11-Imaam Ibn Baaz: Kuwaombea Du'aa Wazazi Katika Swalaah Na Kupeleka Thawabu Za Kusoma Qur-aan Au Twawaaf Kwa Ajili Yao

 

Kuwaombea Du'aa Wazazi Katika Swalaah Na Kupeleka Thawabu

Za Kusoma Qur-aan Au Twawaaf Kwa Ajili Yao

 

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)

 

www.alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Inasemekana kuwa kuwaombea du'aa wazazi katika Swalaah za fardhi hairuhusiwi wala kuwasomea Khitmah   kutegemea thawabu ziwafikie au kuwafanyia twawaaf.

 

JIBU:

 

Hakuna ubaya kuomba du'aa katika Swalaah aidha kwa ajili ya nafsi yake mtu, au kuwaombea wazazi (au wengineo) bali hii inapasa. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mja huwa karibu kabisa na Rabb wake akiwa katika sujuud, hivyo ongezeni kufanya du'aa [humo])) [Muslim]

 

Pia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ama Rukuu ni kumtukuza Allaah, na ama sujuud ni kujitahidi kufanya du'aa kwani ni karibu zaidi na kukubaliwa)) [Muslim]

 

Na katika Swahiyhayn za Imaam al-Bukhaariy na Imaam Muslim kutoka kwa Ibn Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimfundisha tashahhud akasema: ((…na chagua du'aa ambayo unaipenda na uombe [humo]))

Riwaayah nyengine:   ((…na chagua unachotamani))

 

Inavyokusudiwa hapa ni kuwa kabla ya tasliym (kutoa salaam), kwa hiyo akiomba du'aa katika sujuud au mwisho wa Swalaah kwa ajili ya nafsi yake, wazazi wake au Waislamu, hakuna ubaya kwani ni kama ilivyotajwa kwa ujumla katika Hadiyth hizi na nyinginezo.

Ama kusoma khitmah na kutegemea thawabu, au kuwafanyia twawaaf wazazi, au Waislamu wengineo, hii ni mas-ala yenye ikhtilaaf baina ya ‘Ulaama. Lililokuwa ni bora ni kuacha kwani hakuna dalili inayotaja kuruhusiwa kwake. Vitendo vya ibaada vimebainishwa wazi kwa kuthibiti daima kwa hiyo kusitendewe vitendo vingine ila vikiwa vimetajwa katika Shariy’ah ya Dini kwani Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

( من أحدث في أمرنا هذا ما ليس منه فهو رد) متفق عليه.

((Atakayezusha katika mambo yasiyokuwa yetu (Ya Dini yetu) kitarudishwa)) [Al-Bukhaariy na Muslim] 

Katika Riwaayah nyengine:

 

(( من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري

((Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu (katika Dini yetu) basi kitarudishwa)) [Al-Bukhaariy]

 

Wa Billaahi Tawfiyq

 

[Al-Bid’ah wal-Muhdathaat wa Maa Laa aswla lahu – Uk.382]

 

[Majalah al-Buhuuth al-Islaamiyyah  - Mjalada 46, Uk. 198]

 

Share