03-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Biashara: Mlango Wa Ribaa

 

بُلُوغُ الْمَرام

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتَابُ اَلْبُيُوعِ

Kitabu Cha Biashara

 

 

بَابُ اَلرِّبَا

03-Mlango Wa Ribaa

 

 

 

695.

عَنْ جَابِرٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ: {لَعَنَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  آكِلَ اَلرِّبَا، وَمُوكِلَهُ، وَكَاتِبَهُ، وَشَاهِدَيْهِ، وَقَالَ: " هُمْ سَوَاءٌ "}  رَوَاهُ مُسْلِمٌ

وَلِلْبُخَارِيِّ نَحْوُهُ مِنْ حَدِيثِ أَبِي جُحَيْفَةَ 

Kutoka kwa Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amemlaani mlaji ribaa, mwakilishi wake, mwandishi wake, na mashahidi wake wawili na akasema: “Wote wako sawa.”[1] [Imetolewa na Muslim]

Na katika Al-Bukhaariy amepokea kama hiyo katika Hadiyth ya Abuu Juhayfah

 

 

 

696.

وَعَنْ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ عَنْ اَلنَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ قَالَ: {اَلرِّبَا ثَلَاثَةٌ وَسَبْعُونَ بَابًا أَيْسَرُهَا مِثْلُ أَنْ يَنْكِحَ اَلرَّجُلُ أُمَّهُ، وَإِنَّ أَرْبَى اَلرِّبَا عِرْضُ اَلرَّجُلِ اَلْمُسْلِمِ} رَوَاهُ اِبْنُ مَاجَهْ مُخْتَصَراً، وَالْحَاكِمُ بِتَمَامِهِ وَصَحَّحَهُ

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas-‘uwd (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Ribaa ina milango sabini na tatu mwepesi wake ni mfano wa mtu kumuowa mama yake. Kwa hakika ribaa kubwa zaidi ni mtu kuchafua heshima ya Muislam.” [Imetolewa na Ibn Maajah kwa mukhtasari, na Al-Haakim ameipokea kwa ukamilifu na akaisahihisha]

 

 

 

697.

وَعَنْ أَبِي سَعِيدٍ اَلْخُدْرِيِّ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ قَالَ: {لَا تَبِيعُوا اَلذَّهَبَ بِالذَّهَبِ إِلَّا مِثْلًا بِمِثْلٍ، وَلَا تُشِفُّوا  بَعْضَهَا عَلَى بَعْضٍ، وَلَا تَبِيعُوا اَلْوَرِقَ بِالْوَرِقِ إِلَّا مِثْلًا بِمِثْلٍ، وَلَا تُشِفُّوا بَعْضَهَا عَلَى بَعْضٍ، وَلَا تَبِيعُوا مِنْهَا غَائِباً بِنَاجِزٍ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

 Kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Msiuze dhahabu kwa dhahabu isipokuwa sawa kwa sawa, wala msizidishe baadhi yake juu ya baadhi nyingine. Wala msiuze fedha kwa fedha isipokuwa sawa kwa sawa, wala msizidishe baadhi yake juu ya baadhi nyingine, wala msiuze kusichokuwepo kwa kilichopo.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

698.

وَعَنْ عُبَادَةَ بْنِ اَلصَّامِتِ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  {اَلذَّهَبُ بِالذَّهَبِ، وَالْفِضَّةُ بِالْفِضَّةِ، وَالْبُرُّ بِالْبُرِّ، وَالشَّعِيرُ بِالشَّعِيرِ، وَالتَّمْرُ بِالتَّمْرِ، وَالْمِلْحُ بِالْمِلْحِ، مِثْلًا بِمِثْلٍ، سَوَاءً بِسَوَاءٍ، يَدًا بِيَدٍ، فَإِذَا اِخْتَلَفَتْ هَذِهِ اَلْأَصْنَافُ فَبِيعُوا كَيْفَ شِئْتُمْ إِذَا كَانَ يَدًا بِيَدٍ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ 

Kutoka kwa ‘Ubaadah bin Asw-Swaamit[2] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Dhahabu kwa dhahabu, fedha kwa fedha, ngano kwa ngano, shayiri[3] kwa shayiri, tende kwa tende, chumvi kwa chumvi, mfano kwa mfano, sawa kwa sawa, mkono kwa mkono,[4] zitatofautiana aina hizi basi uza unavyotaka muda wa kuwa mauzo yatafanyika mkono kwa mkono.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

