03-Imaam Ibn Baaz: Mwanamke Aliyeingia Katika Ihraam Akiwa Ana Hedhi
Mwanamke Aliyeingia Katika Ihraam Akiwa Ana Hedhi
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)
SWALI:
Mwanamke anauliza – Alitolewa udhuru, yaani alikuwa na hedhi, na familia yake walitaka kwenda kufanya 'Umrah. Angeliachwa nyuma, kungelikuwa hakuna mtu wa kubakia naye. Hivyo alikwenda nao 'Umrah na kutekeleza taratibu zote za 'Umrah pamoja na twawaaf na sa’y, kama kwamba hayumo kwenye hedhi. Amefanya hivyo kwa ujinga wa kutokujua na kuwa na hayaa ya kutaja hedhi yake kwa mlinzi wake. Tanbihi: Yeye hajui kusoma wala kuandika. Je afanye nini?
JIBU:
Ikiwa ameingia ihraam ya 'Umrah, basi lazima arudie twawaaf baada ya ghuslu (kuoga josho) na arudie kukata nywele kidogo.
Ama kufanya sa'y (Swafaa na Marwah), hivyo ndio sahihi kutokana na rai yenye nguvu miongoni mwa ‘Ulamaa. Akirudia kufanya sa'y itakuwa ni bora na vizuri zaidi. Kisha lazima aombe tawbah kwa Allaah kwa twawaaf yake na kuswali Raka'h mbili alipokuwa katika hedhi.
Ikiwa ameolewa, mumewe haimpasi kujamii (kufanya naye kitendo cha ndoa) hadi amalize 'Umrah yake. Ikiwa amejamii na mumewe basi 'Umrah yake imebatilika na lazima achinje kondoo mwenye umri wa mwaka mmoja au mbuzi mwenye umri wa miaka miwili akiwa Makkah na nyama igaiwe kwa masikini.
Pia lazima amalize 'Umrah yake kama ilivyotajwa kabla. Lazima afanye 'Umrah mpya kutoka Miyqaat ile ile aliyoingilia ihraam mwanzo kuibadilisha 'Umrah yake aliyoiharibu. Lakini ikiwa amefanya 'Umrah na wao kwa ajili ya heshima tu na kuona hayaa na sio kusudio lakekuingia katika ihraam kutoka Miyqaat, basi kinachompasa ni kuomba tawbah kwa Allaah. Hii ni kwa saabu Hajj na 'Umrah hazisihi bila ya kuingia katika ihraam. Na mtu huingia katika ihraam kwa ajili ya nia ya Hajj au 'Umrah.
Tunamuomba Allaah muongozo na usalama wetu sote kutokana na wasiwasi wa shaytwaan.