01-Du'aa Za Ruqyah: Kuomba Kuwezeshwa Kutenda Kheri, Kuacha Munkari, Kuwapenda Masikini Kupata Maghfirah na Rahmah, Kuepushwa na Fitnah, Na Kulipata Penzi La Allaah
Du’aa Za Ruqyah (Kinga) Faida Na Sharh Zake
01-Kuomba Kuwezeshwa Kutenda Kheri, Kuacha Munkari, Kuwapenda Masikini Kupata Maghfirah na Rahmah, Kuepushwa na Fitnah, Na Kulipata Penzi La Allaah
Allaah (Tabaaraka wa Ta’alaa) Alimwamuru Kipenzi Chake Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakati alipomwona usingizini, - na njozi ya Manabii ni kweli – aseme anaposwali:
((اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ فِعْلَ الْخَيْرَاتِ، وَتَرْكَ الْمُنْكَرَاتِ، وَحُبَّ الْمَسَاكِينِ، وَأَنْ تَغْفِرَ لِي، وَتَرْحَمَنِي، وَإِذَا أَرَدْتَ فِتْنَةَ قَوْمٍ فَتَوَفَّنِي غَيْرَ مَفْتُونٍ، وَأَسْأَلُكَ حُبَّكَ، وَحُبَّ مَنْ يُحِبُّكَ، وَحُبَّ عَمَلٍ يُقَرِّبُنِي إِلَى حُبِّكَ))
((Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba kufanya mema yote, kuacha munkari zote, na kuwapenda masikini, na Unighufirie na Unirehemu, na Unapotaka kuwatia watu majaribuni (fitnah), basi Nifishe mimi bila kujaribiwa. Na ninakuomba Penzi Lako na penzi la yule anayekupenda, na kuipenda ‘amali itakayonikurubisha kwenye Penzi Lako)). [Imekharijiwa na Ahmad kwa tamko lake 36/423 nambari 22109 na At Tirmidhiy].
Kisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia Maswahaba:
((إِنَّهَا حَقٌّ فَادْرُسُوهَا وَتَعَلَّمُوهَا))
((Hakika njozi hii ni kweli, basi idurusuni na jifundisheni)). [Ziada hii iko kwa Ahmad na At Tirmidhiy. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Swahiyh At Tirmidhiy kwa nambari 2582].
Faida Na Sharh:
Hili ni agizo la Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwetu kuyadurusu yaliyomo ndani yake, kujifunza maana zake na makusudio yake kutokana na umahususi wake.
Du’aa hii bila shaka ni katika du’aa jumuishi zaidi, kamili zaidi na zenye shani kubwa zaidi kutokana na kukusanya kwake maombi kwa Allaah (‘Azza wa Jalla) Ampe mtu tawfiyq ya kuyafanya mambo yote mema yenye kupendeza Kwake, na kumwomba Amkinge na munkari zote na mabaya yote, pamoja na fitna na misukosuko katika Dini, maisha ya hapa duniani na marejeo ya kesho Aakhirah.
Hivyo inabidi Muislamu akithirishe kuomba du’aa hii, ajitahidi kuyajua makusudio yake na maana zake, na kuyafanyia kazi madhumuni yake. Atakayefanya hivyo, basi bila shaka atapata furaha ya hapa duniani na kesho Aakhirah.
Katika du’aa hii, limetajwa suala la kuwapenda masikini. Kuwapenda masikini kunaingia ndani ya wigo wa kufanya mema ya kheri, kwa kuwa watu hawa hawana chochote hapa duniani cha kuwafanya watu wawapende. Na anayewapenda, anakuwa hafanyi hivyo ila kwa ajili ya Allaah (‘Azza wa Jalla), na hilo ni katika ukamilisho wa iymaan ya mtu. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
((من أحب للَّه، وأبغض للَّه، وأعطى للَّه، ومنع للَّه، فقد استكمل الإيمان))
((Mwenye kupenda kwa ajili ya Allaah, akachukia kwa ajili ya Allaah, akatoa kwa ajili ya Allaah na akazuia kwa ajili ya Allaah, basi ameikamilisha vilivyo iymaan yake)). [Hadiyth Marfu’u. Imepokelewa na Abuu Umaamah].