699.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ {اَلذَّهَبُ بِالذَّهَبِ وَزْناً بِوَزْنٍ مِثْلًا بِمِثْلٍ، وَالْفِضَّةُ بِالْفِضَّةِ وَزْناً بِوَزْنٍ مِثْلًا بِمِثْلٍ، فَمَنْ زَادَ أَوْ اِسْتَزَادَ فَهُوَ رِبًا} رَوَاهُ مُسْلِمٌ 

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Dhahabu kwa dhahabu, wizani kwa wizani, mfano kwa mfano, fedha kwa fedha, wizani kwa wizani, mfano kwa mfano, atakayezidisha au akataka kuzidishiwa basi hiyo itakuwa ribaa.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

700.

وَعَنْ أَبِي سَعِيدٍ، وَأَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا {أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  اِسْتَعْمَلَ رَجُلًا عَلَى خَيْبَرٍ، فَجَاءَهُ بِتَمْرٍ جَنِيبٍ، فَقَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  أَكُلُّ تَمْرِ خَيْبَرَ هَكَذَا ؟ " فَقَالَ: لَا، وَاَللَّهِ يَا رَسُولَ اَللَّهِ، إِنَّا لَنَأْخُذُ اَلصَّاعَ مِنْ هَذَا بِالصَّاعَيْنِ وَالثَّلَاثَةِ فَقَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  " لَا تَفْعَلْ، بِعِ اَلْجَمْعَ بِالدَّرَاهِمِ، ثُمَّ اِبْتَعْ بِالدَّرَاهِمِ جَنِيبًا} وَقَالَ فِي اَلْمِيزَانِ مِثْلَ ذَلِكَ. مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

وَلِمُسْلِمٍ: "وَكَذَلِكَ اَلْمِيزَانُ " 

Kutoka kwa Abuu Sa’iyd na Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) wamesema kuwa: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimtawalisha mtu Khaybar,[5] akamjia na tende nzuri. Akasema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ): “Tende zote za Khaybar ziko hivi?” Akasema: “Hapana. Wa-Allaahi Ee Rasuli wa Allaah! Hakika sisi huchukuwa pishi moja ya tende hizi kwa pishi mbili, au tatu (duni ya hizi).” Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Usifanye hivyo, uza tende duni kwa dirhamu kadhaa kisha ununue tende nzuri kwa dirhamu kadhaa.” Na katika mizani alisema kama hivyo.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

Na katika Riwaayah ya Muslim imesema: “…vile vile ilivyopimwa.”

 

 

 

701.

وَعَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اَللَّهِ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {نَهَى رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  عَنْ بَيْعِ اَلصُّبْرَةِ مِنَ اَلتَّمْرِ لا يُعْلَمُ مَكِيلُهَا  بِالْكَيْلِ اَلْمُسَمَّى مِنَ اَلتَّمْرِ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ

 Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amekataza kuuza lundo la tende lisilojulikana kipimo chake kwa kipimo cha tende kilichotajwa.”[6] [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

702.

وَعَنْ مَعْمَرِ بْنِ عَبْدِ اَللَّهِ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ: إِنِّي كُنْتُ أَسْمَعُ رَسُولَ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  يَقُولُ: {اَلطَّعَامُ بِالطَّعَامِ مِثْلاً بِمِثْلٍ " وَكَانَ طَعَامُنَا يَوْمَئِذٍ اَلشَّعِيرَ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ 

Kutoka kwa Ma’mar bin ‘Abdillaah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: Mimi nilikuwa nikimsikia Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akisema: “Chakula kwa chakula, sawa kwa sawa, wakati huo chakula chetu kilikuwa ni shayiri.”[7] [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

703.

