18-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Biashara: Mlango Wa Kutoa Hiba

 

 

بُلُوغُ الْمَرام

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتَابُ اَلْبُيُوعِ

Kitabu Cha Biashara

 

بَابُ اَلْهِبَةِ

18-Mlango Wa Kutoa Hiba[1]

 

 

 

 

 

788.

عَنْ اَلنُّعْمَانِ بْنِ بَشِيرٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا أَنَّ أَبَاهُ أَتَى بِهِ رَسُولَ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  فَقَالَ: {إِنِّي نَحَلْتُ اِبْنِي هَذَا غُلَامًا كَانَ لِي، فَقَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  " أَكُلُّ وَلَدِكَ نَحَلْتَهُ مِثْلَ هَذَا"  ؟. فَقَالَ: لَا . فَقَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  " فَارْجِعْهُ" }

وَفِي لَفْظٍ: {فَانْطَلَقَ أَبِي إِلَى اَلنَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  لِيُشْهِدَهُ عَلَى صَدَقَتِي. فَقَالَ: " أَفَعَلْتَ هَذَا بِوَلَدِكَ كُلِّهِمْ" ؟. قَالَ: لَا. قَالَ: " اِتَّقُوا اَللَّهَ، وَاعْدِلُوا بَيْنَ أَوْلَادِكُمْ " فَرَجَعَ أَبِي، فَرَدَّ تِلْكَ اَلصَّدَقَةَ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

وَفِي رِوَايَةٍ لِمُسْلِمٍ قَالَ: {فَأَشْهِدْ عَلَى هَذَا غَيْرِي" ثُمَّ قَالَ: " أَيَسُرُّكَ أَنْ يَكُونُوا لَكَ فِي اَلْبِرِّ سَوَاءً" ؟ قَالَ: بَلَى . قَالَ: " فَلَا إِذًا} 

 Kutoka kwa An-Nu’maan bin Bashiyr (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa baba yake alienda naye kwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Mimi nimempa zawadi mtoto wangu huyu mtumwa aliyekuwa wangu. Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: Watoto wako wote umewazawadia kama hivyo? Akasema: Hapana. Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: Irudishe.”

Katika tamshi nyingine inasema: “Baba yangu akaenda kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) ili amshuhudishe swadaqah yangu. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: “Umefanya hivi kwa wanao wote? Akasema hapana. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: Mcheni Allaah na mfanye uadilifu baina ya watoto wenu.[2] Baba yangu akarejea na akairudisha swadaqah hiyo.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

Na katika Riwaayah nyingine ya Muslim: “Mshuhudishe jambo hili asiyekuwa mimi. Kisha akasema: Unapendezewa watoto wako wote wakufanyie wema kwa usawa? Akasema: Ndiyo. Akasema: Basi usifanye hivyo.”

 

 

 

789.

وَعَنْ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: قَالَ اَلنَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ {اَلْعَائِدُ فِي هِبَتِهِ كَالْكَلْبِ يَقِيءُ، ثُمَّ يَعُودُ فِي قَيْئِهِ"} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

وَفِي رِوَايَةٍ لِلْبُخَارِيِّ:{لَيْسَ لَنَا مَثَلُ اَلسَّوْءِ، اَلَّذِي يَعُودُ فِي هِبَتِهِ كَالْكَلْبِ يَرْجِعُ فِي قَيْئِهِ}  

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Anayeirudia hiba yake[3] ni kama mbwa anayetapika na kuyarudia matapishi yake.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

Na katika Riwaayah ya Al-Bukhaariy inasema: “Sisi hatuna mfano mbaya, ambaye anayerudia hiba yake ni kama mbwa, anatapika kisha anarudia matapishi yake.”[4]

 

 

 

790.