Pia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimuusia Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akimwambia:
((يا عائشة أحبِّي المساكين، وقرّبيهم، فإن اللَّه يقربك يوم القيامة))
((Ee ‘Aaishah! Wapende masikini na wakurubishe, Allaah Atakukurubisha Siku ya Qiyaamah)). [Imepokelewa na Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu)].
Ama ombi la kughufiriwa na kurehemewa, bila shaka maghfirah na rahmah, viwili hivi vinakusanya kheri zote za Aakhirah. Kwa maghfirah, mja atasalimika na adhabu na shari zote, na kwa rahmah, mja ataingia Peponi. Kuingia Peponi na neema zote zilizoko huko, kunatokana na Rahmah za Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa). Hakuna atakayeingia Peponi kwa amali zake, bali ataingia kutokana na Rahmah za Allaah kama alivyoashiria hilo Rasuli (Swalla Allaahu Alayhi wa Sallam) katika Hadiyth nyingine.
Rahmah ya Allaah (‘Azza wa Jalla) ni bora kuliko vyote vya duniani. Allaah Anatuambia:
وَرَحْمَتُ رَبِّكَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُون
Na Rahmah ya Rabb wako ni bora kuliko wanayoyakusanya. [Az- Zukhruf (43:32)].
Aidha, kutokana na umuhimu wa maghfirah na rahmah, Allaah (‘Azza wa Jalla) Amemwamuru Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na sisi aombe maghfirah na rahmah. Anasema:
وَقُل رَّبِّ اغْفِرْ وَارْحَمْ وَأَنتَ خَيْرُ الرَّاحِمِين
Na sema: “Rabb wangu! Ghufuria na Rehemu, Nawe ni Mbora wa wenye kurehemu. [Al-Muuminuwn 23:118)]
Kisha du’aa hii Aliyoagizwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inagusia suala la fitnah. Inasema: “Ukitaka kuwaingiza watu kwenye fitnah na adhabu katika Dini, au adhabu ya kidunia kati ya misukosuko na mengineyo, basi Nifishe Unirejeshe Kwako kabla ya kutokea hayo.”
Makusudio hapa ni kusalimika na fitnah katika maisha yote ya Muislamu, na kusalimika na shari zote kabla hazijamfikia, na kufa akiwa salama kabla ya kufikiwa na fitnah.
Na hili linadulisha kuwa inajuzu kuomba kifo kwa kuhofia fitnah katika Dini.
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
((اثْنَتَانِ يَكْرَهُهُمَا ابْنُ آدَمَ: الْمَوْتُ، وَالْمَوْتُ خَيْرٌ لِلْمُؤْمِنِ مِنْ الْفِتْنَةِ، وَيَكْرَهُ قِلَّةَ الْمَالِ وَقِلَّةُ الْمَالِ أَقَلُّ لِلْحِسَاب))
((Mawili anayachukia mwana Aadam: Mauti, na mauti ni kheri zaidi kwa Muumini kuliko fitnah. Na anachukia uchache wa mali, na uchache wa mali ni nafuu zaidi kwa hisabu)). [Imepokelewa na Mahmuwd bin Lubayd (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) na kusimuliwa na Ahmad].
Ama penzi, hili bila shaka ndio ombi la juu zaidi na matarajio ghali zaidi kuliko yote. Mja kupendwa na Rabb wake, na yeye kuwa hakuna akipendaye zaidi kuliko Rabb wake na Rasuli Wake, bila shaka hakuna jingine zaidi ya hilo.
Mwenye kulipata Penzi hilo, amali zake zote, maneno yake yote, na vitendo vyake vyote vinakuwa vikielekezwa kwa Allaah (‘Azza wa Jalla) tu. Muumini hupata qabuli kwavyo ardhini na mbinguni kama ilivyo kwenye Swahiyh.