وَعَنْ فَضَالَةَ بْنِ عُبَيْدٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ: {اِشْتَرَيْتُ يَوْمَ خَيْبَرَ قِلَادَةً بِاِثْنَيْ عَشَرَ دِينَاراً، فِيهَا ذَهَبٌ وَخَرَزٌ، فَفَصَلْتُهَا فَوَجَدْتُ فِيهَا أَكْثَرَ مِنْ اِثْنَيْ عَشَرَ دِينَاراً، فَذَكَرْتُ ذَلِكَ لِلنَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ فَقَالَ: "لَا تُبَاعُ حَتَّى تُفْصَلَ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ 

Kutoka kwa Fadhwaalah bin ‘Ubayd[8] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nilinunua mkufu Siku ya Khaybar kwa dinari kumi na mbili, ndani yake kuna dhahabu na kito, nikavitenganisha, nikapata zaidi ya dinari kumi na mbili, nikamuelezea jambo hilo Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akaniambia: “Haiuzwi mpaka ipambanuliwe.”[9] [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

704.

وَعَنْ سَمُرَةَ بْنِ جُنْدُبٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ نَهَى عَنْ بَيْعِ اَلْحَيَوَانِ بِالْحَيَوَانِ نَسِيئَةً} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ، وَصَحَّحَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ، وَابْنُ اَلْجَارُودِ 

Kutoka kwa Samurah bin Jun-dub (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ): amekataza kuuza mnyama kwa mnyama kwa kuchelewesha.”[10] [Imetolewa na Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad) na akaisahihisha At-Tirmidhiy na Ibn Al-Jaaruwd]

 

 

 

705.

 وَعَنِ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  يَقُولُ: {إِذَا تَبَايَعْتُمْ بِالْعِينَةِ، وَأَخَذْتُمْ أَذْنَابَ اَلْبَقَرِ، وَرَضِيتُمْ بِالزَّرْعِ، وَتَرَكْتُمْ اَلْجِهَادَ، سَلَّطَ اَللَّهُ عَلَيْكُمْ ذُلًّا لَا يَنْزِعُهُ حَتَّى تَرْجِعُوا إِلَى دِينِكُمْ} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ مِنْ رِوَايَةِ نَافِعٍ عَنْهُ، وَفِي إِسْنَادِهِ مَقَالٌ

وَلِأَحْمَدَ: نَحْوُهُ مِنْ رِوَايَةِ عَطَاءٍ، وَرِجَالُهُ ثِقَاتٌ وَصَحَّحَهُ اِبْنُ اَلْقَطَّانِ

 Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akisema: “Mtakapouziana kwa Al-‘Iynah,[11] mkashika mikia ya ng’ombe,[12] mkaridhia kulima na mkaacha Jihaad, Allaah Atawasalitisha udhalili ambao hatauondoa mpaka mrudi katika Dini yenu.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd kutoka katika Riwaayah ya Naafi’[13] na katika Isnaad yake kuna maelezo]

Na Ahmad amepokea kama hivyo kutoka Riwaayah ya ‘Atwaa,[14] wapokezi wake ni madhubuti, na akaisahihisha Ibn Al-Qatwaan

 

 

 

706.

وَعَنْ أَبِي أُمَامَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ عَنِ اَلنَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  قَالَ: {مَنْ شَفَعَ لِأَخِيهِ شَفَاعَةً، فَأَهْدَى لَهُ هَدِيَّةً، فَقَبِلَهَا، فَقَدْ أَتَى بَابًا عَظِيماً مِنْ أَبْوَابِ اَلرِّبَا} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَأَبُو دَاوُدَ، وَفِي إِسْنَادِهِ مَقَالٌ 

Kutoka kwa Abuu Umaamah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mwenye kumuombea nduguye uombezi akampa zawadi akaikubali, kwa hakika atakuwa ameingia mlango mkubwa miongoni mwa milango ya ribaa.”[15] [Imetolewa na Ahmad na  Abuu Daawuwd, na katika Isnaad yake kuna maelezo]

 

 

 

707.

وَعَنْ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ عَمْرِوٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {لَعَنَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  اَلرَّاشِي وَالْمُرْتَشِيَ} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ، وَاَلتِّرْمِذِيُّ وَصَحَّحَهُ

 Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amr (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amemlaani mtoa rushwa na mpokea rushwa.”[16] [Imetolewa na Abuu Daawuwd na At-Tirmidhiy akaisahihisha]

 

 

 

708.

