikosea huo kwa kuudhani ni mlima mwingine. Ukweli ni kwamba, maoni yao haya yamekosewa. Kuna mlima kule Al-Madiynah pia, mdogo na wa mviringo, ulioko kaskazini mbele zaidi ya mlima wa Uhud ambao pia unaitwa Thawr.

Share