17-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Biashara: Mlango Wa Waqf
بُلُوغُ الْمَرام
Buluwgh Al-Maraam
كِتَابُ اَلْبُيُوعِ
Kitabu Cha Biashara
بَابُ اَلْوَقْفِ
17-Mlango Wa Waqf[1]
785.
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ قَالَ: {إِذَا مَاتَ اَلْإِنْسَانُ اِنْقَطَعَ عَنْهُ عَمَلُهُ إِلَّا مِنْ ثَلَاثٍ: صَدَقَةٍ جَارِيَةٍ ، أَوْ عِلْمٍ يُنْتَفَعُ بِهِ، أَوْ وَلَدٍ صَالَحٍ يَدْعُو لَهُ} رَوَاهُ مُسْلِم
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mwanadamu akifa amali yake hukatika ila kwa mambo matatu: Swadaqah inayoendelea, na ilmu inayonufaisha, au mtoto mwema anayemuombea du’aa.” [Imetolewa na Muslim]
786.
وَعَنْ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {أَصَابَ عُمَرُ أَرْضًا بِخَيْبَرَ ، فَأَتَى اَلنَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ يَسْتَأْمِرُهُ فِيهَا ، فَقَالَ: يَا رَسُولَ اَللَّهِ ! إِنِّي أَصَبْتُ أَرْضًا بِخَيْبَرَ لَمْ أُصِبْ مَالًا قَطُّ هُوَ أَنْفَسُ عِنْدِي مِنْهُ قَالَ: " إِنْ شِئْتَ حَبَسْتَ أَصْلَهَا ، وَتَصَدَّقْتَ بِهَا " . قَالَ: فَتَصَدَّقَ بِهَا عُمَرُ ، غَيْرَ أَنَّهُ لَا يُبَاعُ أَصْلُهَا، وَلَا يُورَثُ ، وَلَا يُوهَبُ ، فَتَصَدَّقَ بِهَا فِي اَلْفُقَرَاءِ ، وَفِي اَلْقُرْبَى ، وَفِي اَلرِّقَابِ ، وَفِي سَبِيلِ اَللَّهِ ، وَابْنِ اَلسَّبِيلِ ، وَالضَّيْفِ ، لَا جُنَاحَ عَلَى مَنْ وَلِيَهَا أَنْ يَأْكُلَ مِنْهَا بِالْمَعْرُوفِ ، وَيُطْعِمَ صَدِيقاً} غَيْرَ مُتَمَوِّلٍ مَالًا مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ ، وَاللَّفْظُ لِمُسْلِمٍ .
وَفِي رِوَايَةٍ لِلْبُخَارِيِّ: {تَصَدَّقْ بِأَصْلِهِ ، لَا يُبَاعُ وَلَا يُوهَبُ ، وَلَكِنْ يُنْفَقُ ثَمَرُهُ}
Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “’Umar alipata ardhi huko Khaybar. Akamuendea Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akimuomba amri na ushauri katika ardhi hiyo. Akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Nimepata ardhi Khaybar, sijawahi kupata mali iliyo nzuri zaidi kwangu kuliko hiyo (utaniamuru nifanyeje?). Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Ukipenda, uizuie waqf asili yake na uitoe swadaqah yake.” ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) akaitoa swadaqah isipokuwa asili yake haiuzwi wala hairithiwi wala haitolewi hiba. ‘Umar akalitoa swadaqah kwa mafukara, jamaa zake wa karibu, watumwa na katika Njia ya Allaah, msafiri na mgeni. Hapana ubaya kwa anayelisimamia kula ndani yake kwa wema na amlishe rafiki ila asilimbikize mali kwa ajili yake.” [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Muslim]
Katika Riwaayah nyingine ya Al-Bukhaariy imesema: “Akatoa swadaqah asili yake, lakini kwa sharti isiuzwe[2] wala kutolewa kama hiba ila matunda yake hutolewa (kugawiwa watu).”
787.
وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ: {بَعَثَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ عُمَرَ عَلَى اَلصَّدَقَةِ . .} اَلْحَدِيثَ ، وَفِيهِ :{وَأَمَّا خَالِدٌ فَقَدْ اِحْتَبَسَ أَدْرَاعَهُ وَأَعْتَادَهُ فِي سَبِيلِ اَللَّهِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْه
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimtuma ‘Umar kuchukua Zakaah…” mpaka mwisho wa Hadiyth inasesema: “(Nabiy akasema): …ama Khaalid[3] ametoa Waqf deraya na zana zake za vita katika njia ya Allaah…”[4] [Al-Bukhaariy, Muslim]
[1] Waqf ni ile hali ya kuweka mali au feda na kuizuia kwa ajili ya kutumika kwa maslahi ya Ummah, na kubakia asili yake katika uangalizi na siyo kuuzwa, kurithi au kutoa zawadi. Huku ni kama vile mtu kutoa nyumba au sehemu yake kulipia mahitaji ya Msikiti.
[2] Waqf hairuhusiwi kuuzwa. Mdhamini wa Waqf anaweza kuchukua kiasi kidogo cha kuikimu familia yake.
[3] Huyu ni Abuu Sulaymaan Khaalid bin Al-Waliyd bin Al-Mughiyrah Al-Makhzuwm Al-Qurayshi. Mama yake akiitwa Asmaa alikuwa Lubaabah mdogo mtoto wa Al-Haarith na dada wa Ummul-Fadhwl. Khaalid alisilimu mwaka wa 8 Hijriyyah kabla ya ufunguzi wa Makkah. Inasemekana vile vile kuwa alisilimu mwaka wa 5 au wa 6 Hijriyyah. Alishiriki katika ufunguzi wa Makkah katika vita vya Hunayn na Tabuwk. Panga tisa zilikatika mkononi mwake alipokuwa akipigana katika vita vya Mu’ta, wakati huo ndipo Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipompa jina la ‘Upanga wa Allaah’. Abuu Bakr alimtuma kupigana katika vita vya Ar-Ridda (walioritadi), na baada ya hapo akavamia Fursi. Alitumwa Shaam na akateka ardhi nyingi huko na akaendelea kubaki huko hadi ukhalifa wa ‘Umar akiwa kamanda mkuu wa majeshi ya Kiislam Shaam, ‘Umar bin Al-Khatwaab alimuzulu Khaalid. Baada ya hapo Khaalid alikuwa ni muangalizi wa kujitolea wa mji wa Hims hadi alipofariki mwaka wa 21 Hijriyyah, alizikwa katika kijiji kimoja umbali wa maili moja nje ya mji wa Hims.
[4] ‘Umar alidhania kuwa Khaalid alibaki na deraya kwa ajili ya kufanyia biashara. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimjulisha ‘Umar kuwa Khaalid alizitoa deraya kama zile kama Waqf kwa njia ya Allaah.