وَعَنْ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ عَمْرٍو رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا {أَنَّ رَسُولَ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ أَمَرَهُ أَنْ يُجَهِّزَ جَيْشًا فَنَفِدَتْ اَلْإِبِلُ، فَأَمَرَهُ أَنْ يَأْخُذَ عَلَى قَلَائِصِ اَلصَّدَقَةِ. قَالَ: فَكُنْتُ آخُذُ اَلْبَعِيرَ بِالْبَعِيرَيْنِ إِلَى إِبِلِ اَلصَّدَقَةِ} رَوَاهُ اَلْحَاكِمُ وَالْبَيْهَقِيُّ، وَرِجَالُهُ ثِقَاتٌ

 Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amr (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimuamrisha kuandaa jeshi, ngamia wakamalizika, Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akamuamrisha kuchukua katika ngamia wa Zakaah. Akasema: “Nikawa nawabadilisha ngamia wawili wadogo wa Zakaah kwa ngamia mmoja mkubwa.” [Imetolewa na Al-Haakim na Al-Bayhaqiyy na wapokezi wake ni madhubuti][17]

 

 

 

709.

وَعَنْ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {نَهَى رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ عَنِ الْمُزَابَنَةِ، أَنْ يَبِيعَ ثَمَرَ حَائِطِهِ إِنْ كَانَ نَخْلاً بِتَمْرٍ كَيْلاً، وَإِنْ كَانَ كَرْماً أَنْ يَبِيعَهُ بِزَبِيبٍ كَيْلاً، وَإِنْ كَانَ زَرْعاً أَنْ يَبِيعَهُ بِكَيْلِ طَعَامٍ، نَهَى عَنْ ذَلِكَ كُلِّهُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ 

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amekataza Al-Muzaabanah kwa kuuza matunda ya shambani mwake ikiwa ni mtende kwa tende kwa kupimwa na ikiwa ni zabibu kuziuza kwa zabibu kwa kupimwa na ikiwa ni mavuno kuyauza kwa kipimo cha chakula. Ameyakataza yote hayo.”[18] [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

710.

وَعَنْ سَعْدِ بْنِ أَبِي وَقَّاصٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ: {سَمِعْتُ رَسُولَ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  سُئِلَ عَنِ اِشْتِرَاءِ اَلرُّطَبِ بِالتَّمْرِ. فَقَالَ: أَيَنْقُصُ اَلرُّطَبُ إِذَا يَبِسَ ؟ " قَالُوا: نَعَمَ. فَنَهَى عَنْ ذَلِكَ} رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ اَلْمَدِينِيِّ، وَاَلتِّرْمِذِيُّ، وَابْنُ حِبَّانَ، وَالْحَاكِمُ

 Kutoka kwa Sa’d bin Abiy Waqqaasw[19] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nilimsikia Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akiulizwa kuhusu kununua tende mbivu kwa tende kavu, akasema: ‘Je mbivu hupungua zinapokauka?” Wakasema: “Ndio.” Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akakataza kufanya hivyo.” [Imetolewa na Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad) na akaisahihisha Ibn Al-Madiyniyy, At-Tirmidhiyy, Ibn Hibbaan na Al-Haakim]

 

 

 

 711.

وَعَنِ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ نَهَى عَنْ بَيْعِ اَلْكَالِئِ بِالْكَالِئِ، يَعْنِي: اَلدَّيْنِ بِالدَّيْنِ} رَوَاهُ إِسْحَاقُ، وَالْبَزَّارُ بِإِسْنَادٍ ضَعِيفٍ 

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amekataza Al-Kaali (kuuza deni) kwa Al-Kaali (kwa deni).”[20] [Imetolewa na Ishaaq na Al-Bazzaar kwa Isnaad dhaifu]

 

 

[1] Ribaa ni haraam kwa dalili zilizo wazi kabisa katika Qur-aan. Yeyote atakayetoa mkopo kwa sharti la ribaa, na atakayepokea, mwandishi wake na shahidi wake, wote wamelaaniwa.

 

[2] ‘Ubaadah bin Asw-Swaamit bin Qays Al-Answaar, Al-Khazraj, Abul-Waliyd.

 

[3] Shayiri: nafaka inayofanana na ngano inayotumika kwa chakula. Ingawaje maeneo ya huku hutumika zaidi kutengeneza bia.

