02-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Biashara: Mlango Wa Khiyari
بُلُوغُ الْمَرام
Buluwgh Al-Maraam
كِتَابُ اَلْبُيُوعِ
Kitabu Cha Biashara
بَابُ اَلْخِيَارِ
02-Mlango Wa Khiyari
692.
وَعَنْ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا، عَنْ رَسُولِ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ قَالَ: {إِذَا تَبَايَعَ اَلرَّجُلَانِ، فَكُلُّ وَاحِدٍ مِنْهُمَا بِالْخِيَارِ مَا لَمْ يَتَفَرَّقَا وَكَانَا جَمِيعاً، أَوْ يُخَيِّرُ أَحَدُهُمَا اَلْآخَرَ، فَإِنْ خَيَّرَ أَحَدُهُمَا اَلْآخَرَ فَتَبَايَعَا عَلَى ذَلِكَ فَقَدَ وَجَبَ اَلْبَيْعُ، وَإِنْ تَفَرَّقَا بَعْدَ أَنْ تَبَايَعَا، وَلَمْ يَتْرُكْ وَاحِدٌ مِنْهُمَا اَلْبَيْعَ فَقَدْ وَجَبَ اَلْبَيْعُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَّفْظُ لِمُسْلِمٍ
Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Wakiuziana watu wawili basi kila mmoja miongoni mwao yuko katika khiyari[1] maadamu hawajaachana na wapo pamoja, au mmojawapo amkhiarishe mwingine na wakauziana juu ya maafikiano hayo; basi kuuziana kumeshapasa. Na wakiachana baada ya kuuziana, na mmoja kati yao hakuacha kuuza au kununua, basi kuuziana kumeshapasa.” [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Muslim]
693.
وَعَنْ عَمْرِو بْنِ شُعَيْبٍ، عَنْ أَبِيهِ، عَنْ جَدِّهِ، أَنَّ اَلنَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ قَالَ: {اَلْبَائِعُ وَالْمُبْتَاعُ بِالْخِيَارِ حَتَّى يَتَفَرَّقَا، إِلَّا أَنْ تَكُونَ صَفْقَةَ خِيَارٍ، وَلَا يَحِلُّ لَهُ أَنْ يُفَارِقَهُ خَشْيَةَ أَنْ يَسْتَقِيلَهُ} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ إِلَّا اِبْنَ مَاجَهْ، وَاَلدَّارَقُطْنِيُّ، وَابْنُ خُزَيْمَةَ، وَابْنُ اَلْجَارُودِ وَفِي رِوَايَةٍ:{حَتَّى يَتَفَرَّقَا مِنْ مَكَانِهِمَا}
Kutoka kwa ‘Amr bin Shu’ayb amepokea kutoka kwa baba yake kutoka kwa babu yake kuwa amesema Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Muuzaji na mnunuzi wako katika khiyari hadi watakapoachana, isipokuwa iwe na maafikiano ya khiyari, wala si halali kwake kufarikiana naye kwa kuchelea asije akabatilisha mauziano.” [Imetolewa na Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ahmad) isipokuwa Ibn Maajah, na imetolewa na Ad-Daaraqutwniyy, Ibn Khuzaymah na Ibn Al-Jaaruwd]
Katika Riwaayaha nyingine imesema: “…mpaka wafarikiane mahala pao.”
694.
وَعَنِ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: ذَكَرَ رَجُلٌ لِلنَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ أَنَّهُ يُخْدَعُ فِي اَلْبُيُوعِ فَقَالَ: {إِذَا بَايَعْتَ فَقُلْ: لَا خَلَابَةَ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ
Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa mtu mmoja[2] amemuambia Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kuwa yeye hudanganywa katika biashara. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akamuambia: “Unapofanya biashara, muambie unayefanya naye hakuna kuhadaana.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
[1] Ikhtiyaar au Khiyaar ni mtu kuwa na haki ya kuvunja mkataba. Kuna aina nyingi za khiyaar:
i. Khiyaar Majlis: muda wa kuwa muuzaji na mnunuzi wako pamoja, kila mmoja ana haki ya kukataa au kukubali muamala.
ii. Khiyaar Shartw: Muuzaji na mnunuzi wanaweka sharti kuwa hadi muda fulani, basi kila mmoja wao ana haki ya kukubali au kukataa mauzo.
iii. Khiyaar ‘Ayb: Mnunuzi anasema ikiwa bidhaa ni mbovu atairudisha.
Iv. Khiyaar Ru’yah: Mnunuzi anakamilisha muamala kwa sharti kuwa itakamilika baada ya kuona bidhaa.
v. Khiyaar Ta’ayiyn: Ina maana kuwa mnunuzi anaruhusiwa kuchagua anachokitaka.
[2] Bwana huyu akiitwa Habbaan bin Munqadh. Alipata ajali kichwani na kumbukumbu yake ikawa ndogo, baadhi ya watu walikuwa wakimdanganya katika biashara, kwa hivyo Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akamfundisha maneno haya.