05-Imaam Ibn Baaz: Mwanamke Kuvaa Soksi Na Glavu Akiwa Katika Ihraam
Mwanamke Kuvaa Soksi Na Glavu Akiwa Katika Ihraam
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)
SWALI:
Nini hukmu ya mwanamke kuvaa soksi na glavu akiwa katika Ihraam? Je, anaruhusiwa kuvua hizo anapokuwa katika ihraam?
JIBU:
Inapendekezeka mwanamke avae soksi au viatu. Ni bora kwake na bora kujifunika vizuri. Itatosheleza kama atavaa nguo pana (za kumfunika vizuri). Hakuna kipingamizi ikiwa atavaa soksi kisha akazivua, kama vile mwanaume anapovaa viatu kisha akavivua anapotaka hakuna ubaya kufanya hivyo. Lakini hairuhusiwi kwake kuvaa glavu kwani mwanamke amekatazwa kuvaa glavu katika ihraam. Vile vile hatakiwi kuvaa niqaab (kujifunika uso) au chochote kitakachomfunika uso kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza hivyo. Lakini mwanamke ateremshe utaji (ushungi) wake (ajifunike uso) anapokuwa mbele ya wasio Mahram wake. Na inafaa afanye hivyo anapofanya twawaaf na sa'y. 'Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema: "Wapandaji (wanaume) walipita mbele yetu tukiwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Walipokuwa sambamba mbele yetu tuliteremsha utaji (shungi) zetu usoni na vichwani mwetu, kisha walipotoweka tulijifunua)) [Abu Daawuwd na Ibn Maajah]
Mwanamume anaruhusiwa kuvaa kanda mbili au viatu ikiwa havijakatwa. Hii ni rai sahihi. Kwa upande mwengine rai ya ‘Ulamaa wengi ni kwamba wavikate. Na rai iliyo sahihi ni kuwa haijawajibika kwake kuvikata ikiwa hakuweza kuvikata (Viatu). Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alihutubia watu siku ya 'Arafah na akasema: ((Yeyote ambaye hakuweza kuvaa Izaar (nguo ya ihraam ya wanaume ambayo haikushonwa) basi avae suruwali. Na yeyote ambaye hakuweza kupata kanda mbilli (au viatu vya ngozi, au viatu vya makubadhi) basi avae viatu vya wazi)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwaamrisha wavikate viatu vyao hivyo, amri ya kukata imefutwa hapa.
WabiLLaahi At-Tawfiyq
[Fataawaa Muhimmah Tata'allaq bil-Hajji wal 'Umrah – Uk. 18, Fatwa Namba 6]