 

[4] Vitu vilivyotajwa na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) vilikuwa ni dhahabu, fedha, ngano, shayiri, tende na chumvi hakuna nyongeza au punguzo za vitu hivi vilivyotajwa katika kubadilishana navyo. Kwa mfano, mtu anataka aina nzuri ya ngano na mwingine ana aina ya chini, hairuhusiwi kubadilisha kilo 20 za ngano bora kwa kilo 30 za ngano za hali ya chini. Ikiwa mtu anataka kubadilisha aina ya ngano aliyonayo kwa nyingine, ni bora auze aliyonayo kisha kwa thamani ile anunue aina anyingine kwa fedha zile. Mabadilishano ya bidhaa hizi kwa nyongeza au nuksani hairuhusiwi kabisa. Baadhi ya Wanazuoni wamejuzisha zidisho na punguzo kwa baadhi za bidhaa zisizokuwa hizi sita, hata hivyo Maimaam wane hawakubali mabadilishano haya madamu ni aina moja ya bidhaa kwa bidhaa mfano wake.

 

[5] Anayezungumziwa hapa ni Sawaad bin Ghaziyya Al-Answaar.

 

[6] Ina maana ya kwamba bidhaa yoyote inayouzwa kwa kipimo maalumu inabidi iuzwe au kibadilishwe kwa kipimo hicho maalumu na siyo kwa kudhania kipimo au kubahatisha.

 

[7] Katika Hadiyth nyingine inatajwa kuwa chakula cha wakati ule kilikua ni ngano. Ma’mar anataka kuelezea kuwa ngano na shayiri ni sawa sawa na ichukuliwe kuwa ni aiana moja ya chakula na katika kubadilishana kisipungue au kisizidi. Hata hivyo Maswahaba wengine hawakukubaliana hivi. Kama ilivyoripotiwa na ‘Ubaadah bin Swaamit (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) ambayo imeweka wazi kuwa ngano na shayiri ni vyakula vya aina mbili tofauti.

 

[8] Huyu ni Fadhwaalah bin ‘Ubayd Al-Answaar Al-Aws, Abuu Muhammad

 

[9] Hadiyth hii inatoa ushahidi kuwa dhahabu ikichanganywa na kitu kingine isiuzwe isipokuwa iwe imetenganishwa na dhahabu safi nyinginezo, kwani ni vigumu kukadiria uzito wa dhahabu iliyochanganywa na kitu kingine.

 

[10] Inaruhusiwa kumuuza mmoja kwa thamani ya wanyama wawili lakini kumuuza myama kwa mkopo au kwa kuchelewesha kulipa hakuruhusiwi.

 

[11] Al-‘Iynah: mfano wa Al-‘Iynah ni mtu kutaka akopeshwe kiasi cha fedha. Hampi huo mkopo bali humpa kilichokuwa na thamani zaidi ya huo mkopo. Kisha ananunua tena kutoka kwake kwa thamani ya chini ambayo ni sawa na mkopo aliouomba. Kwa hali hii anamfanya mdaiwa kudaiwa zaidi, yaani fedha aliyompa mkopo na ziada yake. Hii ni ribaa; kufanya hivi ni haramu kwa sababu inaingia katika ribaa ya kuchelewesha. Na inadhihirisha kuwa mambo mawili hayo ni sababu ya kumdhalilisha Muislamu; moja ni kuiacha jihaad na ya pili ni kughushi na udanganyifu.

 

[12] “…mkashika mikia ya ng’ombe” yaani mkawa mmeshughulika na mifugo tu.

 

[13] Huyu ni Abuu ‘Abdillaah Naafi’ bin Sirjis Al-Madani, muachwa huru wa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) aliyetekwa katika vita. Ni mtu madhubuti na Mwanazuoni mkubwa katika Taabi’iyna. Amepokea Hadiyth nyingi zilizohadithiwa na Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا). Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) anasema: “Allaah Ametubariki kwa Naafi’.” Imepokewa kuwa Maalik naye amesema: “Nilikuwa sijisumbui kuchukua Hadiyth kwa yeyote maadamu nikiipata kwa Naafi’ kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ).” Al-Bukhaariy vile vile amesema: “Silsila ya upokezi iliyo sahihi zaidi ni ile kutoka kwa Maalik kutoka kwa Naafi’ kutoka kwa Ibn ‘Umar (kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ)).” Watu wengi wamepokea Hadiyth kutoka kwa Naafi’ alifariki mwaka 117 Hijriyyah.

