13-Zawadi Kwa Wanandoa: Karamu ya Harusi (Walima)

 

 

Zawadi Kwa Wanandoa

 

13- Karamu ya Harusi (Walima)

 

الوليمة

 

 

 

 

Walima ni Sunnah iliyokokotezwa kwa neno lake Mtume (Swalla Allaah 'alayhi wa sallam)  kwa A'bdur-Rahmaan bin 'Awf:

 

أولم ولو بشاة 

“Tufanyie Karamu walau kwa mbuzi mmoja.” (Ahmad)

 

Na Mtume (Swalla Allaah 'alayhi wa sallam)  amesema vile vile:

                  

إنه لا بدّ للعرس من وليمة

“Hakika katika harusi hakuna budi kufanywa karamu.”(Ahmad)

 

Mtume (Swalla Allaah 'alayhi wa sallam) aliwafanyia karamu baadhi ya wake zake kwa vibaba (Mudain) viwili vya shairi.” (Al-Bukhaariy na Ahmad)

 

Ama tofauti ya aina ya chakula kinachotumika katika karamu hutegemea desturi za watu na ada zao na uwezo wao wa kifedha. Ni wajibu wa mwenye kualikwa katika karamu kuitikia mwito huo ili kuingiza furaha kwa wale waliomwalika. Mtume (Swalla Allaah 'alayhi wa sallam) amesema:

 

إذا دعي أحدكم إلى وليمة فليأتها 

“Anapoalikwa mmoja wenu katika karamu na ahudhurie.”  (Al-Bukhaariy na Muslim)

 

Na katika hadithi nyingine Mtume juu yake sala na salamu anasema:

 

من ترك الدّعوة فقد عصى الله ورسوله

“Atakayeacha kuitika mwito basi atakua amemuasi Allah na Mtume wake.”(Al-Bukhaariy na Muslim)

 

Na Mtume (Swalla Allaah 'alayhi wa sallam)  amesema vilevile:  

“Lau ningealikwa kwenda kula kongoro basi ningelikwenda, na lau ningalipewa zawadi ya mkono ningalipokea.” (Al-Bukhaariy)

 

Inapendeza wale ambao wataalikwa kwenye karamu wawe ni mafakiri na pasiwepo katika karamu hiyo Munkaraat (ubadhirifu na Israfu), Mtume wa Allaah juu yake Swalah na amani anasema:

 

شرّ الطّعام طعام الوليمة يدعى لها الأغنياء ويترك الفقراء

“Chakula kibaya zaidi ni karamu ambayo wanaalikwa matajiri na kuachwa mafakiri.” (Al-Bukhaariy na Muslim)

 

Na mwaliko huo unapendeza zaidi uitikiwe na waja wema wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  kwa neno Lake Mtume (Swalla Allaah 'alayhi wa sallam) :

 

لا تصاحب إلاّ مؤمتا ولا يأكل طعامك إلاّ تقيّ  

“Usisuhubiane ila na muumini tu, na asile chakula chako ila Mchaji Allaah.” (Abu Daawuwd na At-Tirmidhiy)

 

Matajiri wanahamasihwa washiriki katika kutengeneza chakula cha mafakiri, kwani amesema Anas (Radhiya Allaahu 'anhu)  katika kisa cha Ndoa ya Mtume (Swalla Allaah 'alayhi wa sallam)  kwa bibi Swafiyah, hata ilipofika njiani Bibi Sulaym alitayarisha chakula na akakipeleka usiku, na ilipofika asubuhi yake Mtume (Swalla Allaah 'alayhi wa sallam)  akasema: “Atakayekua na kitu basi aje nacho.” Anas anasema: “Habari zikaenea vitu vikawa vingi! Ikawa kila mmoja anakuja na kitu, wengine walileta samli wengine tende wakatengeneza hays (aina ya chakula kama ugali wa tende uliochanganywa na samli) ikawa wanakula kutokana na chakula kile na wanakunywa katika zile hodhi waliokinga katika maji ya mvua, na hiyo ndio iliyokuwa karamu ya Mtume (Swalla Allaah 'alayhi wa sallam) .” (Al-Bukhaariy na Muslim)

 

Na du'aa inayosomwa kwa Bwana harusi wakati mtu anapohudhuria karamu ni:

 

بارك الله لك, وبارك عليك, وجمع بينكما في خير

“Allaah Akubariki na Akubarikie mke huyo na Awakusanye pamoja katika kheri.” (Abu Daawuwd)

 

Mtume juu yake sala na amani amekataza kupeana pongezi za kijahilia. Hasan bin 'Aqiyl bin Abi Twalib alioa kisha watu wakaingia (kumpongeza) wakisema: upate utajiri na watoto, Hasan (Radhiya Allaahu 'anhu)  akasema msiseme hivyo, kwani Mtume (Swalla Allaah 'alayhi wa sallam)  amekataza hilo. (Ibn Maajah, Ad-Daarimy na Ahmad)

 

Inapendeza kuwaombea dua wanandoa wawili kwa kusema:

على خير والبركة وعلى خير طائر

“Katika kheri na baraka na katika kheri ya kuwa na bahati nzuri na hadhi yake.” (Al-Bukhaariy na Muslim)

 

اللهّم بارك فيهما, وبارك لهما في بنائهما  

“Ee, Allaah! Wabarikie kwa hayo, na uwabarikie wote wawili katika mjengo wao.” (Atw-Twabaraaniy)

 

 

 

Share