وَعَنْ اِبْنِ عُمَرَ، وَابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمْ، عَنْ اَلنَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  قَالَ: {لَا يَحِلُّ لِرَجُلٍ مُسْلِمٍ أَنْ يُعْطِيَ اَلْعَطِيَّةَ، ثُمَّ يَرْجِعَ فِيهَا، إِلَّا اَلْوَالِدُ فِيمَا يُعْطِي وَلَدَهُ"} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَالْأَرْبَعَةُ، وَصَحَّحَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ، وَابْنُ حِبَّانَ، وَالْحَاكِم

Kutoka kwa Ibn ‘Umar na Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمْ) wamesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Si halaal kwa Muislamu kutoa zawadi kisha akairudia isipokuwa baba katika alichompa mtoto wake.”[5] [Imetolewa na Ahmad na Al-Arba’ah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah) na akaisahihisha At-Tirmidhiy, Ibn Hibbaan na Al-Haakim]

 

 

 

791.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  يَقْبَلُ اَلْهَدِيَّةَ، وَيُثِيبُ عَلَيْهَا} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيّ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema kuwa: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akikubali zawadi, na akiilipa.”[6] [Imetolewa na Al-Bukhaariy]

 

 

 

792.

وَعَنْ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {وَهَبَ رَجُلٌ لِرَسُولِ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  نَاقَةً، فَأَثَابَهُ عَلَيْهَا، فَقَالَ: " رَضِيتَ" ؟ قَالَ: لَا. فَزَادَهُ، فَقَالَ: "رَضِيتَ" ؟ قَالَ: لَا. فَزَادَهُ. قَالَ: "رَضِيتَ" ؟ قَالَ: نَعَمْ} رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّان

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Mtu mmoja alimpa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) hiba ngamia, Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akamlipa akasema: Umeridhika? Yule akasema: Hapana. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akamzidishia na akasema: Umeridhika? Akasema Hapana. Akamzidishia kisha akasema: Umeridhika? Akasema: Ndiyo.” [Imetolewa na Ahmad na akaisahihisha Ibn Hibbaan]

 

 

 

793.

وَعَنْ جَابِرٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ { اَلْعُمْرَى لِمَنْ وُهِبَتْ لَهُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

وَلِمُسْلِمٍ: {أَمْسِكُوا عَلَيْكُمْ أَمْوَالَكُمْ وَلَا تُفْسِدُوهَا ، فَإِنَّهُ مَنْ أَعْمَرَ عُمْرَى فَهِيَ لِلَّذِي أُعْمِرَهَا حَياً وَمَيِّتًا، وَلِعَقِبِهِ}

وَفِي لَفْظٍ: {إِنَّمَا اَلْعُمْرَى اَلَّتِي أَجَازَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  أَنْ يَقُولَ: هِيَ لَكَ وَلِعَقِبِكَ، فَأَمَّا إِذَا قَالَ: هِيَ لَكَ مَا عِشْتَ، فَإِنَّهَا تَرْجِعُ إِلَى صَاحِبِهَا}

وَلِأَبِي دَاوُدَ وَالنَّسَائِيِّ:{لَا تُرْقِبُوا ، وَلَا تُعْمِرُوا، فَمَنْ أُرْقِبَ شَيْئًا أَوْ أُعْمِرَ شَيْئًا فَهُوَ لِوَرَثَتِهِ} 

 Kutoka kwa Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Kuzawadia ‘Umraa[7] ni kwa aliyepewa nyumba hiyo.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

Na katika Riwaayah ya Muslim inasema: “Zuieni mali zenu wala msiharibu,[8] hakika anayetoa ‘Umraa basi ikiwa ni ya yule aliyezawadiwa akiwa hai na akifariki ni ya kizazi chake.”

Katika tamshi linguine inasema: “Hakika ‘Umraa aliyoijuzisha Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) ni kusema: Hiba hii ni yako na vizazi vyako. Ama akisema: Hiba hii ni yako muda wa maisha yako. Basi hiba hiyo humrudia mwenyewe (aliyeitoa).”

Na katika Riwaayah ya Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy imesema: “Msitoe mali yenu kwa Ruqbaa wala ‘Umraa, atakayepewa chochote kwa njia ya Ruqbaa[9] au ‘Umraa basi ni cha warithi wake.”

