02-Wasiya Kumi Katika Mwisho Wa Suwrah Al-An’aam: Kuwafanyia Wema Wazazi
Wasiya Kumi Wa Allaah
02-Kuwafanyia Wema Wazazi
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا
na muwafanyie ihsaan wazazi wawili [Al-An’aam: 151]
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wmesisitiza sana kuwafanyia wazazi wema. Baadhi ya dalili zake ni:
Kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kutaja ihsaan kwa wazazi wawili baada ya kutaja kumwabudu Yeye, jambo ambalo linadhihirisha umuhimu wa kuwatendea wema wazazi wawili:
وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا ﴿٢٣﴾
Na Rabb wako Amehukumu kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye Pekee na (Ameamrisha) kuwafanyia ihsaan wazazi wawili. Kama mmoja wao akifikia uzee naye yuko pamoja nawe, au wote wawili basi usiwaambie, Uff! Na wala usiwakemee; na waambie maneno ya heshima.
وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّحْمَةِ وَقُل رَّبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا ﴿٢٤﴾
Na wainamishie bawa la unyenyekevu kwa huruma, na useme: “Rabb wangu! Warehemu kama walivyonilea udogoni.” [Al-Israa: 23-24]
Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَإِذْ أَخَذْنَا مِيثَاقَ بَنِي إِسْرَائِيلَ لَا تَعْبُدُونَ إِلَّا اللَّـهَ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا
Na pindi Tulipochukua fungamano ya wana wa Israaiyl (Tukawaambia): “Msiabudu isipokuwa Allaah; na muwafanyie ihsaan wazazi wawili, [Al-Baqarah: 83]
Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
عَنْ اِبْن مَسْعُود رَضِيَ اللَّه عَنْهُ أَنَّهُ قَالَ : سَأَلْت رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَيّ الْعَمَل أَفْضَل ؟ قَالَ الصَّلَاة عَلَى وَقْتهَا قُلْت ثُمَّ أَيّ ؟ قُلْ بِرّ الْوَالِدَيْنِ قُلْت ثُمَّ أَيّ ؟ قَالَ الْجِهَاد فِي سَبِيل اللَّه)) البخاري و مسلم
Kutoka kwa Ibn Mas’uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Nilimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): Kitendo gani bora kabisa? Akasema: ((Swalaah kwa wakati wake)) Kisha nikasema: Kisha kipi? Akasema: ((Kuwafanyia wema wazazi wawili)): Kisha nikasema: Kisha kipi? Akasema: ((Jihadi katika njia ya Allaah)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Hata wazazi wasiokuwa Waislamu wanapaswa kutendewa wema madamu tu hawataamrisha kumshirikisha Allaah ('Azza wa Jalla) kama Anavyosema:
وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حُسْنًا ۖ وَإِن جَاهَدَاكَ لِتُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۚ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٨﴾
Na Tumemuusia insani kuwafanyia wema wazazi wake wawili. Lakini wakikushikilia kuwa Unishirikishe na ambayo huna elimu nayo, basi usiwatii; Kwangu ni marejeo yenu, Nitakujulisheni yale mliyokuwa mkiyatenda. [Al-‘Ankabuwt: 8]
Wazazi wanapaswa kutendewa wema hata baada ya kufariki kwao kwa kuwatendea ‘amali kadhaa ambazo zinawafikia thawabu zake kwao. Bonyeza kiungo kifuatacho kwa faida zaidi:
‘Amali Za Kuwatendea Wazazi Waliofariki Waendelee Kupokea Thawabu