 

[14] Uwezekano mkubwa ‘Atwaa huyu akawa ni ‘Atwaa Al-Khurasani ambaye akiitwa Abuu ‘Uthmaan ‘Atwaa bin Abiy Muslim Maysarah, muachwa huru wa Al-Muhalab bin Abiy Sufra. Aliishi Shaam na alikuwa ni mtu mwenye hadhi kubwa. Alikuwa ni mtu madhubuti na alikuwa ni mwenye kudumu katika Swalaah za usiku. Kwa bahati mbaya kumbukumbu yake haikuwa nzuri kwa hiyo alikuwa na makossa katika mapokezi yake. Alifariki mwaka 135 Hijriyyah akiwa na miaka 85.

 

[15] Ikiwa zawadi hiyo atapewa kabla ya kumuombea pamoja na kumuombea katika yasiyofaa, uharamu wake umekubaliwa na Wanazuoni wote, na inahesabiwa ni rushwa na sio zawadi. Kuunga mkono yasiyofaa na kuchukua zawadi kwa ajili yake ni katika kundi hili hili. Ikiwa mtu amesaidia katika kufanywa kwa mambo mema kisha akapokea zawadi kwa ajili hiyo inaruhusiwa ikiwa halikuwa katika ahadi au kushurutishwa.

 

[16] Anayepokea rushwa amelaaniwa. Anayelazimishwa kutoa rushwa apate haki yake Allaah atamsamehe. Lakini rushwa ikitolewa kuchepua haki ya mwingine inaelekea mtu kupata laana ya Rabb wake

 

[17] Hadiyth hii ni dalili kuwa hakuna ribaa katika wanyama.

 

[18] Hii ni kwa sababu inahusika na kuuza kitu kisichojulikana thamani yake kwa kinachojulikana thamani yake. Kwa sababu biashara hii ni haraam.

 

[19] Aliitwa Sa’d bin Maalik bin Ahiyb (au Wuhayb)  bin ‘Abd Manaaf bin Zuhrah bin Kilaab bin Murrah bin Ka’b bin Luay, na alikuwa ni wa kabila la Baniy Zuhrah. Ni wa familia ya Aaminah bint Wahb, mamake Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kwa hiyo alikuwa na udugu na ‘ammi zake Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ). Ukoo wake unakutana na Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kwa Kilaab bin Murrah. Jina lake ndilo hilo hilo hata kabla ya kusilimu. Lakabu yake ilikuwa Abuu Ishaaq. Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimbashiria Sa’d Jannah zaidi ya mara moja. Sa’d alikuwa mmoja wa watu kumi walioahidiwa Jannah na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), kumi wamo Jannah: Abuu Bakr yumo Jannah, ‘Umar yumo Jannah, ‘Uthmaan yumo Jannah, ‘Aliy, Az-Zubayr, Twalhah, ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf, Abuu ‘Ubaydah bin Al-Jarraah na Sa’d bin Abiy Waqqaasw.

 

[20] Ipo katika aina mbili: kwa mfano: 1. ‘Aliy ananunua farasi kutoka kwa Bakr kwa Dirhamu mia moja, na anatoa ahadi kulipa baada ya mwaka mmoja, baada ya mwaka mmoja, anashindwa kulipa deni. Anakuenda kwa Bakr na kumuomba kuuziwa farasi tena kwa thamani ya juu. Hii ina maana kuwa ‘Aliy analipa ribaa kwa kuongezewa muda wa ziada wa kulipa. 2. Aina ya pili inaelezwa kwa mfano ufuatao: Jaalia kuwa ‘Umar anamdai Dirhamu kumi Zayd, naye Zayd anamdai kitambaa Bakr. Bakr anamuambia Zayd: “Nitakuuzia kipande cha kitambaa ninachomdai ‘Umar kwa Dirhamu kumi unayodaiwa na ‘Umar.” Hivyo basi, ‘Umar anampa kitambaa Zayd badala ya Bakr, naye anampa dirhamu kumi Bakr badala ya Zayd. Aina hii ya mauzo inakatazwa.

 

Share