 

 

 

794.

وَعَنْ عُمَرَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ: {حَمَلْتُ عَلَى فَرَسٍ فِي سَبِيلِ اَللَّهِ، فَأَضَاعَهُ صَاحِبُهُ، فَظَنَنْتُ أَنَّهُ بَائِعُهُ بِرُخْصٍ، فَسَأَلْتُ رَسُولَ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ عَنْ ذَلِكَ. فَقَالَ: " لَا تَبْتَعْهُ ، وَإِنْ أَعْطَاكَهُ بِدِرْهَمٍ …} اَلْحَدِيثَ. مُتَّفَقٌ عَلَيْه

Kutoka kwa ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nilitoa hiba farasi katika njia ya Allaah, mwenyewe hakujali (niliyempa). Nikadhani kuwa mwenyewe atamuuza kwa bei rahisi (kwa kuwa amedhoofika). Nikamuuliza Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kuhusu jambo hilo akasema: Usimnunue hata akikupa kwa dirhamu moja….” Mpaka mwisho wa Hadiyth[10] [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

795.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ عَنِ النَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ قَالَ: {تَهَادُوْا تَحَابُّوا} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيُّ فِي " اَلْأَدَبِ اَلْمُفْرَدِ " وَأَبُو يَعْلَى بِإِسْنَادٍ حَسَن

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Peaneni zawadi[11] mutapendana.” [Imetolewa na Al-Bukhaariy katika ‘Al-Adab Al-Mufrad’ na Abuu Ya’laa ameipokea kwa Isnaad Hasan]

 

 

 

796.

وَعَنْ أَنَسٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ {تَهَادَوْا، فَإِنَّ اَلْهَدِيَّةَ تَسُلُّ اَلسَّخِيمَةَ} رَوَاهُ اَلْبَزَّارُ بِإِسْنَادٍ ضَعِيفٍ 

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Peaneni zawadi, kwa hakika zawadi huondoa chuki.” [Imetolewa na Al-Bazzaar kwa Isnaad dhaifu]

 

 

 

797.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ {يَا نِسَاءَ اَلْمُسْلِمَاتِ! لَا تَحْقِرَنَّ جَارَةٌ لِجَارَتِهَا وَلَوْ فِرْسِنَ شَاةٍ} مُتَّفَقٌ عَلَيْه

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Enyi wanawake Waislamu! Jirani asidharau kamwe kumzawadia jirani yake japo kwa kwato ya mbuzi.”[12] [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

798.

وَعَنْ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا، عَنْ اَلنَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ قَالَ: {مَنْ وَهَبَ هِبَةً، فَهُوَ أَحَقُّ بِهَا، مَا لَمْ يُثَبْ عَلَيْهَا} رَوَاهُ اَلْحَاكِمُ وَصَحَّحَهُ، وَالْمَحْفُوظُ مِنْ رِوَايَةِ اِبْنِ عُمَرَ، عَنْ عُمَرَ قَوْلُه

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mwenye kutoa hiba yeye ana haki zaidi madamu hajalipwa.”[13] [Imetolewa na Al-Haakim na akaisahihisha. Hata hivyo kauli yenye nguvu ni kuwa ni mapokezi ya Ibn ‘Umar kutoka kwa ‘Umar]

 

 


[1] Hiba ni zawadi kwa ajili ya kupata radhi za Allaah. Waqfu ni milki ya Ummah. ‘Umraa ni mtu kumuachia nyumba yake mtu kama zawadi muda wa umri wake kisha inarudi kwa mwenyewe. Ruqbaa ni nyumba ambayo anapewa zawadi mtu kwa sharti kama mmoja wao atakufa basi nyumba ile itabaki kwa aliye hai katika wao.

 

[2] Kwa mujibu wa Wanazuoni ni kwamba uadilifu na usawa miongoni mwa watoto ni jambo linalopendeza. Ama kwa mujibu wa Imaam Al-Bukhaariy na Muslim jambo hili ni la wajibu.

