02-Du'aa Za Ruqyah: Kuomba Kinga Dhidi Ya Tabia Za Kuchukiza, Matendo, Hawaa Na Magonjwa Yote Mabaya
Du’aa Za Ruqyah (Kinga) Faida Na Sharh Zake
02-Kuomba Kinga Dhidi Ya Tabia Za Kuchukiza, Matendo,
Hawaa Na Magonjwa Yote Mabaya
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anajilinda kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) akisema:
((اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ مُنْكَرَاتِ الْأَخْلَاقِ، وَالْأَعْمَالِ، وَالْأَهْوَاءِ والأدواء))
((Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako na yenye kuchukiza katika tabia, matendo, hawaa na magonjwa)). [At Tirmidhiy 3591]
Faida Na Sharh:
Katika du’aa hii, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anajilinda kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kutokana na tabia zote zinazochukiza, matendo yote yanayochukiza, hawaa na matamanio yote yanayochukiza na magonjwa yote mabaya.
Tabia mbaya zinazochukiza ni kama hikdi, hasadi, kibri, ubakhili, na woga. Pia ulimi mchafu wa kutukana, wa kusingizia watu, kufitinisha na kusema uongo. Tabia zote hizi mbaya ni kiini cha sababu ya shari zote katika jamii, na ndiyo sababu kuu ya kuiweka mbali kheri na jamii. Na tabia zote hizi hazijengi jamii njema, bali zinazidi kuibomoa na kuisambaratisha.
Ama matendo, ni kama zinaa, mauaji, kunywa pombe, wizi, rushwa, ufujaji mali, dhulma, ufisadi, kudhalilisha watu, uonevu, unyanyasaji, ubaguzi, unyanyapaa na kadhalika. Haya yote huleta madhara makubwa ndani ya jamii kama tunavyoshuhudia na kujionea wenyewe haya ndani ya jamii zetu.
Ama matamanio na hawaa, haya ni matamanio ya kinafsi ya kupondokea kwenye anasa batili na za haraam, kuifumbia macho haki, kufuata kibubusa mielekeo batili yenye hoja zisizo na mashiko, kujisahau na starehe za dunia na kuisahau aakhirah, kujisahaulisha kifo na yanayofuatia baada ya hapo na kadhalika.
Ama magonjwa, haya ni yale yote yenye kuwakimbiza watu wasimkurubie mgonjwa kama ukoma, ndui, na mbalanga ambayo hugeuza umbo la mtu. Pia magonjwa yote yenye kuambukiza na magonjwa yenye kiwango kidogo cha kupona kama ukimwi, saratani, pumu na kadhalika. Magonjwa haya humweka mgonjwa katika hali ngumu ya kisaikolojia pamoja na jamaa zake wa karibu mbali na gharama kubwa za matibabu yake.
Katika du’aa nyingine kuhusiana na magonjwa, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anajilinda akisema:
((اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنَ الْبَرَصِ، وَالْجُنُونِ، وَالْجُذَامِ، وَمِنْ سَيِّئِ الأَسْقَامِ))
((Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako na mbalanga, magonjwa ya akili, ukoma na magonjwa mabaya)). [Imepokelewa na Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na kusimuliwa na Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy].
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amejilinda na mambo haya manne, kwa kuwa mwana Aadam hawezi kujibandua nayo katika maisha yake ya usiku na mchana. Ikiwa hatakuwa nayo yeye, basi atayakuta kwa wenzake wanaomzunguka wakiwa Waislamu au wasio Waislamu, na madhara yake yatamgusa pia yeye, atake asitake.
Na kwa kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amejilinda nayo, na kwa kuwa yeye ndiye kiigizo chema kwetu, na yeye ndiye aliye karibu zaidi na Allaah ('Azza wa Jalla), ni vizuri kwa Muislamu awe anaisoma du’aa hii kila siku ili Allaah (‘Azza wa Jalla) Amlinde na hayo yote kutokana na ubaya wake.