 

[3] Ni makubaliano ya Wanazuoni kuwa baba anaweza kuchukua kitu kutoka kwa mwanae na akamrudishia kama hiba (zawadi); lakini jambo hilo hilo haruhusiwi kulifanya kwa ndugu na jamaa zake wengine na akifanya hivyo itakuwa amefanya jambo la haraam.

 

[4] Hadiyth hii ni dalili ya uharamu wa mtu kuirudia hiba yake.

 

[5] Hii ina maana kuwa ni baba peke yake akimpa zawadi mtoto wake, anaweza kuirudia tena na kufanya hivyo hakufanya jambo la haraam. Kwa Wanazuoni wengi mama vile vile anaweza kufanya hivyo katika hiba.

 

[6] Hii ina maana kupokea zawadi kisha kuitoa zawadi hiyo kwa mwingine ni Sunnah.

 

[7] ‘Umraa ni kutoa nyumba kumpa mtu kukaa nayo kwa maisha yake kunaitwa ‘Umraa, ipo katika hali tatu i- Ni ile hali ya kutoa moja kwa moja, ii-Kutoa kwa muda wa umri wa mtu, iii-Kutoa kwa masharti (kwamba irudi kwa mwenyewe baada ya kifo cha aliyepewa). Tulichomaanisha hapa ni ile hali ya mwanzo na ya mwisho.

 

[8] Wakati ule watu walifikiri kuwa ‘Umraa ni mkopo anayepewa mtu kwa muda maalumu, na baada ya muda mwenye mali huichukuwa mali yake. Hata hivyo, Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliweka jambo hili wazi kwa kusema anayeazima kitu chenyewe kinakuwa ni milki yake. Mtoaji anaweza kuwa na niyyah yoyote anapotoa zawadi, hata hivyo jambo hilo huwa haliangaliwi. Kwa hivyo basi inapendekezwa kwa mtu kabla hajatoa zawadi ya ‘Umraa afikirie vizuri kabla ya kujuta kwake.

 

[9] Ruqbaa ina maana ya mtu kumpa mtu mwingine nyumba yake (au anachomiliki) ili aishi humo daima, atabaki na nyumba. Hata hivyo, ikiwa aliyeazimwa akifa kabla nyumba itarudi kwa mwenyewe (mmiliki wa asili). Hii inaitwa Ruqbaa kwani kila mmoja anasubiri kifo cha mwenzake.

 

[10] Hadithi yenyewe inasema hivi: “’Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: Nilimtoa hiba farasi katika njia ya Allaah (nikampa mmoja katika wapiganaji Jihaadi). Yule aliyekuwa naye hakumsimamia vema (yule farasi akadhoofika). Nikataka kumnunua. Nikadhani kuwa mwenyewe atamuuza kwa bei rahisi (kwa kuwa amedhoofika). Nikamuuliza Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: Usimnunue wala usirudie swadaqah yako hata akikupa kwa dirhamu moja. Kwani anayeirudia hiba yake ni kama anaeyarudia matapishi yake.”

 

[11] Hii ina maana jambo la kupeleka au kutoa zawadi linapendeza kishariy’ah. Wapokezi wote katika mlolongo wa Hadiyth hii wana ila. Hata hivyo, wengine wanaungwa na wengine na ndio maana Hadiyth ikaonekana kuwa ni nzuri (Hasan). Angalia kitabu Irwaa Al-Ghaliyl cha Sheikh Al-Albaniy (6/44) namba (16010.

 

[12] Mfano huu unatufundisha mambo ya msingi kuhusu utoaji wa zawadi. Suala la zawadi halijali ukubwa au thamani ya zawadi bali chochote kile. Na atakayepokea aheshimu matakwa ya mtoaji yaani apokee kwa niyyah njema na moyo msafi.

 

[13] Hadiyth hii imezungumzia nukta mbili muhimu: i-Zawadi itakayotolewa ifidiwe, ii-Mtoaji anaweza kubadilisha mawazo na kuirejesha hiba yake. Hata hivyo, mapokezi haya ni dhaifu.

Share